Salamu – Nov, 2017

Bwana Yesu Kristo apewe sifa sana. Tunamshukuru Mungu ambaye ametupa huu mwezi wa kumi na moja.  Ni neema kwakweli ya kuuona huu mwezi .

Katika mwezi uliopita tulikua na semina nyingi kwakweli. Na zilikua nzuri sana. Tulikua na semina Mbeya mjini. Semina ya wanawake tu. tulimuona Mungu sana. Alitufundisha somo zuri lenye kichwa Nguvu ya mwanamke katika kuujenga ufalme wa Mungu na uchumi katika familia yake. Tuliona nguvu iliyowekwa kwenye tumbo la uzazi la mwanamke.

Tukawa na semina watu wasio na ajira. Kwakweli adui aliipiga sana semina hii.. Tulikutana na mambo mengi magumu kwenye maandalizi ya hii semina. Tuliifanya ilikua nzuri. Na semina hii Mungu akipenda tutaiandaa tena kwani watu wengi mno wamebanwa hapo.  Niombi letu kwa Mungu tufunguliwe mlango wa kulifundisha somo hili kwa upana sana katika nchi yetu hii nk.

Pia tulipata muda wa kukutana na watumishi wa Mungu yaani waimbaji. Na Bwana alitupa somo zuri la kuzungumza nao. Ulikua ni muda mchache lakini wenye baraka sana naamini kila muimbaji aliyefika pale alipokea kitu.

Tukasafiri kwenda Dar es Salam. Huko tulikua na siku tano. Tulikua na semina ya aina yake. Tulikutana na wanaume siku moja, wanawake siku moja, vijana siku moja, wanamaombi siku moja watoto siku moja na siku ya mwisho tukawakutanisha woote yaani makundi yote.

Tulijifunza vitu vingi. Tukaondoka kwenda Singida huko Manyoni. Tulikua na somo lenye kichwa jifunze kuJenga  kwa Mungu ili Mungu ajenge kwako. Na nikawa na siku mbili Arusha. Baada ya Arusha tukaludi Mbeya eneo ambalo Mungu ametuhifadhi. Ilikua nikitoka Arusha tuanze semina tarehe moja mpaka tano huko Itigi.

Lakini siku moja kabla ya kuanza semina nikapokea taarifa kuwa ndugu zetu wameomba tuipeleke hiyo semina mpaka mwakani.  Tunamuomba Mungu atufungulie mlango huo hapo mwakani ikiwa ni mapenzi yake.

Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana watu wote ambao Mungu aliwatumia kufanikisha semina hizo kwa njia mbalimbali ambazo Mungu aliwatumia. Mungu awabariki sana sana. Na karibuni tena tuendeleze kazi hii ili ufalme wa Mungu ujengwe.

Sasa nikuletee salamu za mwezi Karibu sana.

Kumbuka tunasalamu zenye kichwa

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA NA KUOLEWA

Katika mwezi uliopita nilikuletea salamu ambazo zilituonyesha jambo lingine muhimu unalo takiwa ulianye kwenye kipengere cha JIFUNZE KUTENGENEZA MAZINGIRA NA USHAWISHI MKUBWA ILI UWE NA UWANJA MPANA WA KUCHAGUA AU KUCHAGULIWA. Na tulijifunza kuhusu habari za  JAMBO LA KWANZA NALO NI ENEO ULIPO

Ebu tujifunze  kitu kingine.

JAMBO LA PILI: JIFUNZE KUKAA KAMA MWANAUME HALISI AU MWANAMKE HALISI

Sikiliza moja ya jambo muhimu ambalo unatakiwa ulifanye ili kutengeneza ushawishi au mazingira mazuri ya kuoa au kuolewa ni hili ninalokuambia la jifunze kukaa kama mwanaume halisi au mwanamke halisi.

Mwanamke ana sifa zake zinazompa nafasi hiyo ya kuitwa mwanamke, na mwanaume pia vilevile anasifa zake zinazomtambulisha kuwa huyu ni mwanaume. Ukipoteza sifa zako zinazokubeba wewe kwenye eneo lako fahamu ni ngumu kuoa au kuolewa .

Ngoa nianze na vijana wa kiume kwanza. Vijana wengi wa kiume waliookoka  wanajikuta mara nyingi kukwama katika sula hili la kuoa kwao  moja ya sababu ni hii ninayokufundisha.  Sikia nikwambie ikiwa wewe mwanaume utakua na tabia za kike fahamu unajitengenezea mazingira magumu ya kuoa kwako.

Fahamu wazi kuwa mwanamke anamhitaji mwanaume wala hamuhitaji mwanamke mwenziwe. Labda awe hana AKILI. Maandiko yako wazi kuwa mwanaume au mwanamke anayemuhitaji mtu wa jinsia moja ya yeye fahamu mtu huyo hana Akili kichwani mwake.

Angalia mistari hii.” Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”(Warumi 1:24-28)

Ukiona mwanamke anamuhitaji mwanamke mweziwe au wanaume wakiwakiana tamaa fahamu akili zao ni mbovu. Sasa mimi nazungumza na  vijana wakiume na wakike walio na AKILI NZURI.

Sikia kijana mwanamke anamuhitaji mwanaume mwenye tabia za kiume. Akikuona unatabia kama za wanawake atavutiwa na nini sasa kwako?  Mwanamke anatamani aolewe na mwanaume ambaye anatabia haswa za kiume.

Mwanaume atakaye kuwa kichwa kweli, yaani kiongozi wa familia, mwanaume atakaye mhakikishia usalama wake, mwanaume atakaye mpa heshima mke wake, mwanaume ambaye ni jasiri atakaye tangulia mbele Kama kiongozi na kupampana na changamoto zozote bila kuogopa

Mwanaume ambaye anajiamini na kumjengea mwanamke uhodari moyoni mwake. Mwanaume asiye wekeza mambo mabaya moyoni mwenye kulaumu weee!! Mwanamke anatazamia aolewe na mwanaume mwenye uwezo wa kutatua matatizo ya huyo mwanamke, mwanaume mwenye  tabia ya kumuamini mwanamke wake.

mwanaume ambaye atakua mjenzi mzuri wa nafsi ya mwanamke wala si wa kumjeruhi moyoni. Mwanaume mwaminifu mwenye kutunza ahadi na mwenye msimamo wa kusimamia  kile kilicho bora. Mwanaume mwenye kujenga misingi bora ya kiroho na ya kiuchumi katika familia.

Mwanamke anamuhitaji mwanaume ambaye atasema kama mwanaume atacheka kama mwanaume nk!!!!

Fikiria kidogo wewe ni mwanaume ambaye ukicheka unacheka kama mwanamke ukilia unalia kama mwanamke. Ikiwa wewe ukilia unalia kama mwanamke unafikiri huyo mwanamke atakuhitaji?

Moja ya jambo baya sana lakini limefichika na linawapunguzia wanaume wengi nafasi mioyoni mwa wanawake ni hili la mwanaume kujikita kwenye makundi ya wanawake. Nakuambia ukweli ukiwa ni mtu wa kuambatana sana na wanawake fahamu kuoa kwako kutakua shida kwelikweli.

Simaanishi kuwa hao wanawake ni wapenzi wako. Namaanisha kuwa ndiyo watu wakaribu na wewe. Wewe fikiri kidogo wanakutuma mpaka uwasaidie kuwapaka rangi za midomo nk

Unajua ni kwanini inakua tabu mtu wa namna hiyo kuoa? Ni kwasababu ni rahisi kuwa kama wao, yaani utakua na tabia za kike  tu. Usishangae sana utajikuta unatabia ya kubinua midomo vile!!! Au kidole juu vile nk.

kama unafikiri nakutania wewe fanya utafiti utaona hiki ninachokuambia. Wanaume wengi wanaojitengenezea mazingira ya kuwa karibu sana na wanawake kuliko wanaume hujikuta wakipata shida sana kuoa. Hata wanawake ni hivyo hivyo.

Wewe fikiria umekopy tabia ya kudeka weee!!!! Eheheeee, unafikiri ni mwanamke gani atataka mwanaume wa kudekaaa? Yeye adeke na wewe udeke wapi na wapi hapo?

Unakuta mwanaume anapenda umbea huyoooo!!! Wanawake wanatabia yao, wanapenda maneno, ndiyo maana wanapenda tamthilia kweli. Sasa wanakukuta na wewe ni mtu wa tamthilia weee unalia kama wao kisa eti Marichui kaonewa!!! Eheheeeeee!!!

Wewe mwanaume haifai uwe unatabia za kuzira-zira weee!! Unanuna  weee!! Hizo siyo tabia za mwanaume bwana. We fikiri ndiyo unaanza mahusiano na huyo mwanamke hata mahali haujapeleka  unampiga,  mara umemnunia wiki, mara wivu weeeeee!!!

Eti  mwanaume analia anasema naniii unaniua mwenzio nakukataza kusikiliza hizo simu inawezekana ni wapesi wako. Sikia huyo mwanamke akijua kuwa wewe ni kilia lia  mpaka unataka kufa kwa wivu eti Mwanaume unalia unakufa kisa kusimamishwa kwa huyo mwanamke  njiani  na wanaume wengine!!!

Ngoja nikufundishe neno gumu sana. Mwanamke mzuri atafuatwa tu.  Sasa lazima wewe mwanaume ujue hilo na ujue namna ya KUMUONGOZA AKIFUTWA AFANYE NINI SI KULIALIA NA KUNUNA WEEE AU KUANZISHA MAGOMVI YASIYO NA MWISHO!! LAZIMA UWE NA MOYO WA CHUMA MWANAUME.

Hizo tabia ninazokuonyesha hapo wala si za kiume. Wewe umeambiwa ukae nae huyo kwa akili. Maana yake wanawake  WANAWEZA KUKULETEA WAO MAMBO. KAMA HAYO ILI WEWE UYAMALIZE. Si wewe uyalete.

Ukiwa mwanaume mshali fahamu unapoteza mvuto kwa wanawake na hapo ndio unapojikuta huna mlango mpana wa kuchagua. Kwani kila umwendeae atakutolea nje tu..

Maandiko yanatupa taarifa kuwa vijana wakiume wanaweza kuwa wa kutamanika kabisaa. Angalia mistari hii.”Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;

vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.”(Danieli 1: 3-4).

Angalia na mistari hii mingine”vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi.”(Ezekieli 23:23B)

Ukiipitia hiyo mistari utaona kuwa kuna sifa za kijana zinazoweza kupelekea Atamanike. Anaweza tamanika kwa wanawake au kwa viongozi au kwa jamii. Kijana wa sifa hii ya kutamanika fahamu mlango wake wa kuchagua hua mpana. Akiwa mtulivu na Bwana Yesu Kristo yumo ndani yake fahamu atapata mke bila mahangaiko mengi

Ukiipitia hiyo mistari utaona baadhi ya sifa za vijana hao wakiume. Unaziona sifa hizi hawana mawaaa, sifa nyingine ni werevu na wenye hekima na ni vijana wenye maarifa.

Kijana yoyote mwenye hekima na maarifa na asiye na mawaa fahamu mlango wake wa kuchaguliwa”kufuatwa ni mpana” ni rahisi yeye kuchagua.

Ngoja nikuambie kitu hiki, ukiwa huna mawaa na unahekima hauwezi kuwachanganya wanawake kwa kumwambia kila mmoja kuwa utamuoa.

Ukiwa na hizo sifa nirahisi Kujua kwanini uliumbwa mwanaume. Ukijitambua kuwa wewe ni mwanaume bwana huwezi hata siku moja kuwaumiza wanawake vijana kwa kuwadanganya kuwa utawaoa huku ukijua kabisaa humuoi.

Huwezi kuwa na wapenzi wawili kwasababu kichwa chako kiko safi bwana. Utamjua nani wa kukufaa na nani hakufai ili usimchanganye.

Mwanaume mwenye kujitambua hadanganywi au hatongozeki kwalugha nzuri kushawishiwa. Wewe soma Biblia utaona mwanamke alidanganywa mwanaume hakudanganywa.   Kwa maana nzuri alikua anajua nini anafanya. Sasa kijana mwenye sifa za kudanganywa au kutongozeka fahamu mwanaume wa namna hiyo anapoteza sifa ya kuitwa mwanaume.

Ukiona wewe kijana huna msimamo uoe nani wala usimsingizie mtu tatizo liko kwako UNATABIA TOFAUTI KABISAA YA UANAUME. Nimewaona vijana wengi hawana msimamo na hujikuta wakiyumbishwa hovyohovyo na maamuzi yao ya kuoa mwisho wa siku hujikuta hawaoi. Wanabaki kudai eti mambo yakuoa ni magumu. Kumbe ni wao tu wanatabia za zinazowaondolea uhalali wa kuoa.

Kwanini yasiwe magumu wakati wewe unajua kabisaa una mtu lakini kila mara wewe unajichanganya kwenye makundi ya mabinti? Huyo mtu wako nakuambia hatakuamini kabisa kuwa wewe ni waminifu.

Mara unarafiki huyu wakike anakutuma hata uende ukachukue fedha kwa mwanaume wake,  Huku ukijua kabisa una mtu wako. Sikia inawezekana ni kweli kabisa hao wasichana ni rafiki zako tu wala huna mahusiano nao ya kimapenzi, lakini lazima utambue kuwa UTAMPOTEZA HUYO MTU WAKO KWASABABU UNASHINDA NA WASICHANA WENGINE.  Wasichana wengi wakiona hivyo hupoteza imani zao kwa hao wanaume na huumia moyoni sana.

Lazima kijana ujue kuwa wanawake wengi (si wote), wanatabia ya kutaka kuona wasichana wenzao hawana amani kabisaa. Wakijua kuwa huyo mtu wako anakukataza usiambatane nao basi ndiyo watajitahidi kumuumiza mpaka akuache. Usifikirie watakuambia basi jitenge nasisi ndiyo watakuganda kama kupe ili wamuumize tu.

Ebu jifunze kutokucheka cheka hovyo na wasichana cheka nao kama mwanaume. Waheshimu watambue kuwa ni dada zako lakini  UKAE NAO KAMA MWANAUME SIYO WAKUZOEEEE WEEE!!!  Na hii itategemea wewe mwenyewe umeamua kuishi kama mwanaume.

Sikiliza mwanamke anatafuta kumuona mwanaume ambaye HANA SHIDA HIVI!!!!  Ndani ya moyo wa mwanamke anafikiri mwanaume hanaga taabu, shida, au msongo wa mawazo. Sasa ukiwa ni mwanaume wa kulialia shida weee kwa wanawake fahamu unapoteza sifa za uanaume.

Mwanamke anatarajia akija kwako akukute wewe  ukiwa shujaa, usiyeyumbishwa na kitu kiitwacho matatizo. Ili yeye akutwishe wewe. Sasa akikuona na wewe unalia au unalalamika kama yeye fahamu hautakua na utofauti naye, sasa akuhitaji wewe kwa kazi gani? Si mpo sawa tu? Yeye akija kwako basi ni kukufariji tuuuuuu!!! Sikia wewe mwanaume ndiye unatakiwa umtie huyo mwanamke moyo na kumfariji.

Ngoja nikupe mfano huu labda utanielewa. Angalia mistari hii utaona Musa alijua namna ya kuingia na kutoka kwa wanawake na watoto na watu wote waliokua chini yake.

Angalia mistari hii “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.”(Kutoka 14:13-16)..

Musa mbele ya watu HALIII ANAWATIA MOYO KWELIKWELI. Alijua pa kulilia ni wapi, alimlilia Mungu tu. Huko kwa Mungu alilia kama mwanamke kabisa, hiii hiii hiiiiii!!! Ndipo Mungu kama Bwana wake anapompa maarifa ya kufanya. Akitoka huko watu wanajua aisee huyu jamaa haogopi kabisaa, kumbe wangejua ni siri ya Musa na Mungu tu kuwa jamaa kalia kwelikweli. Sasa wewe mwanaume unalia weee mpaka bp  unazo hapo haujaoa  sasa ukimuoa si ndiyo utakufa kabisaa?

Jambo lingine mwanamke atalitarajia kuliona kwa mwanaume ni hili ni kwenye eneo la kutunzwa. Ukiwa ni mwanaume mwenye akili utajua kabisa kuwa mwanamke anahitaji matunzo kutoka kwako.

Nimewasikia vijana wengi wakiwalaumu wanawake kisa eti wanatafuta wanaume wenye fedha. Mimi kama mwalimu sitaki nikudanganye JIFUNZE LEO KUWA NA UCHUMI MZURI ILI UWE NA MLANGO MPANA WA KUCHAGUA. Kinyume cha hapo utabaki kuwalaumu wanawake weee!!!

Ngoja niishie hapo katika salamu za mwezi ujao ntakupitisha kwenye kona hii ya UCHUMI YAANI KIJANA ILI UWE NA MLANGO MPANA WA KUCHAGUA LAZIMA UHAKIKISHE UNA VITU VIWILI. Uwe na Bwana Yesu Kristo na uhakikishe una fedha. Umenielewa hapo?

Mungu akubariki na kukusaidia kubadilika kijana.

PIA uunaweza kupata masomo yetu mengine kwenye maeneo yafuatayo.
1.Website yetu ya www.mwakatwila.org
2. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
4.Dvds au Cd
5.Vitabu
6.Kwa njia ya Redio mbalimbali
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222
Mungu akubariki sana.
Wako
Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila