Salamu – Mar, 2017

Bwana Yesu KRisto asifiwe sana. Tunamshukuru Mungu aliyetupa nafasi ya kuuona mwezi huu wa tatu. Mpaka ninapokuletea salamu hizi tumemaliza semina Betheli Kkkt Sae  katika jiji la Mbeya.

Tulikua na semina nzuri sana. Tulipewa somo linalotufundisha namna ya mtu atakaye kupewa uwezo wa kumiliki juu ya nchi inatakiwa afanye nini.  Leo hii nimekuletea salamu za mwezi huu wa tatu nikiendelea kukuonyesha  madhara unayoweza kukutana nayo kama utakosea katika eneo la kutotulia au utawahi kulianzisha suala la kuoa au kuolewa bila muongozo kutoka kwa Mungu.

Hebu tuangalie jambo lingine linaloweza kukutokea ikiwa utawahi kujishughurisha na jambo la mapenzi.

UTAOA AU KUOLEWA NA MTU AMBAYE MUNGU HAKUKUPANGIA

Ikiwa utakosea katika jambo hili la mahusiano yako na mtu yeyote yule wa jinsia tofauti na wewe kwa kujianzishia mahusiano ya kimapenzi kwa tamaa zako tu fahamu ni rahisi sana kuolewa na mwanamume au kuoa mwanamke ambaye Mungu hakukupangia kabisa. Ukisoma maandiko matakatifu utaona wana wa Mungu kwa tamaa zao au haraka zao waliwaoa wanawake ambao Mungu hakuwapangia kabisa wawaoe na jambo hilo lilimuuzi sana Mungu “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike wakizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na wanadamu milele….” (MWANZO 6:1-3).

Ukiyasoma maneno hayo kwa kutulia utagundua hapo jambo hili ninalokuambia kuwa ukiwahi kulianzisha jambo hili la mapenzi utaoa mwanamke ambaye utamchagua wewe wala si Bwana Mungu kukuchagulia. Au itakuwa ni rahisi sana wewe dada kujichagulia mwanaume ambaye wewe unamtaka. Neno la Mungu linatufundisha kuwa hao wana wa Mungu walijichagulia wanawake wowote waliowataka wao. Unajua ni kwanini walifanya hivyo? Jibu ni rahisi hawakumsubiri Mungu, au kwa maana nyingine hawa kuwa na ushirika na Mungu katika jambo hili la kuoa kwao. Hawakumuuliza au kumuomba kwa ajiri ya jambo hili ili wapate muongozo wake na hata kujua majira na wakati wa kuoa au kuolewa kwao. Walijianzishia jambo hilo kwa kuolewa au kuoa ovyo ovyo tu. Walipowaona hao wanawake kuwa ni wazuri basi walijiolea tu, sikiliza dada yangu si kila mwanaume mzuri umuonaye mbele yako ni mwanaume ambaye Mungu anataka akuoe! Hata kama amekuja kwako na kukutaka akuoe kwa kufuata utaratibu mzuri wa kanisa. Sikiliza ndugu yangu si kila mwanamke mzuri aliye mbele yako basi Mungu anataka umuoe kwa sababu macho yako yamemuona ni mzuri. Awe mzuri wa umbo au sura. Vijana wengi sana kwa sababu ya haraka zao za kuanzisha mapenzi mapema wamejikuta wameoa au wameolewa na wanaume ambao kwa kweli Mungu hakuwapangia.

Hata kama Mungu aliwapangia lakini kwa haraka zao wamejikuta wakiolewa mapema au wakioa mapema kabla ya wakati uliopangwa na Bwana. Ebu ona ndoa nyingi leo za mkeka kwa lugha nzuri ndoa za kuoana nje ya utaratibu uliowekwa na kanisa, au hata kutokufuata utaratibu kwa wazazi wao wa pande zote mbili. Ebu ona jinsi mimba nyingi leo hii zilivyozaa ndoa isiyotalajiwa. Vijana wengi wanakosea katika suala hili la mahusiano, wana yaanzisha mapenzi mapema, na matokeo yake ni kupeana mimba na mwisho wake ni kuoana. Ukiangalia kilichosababisha wakaoana ni mimba hiyo iliyotungwa kwa tamaa zao tu. Ebu kaa ufikilie kwanini leo hii wana ndoa wengi wanaishi maisha ya kugombana? Jibu utagundua lipo hapo, wengi waliyaanzisha mapenzi mapema kwa kutamaniana wala si kwa kupendana. Sikiliza ndugu upendo wa kuoa au kuolewa ni tofauti sana na kutamaniana. Pendo hili nakuambia ukweli linakuja kwa wakati muafaka kutoka kwa Bwana. Vijana wengi wakiona makalio ya mwanamke fulani basi tamaa inawaka ndani yao na kufikiria kuishi pamoja na hao wanawake wakati ndio wako shule wanayaanzisha mapenzi ya kitoto matokeo yake ni mimba.

Na baada ya mimba ni kuoana, baadaye ndipo matatizo ya kutoelewana yanapoanza kwa sababu hakuna upendo katikati yao bali tamaa tu ndio iliyokuwa imewajaa, mwisho wake ni shida tupu. Nimewaona watu wengi sana leo hii ndoa zao zina matatizo kweli, kisa ni hiki ninacho kuambia cha kuyaanzisha mapenzi mapema, ni meona watu wengi wakisema “wazazi walinilazimisha kumuoa binti huyu, mimi sikuwa tayari kumuoa sasa hivi labda baadaye” unajua kijana huyo anasema hivyo wakati tayari kampa mimba binti huyo Sasa unafikiria aende wapi binti huyo? Na kama ulikuwa bado kwanini uliyaanzisha mapenzi mapema? Ukiwa kulianzisha jambo hili ni rahisi pia kumkataa yule ambaye kweli Mungu kakupa! Sikiliza, watu wengi kwa kutokujua kwao utawaona wanalianzisha mapema jambo hili la kuoa na kuolewa, tena wanalianzisha mapema sana, wanakaa na kupanga kabisa kuwa wataishi pamoja, lakini baada ya siku chache tu matatizo yanapowatokea utasikia mmoja anaanza kusema, sina amani ya kumuoa au kuolewa na fulani! Sikiliza, kukosa amani kuolewa au kumuoa huyo dada si kwamba labda Mungu hataki muishi pamoja! Ila inawezekana mume wahi mapema! Mungu hajapanga muishi pamoja kwa wakati huo mliojichagulia nyinyi.

Ngoja nikupe mfano huu wa maisha yangu, siku moja nilipokuwa naomba jambo hili la kuoa kwangu unajua mimi nilikuwa naomba sana Mungu anipe mke. Siku moja baada ya maombi yale, Mungu alinionyesha ono, ono lenyewe lilikuwa hivi “Niliona mti mkubwa sana wa mwembe na mti huo ulikuwa na matunda mengi sana, nilipoyaangalia hayo maembe mimi niliyaona kuwa yamekomaa, kumbe yalikuwa bado kukomaa. Yalikuwa mekundu kwa kupigwa na jua, na amini umewahi kuyaona maembe ya namna hiyo, kwa mbali utaliona kama limeiva kumbe bado kabisa. Sasa mimi nikachukua jiwe nikaanza kuyapiga hayo maembe, nikayapiga kweli tena kwa nguvu sana. Ila, hayaku dodoka chini. Sikudodosha hata embe moja chini! Baada ya kuangaika sana ndipo nikasikia sauti ya Bwana ikiniambia hivi “Steven maembe hayo bado ni mabichi, na hata ukifanikiwa kuliangusha hilo embe huwezi kulila ukalimaliza kwa sababu bado bichi litakuumiza meno, na likikuumiza meno utalitupa, akasema utalitupa kama fulani alivyolichuma mapema embe hilo kama hilo likiwa bichi na alipolila meno yakamuuma sana”

Unajua baada ya ono hilo, nika muomba Mungu aniambie nini maana ya ono hilo. Bwana alinifundisha kwa kuniuliza swali hili, Je! Ulikuwa unaomba nini? Nikakumbuka nilikuwa naomba habari za kupewa mke! Ikawatayari nimepata jibu kuwa nimewahi mapema kumbe Mungu alikuwa bado hajalianzisha jambo hilo. Na kweli nikafuatilia huyo ndugu niliyembiwa kuwa alikula embe kama hilo bichi na likamuumiza sana meno. Unajua nilikujakufahamu suala la kuolewa kwa huyo dada lilikuwa gumu sana, kwani alipolipeleka kwa wazazi wake wazazi wake walilikataa. Kisa kilikuwa huyo dada alipokutana na huyo kaka na kupatana kuolewa naye, badala ya kuwaambia wazazi wake aliwafuata viongozi wa kanisa haraka sana, na kuwaambia kuwa amepata mume mtalajiwa, na hao viongozi wa kanisa pasipo kutulia nao wakafanya papara kuanza kulitangaza kabla ya hao wazazi wa huyo dada kufahamu. Unajua wazazi wa huyo dada walilopolisikia kutoka kwa watu walikaa kimya. Siku yule dada anakwenda kuwaambi hao wazazi wake habari za kupata mume mtalajiwa wazazi wake walimkatalia kwa kusema wao sio wazazi wake bali hao viongozi wa kanisa ndio wazazi wake. Unajua jambo hilo lilikuwa gumu sana, na hata ndoa ya huyo dada ilikuwa na matatizo sana, unajua ndipo nilipopata maarifa kuwa kumbe suala hili linahitaji utulivu sana, hali hitaji papara kabisa. ukifanya haraka tu utaharibu kila kitu!

Sikia ndugu yangu watu wengi kwa kutotulia kwao wamesababisha kuwaacha wale ambao Mungu alikusudia kuwaona wanaishi pamoja kama mtu mke na mtu mume kwa sababu ya haraka zao. Inawezekana kabisa Mungu akakuambia na akatia upendo wake ndani yako wa kuolewa au kumuoa mtu fulani. Lakini kwa sababu ya kutotulia kwako ukakurupuka kwenda kumuambia wakati yeye Mungu bado hajamweka sawa katika suala hili. Yaani yeye bado wiito huo haujakaa sawasawa ndani yake wewe kwa haraka zako unafika na kumtamkia habari za kutaka kumuoa unafikiri kitatokea nini? Nakuambi ukweli atakukatalia na hata kukutangaza vibaya sana kwa wenzake! Matokeo yake utakata tamaa na kujianzishia jambo lingine kabisaa, umeelewa hapo? Tulia usiwe na papara katika kila jambo. Wengine iko hivi, Mungu anaweza kabisa kuwapangia kuoana na kuweka upendo ndani yao kabisa na wakakutana na kukaa na kulizungumzia suala hili la kuishi pamoja kama mke na mume hapo mbeleni na kupatana kabisa kuwa mbeleni wataishi pamoja kama mke na mume. Lakini kwa haraka zao wanajibeba na kulipeleka jambo hilo kwa wazazi wao bila kumshirikisha Mungu kuwa sasa tunataka kuwaambia hao wazazi wetu je! ni majira na wakati wazazi wetu walifahamu jambo hilo? Unajua Mungu anajua kila kitu. Ukiwana ushirika nae na ukamtaka ushauri nakuambi ukweli ikiwa majira yaliyopangwa kuwaambia wazazi wenu bado atakuambia usiende, mtashangaa mnakosa amani kabisa ya kuwaambia wazazi wenu. Anazo njia nyingi sana za kusema, ninachofahamu ni kuwa atasema tu nawewe kulingana na jinsi ulivyo. Sasa kwa sababu ya haraka, wengi baada tu ya kuambiwa ntakuoa basi, wana kimbia mbio kwa mama! utasikia wanasema “Mama Mungu ni mkubwa amenipa mume ambaye anataka anioe na amenitamkia na ni mcha Mungu mwenzangu”

Mama atauliza ni nani huyo? Ukimtajia tu, unajua atachosema? Atakukatalia kisa, eti hana kazi, au hamtaki huyo ni wa kabila fulani, au ni wa kanisa fulani, au mama yake anajidai sana au ukoo wake ni mbaya nk. Unajua vita ndio itaanzia hapo na mara nyingi ni kushindwa tu! Inawezekana hata wewe ulikutana na tatizo kama hili inawezekana ni kwasababu uliwahi mapema kuwaambia wazazi wako kabla ya wakati wake wa kuwaambia. Unaweza kuharibu kabisa mpango wa Mungu aliokupangia kwa kutokutulia kwako tu. Unaweza kusema mtumishi hivi mwanadamu anaweza kuharibu mpango wa Mungu? Nakumbia ukweli mwanadamu anaweza kuuharibu mpango ambao Mungu kaupanga. Wewe ebu jiulize swali hili je! Mungu alipanga kuwauwa wana wa Israeli jangwani? Sikiliza Mungu hakuwa na mpango huo kabisa. Mungu aliwapangia mpango mzuri kabisa wa kuwapeleka Kanani. Lakini wana wa Israeli wenyewe ndio waliouharibu mpango huo kwa sababu ya kutoamini kwao! Matokeo yake ni kufa jangwani! Umeelewa hapo? Ngoja nikupe mfano huu mzuri wa mtu mmoja ninaye mfahamu sana na ni mtu wa karibu sana na mimi. Yeye alipokuwa katika hali ya uhitaji wa kupewa mke kweli Mungu alisema naye juu ya kumuoa binti mmoja, na binti huyo alikuwa mbali sana na mahali anapoishi huyo ndugu. Yule ndugu akamuomba Mungu kuwa ikiwa kweli Mungu kampa huyo dada kuwa mkewe mtalajiwa basi awakutanishe. Unajua kweli Mungu alimkutanisha na huyo dada. Huyo ndugu alipomuona huyo dada siku ileile alimuogopa sana Mungu. Pia kwa kuwa yeye hakuwa na uhakika wa kumuoa huyo dada, unajua ilimchukua siku kumi na moja akiogopa kumwambia huyo dada. Baada ya siku kumi na moja za kuogopa kumwambia huyo ndugu alimuomba Mungu amtie nguvu za kukutana na huyo dada, anasema Mungu alimwambia hivi nenda kamuulize huyo dada kuwa Mungu ameniambia kuna jambo lililo kuleta na linanihusu mimi naomba uniambie!

Anasema alikutana na huyo dada na akamwambia kama alivyopewa neno la maarifa kutoka kwa Mungu. Anasema huyo dada akasema ni kweli nimekuja huku kwa sababu nimepewa neno na Bwana kuwa nije nikuone wewe, na mimi ninakusubili wewe uniambie neno. Yule dada akasema naomba wewe uniambie ulikuwa unaomba nini ndipo na mimi ntakuambia kilicho nileta. Huyo ndugu anasema alimwambia nilikuwa naomba kuhusu suala la kuoa kwangu, huyo dada akasema kweli hata mimi nilikuwa naomba jambo la kuolewa kwangu nikaambiwa nije huku na nimeambiwa wewe unajambo utaloniambia katika suala la kuolewa kwangu! Huyo ndugu akamwambia kuwa nimeambiwa kuwa wewe ndio mke wangu. Yule dada akalipokea jambo hilo. Unajua wakapatana kuoana. Huyo ndugu anasema Mungu alimwambia amwambie huyo dada asiende kuwaambia wazazi wake kwanza mpaka pale watakapo ambiwa kuwa wawa ambie wazazi wa upande wa mwanamke. Na akamwambia huyo dada na huyo dada akasema sawa hata waambia wazazi wake. Unajua siku ileile yule dada akawaambia hao wazazi wake. Matokeo yake wazazi wa huyo dada wakamkataa kabisa huyo kijana, kisa walisema hana kazi ni masikini. Yule dada alivumilia kama miezi mitatu hivi, baadaye akaiondoa ile imani aliyokuwa nayo kwanza akavunja patano lake na huyo ndugu.

Huyo dada akaolewa na mtu mwingine, ikabidi huyo kijana aanze upya maombi kwa Mungu ya kupewa mke. Na kweli Mungu akampatia mke ambaye anae mpaka sasa na wanaishi vizuri sana na Mungu kawabariki sana, sio kidogo sana. Kwa kweli wamebarikiwa kiroho hata kiuchumi, na kiutumishi umeuona mfano huo? Haraka zinaweza kukusababishia ukosee na kupoteza muujiza wako kutoka kwa Mungu. Ebu tulia, msubiri Bwana ili usije ukaoa au kuolewa na mtu ambaye Mungu hakukupangia.

Naamini umezipokea salamu zetu za mwezi huu katika kona hii kwa moyo mkunjufu kabisa. Mungu akusaidie kuyatendea kazi haya uliyojifunza. Tuonane tena mwezi ujao katika kona hii.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila

Salamu – Feb, 2017

Ndugu zetu katika Bwana Yesu Kristo Salaamu!!! Tunawakaribisha tena katika kona hii ya salamu za mwezi wa pili. Mwezi  ulipita tulianza kuwaletea salamu za mwezi zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKAIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA AU KUOLEWA).

Mwezi huu Ebu tuendelee mbele kidogo. Tuangalie jambo hili

NJIFUNZE KUTULIA

Ili upate kufanikiwa sana katika jambo hili la kuoa au kuolewa kwako unatakiwa utulie, usifanye haraka katika jambo hili, jilinde sana katika eneo hili, mwamini Mungu kuwa atakupa mumeo au mkeo usifanye hakikisha haufanyi papara. Kwanini leo hii vijana wengi sana katika suala hili wanahangaika sana? Ni kwa sababu wengi hawamwamini Mungu. Ndio maana wengi wanakuwa na haraka sana, wengi wanafikiri kama wanaume wanaisha au wanawake wanaisha hivi! Sikia wala hawaishi wapo na wataendelea kuumbwa tu. Vijana wengi na mabinti wengi wanasema tunamuamini sana Mungu katika jambo hili mtumishi, lakini ukiwaangalia ni watu wasio na imani kabisaa, kumbuka imani kuwa na hakika wa jambo litalajiwalo. Wengi hawana uhakika na jambo hilo. Ndio maana wanapapara sana.

Wengi hawajatulia, wengi wakiona binti anamchekea tu basi mawazo yao yana wapelekea kufikiri kuwa huenda huyu ndiye mke wangu. Kinadada ndio kabisaaaa! Asisaidiwe jambo na kaka fulani. Wengi huanza kufikiria na kujijengea moyoni mawazo na kufikiria kuwa huyo ni mume wake mtalajiwa Mungu kampa. Sikia dada yangu tulia. Usifanye haraka hujachelewa, usiwaze kuwa muda unaenda, fahamu wapo wanaume wengi tu leo hii ambao muda umeenda ila bado hawajaoa bado! Shetani asikudanganye kwa kukuzomea kuwa umechelewa, sikia haujachelewa muda bado upo ambao Mungu anataka akupeleke kwa huyo mwanaume aliyekuandalia yaani ubavu wako hasa. Mungu ndiye aliyeufahamu muda muafaka wa kumpeleka Hawa kwa Adamu. Mungu yeye ndiye aliyeona kuwa kwa muda huu sasa mwanamke huyu ndio unafaa nimpeleke kwa mume wake, hata wewe muda utafika tu wa kukupeleka kwa huyo mwanaume na muda huyo ukifika ndio huyo mwanaume utapomfahamu. Sikia, ebu ondoa mawazo ya kuwafikiria hao wanaume wengi ndani ya moyo wako kuwa fulani au fulani ndio atakaye kuoa eti kwa sababu anaonyesha kuwa anakupenda, sikia hakupendi ila anakutamani tu huyo tulia, usifanye haraka, neno la Bwana linasema hivi, “….Yeye aaminiye hatafanya haraka” (ISAYA 28:16B)

Ikiwa leo hii wewe unaimani kuwa Mungu ndiye atayekupa mke au mume basi unatakiwa usifanye haraka msubiri yeye au kwa maana nyingine tulia, acha kujiangaisha wewe katika suala hili. Msubiri Mungu akuhangaikie yeye. Fahamu Mungu anaposema usichochee wala kuyaamsha mapenzi anajua kuwa ukiwahi kulifanya jambo hili kuna madhara mengi sana utakutana nayo, nayo ni haya ebu tuangalie la kwanza.

UTACHOMEKEWA VINYAGO MOYONI MWAKO

Nimekutana na watu wengi wa kike na wakiume, wengi sana wamekuwa na maswali yanayofanana, wengi wameniuliza swali hili wakitakaushauri kwangu, utawasikia wakisema hivi. Mtumishi nimekuwa na shida inayonisumbua sana moyoni mwangu, nayo ni hii Mungu ananiambia kuwa ntamuoa fulani, au ntaolewa na fulani, lakini baada ya siku si nyingi na ambiwa au naonyeshwa mwanamke mwingine nashindwa kuelewa ni yupi sasa ntakaye muoa au atakaye kuwa mume wangu?

Naamini hata wewe inawezekana umekuwa na maono ya wanaume wengi au maono ya wanawake wengi kuwa ndio utakao waoa mpaka unachanganyikiwa kabisa kuwa ni nani. Wengine wamehisi huenda wanamapepo hivi. Sikia ukiwahi mapema katika jambo hili kuna hatari ya kuchomekewa moyoni mwako picha za wanaume au wanawake ambao utakuwa ukiwafikiria utawaoa, leo utamfikiria ni huyu baada ya siku si nyingi utapokea mwingine. Watu wengi sana kwa sababu ya kuwahi kwao kulianzisha jambo hili wamejikuta wakiwafikiria wake za watu kuwa ndio wake zao kisa eti wameona maono! Fahamu maono ya namna hiyo mara nyingi yanaletwa na kutotulia, hata ndoto za namna hiyo mara nyingi zinakuja kwa sababu ya kutotulia, ebu sikia maneno haya utaelewa ninacho sema. “Kwa maana ndoto huja kwa shughuri nyingi…” (MHUBIRI 5:3A)

Maono mengi na ndoto nyingi ambazo watu wengi wanaona hasa katika jambo hili la kuolewa au kuoa na kutokuwa za kweli baadaye au kuona kuwa fulani ndiye atakuwa mkeo mtalajiwa kumbe ni mke wa mtu au kuona fulani ndiye atakuwa mumeo kumbe ni mume wa mtu, maono hayo mara nyingi yanatoke kwa sababu ya kutotulia kwa hao wayaonao hayo maono! Wengi hujishughulisha kwa kuwaza na kutafakari sana jambo hilo na hata kujiangaisha kwa kutafuta kwa juhudi zao kuolewa au kuoa, na matokeo yake ni haya ya kuchomekewa ndani ya mioyo yao picha za watu fulani, na hata kuanza kusema kwa watu wengine kuwa Mungu amenifunulia fulani ndiye atakuwa mume wangu! Au ndiye atakuwa mke wangu! Kumbe mpendwa hicho ni kinyago tu ambacho tena umekitengeneza wewe mwenyewe kwa kuwaza kwako!

Watu wengi humuendea Mungu awape wake au awape wanaume huku ndani ya mioyo yao wakiwa na picha au wakiwa wameweka mtu fulani kuwa ndiye atakuwa mume wake au mke wake. Wanaenda kwa Mungu na kumuomba, “Baba Mungu naomba unipe mume wangu au unionyeshe ni nani atakaye kuwa mume wangu au atakaye kuwa mkewangu” wakati huo ndani ya akili zao kwa sababu ya haraka zao tayari wameishamfikiria mtu fulani kuwa huenda ndiye. Unajua Mungu atakujibu nini? Sikiliza atakujibu sawasawa na jinsi unavvofikiri wewe! Ebu msikilize Mungu asemavyo katika neno lake kuhusu jambo hili “Basi sema nao, uwaambie, Bwana Mungu asema hivi; kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi, Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkaguze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote. Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake kisha kumwendea nabii, na kumuuliza neno kwa ajili ya nafsi; mimi Bwana nitamjibu mimi mwenyewe” (EZEKIELI 14:4-7)

Ukisoma maneno hayo utagundua kuwa ikiwa umeweka ndani yako mawazo fulani au vinyago kama neno la Mungu lisemavyo, fahamu Mungu atakujibu sawasawa na jinsi ulivyoweka vinyago moyoni mwako. Neno sanamu au vinyago ni mawazo yako wewe mwenyewe au ni tamaa yako, neno la Mungu linaposema habari za vinyago au sanamu linasema ni mawazo mabaya au tamaa mbaya. Ona maneno haya yasemavyo. “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu” (WAKOLOSAI 3:5). Umeyasikia maneno hayo mpendwa? Mungu anaposema wameweka sanamu zao moyoni mwao ana maana kuwa watu hao wameweka mawazo yao au tayari wana sura ya mwanaume au mwanamke mioyoni mwao. Halafu ndio wanamwendea Mungu eti awape mume au mke. Ikiwa ndani ya moyo wako una picha ya mwanaume fulani au mwanamke na ukamwendea Bwana Mungu kumuomba akupe mke au mume, Fahamu atakujibu sawa sawa na ulivyoweka moyoni mwako! Watu wengi wamejikuta leo hii wakiyaanzisha mambo ya mapenzi mapema yaani kabla ya wakati, na wanakuwa na wanaume au wanawake wanaowafikiria kuwa kama wangewaoa au kama wangeolewa na wanaume hao basi ingekuwa vema sana. Na hapo ndipo matatizo yanapoanzia, kwani mtu huyo anaanza kushikilia hilo ono alilojibiwa au aliloliona kuwa ndio sahihi kabisaa, mtu anashikilia jambo hilo kwa muda mrefu.Tena inawezekana hata huyo mlegwa hajui kitu chochote kinachoendealea kweny e moyo wa mwenzie. Siku anapotaka kuoa au kuolewa na mtu mwingine ndipo hapo huyo aliweka kinyago moyoni anapojikuta katika hali mbaya sana. Mtu huyo hujeruhika sana moyoni mwake, na wengine wanakata tamaa kabisa ya kuendelea na wokovu au hata kujikuta wanakonda na kuona Mungu kawadanganya au kujihisi wanamapepo nk.

Umeelewa hayo mpendwa? Ukiwahi tu ni rahisi sana kuchomekewa sura za wanaume au wanawake ndani ya moyo wako, na matokeo yake utapata shida sana katika safari yako ya kwenda mbinguni na hata katika maisha yako ya hapa duniani. Mabinti wengi sana jambo hili linawasumbua sana, kwa haraka zao wamejikuta wakiwafikiria wanaume furani kuwa ndio watakao waoa na hata kutangaza kwa wenzao wakati siyo kweli. Ebu tulia msubiri Bwana alianzshe jambo hilo katika maisha yako. Mungu atakupa yule amtakaye na ikiwa umefika wakati nakuambia ukweli atakupa upako ambao utakuongoza moja kwa moja kwa huyo ambaye Mungu anataka akuoe au uolewe naye. Pia upako huo utakusaidia kukulinda na vinyago, na amini katika sehemu hiyo umeelewa.

MUNGU AKUBARIKI NA KUKUSAIDIA KUYAFANYIA KAZI HAYO ULIYOJIFUNZA. Barikiwa sana.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila

Salamu – Jan, 2017

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Mimi na familia yangu Tunamshukuru sana Mungu ambaye ametupa uzima na kutujaria kuona mwaka huu wa 2017. Mwaka jana tumemuona Mungu akitubariki sana na kutupigania na mambo mengi mno.

Naamini hata wewe ni hivyohivyo. Tunamuamini Mungu mwaka huu pia atazidi kututendea mambo makubwa mno na kutupa matumaini katika kila jambo.  Katika kona hii ya salamu za mwezi mpya. Na niimani yetu kuwa kila mtu ambaye atapitia salamu hizi atapokea kitu

Hebu mruhusu Roho Mtakatifu akufundishe somo hili. Salamu zetu zimewalenga sana watu wale ambao bado hawajoa au kuolewa.

Kuna mambo ambayo Mungu ametufundisha nasi tumeona tuyaachilie kwa kila mtu hata yule aliyeoa au kuolewa ili ajifunze kitu na awafundishe vijana na mabinti wengine. Ebu pokea salamu hizi

(MAMBO MUHIMU UNAYOTAKAIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA AU KUOLEWA).

Katika somo hili ambalo tunaanza kujifunza leo, tutapita na kuona mahusiano ya watu wa jinsia mbili, yaani jinsia ya kiume na jinsia ya kike, Namwamini Mungu kuwa ata kwenda kukupatia kitu katika somo hili, kwani leo hii watu wngi sana ambao hawajaoa au kuolewa walifikiripo jambo hili huwapa taabu sana. Wengi linawachanganya sana, na ukiangalia suala hili la mahusiano kati ya watu wa jinsia hizi mbili tofauti yaani jinsia ya kiume na jinsia ya kike linapokosewa kwa kutokukaa katika utaratibu ambao Mungu ameuweka linaweza kuleta madhara makubwa kiroho pia hata kukatisha maisha. Watu wengi kwa kukosea katika suala hili la mahusiano kati ya watu wa jinsia hizi mbili wamejikuta wakipata shida sana hata kufa mapema kabla ya wakati. Neno la Bwana linasema kuwa wapo watu wanao kufa kabla ya wakati wao ebu lisikilize neno la Bwana linavyosema “Usiwe mwovu kupita kiasi; wala usiwe mpumbavu; kwani ufe kabla ya wakati wako?” (MHUBILI 7:17). Fahamu ndugu yangu kuwa ukikosea leo hii katika suala hili la mahusiano yako na mtu wa jinsia tofauti kwa kuwa na uhusiano uliokinyume na maagizo ya Bwana Mungu, fahamu hata wewe unaweza kufa kabla ya wakati, vijana wengi sana leo wamejikuta wakiyakatisha maisha yao kwa kupitia jambo hili la mahusiano kati ya watu wa jinsia mbili yaani ya kike na kiume.

MATATIZO KATIKA NDOA NYINGI LEO

Ukiangalia hata ndoa nyingi leo hii zilivvo utaona, wanandoa wengi hawana mahusiano mazuri ni kwa kwa sababu ya makosa mengi waliyoyafanya kabla hawajaoa au kuolewa. Kwa kukosea kwao katika eneo hili la mahusiano yao na watu wa jinsia tofauti nao, yaani wengi wakati wa ujana wao walikosea katika eneo hili, leo hii wanajikuta katika magumu mengi sana, katika ndoa zao, Sikiliza ewe wewe dada inatakiwa uwe makini sana katika suala zima la mahusiano yako na wanaume wote, ukikosa tu katika eneo hili nakuambia ukweli utajikuta unaishi maisha ya shida sana huko mbeleni, hata maisha yako ya kiroho yanaweza kuhalibika kabisa, pia wewe kijana wa kuime unatakiwa uwe makini sana katika suala hili la kimahusiano na kinadada wote, kwani ukikosea tu utajikuta unaishi maisha ya tabu sana, Hata maisha yako ya kiroho yataharibika kabisa. Leo hii watu wengi sana kwa sababu ya kukosea katika suala hili la mahusiano wakati wa ujana wao wamejikuta wakijeruhika sana ndani ya mioyo yao.

Nimekutana na vijana wengi sana wakike na wakiume, wengi wao wamekuwa na majeraha sana ndani ya mioyo yao na majeraha hao yametoka na suala hili la mahusiano yao na watu wa jinsia tofauti nao. Wengi wanasikitika sana kwa kuachwa na watu waliowafikiria kuwa watawaoa, au wataolewa naonk. Vijana wengi leo hii wanapo ona jinsi wanandoa wengi wanavyoishi maisha ya magomvi katika ndoa zao, wanajukuta katika wakati mgumu sana wapofikiria kuhusu suala la kuoa au kuolewa kwao litakuwaje. Wengi hufukiri kuwa ikiwa leo hii wanandoa wengi wanaishi maisha bila mahusiano mazuri kwa kugombana na hata kuachana wanafikiri kuwa kama maisha ya kuoa au kuolewa ndivyo yalivyo basi hakuna haja ya kuoa au kuolewa.

Nimekutana na watu wengi ambao bado hawajao au kuolewa wengi wameniambia jambo hili la kuoa au kuolewa linawachanganya sana tena ni gumu mno. vijana wengi wa kiume wanaogopa sana kuoa wanawake wakolofi ambao wao wanaona kuwa watawasumbua, na hata kinadada pia wanamawazo hayo hayo. Wanaogopa sana kuolewa na wanaume ambao sio waaminifu, wanaume wakolofi watakao wapiga na kuwatesa wana hofu ya wanaume watakao shindwa kuwatunza vema nk. Kinadada wengi sa na walifikiripo suala hili linawapa shida sana. Kina dada wengi sana ndani ya mioyo yao nia yao kubwa sana ni kuolewa, wengi ndani ya mioyo yao wanafikiria sana kuwa wasipoolewa katika kipindi kile ambacho wao kwa akili zao wanaona kinafaa, wana ona kama ni aibu kubwa sana iliyowaangukia. Wengi ndani ya mioyo yao jambo hili linawapa shida sana, inawezekana hata wewe dada ndivyo ulivyo ndani ya moyo wako, i nawezekana umejeruhika sana au unajiuliza ufanye nini kabla hujaolewa ndani ya somo hili kuna mambo muhimu ambayo Bwana ameyaweka ndani ya moyo wangu ili nikuambie ili upate kufanikiwa katika suala hili la kuoa au kuolewa. Ebu tuone jambo la kwanza muhimu sana ambalo unatakiwa ulifanye nalo ni hili.

JAMBO LA KWANZA MSUBIRI MUNGU AANZISHE

Watu wengi sana jambo hili la kuoa au kuolewa linawapa tabu na wengi wamejikuta wamekwama na kukata tamaa ni kwa sababu ya kuwahi kwao kulianzisha jambo hili kabla ya majira na wakati ulioamuriwa na Bwana Mungu, ukiyasoma maneno ya Mungu kwa makini utaona wazi kuwa suala la kuoa ua kuolewa anaetakiwa kulianzisha ni Mungu wala si wewe! Ngoja niludie tena, suala hili la kuoa au kuolewa anaetakiwa alianzishe ni Mungu. nilikuwa najiuliza swali kwanini watu wngi sana hasa vijana wanajikuta leo hii wanahangaika sana katika suala hili la kuoa au kuolewa, na mahangaiko yao makubwa yapo pale wanapojikuta wakiwa wanawachumba wengi, yaani leo hii anafikiri fulani ndiye atakaye kuwa mke wake mtalajiwa au atakuwa mume mtalajiwa, vijana wengi wamejikuta wakihangaika kwa kuona watalajiwa hao wakiyeyuka kama nta iliyokutana na moto! Hivi hujaona watu wengi wakiwa na wachumba zaidi ya watano na asiwepo hata mmoja atakayemuoa! Na inawezekana wote hao walikuwa na mahusiano ya kuwa mke mtalajiwa au mume mtalajiwa, lakini cha ajabu inatokea baadaye asiolewe au asimuoe hata mmoja katika hao watu watano. Umewahi jiuliza ni kwanini inatokea hivyo? Jibu ni hili wengi wanawahi mapema kabla ya majira na wakati ulioamuliwa na Bwana. Nimeliona hili jambo limewatokea vijana wengi sana na limewachanganya sana, nimewaona watu wakaribu na mimi kabisa yaani rafiki zangu hata wapendwa wengi sana wakihangaika sana katika eneo hili, hata mimi kabla sijaoa nilipita katika kipindi kama hiki cha mahangaiko sana mpaka siku moja Bwana alipoamua kunifundisha kuwa inatakiwa nimsubilie yeye kwanza alianzishe jambo hili ndipo ntakapo fanikiwa kumpata mke mwema kutoka kwa Bwana! Tatizo kubwa liloko kwa watu wengi ni hili, Wengi wanawahi yaani wanalianzisha wao jambo hili kabla Bwana hajalianzisha! Ukiyasoma maneno ya Mungu kwa makini utaona jambo hili anayetakiwa alianzishe ni Mungu, ona mfano mzuri sana pale Adamu alipopewa mke na Bwana, maneno ya Mungu yanatufundisha kuwa aliyelianzisha jambo hilo alikuwa ni Bwana Mungu, ebu ona ilivyokuwa “Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” (MWANZO 2:18). Ndugu yangu mpendwa umeyasikia maneno hayo yanavyosema? Neno la Mungu linatufundisha kuwa Mungu ndiye aliyelianzisha suala hili la Adamu kuwa na mke wake! Mungu ndiye aliejua majira na wakati unaofaa Adamu awe na mke, ukiyasoma maneno hayo si Adamu aliyekwenda kwa Mungu na kuanza kumdai ampe mke! Bali Mungu ndiye aliye sema si vema mtu huyu awe peke yake! Ukiyaelewa maneno hayo nakuambia ukweli huta babaika katika suala hili la kuoa au kuolewa! Kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu akilianzisha jambo hili Mungu fahamu lazima atalimaliza tu. Neno la Bwana linasema hivi “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (FLP 1:60)

Bwana akianzisha jambo lolote lile ni lazima atalimaliza tu, ndivyo neno la Bwana linavyotufundisha, umeanza kufunguka sasa! jibu ni hili wengi sana wanalianzisha wao kwa sababu ya tamaa zao na haraka zao matokeo yake wanashindwa kulimaliza jambo hilo na ndipo wengi hujikuta wakiwa na majeraha ya kuachwa na hao watalajiwa wao, mabinti wengi sana wanajikuta katika msukumo mkubwa sana katika jambo hili la kuwahi, kwa sababu ya kutojua kwao kuwa kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa jambo hili la kuoa au kuolewa katika Biblia linaitwa “MAPENZI” sikia dada yangu usilianzishe jambo hili liache Mungu alianzishe yeye mwenyewe ndipo utakapo fanikiwa kumpata mume atokaye kwa Mungu ambaye atakutunza na kukupenda sio kukutamani! Neno la Mungu lina sema hivi “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe” (WIMBO ULIO BORA 2:7) Umeyasikia maneno hayo ya Bwana ewe binti mwenye kupendwa na Bwana? Hata wewe kijana umeyasikia maneno hayo ya Bwana? Sikia Mungu anawaonya vijana wote wahakikishe hawayaanzishi mambo ya mapenzi wao wenyewe, bali wasuburi yeye ayaanzishe! Mungu ameendelea kulisisitiza jambo hili hata kwenye kitabu cha (WIMBO ULIO BORA 3:5) “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe” Bwana Mungu aliamua kusisitiza sana jambo hili la kutoyaanzisha na kuyachochea mapenzi kwa vijana wake, anawafundisha vija wake wakike na kiume wasubiri mpaka yatakapoanza yenyewe..

Ukiyasoma maneno hayo ya Bwana utagundua jambo hili ninalolisema. Watu wengi leo hii jambo hili linawasumbua na hata kuwatesa na kuwapa majeraha mengi ndani ya mioyo yao ni kwa sababu ya kuwahi kwao kulianzisha jambo hili la mapenzi kama Biblia ilivyoliita. Ukiyaangalia maneno hayo utagundua kuwa kumbe kinadada wanaweza wao wenyewe kwa tamaa zao kulianzisha jambo hilo kabla ya majira na wakati wake! Ngoja nikuulize swali hili je! wewe hili jambo umepona? Au ndio tayari umelianzisha moyoni mwako? Sikia kama umelianzisha wewe mwenyewe kwa sababu ya tamaa zako nakushauri liache litakugharimu sana.Vijana wengi sana leo wamejikuta wakianzisha mahusiano ya kimapenzi wakati majira yaliyokubarika na Bwana bado kabisa, ngoja nikupe mfano huu, leo hii wewe kijana ndio kwanza unaaanza kusoma kidato cha kwanza umefika shuleni na umempata mpenzi ambaye unajidanganya kuwa atakuoa au mtaoana na mnaanza mahusiano ya mume mtalajiwa na mke mtalajiwa hivi unafikiri utamuoa huyo binti? au unafikiri huyo mwanaume atakuoa? Nakuhakikishia kwa asilimia kubwa sana hatakuoa wala hutamuoa huyo binti! Na msipoangalia mtaanguka kwenye zinaa tu, na kujisababishia majeraha makubwa ndani ya nafsi zenu, na hata kupoteza mwelekeo mzima wa maisha yako ya mbeleni, ya kiroho na kiuchumi. Unajua ni kwanini mtaanguka? Ni Kwa sababu hamna upako wa kuwasaidia katika kungojeana kwenu! Sikia Bwana akilianzisha jambo hilo anawapa hao watalajiwa upako wa kungojeana hawaingii kuzini, ila kama wamejianzishia wao hayo mahusiano, na amini watazini tu. Kama walivyo vijana wengi sana Wakikristo leo wanavyojikuta wakimkosea Mungu sana kwa kufanya dhambi ya uzinzi kwa sababu ya kuwahi kwao kuingia kwenye mapenzi kabla ya majira na wakati.

Sikia wewe kijana na wewe binti baba yako amekupeleka shule ili usome hakukupeleka hapo shule kwa ajiri ya kutafuta wake au waume, bali amekupeleka ili usome, fahamu hata Mungu anakushangaa sana kwa kuyachocha mapenzi kabla ya wakati, ebu achana na jambo hilo fanya kile ulichopelekewa hapo shuleni, jenga mahusiano na huyo binti au huyo kaka kama dada yako au kaka yako, ondoa hizo haraka zenu za kutaka muwe wapenzi. Hayo mambo Biblia inasema yatakuja kwa wakati wake, wewe soma Biblia utashangaa ukiona jinsi Isaka na Yakobo muda wakuoa kwao ulipofika walipewa wake zao ambao hawakuwahi hata kuwaona maishani mwao kwanza. Sikia huyo dada unayemfikiria kuwa utamuoa eti kwa sababu mnashinda naye nakuambia kwa asilimia kubwa sana siyo mkeo wala sio mumeo, umemtamani tu kwa sababu unaye karibu, na hata Mungu hajalianzisha jambo hilo ila wewe ndie uliyelianzisha. Vijana wengi leo hii wao ndio kila siku wanakwenda mbele za Mungu kumchokoza awape wake au waume, Fikiria kijana huyo leo hii bado anaishi kwa baba yake baba yake anamsomesha shule, unamtegeme babaya ko kwa kila kitu, lakini cha ajabu unakazana kwenye maombi Mungu akupe mke huoni kuwa umewahi sana katika jambo hilo? Hivi akikupa huyo mwanamke utampeleka wapi huyo mtoto wawatu?

Nimeona siku hizi vijana wengi sana kwa haraka zao wamejikuta wakiwapeleka wake zao kwa baba zao na kuanza kuishi nao hapohapo nyumbani kwa wazazi wao. Sikia Mungu anasema ukifika wakati ambao yeye ameupanga akupe mke au mume ni lazima uachane na baba yako na mama yako! “Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (MWANZO 2:24). Ukilifanya jambo hili kwa wakati wake ni lazima haya yatatokea, hutampeleka mkeo nyumbani kwenu ili muishi naye hapo utakuwa na mji wako kabisaa, sikia dada ukiliwahi hili jambo utajikuta unampeleka mtoto wako uliyemzaa kabla ya majira yaliyokusudiwa ya wewe kuwa na watoto kwa mama yako au kwa bibi yako nk. Ninapolizungumzia jambo inaweza ikawanivigumu kunielewa, lakini fanya hivi anza ku waangalia vijana wengi sana Wakikristo leo jinsi wanavyowahi sana katika suala hili la mapenzi. Wengi wanawahi sana wanayachochea sana mapenzi siku hizi, matokeo yake ni kuharibika kiroho na wengi wanakufa kabla ya wakati wake! Nenda mashuleni uone jinsi vijana wengi walivyo na wake watalajiwa na hao mabinti pia wanaharaka kupita dunia inavyolizunguka jua katika suala hili la kuchochea mapenzi. na matokeo yake mbeleni ni maanguko na majeraha sana.

Angalia wewe ukoje? Tubu tengeneza na uyafanyie kazi yale uliyoyapokea katika salamu hizi

Hebu leo tuishie hapo. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao. Barikiwa sana

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila