Salamu – Sep, 2017

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Ninawasalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo aliye hai. Ni imani yangu kuwa Mungu ameendelea kukutunza na kukupatia nafasi ya kuuona mwezi huu.
Katika mwezi uliopita tulikua na semina Tukuyu mjini ilikua nzuri sana. Na tulipomaliza Tukuyu Mjini tukaunganisha Chunya mjini.

Tukuyu tulifanikiwa pia kuwa na siku mbili za kukaa na vijana. Tunamshukuru Mungu alitutembelea kwa namna yakipekee sana. Hebu tupokee salamu zetu za mwezi.

Kumbuka tunasalamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA NA KUOLEWA

Na tunaangalia eneo la

USIMUWEKEE MUNGU MIPAKA KATIKA SUALA HILI LA KUOA AUKUOLEWA

Ebu tusogee mbele kidogo katika eneo hili hili.

Sikia mimi Mungu alinianzishia mipango ya kuoa kabla sina kazi, kipindi hicho ndiyo wala sijui ntakula nini, unajua alinianzishia yeye,najua ninachosema, watu wengi walisema sasa utapata wapi mahali ya kuolea huyo mke? Je! Atakula nini,tena mkeo kasoma kuliko wewe,unajua ilikuwa taabu kwelikweli, niliwaambia Bwana ameniambia kuwa ni wakati uliokubalika mimi nioe.

Nakumbuka Baba yangu aliniambia sawa lakini usubiri mpaka mwaka ujao ndio ntakupa mahali ya kuolea, unajua Mungu ni Mungu akikuambia jambo wewe amini lianzishe yeye anajua kulimaliza kisawasawa, nakumbuka alikuja mtu mmoja akaniletea shilingi elfu ishirini, kipindi hicho kwa sisi wanyakyusa elfu ishirini ilikuwa ni fedha ya kishika uchumba.

Akaniambia Mungu ameniambia fedha hii umpe yule utakaye kumuoa akaseme kwa wazazi wake, mimi kwa kuwa na mheshimu Mungu nilikwenda kwake Mungu kumuuliza je! ni kweli hicho alicho niambia huyo ndugu kimetoka kwako?

Bwana akanijibu ni kweli, nikaenda kwa wazazi wangu nikwaambia, unajua baba yangu na mama yangu wakaniambia sasa ukimpa hiyo fedha watakuita na sasa hatuna mahali ya kukupa,itakuwa aibu, lakini kwa kuwa baba yangu na mama yangu wanamjua Mungu wakasema kama kweli Mungu kakuambia, basi ebu fanya alivyo kuambia, ni kampa Bett fedha hiyo akaipeleka nyumbani kwao, unajua kipindi hichohicho ndipo Mungu aliponitendea mambo makubwa sana, akanipa kazi, siku hiyohiyo ninapata kazi nikajiriwa na shirika moja la kimataifa ni la Wamarekani, Nikashangaa wakanipa nafasi ya kusimamia mkoa Mbeya, Na walinipa fedha nyingi sanaaa, tena baada ya miezi mitano nikapata gari, Siku kaa vizuri wakanipa nafasi ya kusimamia kanda.

Kanda hiyo ilikua inahusisha na nchi yoote ya Malawi. Unajua Siku ileile naajiliwa fedha ile waliyonipa ndiyo nilienda kutolea mahali.nilipeleka mahali!

Baba yangu nilipompigia simu kuwa aandae mshenga tutapeleka mahali, akaniambia mbona nimekuambia mahali ntakupa mwezi wa sita? Kwani kipindi hicho nilichokuwa namwambia ilikuwa ni mwezi wa tatu.

Mungu akamtangulia baba yangu miezi mitatu mizima, nilipomwambia kuwa baba nimepata kazi,tena ya maana sana kazi ambayo hailingani na umri wangu na hata elimu yangu,na pia nimepata fedha nzuri tu.

Alishangaa sana Tukaenda kupeleka mahali baada ya miezi michache nikaoa, nikapata mahali pa kuishi na mke wangu kwa amani mahali pazuri sana kiasi ambacho watu wanahisi hapo anaishi mzungu Fulani! Ehehee sifa na utukufu apewe Yesu Kristo Bwana wetu.

Kwa sehemu na amini ushuhuda huu umekufungua macho,usimwekee Mungu mipaka, mimi naishi vema na mke wangu hajanidharau eti kwa sababu anaelimu, sikia usijiwekee mpaka Kwa kumuomba Mungu eti akupe mwanamke asiye na elimu, au usiolewe na mwanaume asiye na elimu kama yako, au usiogope kuoa au kuolewa na mtoto wa masikini au tajiri,usijiwekee mipaka kuwa sitaoa au kuolewa na mtu wa kabila lingine,au kabila Fulani, kumbuka Musa alioa mkushi hata ndugu zake kina Haruni na Miliamu walikuwa na mashaka na Musa.

Maandiko yanasema hivi. “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana,alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.wakasema je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao………” {HESABU 12:1-10}

Umeyasikia maneno hayo? Musa hakumwekea,Mungu mipaka katika suala zima la kuoa kwake alioa Mkushi kitendo hicho kilipokelewa tofauti na ndugu zake hao, lakini hao ndugu hawa kujua kuwa Mungu ndiye aliyempa Musa mwanamke huyo.

Ukisoma mistari ya sita mpaka kumi utaona Mungu aliwakasirikia mpaka akampiga Miriamu, akawa na ukoma, hata wewe usimuwekee Mungu mipaka, sikiliza yupo mkeo au mumeo uliyewekewa na Mungu, ebu ukifika wakati mwombe akupe amtakaye yeye kwa faida yako.

Mpaka mwingine ambao nakushauri usimuwekee Mungu ni huu wa DHEHEBU. Sikiliza watu wengi leo wanajikuta wamekwama katika suala la kuoa na kuolewa ni kwa sababu ya kumuwekea Mungu mpaka wa kutoolewa na mtu wa dhehebu tofauti na lake au faragha yao.

Sikiliza Mungu yeye alivyo anaagalia mwili wake yaani watoto wake walioko duniani, wale waliomwamini Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, yeye haangalii watu wa dhehebu fulani, au faragha fulani. bahati mbaya sana watoto wa Mungu wengi akili zao zimefungwa na udhehebu sana, wanapofikiria habari za kuoa au kuolewa wanaangalia watu wale wanaokutana nao kanisani au faraghani kwao.

Kumbe mkeo au mumeo hayupo hapo kabisa, yupo kwenye dhehebu lingine kabisaa, sasa kama unamwomba akupe huyo mkeo au mumeo naye akikuona wewe unamawazo ya hapo hapo ulipo kwenye hilo dhehebu fahamu hata kupa, mpaka utakapo ondoa huo mpaka, ndipo atakapokupa mkeo au huyo mumeo.

Na mpaka huu ndio unaopelekea watoto wa Mungu wengi wajikute wamekwama kwenye eneo la kuoa au kuolewa.. Na hata kupelekea wengine kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu leo hii ndoa zao zina shida kweli ingawa wameokoka.

Watu wengi wanatafuta ushauri kwangu, utasikia ndugu ninaomba ushauri, nimepata mtu ambaye tumepanga kuishi kama mtu mke na mume, lakini kunatatizo, unamuuliza swali tatizo gani? Anakuambia tatizo nikuwa hatusali dhehebu moja.

Nikimuuliza je! Ameokoka anasema ndio, ila hatusali pamoja na viongozi wangu wa kanisa wanasema lazima nimpate mke humuhumu ndani ya dhehebu letu siyo nje ya dhehebu letu. lakini naona kabisa huyo ndiye anaye nifaa nifanyeje Mtumishi?

Inawezekeana hata wewe unatatizo hilo, nakushauri usimwekee Mungu mipaka, inawezekana yupo dhehebu tofauti lakini katika ulimwengu wa roho nyinyi wawili mpo pamoja yaani ni kanisa la Bwana Yesu Kristo. Unatakiwa uwe makini sana usifikiri mkeo mtalajiwa au mumeo mtalajiwa yupo hapo dhebuni kwenu, inawezekana kabisa hayupo hapo yuko kule ambako wewe hufikirii kuwa hao nao wameokoka kwa kuwa hamchangamani nao katika dhehebu lenu.

Ninaposema dhehebu ninamaana NI WAKRISTO WENZENU WALIOAMUA KUMWABUDU MUNGU KWA UTARATIBU WAUONAO WAO KUWA MZURI KULIKO WA WENGINE. Si zungumzii watu waabuduo miungu mingine. Si zungumzii watu WASIOMWAMINI BWANA YESU Kristo. Nataka nieleweke vizuri hapa. Usije ukasema mwalimu Mwakatwila kasema tuoane na WAPAGANI.

Mpaka mwingine ni huu, Usijikatie tamaa. kuna watu wengine wamejiwekea mpaka wa kuto olewa eti kwa sababu walizalia nyumbani. Sikiliza Mungu ndani ya moyo wake yupo tayari kukupa mumeo lakini umemuwekea mpaka huo, ulipokosea na kupata mtoto huyo kabla ya kuolewa sio tiketi ya kukufanya wewe usipewe mumeo na Mungu.

Ikiwa leo hii umempokea Yesu moyoni mwako au ulianguka baada ya kuokoka na ukatubu, unayo haki ya kwenda kwa Mungu ili akupe mumeo na nina amini atakupa kabisaaa. Unapokaa na kutulia utaona wazi kuna wanawake ambao walifanya uzinzi na wakazaa kabla ya kuolewa, lakini Mungu aliwapa waume na waliolewa na wakazaa watoto tena watoto ambao ni watumishi wa Mungu.

Unaposoma maandiko unaona kuna wanawake ambao walikuwa makahaba walibadilika na kuambatana na Mungu,na Mungu akawapa waume zao kabisaa. ona mfano wa mwanamke Rahabu Angalia mistari hii. “ Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye,je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo,hapo alipowakaribisha wajumbe,akawatoa nje kwanjia nyingine? { YAKOBO 2: 25 }

Rahabu alikuwa kahaba, lakini siku moja alipobadilika na kuamua kushikamana na Mungu kwa kuwasaidia wana wa Israeli Mungu alimpa Rahabu mume na kwa kupitia yeye uzao mtakatifu wa kizazi chake ulitokea, soma uzao wa Bwana Yesu Kristo utaona yumo Rahabu katika ukoo huo.

Angalia mistari hii uone.”Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese;Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria;Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia;Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia;Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori;Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi;Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo;Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.”(Mathayo 1:5-16)

Ukiipitia hiyo mistari unamuona Rahabu katajwa katika uzao mtakatifu. Hapo utapata picha kuwa Mungu anao uwezo wa kukupa wewe mumeo kabisa hata kama ulifuruga sana katika usichana wako, sikiliza usimuwekee Mungu mpaka hooo!! Mimi siwezi kuolewa kisa eti nilisha haribu nikafukuzwa shule nikazaa nyumbani nk. Tena ukijipanga vizuri na Mungu atakupa mwanaume ambaye hajawahi hata kuzini nakwambia.

Mpaka mwingine ambao watu wengi wanamuwekea Mungu ni huu. Kukataa kuolewa tena baada ya kufiwa na mume wa Kwanza.

Wanawake wengi leo hii baada ya kufiwa huwa wana muwekea Mungu mpaka wa kukataa kuolea tena. Neno la Mungu linatufundisha wazi kuwa, wanandoa wanafunguliwa tu pale mmoja wao anapokufa .

Huyo anaebaki anapata ruhusa ya kuoa au kuolewa tena. Pia neno la Mungu linapozungumzia mwanamke mjane, linasema wazi kuwa mwanamke apaswaye kuandikwa kuwa ni mjane ni yule ambaye ana pata umri wa miaka sitini.

Angalia mistari hii “Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja….……. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, watawale na madaraka ya nyumbani; wasimpe adui nafasi ya kulaumu maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata shetani.” { 1TIMOTHEO 5: 9 ; NA 14 -15}

Sasa ebu angalia Mungu anavyoona na sisi tunavyoona, utaona tunaona vitu tofauti sana, ona wanawake wengi ambao bado wana umri mdogo kabisa, Wanavyomwekea Mungu mpaka wa kuolewa baada ya kuondokewa na waume zao.Wengi hujiita wajane wakati Mungu hawatambui kuwa wajane. Kwasababu hawajafika miaka sitini.

Ni elimu ngumu sana tu hii ninayokuambia. Akifa mumeo Mungu hajakuwekea wewe mpaka wa kuolewa ni wewe tu unayeweza kuuweka huo mpaka. Sasa ukimuwekea mpaka unakua umemzuia asikutendee jambo la kukupatia mumeo ambaye angetunza hiyo familia yako na wewe mwenyewe kwa uzuri kabisaaa.

Bahati mbaya watu wengi kwa kukosa mafundisho wakimuona mwanamke aliyefiwa anaolewa tena huwa wana,chukulia kama mdhambi hivi. Ila mwanaume anapooa baada ya kufiwa watu hawashangai sana. Tena utasikia wanamtetea eti Aisee kukaapeke yake ni kazi sana afadhali kaoa!!!

Kwani mwanamke yeye kwake siyo kazi kukaa peke yake? Lazima tuwe na akili wapendwa. Mungu amemruhusu mwanamke kuolewa baada ya kufiwa kabisaa na anasema wazi kuwa wanawake ambao ni vijana wasipoolewa na wakakaa kwenye huo ujane mara nyingi hutumbukia dhambini. Angalia mistari hii uone na utajua umuhimu wa mwanamke kijana akifiwa inatakiwa aolewe.

Angalia anasema hivi.”Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja;naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Mwanamke aaminiye, akiwa ana wajane, na awasaidie mwenyewe, Kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.”(1Timotheo 5:9-16).

Ukiipitia hiyo mistari utanielewa haraka ninapokuambia usimuwekee Mungu mpaka ya kuolewa kwako kisa eti umefiwa. Mimi Mungu namwamini sana, anapotoa sifa za wajane vijana usifikiri anakosea. Wengi wamebanwa kwenye hayo Mungu kayasema.

Ushauri wangu kwako, ni huu, usimuwekee Mungu mpaka anza kumuomba akupe mumeo baada ya yule wakwanza kufariki. Ondoa wazo lakua siwezi olewa kwasababu wasioolewa wapo mimi nani ataniangalia baada ya kufiwa.?

Mwingine anasema mbona sasa mimi namalazi haya naolewaje mtumishi? Nikuulize swali kwani hujui kuwa wapo wanaume na wao wanamalazi? Wapo wanaume wengi tu wameoa wanawake wenye maradhi na si kua hawajui wanajua sana. Ninamna ya kukaa na wataalamu watakuelimisha nini cha kufanya.

Sikiliza usimuwekee Mungu mpaka katika habari hii ya kuoa au kuolewa kwako. Ukiweka mpaka inaweza fika kipindi ukahitaji kuolewa lakini kwa kuwa umuwekea mpaka inakuwa ngumu sana hasa kwako wewe uliye muwekea mpaka wa kuolewa au kuoa kwako.

Naamini umenielewa. Ebu tuachane hapa na tuonane mwezi ujao katika salamu za mwezi ujao. Mungu akubariki sana na amani yake Bwana Yesu Kristo ikae nawe.

PIA uunaweza kupata masomo yetu mengine kwenye maeneo yafuatayo.
1. Website yetu ya www.mwakatwila.org
2. Youtube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
3. Facebook ingia katika hiyo tovuti/website yetu utaona alama ya facebook (f) like na utapata maelezo ya kujiunga
4. Dvds au Cd
5. Vitabu
6. Kwa njia ya Redio mbalimbali

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222

Mungu akubariki sana.
Wako
Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila