Salamu – Oct, 2017

Mimi Steven na mke wangu Beth tunawasalimu Ndugu zetu katika Bwana. Sisi ni wazima tunamshukuru Mungu.

Tumekuletea leo Salamu za mwezi. Hizi ni salamu za mwezi wa kumi. Kumbuka mwezi uliopita tulikuletea mfululizo wa somo ambalo tunaendelea nalo  lenye kichwa

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA NA KUOLEWA

Na tuliangalia kipengere cha kutokumuwekea Mungu mipaka. Mwezi huu wa kumi nataka nikufundishe jambo lingine muhimu sana. Nalo ni hili.

JIFUNZE KUTENGENEZA MAZINGIRA NA USHAWISHI MKUBWA ILI UWE NA UWANJA MPANA WA KUCHAGUA AU KUCHAGULIWA.

Naomba unisikilize kwa makini. Mungu ndiye ampaye mtu mke au mume.  Hili ni jambo ambalo kila mtu aaminie analijua. Lakini ili Mungu ampe mtu kitu kuna mambo maalumua mbayo huyo mtu apewaye hicho kitu ili apewe lazima ayafanye

Sikia  hata katika masuala ya kupewa mume au mke yako hivyo hivyo. Sikia Mungu ili ampe mtu mke au mume ni lazima mtu huyo ajifunze kutengeneza mazingira mazuri ya kupewa na Mungu mke au mume na Mungu.

Watu wengi sana hujikuta wakiwa wamekwama kwenye jambo hili ni kwasababu ya wao kutokutengeneza mazingira au ushawishi mwema wa kupewa mume au mke na Mungu katika muda sahihi.

Ntakuonyesha mambo machache ambayo yanaweza kukubana kama haujayaweka sawa.

JAMBO LA KWANZA NI  ENEO ULIOPO.

Unaposoma Biblia unaona wazi kuwa eneo linaweza kuwa ndiyo mlango wa baraka zako.  Mungu alipokua ana nia ya kumbariki Ibrahimu alianza kwanza kumtengenezea Ibrahimu uepesi wa kuzipata baraka zake kwa kumpeleka kwenye  ENEO AMBALO AKIWEPO TU HUKO ATAZIPATA HIZO BARAKA ZAKE.

Angalia mistari hii.” “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.”(Mwanzo 12:1-4)

Ukiisoma hiyo mistari utaona wazi kuwa mlango wa baraka za Ibrahimu ulikua kwenye eneo. Na  Ili azipate hizo baraka ilitakiwa Ibrahimu awepo kwenye eneo hilo. Kama akiwa mbali na eneo hilo fahamu ni ngumu kupokea baraka zake halali kutoka kwa Mungu.

Unaweza kujiuliza kivipi? Msikilize Mungu ambaye ndiye mtoa hizo baraka anavyomfundisha Ibrahimu juu ya nini afanye ili azipate hizo baraka zake. Maandiko yanasema “Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru;” Mungu alimuamuru Ibrahimu kwa ajili ya suala la eneo la yeye kuwepo.

Sikiliza ALIMUAMURU!!! Hiyo ilikua amri ya mafanikio ya Ibrahimu. Akitii atapata akigoma hapati. Mungu akiamuru hakuna jambo lingine litakalo ondoa kile alichokiamuru NI YEYE MWENYEWE AKIAMUA KUONDOA HICHO ALICHO AMURU.

Nimekupa huo mfano kwa makusudi kabisa ili ukione kile ninachotaka kukufundisha. Sikia, ukikosea eneo la kuishi fahamu unaweza kujikuta ukikwama au ukijichelewesha sana katika suala la kuoa au kuolewa. Kumbuka suala la kuolewa kwako au kuoa kwako ni baraka.

Sasa angali kama baraka za mtu zinamahusiano na  eneo fahamu hata wewe ili suala la baraka hizi likukalie lazima uwepo mahali pale unapotakiwa uwepo na katika majira maalumu ya wewe kuwepo mahali hapo.

Ngoja nikupe mfano huu. Fikiria kidogo wewe leo hii unamuomba Mungu akupe mume au mke na mumeo au mkeo huyo mtarajiwa yupo  Kigoma tena kijijini kweli, na wewe ndiyo unaishi Dar es Salaam, Umezaliwa hapo umekulia hapo.

Na unaomba sana  kwa Mungu akupe mumeo au huyo mke na ndiyo yuko huko. Unafikiri Mungu atafanya nini? Naamini atakupeleka huko aliko. Kama hajakutoa huko Kigoma kukuleta Dar es Salaam basi atakutoa Dar es Salaam kukupeleka kigoma. Hapoooo!!! sasa ndipo penye shughuli kubwa!!! Eheheee. Utoke  jijini uende kijijini inakuja hiyo?

Mungu ana njia nyingi sana za kukupeleka huko ili huko ukakutane na baraka zako. Tatizo lipo kwenye eneo la kutii kile alichokuamuru. Ibrahimu alitii akawa baraka. Usifikiri ilikua ni jambo jepesi. Kutoka mahali ulikozaliwa na kukulia na ukajiwekea na kamji kako hapo na kwenda mahali pengine ni jambo gumu sana kukubalika.

Ngoja nikupe mfano. Fikiria ndiyo ulikua umeomba nafasi za kazi iwe serekalini au kwenye shirika nk  Na unashangaa umepangiwa Kigoma. Na una watu wenye nafasi ya kupangua huo uamisho na hujui kuwa  Eneo hilo la Kigoma ndiko aliko huyo awe ni mwanaume au mwanamke, na mkafanikiwa kabisaa kuupangua huo uamisho, na ukafurahi kweli kumbe, ndiyo umelipangua jambo la kuolewa kwako au kuoa kwako wewe mwenyewe na hao waliokusaidia..

Natamani kila mtu ajifunze. Unapopokea taarifa ya wewe kuishi eneo furani usikurupuke kukataa au kulikubari kirahisi rahisi tu. Jifunze kumuomba Mungu akujulishe ndani ya hilo eneo kuna nini? Huenda huko ndani ndiyo kuna mkeo au mumeo mtarajiwa.

Watu wengi hawalijui hili. Mungu anapokuletea mke au mume fahamu atampitisha kwenye familia furani.  Sasa hujui hiyo familia iko wapi. Na pia inawezekana Mungu kwa makusudio mema kabisaa akawa amemuweka huyo mwanamke au mwanaume kwenye eneo tofauti kabisaa na fikra zako.  Unaweza fikiri wewe kuwa yuko Arusha kumbe yuko Ruvuma hukoooo ndani kabisaa..

Sasa unapomuomba Mungu akupe huyo fahamu anaweza akakupeleka huko. Mwingine ndiyo anaomba utasikia anaomba anasema” Baba Mungu mlete sasa kwa jina la Yesu Kristo? Sikia MUNGU ANAWEZA AKAKUPELEKA WEWE BADARA YA YEYE KULETWA HAPOOO ULIPO!!!!

Kwanza wewe ndiye mwenye mzigo wa kuolewa au kuoa , yeye huo mzigo hana anahitaji kushituliwa hivi, unafikiri ninani anatakiwa aende huko? Si wewe mwenye mzigo?  Wewe ndiyo unatakiwa upelekwe huko.

Ngoja nikuulize swali kwa akili zako wewe unafikiri huyo mwanaume wa kukuoa au mwanamke wa kumuoa yupo kwenye eneo hilo ulilopo leo?  Kama jibu hujui kwanini  unakataa na huna wazo kabisaa la  kuishi mahali pengine?

Kama hujui kwanini ulifanya haraka kuondoka kwenye huo mji uliokuwa unaishi bila kumuuliza Mungu? Usishangae ulipoondoka tu ndiyo huyo akaletwa mjini hapo KAKUKOSA SASA unamsumbua Mungu weeee kumbe  wewe ndiye haujawa na utulivu.  Umeomba uamisho kwenda mahali pengine kumbe yeye ndiye  anaingia mjini hapo umeiona hiyo picha ilivyo? Kwa mtindo huo Kwanini usichelewe kuoa au kuolewa?

Sikia Yakobo ili apate mke mwema ilitakiwa aondoke kwenye eneo alilokua anaishi na akaenda eneo la mbali kabisaa,  Ona maandiko yanasema  aliambiwa hivi.”Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani.Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako.” (28:1-2)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Yakobo aliwekewa mke wake mahali furani. Kama asingeondoka katika mji huo aliokuwa akiiishi fahamu asingekutana na mkewe kabisaa.  Ukitaka kujua kuwa Mungu alimpeleka huko wewe soma kitabu chote cha Mwanzo  sura ya ishirini na nane mpaka  sura ya therathini na moja.

Utaona  hiki ninachokuambia. Mungu alikua pamoja naye.mkabisa katika suala kuondoka mahali alipokua akiishi na wazazi wake.

Hata Isaka  muda wake wa kupata mke ulipowadia utaona baba yake yaani mzee Ibrahimu alijua mke wa mtoto wake yuko mbali na eneo alilokuwepo Ibrahimu.

Ibrahimu alimuagiza msimamizi mkuu wa mali zake asafiri na kwenda mbali ili kumtafutia mwanae mke. Maandiko yanasema mpango huo uliratibiwa na Mungu. Angalia mistari hii.”BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko;na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko.Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.”(Mwanzo 24:7-10)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kabisa kuwa eneo au mahali furani mbali na ulipo kunaweza kukawa ndiko aliko huyo mwanamke au huyo mwanaume. Sasa usipolijua hili. Ni ngumu sana kupewa mke au mume katika majira sahihi.  Mpaka utakapo kuwepo mahali hapo.

Fikiria kidogo. Kama Ibrahimu bahati mbaya angekua hajui mke wa mwanawe yuko mahali gani ingekuwaje ? Mimi naamini Ibrahimu alilijua hili jambo mapema mno. Ndiyo maana alimwambia huyo ndugu kuwa malaika wa Mungu atampelekwa mbele ya huyo ndugu yaani atamuongoza mpaka mahali sahihi kwa mwanamke sahihi.

Ninachotaka kukujengea ni hiki jifunze kujua kuwa kuna eneo lililo mhifadhi mwanamke au mwanaume sahihi ambaye ndiye mkeo au mumeo mtalajiwa.  Ukilijua hili hauta ishi au kwenda mahali  popote hovyo-hovyo.

Unapomuomba Mungu kuhusu uongozi wake katika suala hili  la kuoa kwako au kuolewa kwako ni lazima ujue utaongozwa au kupelekwa mahali furani inaweza ikawani mbali mno na eneo unaloishi sasa.

Ngoja nikuchekeshe kidogo.  Inawezekana kabisaa ukashangaa unapata msukumo moyoni wa kwenda kumtembelea nduguyo au kwenda kwenye mkutano au kambi ya maombi au safari za kimapumziko mahali furani.

Msukumo huo ukikujia tulia, muombe Mungu, akikupa kibari cha kwenda huko kaa mkao wa kukiona kile Mungu anataka ukione. Si tu utakutana na baraka za kuwaambia watu habari njema au kufundishwa neno la Mungu au kuombea watu tuuu nk. Fahamu unaweza ukamkuta huko huyooo mtarajiwa.

Wewe waulize watu wengi waliooa leo. Utashangaa watakuambia tulionana kwa mara ya kwanza katika mji au nchi furani. Utamsikia mtu anasema, Mimi nilienda huko kimasomo mwenzangu alikuwepo kwenye mji huo kama mfanyakazi. Sasa tulionana kanisani. Unajua ndipooooooo……!!!!! Fikiria kidogo uliomba nafasi za kusoma kwenye nchi nyingi tu au kwenye vyuo vingi tu.

Ukashangaa unapata nchi kwanza hukuipenda hata katika uchaguzi wako ulikua ni uchaguzi wa mwisho kabisaa. Huko ndiko uliko kutana na mtu muhimu maishani mwako. Fikiri kidogo mtu wa namna hiyo angegoma kwenda huko ingekuwaje?

Unaweza kusema Mungu hashindwi bwana. Ni kweli lakini lazima ujue utaingia gharama ya kuusubiri mpango mpya wa Mungu kukukutanisha na huyo mtu. Kwa lugha nzuri utachelewa sanaaa.

Unapopewa uhamisho hata wa idara tu kwenda idara nyingine au ofis hii kwenda ofisi nyingine usikubali au kuukataa kirahisi rahisi tu.  Tulia muulize Mungu uhamisho huu ni kutoka kwako? Kuna nini ndani yake? Utashangaa Roho Mtakatifu anaweza kukujulisha kuwa ndani ya uhamisho huo kuna mumeo au mkeo mtarajiwa

Unaweza ukawa ni uamisho mgumu sana kwako, ni kama uhamisho wa kukupunguzia heshima hivi, kumbe huko ushukako ndiko yuko wakwako, ungekaa huko juu wala usingemkuta kwasababu yuko chini ili umpate lazima ushuke chiniiiiii?

Ngoja nikufundishe kitu cha kawaida tu. Fikiria kidogo unaishi eneo furani kwa muda wa miaka mingi upo hapo, na kila mtu katika ene hilo anakufahamu ndani nje. Na wewe mwenyewe unajua kabisaa ulishaharibu sana mjini hapo, na sasa umetulia na unahitaji mke au mumeo. Unafikiri wenyeji wa mji huo watakupa mke au mume wakati wanakujua kweli kweli kuwa wewe ulikua au ni kicheche?  Yaani  mtu ambaye haukutulia au haujatulia?

Unajua watakao kufuata  ili wakuoe ni wageni tu waliokuja mjini hapo. Na usishangae sana kuona wenyeji watawashitua tu.  Inawezekana wewe ni mtu mzuri tu lakini familia yako hapo kwenye hilo eneo ni familia isiyokubalika kwa jamii hiyo iliyokuzunguka, unafikiri itakua rahisi kuolewa au kuoa ukiwa kwenye eneo hilo?  Nakwambia eneo litakubana tu. Labda aje mgeni tu ndiyo utaona nuru kidogo hivi ya kuulizwa swali kama hili VIPI UMEOLEWA?

Ukienda maeneo mageni huko hata harufu yako watu hawaijui, hawajui kuwa ulikua mtu mbaya uliyebadilika. Kama watasikia ni harufu kwa mbali sanaaaa!!! Unajua kwanini nasema hivyo? Ni kwasababu wanadamu wengi hushika sana mabaya ya watu kuliko mema yao. Pia wanadamu wengi hukumbuka maovu ya watu kuliko mema yao. Wanadamu wengi wanasamehe lakini hawasahau. Wanayakumbuka mabaya ya watu tuuuu. Ni watu wachache wamepona hapo

Ni watu wachache sana husamehe na kusahau. Kwahiyo tabia zako mbaya ulizozifanya ukiwa katika eneo au mji huo fahamu zitakutengenezea mazingira magumu sana ya kuolewa au kuoa kwako.  Pia ni hekima kutoka mahali hapo kwa ajili ya afya yako ya kuoa au kuolewa La sivyo utakua mgonjwa tu yaani HAUTAPATA TIBA YA KUOLEWA AU KUOA MPAKA UHAMEEEEE!!!!!

Fanya majaribio hata ya mwezi mmoja tu ondoka mjini hapo nenda mji mwingine utaona KANURU KAKUOLEWA AU KUOA KANAANZIA TOKEA KWENYE BASI HIVI!!! Eheheee

Mtu mwingine hajanielewa ngoja nijaribu tena , na maana hii. Fkiria ulikua kahaba mjini hapo, na unataka kuolewa usifikiri ni rahisi mama  au dada wa mwanaume huyo atakaye kukuoa watakukubari uolewe na mwanawe au kaka yao kirahisi rahisi wakati wanajua kabisaa ulikua ni mdada wa namna gani HATA UKITULIA NAKWAMBIA wtakumbuka tu kuwa huyu si ndiyo yule binti wa furani alikua na tabia hiiii?

Ninakuambia ukweli mama huyo au kina dada hao  hawata kuamini kabisaa. Vita yako haitakua nyepesi tokea mnaanza mikakati ya kuoana mpaka kuolewa kwako na hata  ukiwa ndani ya ndoa yako ni rahisi kuivunja kwa maneno yao magumu

Ngoja nikuulize swali umenielewa sasa? Naamini sasa umenielewa,  Sikiliza swali hili hapo  ni kwa kila mtu ambaye ana wito wa kuoa na kuolewa na unaona kabisaa muda wako ni sasa au ndiyo umeanza hata kupita, umemuomba sana Mungu  nataka nikuuulize swali hili Unaishi wapi?

Je!! Una uhakika kuwa huyo mtarajiwa yuko mjini hapo? Kama huna uhakika ebu muombe Mungu juu ya suala hili, Nataka nikuongezee mfumo mwingine wa maombi yako.

Jifunze kuombea maeneo unayotakiwa uwepo kwa wakati sahihi ili ukutane naye huko.  Ngoja nikuchekeshe ingawa ni ukweli JIFUNZE KUSAFIRI SAFIRI UNAWEZA UKABAHATISHA KUKUTANA NAYE HUKO!!!!!!

Tuonane tena kwenye eneo hili la salamu za mwezi ujao. Mungu akubariki mno kwa kunisikiliza. Asante

PIA uunaweza kupata masomo yetu mengine kwenye maeneo yafuatayo.

  1. Website yetu ya mwakatwila.org
  2. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
  3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
  4. Dvds au Cd
  5. Vitabu
  6. Kwa njia ya Redio mbalimbali

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222

Mungu akubariki sana.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila