Bwana Yesu asifiwe sana, Tunakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo, sisi ni wazima tunamshukuru Mungu ambaye ametupa nafasi ya kuuona mwaka huu mpya wa 2011. Nina amini Mungu amekupa nawe mwaka huu mpya, jambo hilo ni la kumshukuru sana Mungu. Unajua Mungu kukupa nafasi ya kuona mwaka mpya ni neema. Mungu amekupa nafasi ya kuona mwaka mpya na amini anakusudi na wewe. Hebu jipange au muombe akujulishe kusudi la yeye kukupa nafasi ya kuishi na kuuona mwaka huu wa 2011. Mimi na familia yangu tumemuona Bwana akitulinda na kutufanikisha katika mambo mengi sana katika mwaka uliopita, tumekuwa na huduma nyingi ambazo Bwana alituwezesha kuzifanya. Tuna omba Mungu atuwezeshe mwaka huu kumtumikia kwa upana sana, na ili tufanikiwe sana Tunahitaji maombi yako sana, usinyamaze mpendwa tuombee, narudia tena tunaomba maombi yako.
Tumekuletea Salamu zetu za kila mwezi. Ni salamu maalumu kwa mwezi huu wa kwanza wa mwaka huu wa 2011. Kumbuka tumekuwa na mfululizo wa Salamu zenye kichwa kiitwacho MWOMBE MUNGU AKUGEUZE NIA YAKO. Hebu tusonge mbele katika eneo hilo la kugeuzwa nia. Kumbuka Mungu anataka ugeuzwe nia yako, neno la Mungu lina sema hivi. “…Bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yakupendeza, na ukamilifu.” (WARUMI 12: 2B). Ukiyasoma maneno hayo utaona wazi kuwa Mungu anataka ndugu yangu ugeuzwe nia yako, neno nia ni kusudio au fikra, kwa maana nzuri sana niseme ni mfumo mzima wa akili zako.
Katika salamu zetu za mwezi uliopita, tuliangalia jambo la pili linaloweza kuharibu hiyo nia yako nalo lilikuwa ni MAZOEA AU MAZINGIRA UNAYOISHI. Mwezi huu tusonge mbele kidogo tuangalie jambo la tatu nalo ni.….
NGUVU ZA GIZA
Sikiliza, moja ya mambo yanayoweza kupelekea fikra za mwanadamu kuharibiwa ni hili la adui kutumia nguvu za giza ili kuharibu mfumo mzima wa akili za mwanadamu. Adui anaweza kutumia mapepo au wachawi katika kuhakikisha anazihalibu fikra au akili za mtu, Sikiliza maneno haya ya Bwana yasemavyo, “….ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikra zao wasioamini……” (2KOR 4:4A). Ukiyasoma maneno hayo utaona neno mungu wa dunia hii limeanza na helufi ndogo, maana yake mungu huyo aliye andikwa hapo si Mungu Mkuu. Kama habari hiyo ingemuhusu Mungu mkuu aliye hai neno mungu lingeandikwa kwa helufi kubwa kama hivi “Mungu” ile helufi ya “m” ingekuwa ni ya herufi kubwa “M”. Ninaamini umenielewa hapo. Sikiliza, neno linasema mungu wa dunia hii amepofusha fikra zao! Lazima ujue wazi kuwa shetani anaweza kupofusha au kuziharibu fikra za mtu, au kwa lugha nzuri kuzigeuza, ama kuzipunguza au kuziondoa kabisa. Mtu anaweza kupungukiwa na akili au kuondolewa kabisa. “kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto walipungukiwa na akili wala hawana ufahamu……” YEREMIA 4:22) Adui anaweza kutumia nguvu za giza ili kuondoa ufahamu wako na kuzipunguza kabisa akili zako au za watu wengine.
Hebu yasikilize maneno haya ya Bwana yasemavyo, “(Maana Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zinauwezo katika Mungu hata kuangusha ngome); Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, na kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo.” (2KOR 10:4-5). Ukiyaangalia maneno hayo kwa kutulia utagundua haya niliyo yaona mimi na zaidi ya haya. sikiliza. Maneno ya Bwana yanasema hapo kuwa adui anaweza KUINUA kitu ambacho kinaweza kuharibu fikra ya mtu. Ona anasema tukiangusha ngome. hiyo ngome ukiiangalia ni ngome iliyoizingira fikra ya mtu isiwe huru. au isiwe kama vile Mungu alivyotaka iwe au niseme ni ngome iliyo ishikiria fikra au kuikandamiza. Fahamu mtu akikamatwa fikra yake hawezi kuwa na mawazo mema, au mawazo mazuri, atakuwa na mawazo mabaya tu, mawazo yasiyo ya maana katika habari za kumjua Mungu, katika habari za kiuchumia au za kimaendeleo. Mtu wa namna hiyo hafikirii habari za maisha yake ya kiroho au ya kiuchumi. Kwa sababu fikra zake zimezungushiwa ngome zizifikiriye kitu chema chochote.
Adui anaweza kuzipotosha fikra zako kwa kutumia nguvu za giza za kichawi, ona maneno haya ya Bwana ya semavyo. “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli, waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi(maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akisema Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa ibilisi, adui wa haki yote huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyooka?” (MDO 13:6-10).
Ukisoma maandiko hayo utaona kuwa Adui kwa kutumia uchawi alizipotoa akili za Sergio zilizokuwa nyingi. Neno lina sema Sergio alikuwa na akili nyingi, yaani mfumo wa fikra zake ulikuwa sawasawa, mawazo yake yalikuwa sawasawa, ufahamu wake ulikuwa mzuri kweli. Lakini ghafla….! alijikuta anaharibiwa akili zake na mchawi huyo. Kama si Mtume Paulo kuonyeshwa na Roho Mtakatifu mambo yanayoendelea kwenye ulimwengu wa roho, nakuambia ukweli akili za huyo ndugu wala zisingemjua Yesu kuwa ndiye Kristo. Kwa sababu zilikwisha potoshwa na huyo mchawi! Umeelewa hapo? Sikiliza, adui anaweza kuziharibu akili za mke wako, watoto wako, mume wako, au watu unaowafundisha liwe ni neno la Mungu au darasani. Ngoja nikuulize swali hili, haujawahi kuona mtu alikuwa na uwezo mkubwa sana wa akili darasani, lakini baada ya siku si nyingi mtu huyo akajikuta hana uwezo tena hapo darasani? Angalia inawezekana hata wewe umekutana na kitu kama hicho, zamani ulikuwa na fikra nzuri sana, au ni seme ulikuwa na akili nyingi, lakini sasa hivi wewe mwenyewe unajishuhudia kuwa huna uwezo ule wa kwanza, sikiliza inawezekana adui ameziloga akili zako! Amezipotoa haziendi vile Mungu alitaka ziende, zinaenda tofauti kabisaaa.
Watu wengi adui kaziharibu fikra zao, lakini hawajui. Ameziondoa lakini hawajui, wanafanya mambo ambayo mtu mwenye akili nzuri hawezi kufanya. Angalia sana ndugu yangu, inawezekana hata wewe umenasa kwenye kona hiyo, akili zako zimeharibiwa au zimelogwa na adui ndio maana humpendi mke wako kama ulivyokuwa unampenda zamani, au wewe mke humpendi mume wako kama ulivyokuwa unampenda zamani. Adui anaweza kutumia mapepo kuziharibu fikra zako zisimuone mke wako zikapotoka kabisa na kuanza kuangalia mwanamke mwingine au zikaangalia mapepo! Sikiliza wapo watu wengi hasa wanawake ambao mapepo yamewaharibu akili zao na wakajikuta wanaolewa na hayo mapepo. Hata wanaume wapo ambao wameolewa na hayo mapepo. Adui aliwaingilia kwenye akili zao akazipotoa na kuzifanya zielekee njia zisizo za Bwana Yesu. Watu wengi leo hii wameacha wake zao na familia zao na kuwaoa wanawake wengine kwa sababu hii AKILI ZAO ZIMEROGWA!. Waswahili wana sema wamelishwa limbwata. Sikiliza adui anatumia pepo linalowekwa katika hilo limbwata ili kuhalibu akili za mwanaume aliyekusudiwa kutekwa akili, mtu wa namna hiyo usifikilie anajua afanyacho, hafahamu kitu mpaka akili zake zigeuzwe ndipo atajua ameacha mke na watoto sehemu Fulani.
Ukisoma maandiko matakatifu utaona siku moja Mtume Paulo aliwauliza Wagalatia swali hili “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? (GAL 3:1). Angalia maneno hayo utaona hao watu Mtume Paulo aligundua kuwa hawana akili. Na aligundua kuwa wamelogwa! Adui aliwaondolea hao WAGALATIA AKILI ZAO ZILIZOKUWA NZURI KWA KUWAROGA! Umeelewa mpendwa?
Kama leo hii unataka uwe na akili au nia ama fikra njema lazima ulijue jambo hili la tatu, Wakristo wachache sana ambao wanafanya maombi maalumu ya kuzilinda akili zao zisilogwe, au za watoto wao au za waume zao ama za wake zao nk. Sikiliza hao Wagalatia waliologwa akili zao fahamu walikuwa ni Wakristo. Walimpokea Yesu na walimfahamu kabisa Yesu Kristo. Lakini adui akazipotosha akili zao kwa kuwaloga wakajikuta wanaanza kupita njia nyingine kabisa ambayo Yesu hajawaagiza waipite. Wewe angalia leo hii Wakristo wengi walivyo. Utaona wana tabia ileile kama ya Wagalatia walio logwa akili zao. Ona wanavyotaka kutembea kwenye njia ileile waliyoipita Wagalatia ambayo Mtume Paulo aliigundua kuwa ni njia iliyotokana na kulogwa akili.
Njia yenyewe ilikuwa ni ya kupita kwenye sheria badala ya Imani. Wewe soma kitabu chote cha Wagalatia ndipo utagundua hiki ni nacho kuambia. Wakristo wengi wanafikiri kama Wagalatia walivyokuwa wanafikiri kwa fikra zao zilizologwa kuwa wataukamilisha Ukristo wao kwa sheria Fulani walizo jiweke, kwa lugha nzuri niseme mapokeo yao. Ukisoma maneno hayo katika kitabu chote cha Wagalatia utajitathimini wewe mwenyewe kuwa je! Adui kaziloga hizo akili zako au la. Kama utaona kuwa akili zako zimehalibiwa kwa kutumia nguvu za giza, anza kufanya maombi maalumu ili Yesu Kristo azigeuze hizo akili au fikra zako zilizologwa, au zilizo tekwa na kutumikishwa na mapepo.
Angali je! Umekuwa ni mtu mwenye kusahau sahau? Au kutokuelewa? Au kuwa na hofu kila unaposhauriwa kufanya jambo ambalo wewe mwenyewe unaona ni zuri? Kama una sifa hizi fahamu inawezekana akili zako zimelogwa. Fanya maombi maalumu ya kuzikomboa akili zako, omba Mungu azigeuze akili zako hizo, Nakushauri maombi ya namna hiyo yafanye mara kwa mara si ya mara moja ni ya kudumu katika maisha yako yote. Kemea nguvu za giza zilizo haribu akili zakol Zivunje ngome zilizo kandamiza mawazo yako au mfumo mzima wa Akili zako. Tumia jin la Yesu Kristo katika kuvunja hizo ngome na Damu ya Yesu pia omba Nguvu za Roho Mtakatifu zikufungue na kukulinda kila mara.
Hizo ndizo salamu zetu za mwezi huu wa Kwanza kwako ndugu yetu mpendwa.
Mungu akubariki sana.
Wako katika Bwana Yesu Kristo
Mr Steven & Beth Mwakatwila.