Ndugu zetu katika Bwana Yesu Kristo Salaamu!!! Tunawakaribisha tena katika kona hii ya salamu za mwezi wa pili. Mwezi  ulipita tulianza kuwaletea salamu za mwezi zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKAIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA AU KUOLEWA).

Mwezi huu Ebu tuendelee mbele kidogo. Tuangalie jambo hili

NJIFUNZE KUTULIA

Ili upate kufanikiwa sana katika jambo hili la kuoa au kuolewa kwako unatakiwa utulie, usifanye haraka katika jambo hili, jilinde sana katika eneo hili, mwamini Mungu kuwa atakupa mumeo au mkeo usifanye hakikisha haufanyi papara. Kwanini leo hii vijana wengi sana katika suala hili wanahangaika sana? Ni kwa sababu wengi hawamwamini Mungu. Ndio maana wengi wanakuwa na haraka sana, wengi wanafikiri kama wanaume wanaisha au wanawake wanaisha hivi! Sikia wala hawaishi wapo na wataendelea kuumbwa tu. Vijana wengi na mabinti wengi wanasema tunamuamini sana Mungu katika jambo hili mtumishi, lakini ukiwaangalia ni watu wasio na imani kabisaa, kumbuka imani kuwa na hakika wa jambo litalajiwalo. Wengi hawana uhakika na jambo hilo. Ndio maana wanapapara sana.

Wengi hawajatulia, wengi wakiona binti anamchekea tu basi mawazo yao yana wapelekea kufikiri kuwa huenda huyu ndiye mke wangu. Kinadada ndio kabisaaaa! Asisaidiwe jambo na kaka fulani. Wengi huanza kufikiria na kujijengea moyoni mawazo na kufikiria kuwa huyo ni mume wake mtalajiwa Mungu kampa. Sikia dada yangu tulia. Usifanye haraka hujachelewa, usiwaze kuwa muda unaenda, fahamu wapo wanaume wengi tu leo hii ambao muda umeenda ila bado hawajaoa bado! Shetani asikudanganye kwa kukuzomea kuwa umechelewa, sikia haujachelewa muda bado upo ambao Mungu anataka akupeleke kwa huyo mwanaume aliyekuandalia yaani ubavu wako hasa. Mungu ndiye aliyeufahamu muda muafaka wa kumpeleka Hawa kwa Adamu. Mungu yeye ndiye aliyeona kuwa kwa muda huu sasa mwanamke huyu ndio unafaa nimpeleke kwa mume wake, hata wewe muda utafika tu wa kukupeleka kwa huyo mwanaume na muda huyo ukifika ndio huyo mwanaume utapomfahamu. Sikia, ebu ondoa mawazo ya kuwafikiria hao wanaume wengi ndani ya moyo wako kuwa fulani au fulani ndio atakaye kuoa eti kwa sababu anaonyesha kuwa anakupenda, sikia hakupendi ila anakutamani tu huyo tulia, usifanye haraka, neno la Bwana linasema hivi, “….Yeye aaminiye hatafanya haraka” (ISAYA 28:16B)

Ikiwa leo hii wewe unaimani kuwa Mungu ndiye atayekupa mke au mume basi unatakiwa usifanye haraka msubiri yeye au kwa maana nyingine tulia, acha kujiangaisha wewe katika suala hili. Msubiri Mungu akuhangaikie yeye. Fahamu Mungu anaposema usichochee wala kuyaamsha mapenzi anajua kuwa ukiwahi kulifanya jambo hili kuna madhara mengi sana utakutana nayo, nayo ni haya ebu tuangalie la kwanza.

UTACHOMEKEWA VINYAGO MOYONI MWAKO

Nimekutana na watu wengi wa kike na wakiume, wengi sana wamekuwa na maswali yanayofanana, wengi wameniuliza swali hili wakitakaushauri kwangu, utawasikia wakisema hivi. Mtumishi nimekuwa na shida inayonisumbua sana moyoni mwangu, nayo ni hii Mungu ananiambia kuwa ntamuoa fulani, au ntaolewa na fulani, lakini baada ya siku si nyingi na ambiwa au naonyeshwa mwanamke mwingine nashindwa kuelewa ni yupi sasa ntakaye muoa au atakaye kuwa mume wangu?

Naamini hata wewe inawezekana umekuwa na maono ya wanaume wengi au maono ya wanawake wengi kuwa ndio utakao waoa mpaka unachanganyikiwa kabisa kuwa ni nani. Wengine wamehisi huenda wanamapepo hivi. Sikia ukiwahi mapema katika jambo hili kuna hatari ya kuchomekewa moyoni mwako picha za wanaume au wanawake ambao utakuwa ukiwafikiria utawaoa, leo utamfikiria ni huyu baada ya siku si nyingi utapokea mwingine. Watu wengi sana kwa sababu ya kuwahi kwao kulianzisha jambo hili wamejikuta wakiwafikiria wake za watu kuwa ndio wake zao kisa eti wameona maono! Fahamu maono ya namna hiyo mara nyingi yanaletwa na kutotulia, hata ndoto za namna hiyo mara nyingi zinakuja kwa sababu ya kutotulia, ebu sikia maneno haya utaelewa ninacho sema. “Kwa maana ndoto huja kwa shughuri nyingi…” (MHUBIRI 5:3A)

Maono mengi na ndoto nyingi ambazo watu wengi wanaona hasa katika jambo hili la kuolewa au kuoa na kutokuwa za kweli baadaye au kuona kuwa fulani ndiye atakuwa mkeo mtalajiwa kumbe ni mke wa mtu au kuona fulani ndiye atakuwa mumeo kumbe ni mume wa mtu, maono hayo mara nyingi yanatoke kwa sababu ya kutotulia kwa hao wayaonao hayo maono! Wengi hujishughulisha kwa kuwaza na kutafakari sana jambo hilo na hata kujiangaisha kwa kutafuta kwa juhudi zao kuolewa au kuoa, na matokeo yake ni haya ya kuchomekewa ndani ya mioyo yao picha za watu fulani, na hata kuanza kusema kwa watu wengine kuwa Mungu amenifunulia fulani ndiye atakuwa mume wangu! Au ndiye atakuwa mke wangu! Kumbe mpendwa hicho ni kinyago tu ambacho tena umekitengeneza wewe mwenyewe kwa kuwaza kwako!

Watu wengi humuendea Mungu awape wake au awape wanaume huku ndani ya mioyo yao wakiwa na picha au wakiwa wameweka mtu fulani kuwa ndiye atakuwa mume wake au mke wake. Wanaenda kwa Mungu na kumuomba, “Baba Mungu naomba unipe mume wangu au unionyeshe ni nani atakaye kuwa mume wangu au atakaye kuwa mkewangu” wakati huo ndani ya akili zao kwa sababu ya haraka zao tayari wameishamfikiria mtu fulani kuwa huenda ndiye. Unajua Mungu atakujibu nini? Sikiliza atakujibu sawasawa na jinsi unavvofikiri wewe! Ebu msikilize Mungu asemavyo katika neno lake kuhusu jambo hili “Basi sema nao, uwaambie, Bwana Mungu asema hivi; kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi, Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkaguze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote. Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake kisha kumwendea nabii, na kumuuliza neno kwa ajili ya nafsi; mimi Bwana nitamjibu mimi mwenyewe” (EZEKIELI 14:4-7)

Ukisoma maneno hayo utagundua kuwa ikiwa umeweka ndani yako mawazo fulani au vinyago kama neno la Mungu lisemavyo, fahamu Mungu atakujibu sawasawa na jinsi ulivyoweka vinyago moyoni mwako. Neno sanamu au vinyago ni mawazo yako wewe mwenyewe au ni tamaa yako, neno la Mungu linaposema habari za vinyago au sanamu linasema ni mawazo mabaya au tamaa mbaya. Ona maneno haya yasemavyo. “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu” (WAKOLOSAI 3:5). Umeyasikia maneno hayo mpendwa? Mungu anaposema wameweka sanamu zao moyoni mwao ana maana kuwa watu hao wameweka mawazo yao au tayari wana sura ya mwanaume au mwanamke mioyoni mwao. Halafu ndio wanamwendea Mungu eti awape mume au mke. Ikiwa ndani ya moyo wako una picha ya mwanaume fulani au mwanamke na ukamwendea Bwana Mungu kumuomba akupe mke au mume, Fahamu atakujibu sawa sawa na ulivyoweka moyoni mwako! Watu wengi wamejikuta leo hii wakiyaanzisha mambo ya mapenzi mapema yaani kabla ya wakati, na wanakuwa na wanaume au wanawake wanaowafikiria kuwa kama wangewaoa au kama wangeolewa na wanaume hao basi ingekuwa vema sana. Na hapo ndipo matatizo yanapoanzia, kwani mtu huyo anaanza kushikilia hilo ono alilojibiwa au aliloliona kuwa ndio sahihi kabisaa, mtu anashikilia jambo hilo kwa muda mrefu.Tena inawezekana hata huyo mlegwa hajui kitu chochote kinachoendealea kweny e moyo wa mwenzie. Siku anapotaka kuoa au kuolewa na mtu mwingine ndipo hapo huyo aliweka kinyago moyoni anapojikuta katika hali mbaya sana. Mtu huyo hujeruhika sana moyoni mwake, na wengine wanakata tamaa kabisa ya kuendelea na wokovu au hata kujikuta wanakonda na kuona Mungu kawadanganya au kujihisi wanamapepo nk.

Umeelewa hayo mpendwa? Ukiwahi tu ni rahisi sana kuchomekewa sura za wanaume au wanawake ndani ya moyo wako, na matokeo yake utapata shida sana katika safari yako ya kwenda mbinguni na hata katika maisha yako ya hapa duniani. Mabinti wengi sana jambo hili linawasumbua sana, kwa haraka zao wamejikuta wakiwafikiria wanaume furani kuwa ndio watakao waoa na hata kutangaza kwa wenzao wakati siyo kweli. Ebu tulia msubiri Bwana alianzshe jambo hilo katika maisha yako. Mungu atakupa yule amtakaye na ikiwa umefika wakati nakuambia ukweli atakupa upako ambao utakuongoza moja kwa moja kwa huyo ambaye Mungu anataka akuoe au uolewe naye. Pia upako huo utakusaidia kukulinda na vinyago, na amini katika sehemu hiyo umeelewa.

MUNGU AKUBARIKI NA KUKUSAIDIA KUYAFANYIA KAZI HAYO ULIYOJIFUNZA. Barikiwa sana.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila