Bwana Yesu KRisto asifiwe sana. Tunamshukuru Mungu aliyetupa nafasi ya kuuona mwezi huu wa tatu. Mpaka ninapokuletea salamu hizi tumemaliza semina Betheli Kkkt Sae  katika jiji la Mbeya.

Tulikua na semina nzuri sana. Tulipewa somo linalotufundisha namna ya mtu atakaye kupewa uwezo wa kumiliki juu ya nchi inatakiwa afanye nini.  Leo hii nimekuletea salamu za mwezi huu wa tatu nikiendelea kukuonyesha  madhara unayoweza kukutana nayo kama utakosea katika eneo la kutotulia au utawahi kulianzisha suala la kuoa au kuolewa bila muongozo kutoka kwa Mungu.

Hebu tuangalie jambo lingine linaloweza kukutokea ikiwa utawahi kujishughurisha na jambo la mapenzi.

UTAOA AU KUOLEWA NA MTU AMBAYE MUNGU HAKUKUPANGIA

Ikiwa utakosea katika jambo hili la mahusiano yako na mtu yeyote yule wa jinsia tofauti na wewe kwa kujianzishia mahusiano ya kimapenzi kwa tamaa zako tu fahamu ni rahisi sana kuolewa na mwanamume au kuoa mwanamke ambaye Mungu hakukupangia kabisa. Ukisoma maandiko matakatifu utaona wana wa Mungu kwa tamaa zao au haraka zao waliwaoa wanawake ambao Mungu hakuwapangia kabisa wawaoe na jambo hilo lilimuuzi sana Mungu “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike wakizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua. Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na wanadamu milele….” (MWANZO 6:1-3).

Ukiyasoma maneno hayo kwa kutulia utagundua hapo jambo hili ninalokuambia kuwa ukiwahi kulianzisha jambo hili la mapenzi utaoa mwanamke ambaye utamchagua wewe wala si Bwana Mungu kukuchagulia. Au itakuwa ni rahisi sana wewe dada kujichagulia mwanaume ambaye wewe unamtaka. Neno la Mungu linatufundisha kuwa hao wana wa Mungu walijichagulia wanawake wowote waliowataka wao. Unajua ni kwanini walifanya hivyo? Jibu ni rahisi hawakumsubiri Mungu, au kwa maana nyingine hawa kuwa na ushirika na Mungu katika jambo hili la kuoa kwao. Hawakumuuliza au kumuomba kwa ajiri ya jambo hili ili wapate muongozo wake na hata kujua majira na wakati wa kuoa au kuolewa kwao. Walijianzishia jambo hilo kwa kuolewa au kuoa ovyo ovyo tu. Walipowaona hao wanawake kuwa ni wazuri basi walijiolea tu, sikiliza dada yangu si kila mwanaume mzuri umuonaye mbele yako ni mwanaume ambaye Mungu anataka akuoe! Hata kama amekuja kwako na kukutaka akuoe kwa kufuata utaratibu mzuri wa kanisa. Sikiliza ndugu yangu si kila mwanamke mzuri aliye mbele yako basi Mungu anataka umuoe kwa sababu macho yako yamemuona ni mzuri. Awe mzuri wa umbo au sura. Vijana wengi sana kwa sababu ya haraka zao za kuanzisha mapenzi mapema wamejikuta wameoa au wameolewa na wanaume ambao kwa kweli Mungu hakuwapangia.

Hata kama Mungu aliwapangia lakini kwa haraka zao wamejikuta wakiolewa mapema au wakioa mapema kabla ya wakati uliopangwa na Bwana. Ebu ona ndoa nyingi leo za mkeka kwa lugha nzuri ndoa za kuoana nje ya utaratibu uliowekwa na kanisa, au hata kutokufuata utaratibu kwa wazazi wao wa pande zote mbili. Ebu ona jinsi mimba nyingi leo hii zilivyozaa ndoa isiyotalajiwa. Vijana wengi wanakosea katika suala hili la mahusiano, wana yaanzisha mapenzi mapema, na matokeo yake ni kupeana mimba na mwisho wake ni kuoana. Ukiangalia kilichosababisha wakaoana ni mimba hiyo iliyotungwa kwa tamaa zao tu. Ebu kaa ufikilie kwanini leo hii wana ndoa wengi wanaishi maisha ya kugombana? Jibu utagundua lipo hapo, wengi waliyaanzisha mapenzi mapema kwa kutamaniana wala si kwa kupendana. Sikiliza ndugu upendo wa kuoa au kuolewa ni tofauti sana na kutamaniana. Pendo hili nakuambia ukweli linakuja kwa wakati muafaka kutoka kwa Bwana. Vijana wengi wakiona makalio ya mwanamke fulani basi tamaa inawaka ndani yao na kufikiria kuishi pamoja na hao wanawake wakati ndio wako shule wanayaanzisha mapenzi ya kitoto matokeo yake ni mimba.

Na baada ya mimba ni kuoana, baadaye ndipo matatizo ya kutoelewana yanapoanza kwa sababu hakuna upendo katikati yao bali tamaa tu ndio iliyokuwa imewajaa, mwisho wake ni shida tupu. Nimewaona watu wengi sana leo hii ndoa zao zina matatizo kweli, kisa ni hiki ninacho kuambia cha kuyaanzisha mapenzi mapema, ni meona watu wengi wakisema “wazazi walinilazimisha kumuoa binti huyu, mimi sikuwa tayari kumuoa sasa hivi labda baadaye” unajua kijana huyo anasema hivyo wakati tayari kampa mimba binti huyo Sasa unafikiria aende wapi binti huyo? Na kama ulikuwa bado kwanini uliyaanzisha mapenzi mapema? Ukiwa kulianzisha jambo hili ni rahisi pia kumkataa yule ambaye kweli Mungu kakupa! Sikiliza, watu wengi kwa kutokujua kwao utawaona wanalianzisha mapema jambo hili la kuoa na kuolewa, tena wanalianzisha mapema sana, wanakaa na kupanga kabisa kuwa wataishi pamoja, lakini baada ya siku chache tu matatizo yanapowatokea utasikia mmoja anaanza kusema, sina amani ya kumuoa au kuolewa na fulani! Sikiliza, kukosa amani kuolewa au kumuoa huyo dada si kwamba labda Mungu hataki muishi pamoja! Ila inawezekana mume wahi mapema! Mungu hajapanga muishi pamoja kwa wakati huo mliojichagulia nyinyi.

Ngoja nikupe mfano huu wa maisha yangu, siku moja nilipokuwa naomba jambo hili la kuoa kwangu unajua mimi nilikuwa naomba sana Mungu anipe mke. Siku moja baada ya maombi yale, Mungu alinionyesha ono, ono lenyewe lilikuwa hivi “Niliona mti mkubwa sana wa mwembe na mti huo ulikuwa na matunda mengi sana, nilipoyaangalia hayo maembe mimi niliyaona kuwa yamekomaa, kumbe yalikuwa bado kukomaa. Yalikuwa mekundu kwa kupigwa na jua, na amini umewahi kuyaona maembe ya namna hiyo, kwa mbali utaliona kama limeiva kumbe bado kabisa. Sasa mimi nikachukua jiwe nikaanza kuyapiga hayo maembe, nikayapiga kweli tena kwa nguvu sana. Ila, hayaku dodoka chini. Sikudodosha hata embe moja chini! Baada ya kuangaika sana ndipo nikasikia sauti ya Bwana ikiniambia hivi “Steven maembe hayo bado ni mabichi, na hata ukifanikiwa kuliangusha hilo embe huwezi kulila ukalimaliza kwa sababu bado bichi litakuumiza meno, na likikuumiza meno utalitupa, akasema utalitupa kama fulani alivyolichuma mapema embe hilo kama hilo likiwa bichi na alipolila meno yakamuuma sana”

Unajua baada ya ono hilo, nika muomba Mungu aniambie nini maana ya ono hilo. Bwana alinifundisha kwa kuniuliza swali hili, Je! Ulikuwa unaomba nini? Nikakumbuka nilikuwa naomba habari za kupewa mke! Ikawatayari nimepata jibu kuwa nimewahi mapema kumbe Mungu alikuwa bado hajalianzisha jambo hilo. Na kweli nikafuatilia huyo ndugu niliyembiwa kuwa alikula embe kama hilo bichi na likamuumiza sana meno. Unajua nilikujakufahamu suala la kuolewa kwa huyo dada lilikuwa gumu sana, kwani alipolipeleka kwa wazazi wake wazazi wake walilikataa. Kisa kilikuwa huyo dada alipokutana na huyo kaka na kupatana kuolewa naye, badala ya kuwaambia wazazi wake aliwafuata viongozi wa kanisa haraka sana, na kuwaambia kuwa amepata mume mtalajiwa, na hao viongozi wa kanisa pasipo kutulia nao wakafanya papara kuanza kulitangaza kabla ya hao wazazi wa huyo dada kufahamu. Unajua wazazi wa huyo dada walilopolisikia kutoka kwa watu walikaa kimya. Siku yule dada anakwenda kuwaambi hao wazazi wake habari za kupata mume mtalajiwa wazazi wake walimkatalia kwa kusema wao sio wazazi wake bali hao viongozi wa kanisa ndio wazazi wake. Unajua jambo hilo lilikuwa gumu sana, na hata ndoa ya huyo dada ilikuwa na matatizo sana, unajua ndipo nilipopata maarifa kuwa kumbe suala hili linahitaji utulivu sana, hali hitaji papara kabisa. ukifanya haraka tu utaharibu kila kitu!

Sikia ndugu yangu watu wengi kwa kutotulia kwao wamesababisha kuwaacha wale ambao Mungu alikusudia kuwaona wanaishi pamoja kama mtu mke na mtu mume kwa sababu ya haraka zao. Inawezekana kabisa Mungu akakuambia na akatia upendo wake ndani yako wa kuolewa au kumuoa mtu fulani. Lakini kwa sababu ya kutotulia kwako ukakurupuka kwenda kumuambia wakati yeye Mungu bado hajamweka sawa katika suala hili. Yaani yeye bado wiito huo haujakaa sawasawa ndani yake wewe kwa haraka zako unafika na kumtamkia habari za kutaka kumuoa unafikiri kitatokea nini? Nakuambi ukweli atakukatalia na hata kukutangaza vibaya sana kwa wenzake! Matokeo yake utakata tamaa na kujianzishia jambo lingine kabisaa, umeelewa hapo? Tulia usiwe na papara katika kila jambo. Wengine iko hivi, Mungu anaweza kabisa kuwapangia kuoana na kuweka upendo ndani yao kabisa na wakakutana na kukaa na kulizungumzia suala hili la kuishi pamoja kama mke na mume hapo mbeleni na kupatana kabisa kuwa mbeleni wataishi pamoja kama mke na mume. Lakini kwa haraka zao wanajibeba na kulipeleka jambo hilo kwa wazazi wao bila kumshirikisha Mungu kuwa sasa tunataka kuwaambia hao wazazi wetu je! ni majira na wakati wazazi wetu walifahamu jambo hilo? Unajua Mungu anajua kila kitu. Ukiwana ushirika nae na ukamtaka ushauri nakuambi ukweli ikiwa majira yaliyopangwa kuwaambia wazazi wenu bado atakuambia usiende, mtashangaa mnakosa amani kabisa ya kuwaambia wazazi wenu. Anazo njia nyingi sana za kusema, ninachofahamu ni kuwa atasema tu nawewe kulingana na jinsi ulivyo. Sasa kwa sababu ya haraka, wengi baada tu ya kuambiwa ntakuoa basi, wana kimbia mbio kwa mama! utasikia wanasema “Mama Mungu ni mkubwa amenipa mume ambaye anataka anioe na amenitamkia na ni mcha Mungu mwenzangu”

Mama atauliza ni nani huyo? Ukimtajia tu, unajua atachosema? Atakukatalia kisa, eti hana kazi, au hamtaki huyo ni wa kabila fulani, au ni wa kanisa fulani, au mama yake anajidai sana au ukoo wake ni mbaya nk. Unajua vita ndio itaanzia hapo na mara nyingi ni kushindwa tu! Inawezekana hata wewe ulikutana na tatizo kama hili inawezekana ni kwasababu uliwahi mapema kuwaambia wazazi wako kabla ya wakati wake wa kuwaambia. Unaweza kuharibu kabisa mpango wa Mungu aliokupangia kwa kutokutulia kwako tu. Unaweza kusema mtumishi hivi mwanadamu anaweza kuharibu mpango wa Mungu? Nakumbia ukweli mwanadamu anaweza kuuharibu mpango ambao Mungu kaupanga. Wewe ebu jiulize swali hili je! Mungu alipanga kuwauwa wana wa Israeli jangwani? Sikiliza Mungu hakuwa na mpango huo kabisa. Mungu aliwapangia mpango mzuri kabisa wa kuwapeleka Kanani. Lakini wana wa Israeli wenyewe ndio waliouharibu mpango huo kwa sababu ya kutoamini kwao! Matokeo yake ni kufa jangwani! Umeelewa hapo? Ngoja nikupe mfano huu mzuri wa mtu mmoja ninaye mfahamu sana na ni mtu wa karibu sana na mimi. Yeye alipokuwa katika hali ya uhitaji wa kupewa mke kweli Mungu alisema naye juu ya kumuoa binti mmoja, na binti huyo alikuwa mbali sana na mahali anapoishi huyo ndugu. Yule ndugu akamuomba Mungu kuwa ikiwa kweli Mungu kampa huyo dada kuwa mkewe mtalajiwa basi awakutanishe. Unajua kweli Mungu alimkutanisha na huyo dada. Huyo ndugu alipomuona huyo dada siku ileile alimuogopa sana Mungu. Pia kwa kuwa yeye hakuwa na uhakika wa kumuoa huyo dada, unajua ilimchukua siku kumi na moja akiogopa kumwambia huyo dada. Baada ya siku kumi na moja za kuogopa kumwambia huyo ndugu alimuomba Mungu amtie nguvu za kukutana na huyo dada, anasema Mungu alimwambia hivi nenda kamuulize huyo dada kuwa Mungu ameniambia kuna jambo lililo kuleta na linanihusu mimi naomba uniambie!

Anasema alikutana na huyo dada na akamwambia kama alivyopewa neno la maarifa kutoka kwa Mungu. Anasema huyo dada akasema ni kweli nimekuja huku kwa sababu nimepewa neno na Bwana kuwa nije nikuone wewe, na mimi ninakusubili wewe uniambie neno. Yule dada akasema naomba wewe uniambie ulikuwa unaomba nini ndipo na mimi ntakuambia kilicho nileta. Huyo ndugu anasema alimwambia nilikuwa naomba kuhusu suala la kuoa kwangu, huyo dada akasema kweli hata mimi nilikuwa naomba jambo la kuolewa kwangu nikaambiwa nije huku na nimeambiwa wewe unajambo utaloniambia katika suala la kuolewa kwangu! Huyo ndugu akamwambia kuwa nimeambiwa kuwa wewe ndio mke wangu. Yule dada akalipokea jambo hilo. Unajua wakapatana kuoana. Huyo ndugu anasema Mungu alimwambia amwambie huyo dada asiende kuwaambia wazazi wake kwanza mpaka pale watakapo ambiwa kuwa wawa ambie wazazi wa upande wa mwanamke. Na akamwambia huyo dada na huyo dada akasema sawa hata waambia wazazi wake. Unajua siku ileile yule dada akawaambia hao wazazi wake. Matokeo yake wazazi wa huyo dada wakamkataa kabisa huyo kijana, kisa walisema hana kazi ni masikini. Yule dada alivumilia kama miezi mitatu hivi, baadaye akaiondoa ile imani aliyokuwa nayo kwanza akavunja patano lake na huyo ndugu.

Huyo dada akaolewa na mtu mwingine, ikabidi huyo kijana aanze upya maombi kwa Mungu ya kupewa mke. Na kweli Mungu akampatia mke ambaye anae mpaka sasa na wanaishi vizuri sana na Mungu kawabariki sana, sio kidogo sana. Kwa kweli wamebarikiwa kiroho hata kiuchumi, na kiutumishi umeuona mfano huo? Haraka zinaweza kukusababishia ukosee na kupoteza muujiza wako kutoka kwa Mungu. Ebu tulia, msubiri Bwana ili usije ukaoa au kuolewa na mtu ambaye Mungu hakukupangia.

Naamini umezipokea salamu zetu za mwezi huu katika kona hii kwa moyo mkunjufu kabisa. Mungu akusaidie kuyatendea kazi haya uliyojifunza. Tuonane tena mwezi ujao katika kona hii.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila