Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Mimi na familia yangu tunamshukuru Mungu sana ambaye amekua mwema kwetu na kutupatia huu mwezi wa pili katika huu mwaka.

Mwezi uliopita yaani wa kwanza tumekua na semina ya mabinti. Kwa kweli ilikua semina nzuri sana. Tulimuona Mungu akiwahudumia mabinti waliofika pale. Pia kwetu ulikua ni mwezi mgumu sana kwasababu  baba yetu mkubwa alitwaliwa na Bwana. Kwa kweli ilituumiza sana.

Lakini tunajenga tumaini kwa Mungu ambaye ni mwaminifu  ambaye tunaamini ataendelea kutufariji watoto na wajukuu na vituguu wake wote. Pia naamini ataendelea kuwatia nguvu wadogo zake wakike na wakiume.

Ebu tuanze kukuletea salamu zetu. Katika salamu zilizopita nilikufundisha kijana jambo muhimu ambalo unatakiwa uhakikishe unalifanya ili uwe mtu wa mafanikio na kuutengeneza mlango mpana wa kuchaguliwa au kujirahizishia mfumo wa kuchagua na kukubalika kiurahisi.

Nilikufundisha eneo la ondoa uvivu. Nilikuonyesha kona ya kwanza ya kuhakikisha unaacha kuwa mvivu wa kufikiri. Ebu tuone aina nyingine ya uvivu

ONDOA UVIVU KATIKA ENEO LA UTENDAJI KAZI WAKO

Katika salamu za mwezi huu nataka nikuonyeshe eneo la uvivu wa kufanya kazi au kutumia fulsa jinsi jambo hili llinavyoweza kukusababishia ushindwe kuwa na uchumi mzuri.”Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.”( Mithali 29:15).

Angalia na mistari hii.”Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.”(Mithali 12:24).

Ukiipitia mistari hiyo utaona kuwa mtu mvuvi hawezi kutawala. Fahamu Kiblia mwanaume ni mtawala. Kama mtu mvivu hawezi tawala,  Kwa Maana  nyingine atatawaliwa.

Ukiitazama hiyo mistari kwa kutulia utagundua wazi kuwa uvivu ndiyo chanzo cha watu kukutana na njaa na hata kutawaliwa. Kumbuka mwanaume ni kichwa yaani mtawala, sasa sikia kijana.

Ukiwa mvivu tu umasikini utakutawala, na ni ngumu kwako kupata mke umtakaye nakwambia. Vijana wengi sana hawajui kuwa kipindi chao cha ujanani ndiyo kipindi cha kujituma kufanya kazi kwa bidii. Ili ulitimize ono ulilonalo lolote lile. fahamu utatakiwa uhakikishe unajituma kufanya kazi kwa bidii.

Usiwe mvivu kuchangamkia fulsa halali ziwezazo kukuingizia kipato. Maandiko yanatufundisha kuwa tunatakiwa tufanye kazi. Angalia mistari hii.”Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote.”(1The 4:11-12).

Ukiipitia hiyo mistari utaona kuwa tumeagizwa tufanye kazi ili tusiwe na haja ya kitu chochote. Vijana wengi wakipata kazi ni wavivu kuifanya hiyo kazi. Hata kuwa wabunifu yaani kujiongeza  hawawezi.

Mimi naamini ikiwa leo hii tunataka mishahara mikubwa ni lazima tukubali kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa ili kuikuza hizo kazi ndipo kipato kitakua kikubwa.

Kama hakuna uzalishaji mkubwa fahamu faida haiwezi kubwa,  nirahisi sana kutafuta nyongeza za mishahara wakati uzalishaji ni mdogo. Fikiria kidogo umepewa mtaji ufanye biashara lakini uko mvivu unafikiri utafanikiwa kweli?

Ngoja nikupe mfano huu,  Unamkuta mtu ni fundi iwe ujenzi au fundi magari au fundi kushona nguo,fundi simu au tv na redio nk, lakini muangalie,  mvivu huyoo!!!

Unafikiri utafanikiwa kwenye mfumo wa maisha yako kwasababu unaomba sana? Mungu ukimuomba akuletee wateja atawaleta wengi sasa hapo ndipo wewe unatakiwa ujiongeze kwa kufanya kazi kwa bidii mno ili akuletee wateja wengine. Nimeona kuna watu hawapewi kazi kisa wavivu tu.

Unampelekeaje kazi mtu ambaye anafanya kazi leo kesho anasingizia mgonjwa au kafiwa? Kwasababu mafundi wengi hawakawii kufiwa!!! Eheheee!!!

Wapendwa wengi vijana ni wavivu na wanatumia fulsa hiyo kumsingizia Mungu. Utasikia hoo!!!! kulikua na maombi kanisani, au hooo!!! tuna mkutano kanisani nimeshindwaa kufanya kazi jamani hivi ni kweli? Hapana

Si kweli kabisaaa. Ni uvivu tuu!! Kwanza nikuulize wewe ndiyo muhubiri eti? Utaniambia nimuimbaji, unaimba masaa 48? Kwanini tunasema uongo jamani?

Ebu msomeni Daniel utagundua alikua anaomba kila siku mara tatu, na alikua na kazi nzito mnoo serekalini lakini hakuna sehemu yoyote iliyolalamika kuwa haitumikii vema. Yaani serekalini na kwa Mungu. Leo hii ukikutana na vijana wengi hawawezi kuwa kama Danieli, lazima upande mmoja utalalamika tu.

Nchi nyingi za Kiafrika leo ni watumwa wawazungu kisa ni hiki hiki cha vijana wengi ni wavivu mnooo!!!

Vijana wengi wa Kiafrika hasa tuliookoka ni wavivu sana. Wengi hawapendi kufanya kazi.  Tunatafuta vitu vya mtelemko hatupendi kufanya kazi, wewe nenda angalia leo hii watu wanavyopenda kuishi kimiujiza. Wanapenda kutabiriwa wapewe unabii, ndiyo maana waaguzi siku hizi ni wengi wakiwaagulia watoto wa Mungu. NA HIKI NIKITU CHA HATARI MNOOOO  KINACHO WAMALIZA WATOTO WA MUNGU WENGI MNO.

Pita kwenye maandiko utaona Mungu hakutuumba sisi tuishi kimiujiza!!! Sijakosea, Mungu hakumuumba mtu aishi kwa miujiza!!!

Ukitaka kuwa mtu wa mafanikio shika hili ninalo kuambia. Watoto wa Mungu wengi wanajidanganya kuwa kufanya kazi ni sehemu ya laana. Si kweli. Adamu aliambiwa alime kabla hajafanya dhambi na laana kuikalia aridhi.

Leo hii unapata nafasi ya kusoma lakini uvivu unakujaa na hausomi, visingizio vingi weee!!! Ohoo sielewi!! Ohoo ninaroho yakurithi ya kutokusoma!!! Sasa ndugu kama umejua unahiyo hiyo roho si ndiyo ushindi wako?

Ukijua unatatizo gani unachotakiwa ufanye ni kutafuta kwa bidii maarifa ya kulitatua tatizo. Si kulifanya tatizo kama ndiyo kisingizo chako.

Kusema ukweli Vitu vingine ni uvivu tu. Wenzio wanaenda kusoma wewe unaenda kwenye maombi huoni kama ni uvivu wa kusoma tu? Sikiliza, Maombi yanasehemu yake na kusoma kunasehemu yake. Tusiwe wajinga watoto wa Mungu

Hata huyo Mungu ambaye kila siku unasema unaenda kumtafuta haumuoni kisa uvivu tu. maandiko yanasema.” Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.(Mithali 8:17-21).

Mungu anataka tumtafute kwa bidii kwa lugha nzuri hapendi wavivu anapenda watu wenye bidii kwenye kila kona. Ikiwa kwenye kumtafuta iwe kwa bidii, ikiwa kwenye kusoma iwe kwa bidii ikiwa kwenye biashara iwe kwa bidii ikiwa kwenye kufanya kazi zote iwe kwa bidiii.

Watu wengi leo hii hawataki WAO WENYEWE KUWEKA BIDII YA KUMTAFUTA MUNGU WAO WENYEWE. Utaona walivyo na bidii YA KUKIMBILIA KWENYE KILA KIKUNDI AU MAHALI WASIKIAPO KUNA MAOMBI YA KUOMBEWA . Si yawao kuomba ila kuombewa!!! Inasikitisha sana.

Wakati ule naokoka kulikua hakuna waalimu kama leo hii. Unajua Mungu aliniambia TULIA NINAO UWEZO WA KUKUFUNDISHA. Weka bidii wewe mwenyewe kusoma Biblia na kuomba. Watu wengi wanapenda watafuniwe  kila kitu. Usishangae kusikia mtu akisema, Mtumishi uwe unaweka mistari siyo kutupa  milango na sura na na namba za mistari ili tukasome, tuna mambo mengi.

Ukimtazama mtu mwenyewe anayesema anamambo mengi hata hata nusu ya mambo mengi hajafikia, ni uvivu tu.

Sikiliza kijana, soma kwa bidii ili kwa kupitia elimu yako hiyo ono ulilonalo lije kutimia. Uvivu huwafanya watu wengi wawe washirikina. Hawataki kufanya kazi kwa bidii wanakimbilia kwa waganga ili wapate fedha ya mapepo. Kinachowafanya watu waende huko wengi ni uvivu wao tu, uwe wa kufikiri au wa kutenda kazi.

Najua ninachokisema, Wewe angalia utashangaa vijana wengi leo hii wamejaa makanisani hawana kazi. Kisa wanasubiri waajiliwe au wapewe mitaji, Ndiyo miaka inaenda. Hivyo kazi hakuna mitaji hakuna!!!

Mimi huwa najiuliza sana hivi vijana wengi wanasubiri kazi gani? Angalia mfano huu, Utasikia hapo kanisani kunaujenzi unaendelea huoni vijana wakija kuomba kazi kwa mchungaji wawe wanamsaidia fundi kusogeza simenti na wapate fedha yao na watoe sadaka ili wazidi kubarikiwa. Ila wanasubiri ajira zitoke sawa subiri utaona.

Unaenda kanisani unaona kabisa angetokea mtu apande hata maua hapo angepata fedha tu. Na zaka angeiachia hapo hapo. Ila kwenye kucheza pambio ndiyo utasikia Roho
wa Mungu kaniongoza leo tucheze sana. Roho Mtakatifu hapatani na wavivu wasio na kazi za kufanya ili wapate kipato.

Tafuta kazi hata ya kujishikia tu ili mladi usionekane upoupo tu. huwezi kuwa na mlango mpana wa mafanikio. Siku moja nilijiuliza sana. Leo hii nikiwa naenda maeneo mbalimbali na hema yetu, tunapolifunga au kulifungua utaona watu tunao wapa kazi hizo ni watu wasiookoka kabisaa. Ndiyo wanaokuja na kuchangamkia tenda wanashusha bomba wanafunga hema wanapata fedha.

Lakini vijana waliookoka ambao hawana ajira hata fedha ya sadaka tu, ndiyo wanakuja kama wafalme wamefaa tai na wanaketi vitini kama matajiri hivi. Huku hata sadaka tu hapo hawana. Na unaweza kuta hili si linatokea kwetu tu.  Naamini hata kwa watumishi wengine ni hivyo hivyo.

Wapendwa hawataki kufanya kazi kisa wanajiona ni wafalme. Kweli wewe ni mfalme. Lakini ufalme wa Mungu unakutaka wewe mfalme ufanye kazi tena kwa bidii.  Wapendwa wengi wanataka wawe madereva  wakati kazi ya utingo hawaitaki. Uliza basi uone. Madereva wengi walianzia utingo!!!

Wewe unataka uwe nabii mkubwa au uwe mtumishi mkubwaa sikiliza Joshua alimbebea mizigo Musa ndiyo siku moja akaachiwa kuwa KIONGOZI WA WA WANA WA ISRAELI.

Wapendwa wengi wako hivi. Wanaupigia hesabu mshahara wa mkulugenzi mkuu wa kampuni wakati ndiyo kwanza wanaaanza kazi. Utasikia ohooo mshahara wa boss ni mkubwa tupewe sawasawa, eheheee!!! Sikia Tunaanza huku chini wapendwa ndiyo Mungu anaenda kutuketisha na wakuuu!!!!

Fanya kazi kwa bidiii. Penda kufanya kazi huo ndiyo UKRISTO. Naamini umenielewa

Mungu akujarie kuyatendea kazi haya.AMANI YA MUNGU IWE NANYI.

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila

Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii  uunaweza kupata masomo yetu mengine kwenye maeneo yafuatayo.

1.Website yetu ya www.makatwila.org

2. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
4.Dvds au Cd

5.Vitabu

6.Kwa njia ya Redio mbalimbali Rungwe fm102.5 Kila siku Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku
na  Baraka Fm107.5 kila siku ya jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku na  Bomba fm 104.1 kila siku ya ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku
Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222