Salamu – Januari, 2012

MAMBO MUHIMU UNAYO TAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO.  

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Mimi na familia yangu tunawasalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai. Mimi na familia yangu hatujambo kabisa. Tunamshukuru Mungu aliye tuokoa na kutupigania. Mwezi huu tunaanza kuziangalia salamu zenye somo lenye kichwa 

MAMBO MUHIMU UNAYO TAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO 

Ni somo la ndoa lakini kila mtu mwenye akili timamu anaweza kujifunza. Mwombe Roho Mtakatifu akufundishe kile alicho kikusudia kukufundisha, nakukaribisha karibu tuanze kujifunza. Hebu yasikie maneno haya ya Bwana jinsi yasemavyo  

“Bwana mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” (Isaya 48:17) 

Mpango wa Mungu katika somo hili ni kukupa wewe faida. Hebu mnyenyekee Mungu katika ujumbe huu, ninakuakikishia kweli, utapata faida baada ya kujifunza kila kitu kilichomo ndani ya somo hili. Mungu akubariki sana karibu tujifunze. 

MATATIZO MAKUBWA 

Siku moja nilikuwa nimepata mwaliko kutoka kwa Askofu mmoja. Alinialika niende pamoja naye kwenye shughuli za kuwaweka wakfu watumishi wa Mungu katika huduma ya uchungaji. Nilimkubalia kwani nilipata kibali kutoka kwa Bwana kwenda huko, nikaukubali mwaliko huo. Sehemu hiyo ilikuwa mbali sana na sehemu ninayoishi, ilinilazimu kulala huko huko kwa usiku mmoja. Baada ya shughuli zile, usiku nilipokuwa nataka kulala tu, Roho Mtakatifu aliniambia maneno haya “Steven nataka nikufundishe somo la ndoa” Nikalipokea neno hilo moyoni mwangu, baada ya kulipokea neno hilo, nilipata maswali mengi sana, ambayo nilijiuliza mwenyewe. Nilijiuliza Je! Ndoa yangu ina matatizo? Sijui kuishi vema na mke wangu? nk. Nilipokuwa katika kujiuliza sana maswali hayo, Roho Mtakatifu akasema nami tena, akaniambia somo hilo ni kwa ajili ya watu wote. Unajua, Mungu anapokuambia watu wote ni tofauti sana na anapokuambia ni kwa ajiri ya watoto wangu. Sasa nikatambua kuwa somo hili ambalo Bwana amekusudia kulifundisha ni kwa ajili ya watu wote, yaani watoto wa Mungu na watu wake wote. Niliporudi kutoka safari ile nikamshirikisha mke wangu kitu hicho alichoniambia Bwana, tukaanza kuomba ili Bwana atufundishe kama alivyokusudia, nikakaa mkao wa kujifunza. 

Jambo la kwanza kabisa ambalo Bwana alianza kunifundisha alianzia kunionyesha namna watu wake walivyo na matatizo mengi, wawe waliookoka, wasiokoka, watumishi wake Mungu, viongozi wa serekari n.k. Alianza kwa kuniwekea kitu hicho, nilianza kuona kila tulipokwenda sehemu mabalimbali kwenye huduma za kufundisha semina ziwe siku za nyuma na hata wakati huu, tunakutana na watu wengi wakiwa na matatizo mengi sana. Watu wengi wanatufuata wakihitaji maombi na hata wengine wakitupigia simu na kutuandikia jumbe nyingi sana kwa kutumia simu au barua kwa njia ya mtandao wa internet wakiomba ushauri au maombi. Tulipoanza kuyaangalia hayo matatizo yao tukagundua kuwa katika asilimia mia ya hayo matatizo asilimia themanini ni matatizo yanayotokana na magomvi katika ndoa zao. Baada ya kujifunza hapo, ndipo tulipoweka bidii ya kujifunza hicho Bwana anachotaka kutufundisha. Ndoa nyingi sana hazipo vizuri, na kwa kuwa hazipo vizuri imepelekea maumivu makali sana kwa hao wana ndoa. Ukifuatilia kwa makini utagundua kuwa, watu wengi sana wanaoumwa leo hii au walio na matatizo ya kiuchumi au watu wanaokufa mapema chanzo chake ni magumu yaliyomo ndani ya ndoa. 

Angalia, leo hii matatizo yanayotokea kwa watoto wengi ya kukosa maadili na hata uwezo mdogo darasani kisa kikubwa kinatokana na matatizo yalimo ndani ya ndoa. Hata leo hii ukifuatilia watu wengi sana ambao Mungu amewaita kwenye utumishi wake wamekwama kisa kikubwa kilicho kwamisha ni tatizo lililomo kwenye ndoa yao. Matatizo yanayotokea kwenye ndoa yanapelekea watu wengi kukosa kuupata uzima wa milele, kwa sababu tu hawakukaa vizuri katika ndoa zao. Watu wengi sana wana matatizo kwenye eneo la kupokea majibu yao, tulipotulia tukagundua tatizo linalopelekea washindwe kupokea majibu yao ni kutokana na lililopo kwenye ndoa yao. Baada ya kuyaona hayo tukapata hamu ya kuanza kujifunza kwa bidii kile amabacho Mungu anataka kutufundisha ili tuwafundishe watu wake. Fahamu neno la Mungu linasema  hivi; 

“Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” (Isaya 48: 17) 

Mungu anataka upate faida katika kila jambo au kwa maana nzuri anataka ufanikiwe. Ili upate mafanikio anachofanya anakuletea mafundisho 

UHABA WA SOMO LA NDOA 

Jambo la pili ambalo Bwana alitufundisha ambalo ndilo linalopelekea leo hii kuwe na matatizo kwenye ndoa nyingi ni hili la watu kukosa ufahamu wa ni nini kiwapasacho kufanya waingiapo kuishi katika maisha ya ndoa. Ukiangalia utagundua kuwa somo la ndoa ni haba kanisani. Wewe angalia mwaka jana umesikia somo kama hilo hapo kanisani kwenu? Aumwaka huu kuna semina ya ndoa imepita hapo kanisani kwenu? Unajua hata zipitapo ona maandalizi yake yalivyo bubu. Leo hii ni rahisi kuwalaumu watu kuwa hawaishi maisha mema katika ndoa zao bila ya kuangalia chanzo cha matatizo ni nini. 

Ngoja nikuulize swali; Kabla haujaoa au kuolewa ulipokea mafundisho kutoka kwa mchungaji wako akikufundisha mambo muhimu unayotakiwa uyafanye utakapo anza kuishi na huyo mumeo au mkeo? Na kama alikufundisha Je! Alikufundisha kwa undani kabisa? Au ndio jujuu tuu? Wewe jijibu mwenyewe, utaona wengi hawana elimu ya namna hiyo, naizungumzia elimu ya Kibiblia, ile ya kumuona mama anavyoishi na baba au baba anavyoishi na mama au kaka anavyoishi na mke wake. Somo la ndoa kanisani limekuwa siri kubwa. Hilo ndilo tatizo kubwa. Angalia utagundua kuwa leo hii watu wengi wanaanza kujifunza kuishi maisha mema ya ndoa wakiwa ndani ya ndoa. Fikiri wameanza kujifunza wakiwa na miaka kumi au ishirini kwenye hiyo ndoa, swali langu kwa nini wasianze kujifunza somo hilo kabla ya kuingia ndani ya ndoa? 

Ninavyosema somo la ndoa, unaweza kuwaza habari za tendo la ndoa, sikia maisha ya ndoa ni zaidi ya tendo la ndoa! Kuna mambo mengi ambayo wanandoa wanapaswa wajifunze kuliko hilo moja tu, ambalo ndilo siri. Mungu alianza kwa kutufundisha hayo, nakumbuka alinifundisha kuwa kila mtu ambaye ana akili timamu anapaswa kujifunza awe ndani ya ndoa au akitarajia kuoa ama kuolewa siku moja. Leo hii watu wanaanza kujifunza wakiwa tayari ndani ya ndoa, wana watoto tayari nk. Unajua watu wa jinsi hiyo ni vigumu sana kupokea kitu kipya, wewe ona leo hii, kama kuna semina ya ndoa, utaona wanaokimbilia ni kina mama, unajua ni kwa nini? Wanaume wengi, wanajiona wanajua kwa kuwa wameoa na wamepata watoto, sasa unapomwambia kuna somo la ndoa haoni umuhimu wake. Ngoja nikupe mfano, unawafahamu madareva? Kila dereva anajiona yeye ni bora kuliko mwenzake, sasa ukimwita dereva eti umfundishe kuendesha gari wakati yeye anajiona anajua ni ngumu sana kukuelewa. Ndivyo ilivyo hata leo kwa watu wengi sana ni shida kuitikia wito wa kuja kujifunza somo hili la ndoa. Hebu sisi tuanze kujifunza 

SI MPANGO WA MUNGU NDOA IWE SEHEMU YA MATATIZO 

Ukiziangalia leo hii ndoa nyingi utaona wazi kuwa ndoa hizo zipo kwenye taabu sana. Wana ndoa wengi baada ya kuanza kuishi kama mke na mume wamejikuta wameangukia kwenye magomvi yanayopelekea maumivu makubwa. Na wengi wamefikiri au wamepokea na kuamini kuwa hayo ndiyo maisha ya ndoa. Unajua wengi wanafikiri hivyo, wewe sikiliza mahubiri au nasaha za wazazi siku ya sherehe ya ndoa. Utasikia muhubiri akisisitiza sana habari za kuvumiliana. Hata wazazi wa hao wanandoa utawasikiliza wakisema sana habari hizo za kuvumiliana, kwanini kuvumiliana? Kama si kutuambia kuwa huko kuna matatizo? Huwezi sema vumilia kama hakuna teso, kwa kuwa ndoa nyingi sana zimekuwa ni sehemu ya mateso ni rahisi kuona na kukubali kuwa ndoa ni sehemu ya mateso. Nakumbuka miaka ile ya nyuma kabla sijaoa tulikuwa na msemo mmoja, tukiona kijana mwenzetu anaoa, tulisema “Jamaa ananunua matatizo”. Unajua ni kwa nini tulikuwa na msemo huo? Tuliona ndio mfumo wa ndoa nyingi zilivyo. Mimi baba yangu alikua askari, bahati nzuri baba alikuwa afisa mkubwa tu, kesi nyingi ziliamuliwa hapo nyumbani, hasa za masuluhisho ya ndoa. Niliona namna kina mama wanavyopigwa na waume zao na hata wanaume wanaopigwa na wake zao! Ilikuwa ni kitu cha kawaida kusikia fulani amemtandika mke wake na kesho tukamuona huyo mama akiwa amevimba kweli usoni. Tuliona kuwa hayo ndiyo maisha ya ndoa, niliona namna watu wanavyofukuza wake zao na kuoa wengine hiyo ilikuwa ni jambo la kawaida kabisa. 

Tulipokua tulijenga mawazo kama hayo kuwa maisha ya ndoa ni ya matatizo tu, naamini hata watu wengi wanafikiri hivyo wamepokea hivyo, ndio maana kila anayeoa au kuolewa lazima aambiwe kuwa kavumilie. Sijui wewe uliambiwaje? Watu wengi wanatiana moyo utasikia wakisema, “Jipe moyo mpendwa hilo ndilo jaribu lako”. Utafikiri kweli Mungu ndio kalipanga hilo jaribu, sikiliza, si mpango wa Mungu kuwa ndoa iwe sehemu ya mateso au iwe ni sehmu ya matatizo yanayopelekea watu kukosa amani na hata kupata magonjwa na kufa au kushindwa kumtumikia Mungu wao 

MUNGU ANACHUKIA AONAPO MATATATIZO KATIKA NDOA 

Hebu uangalie moyo wa Mungu ulivyo, anasema; 

“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani, wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremiah 29:11) 

Fikiria hayo ndani ya moyo wako, Mungu hajawahi kukuwazia wewe mabaya, anakuwazia amani na matumaini au mafanikio, kama hajawahi kukuwazia mabaya, basi hata hilo tatizo kwenye ndoa yako yeye hajawahi kuliwazia likutokee. Anaiwazia amani na mambo mema na utulivu katika hiyo ndoa yako. Ukiona magumu katika ndoa yako fahamu chanzo chake ni adui shetani. Unajua ni kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu Mungu anaiheshimu sana ndoa yako. Ona maneno haya yasemavyo.  

“Ndoa na iheshimiwe na watu wote…….” (Ebr 13:4) 

Mungu amemwagiza kila mtu aiheshimu ndoa. Iwe yake au ya mtu mwingine. Hilo ni agizo mojawapo ambalo kila mtu amepewa haijalishi ni mtumishi wa Mungu, baba au mama, wifi, shangazi au mjomba, mkuu wako wa kazini nk. 

Mungu asingelituagiza sisi watu wake tuziheshimu ndoa zetu kama yeye haziheshimu hizo ndoa. Mungu anaziheshimu ndoa zetu sana. Nataka nikuulize swali je! Wewe unaiheshimu ndoa yako? Au ya watoto wako? Au ya jirani yako? Au ya ndugu yako? Au ndoa ya muumini hapo kanisani? Watu wengi hapo wamekwama. Wengi hawaziheshimu ndoa zao au za watu wengine. Ona mfano huu utaelewa, Kuhani Haruni mtumishi wa Mungu yeye na dada yake aitwaye Miriamu, hawakuiheshimu ndoa ya ndugu yao Musa. Mungu aliwakasirikia sana angalia maneno haya; 

“Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi……………. Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma”(Hesabu 12: 1-16) 

Mungu alimkasirika sana Miriamu na Haruni, kisa, hawakuiheshimu ndoa ya Musa! Fikiria Mungu alimpiga Miriamu kwa ukoma. Nataka nikuambie, ikiwa hauiheshimu ndoa yako au ya nduguyo ama jirani ukawaka kama hawa ndugu wawili kwa kusema “kaka au dada ama mtoto wangu kaoa dudu dudu” nakuambia ukweli Mungu anakukasirikia, tubu leo, tengeneza ndipo Mungu atakuondolea huo ukoma au laana iliyokukalia. Leo tumalizie kwa namna hiyo, tuonane tena mwezi ujao. Barikiwa 

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila