Tunamshukuru sana Mungu ambaye ametupa huu mwaka Mpya. Naamini utakua mwaka mzuri sana kwa kila mtoto wa Mungu ambaye atajipanga vizuri na Mungu hasa kwenye eneo la kumtumikia Mungu, iwe kwa kuhubiri, kufundisha, kuchunga na kwa kutoa mali zao ili watenda kazi waende.

Kwa kweli mwezi uliopita tumekua na semina nyingi mno. Tokea mwanzoni mpaka tarehe moja ya mwezi wa kwanza tumekua na semina. Pia tulikua na kambi zuri sana mwaka huu. Nikualike mpendwa hasa vijana katika kambi la mwaka huu wa 2018. Tunatarajia tarehe 29-31-12-2018 Tutakua na hiyo kambi. Tuombeeni ili tuiiandae vema.

Ebu pokea salamu zetu za mwezi huu wa Kwanza. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE KABLA YA KUOA NA KUOLEWA.

Tumezileta salamu hizi kwa urefu kidogo. Ni kweli niliona moyoni mwangu nisikatishe ujumbe huu. Nikupe angalau kwa upana kidogo kwasababu ni muhimu mno.

Katika salamu zilizopita nilikuonyesha eneo la kijana jifunze kutengeneza mazingira mazuri ambayo yatakufungulia wewe mlango mpana wa kuchaguliwa. Fahamu unapopata nafasi ya kuwa kijana utakae kuoa nilazima ujitengenezee wigo mpana wa wewe kuchagua. Ili uchague lazima ujue kuwa nawewe utachaguliwa.

Kijana ondoa wazo la kufikiri kuwa utajichagulia tu binti wa kuoa kisa eti Mungu kakuonyesha. Fahamu kuna ridhaa ya mchaguliwa. Akikataa usifikiri Mungu atamlazimisha aje kwako. Watu wengi hujitahidi sana kuomba wapate kukubaliwa na hao mabinti waliowalenga kabisa kuwaoa.

Sikiliza maombi yanasehemu yake na kuna muonekano furani kwako ambao unatakiwa uwe nao ili ujirahizishie au umrahizishie huyo binti kusema ndiyo kwako. Jambo mojawapo muhimu ni hilo la kuwa na uchumi mzuri.

Ili leo hii uwe na uchumi mzuri yapo mambo mengi mnoo unayotakiwa uyafanye. Sitayaachilia yoote hapa. Fuatilia masomo yetu mbalimbali utakutana na masomo ya namna hiyo au soma vitabu vya watumishi wa Mungu mbalimbali walivyoviandika kuhusu habari za kufanikiwa.

Jambo mojawapo muhimu ninalotaka kukuonyesha hapa ni hili.

KIJANA ONDOA UVIVU KATIKA MAISHA YAKO

“Biblia inasema hivi.”Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang’anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”(Mithali 6:9-11)

Ukiipitia hiyo mistari unaona wazi kuwa chanzo cha umasikini kinaweza kuwa tabia hii ya uvivu. Neno mhitaji lina maana maskini. Ili kijana ufanikiwe katika maisha yako lazima uhakikishe unaukimbia uvivu.

Uvivu unaweza kuuangalia kwenye maeneo mengi tu. Unaweza kuuangalia kwenye eneo la uvivu wa kutenda kazi, pia unaweza kuutazama uvivu kwenye eneo la kufikili au kupanga na kusimamia kile ulichopanga.

Maandiko yanatufundisha kuwa vijana wamepewa nafasi ya kuwa na maono. Angalia mistari hii. “Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.”(Mdo 2:17).

Katika siku hizi tunazoishi baada ya Roho Mtakatifu kuja, kila kijana amepewa nafasi ya kuwa na maono. Maono nini hasa? Maono ni picha harisi ikaayo ndani ya mawazo ya mtu ya kile alichokikusudia kukimiliki.

Hapa sizungumzii maono yale ambayo Mungu anaweza kukuonyesha iwe waziwazi au usingizini. Nazungumzia mfumo mzima wa mpango wa maisha yako. Mungu amempa nafasi kijana kwa kupitia mawazo yake kuwa na picha ya maisha yake yoote. Picha hiyo ndiyo inakua ramani ya maisha yake yoote.

Sikiliza Mungu akija kwako kijana fahamu atakachokitafuta kwako ni kuiona picha hiyo uliyoiandaa wewe mwenyewe kwanza huko ndani ya moyo wako.

Maandiko yanasema hivi.”Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.”(1Nya 28:9-10).

Mfalme Daudi alimfundisha mwanaye juu ya jambo hilo. Daudi alijua sana kuwa Mungu anatabia ya kutafuta-tafuta mawazo ya mtu. Unajua anatafuta ili aone nini? Ili aone fikra za huyo mtu zimebeba picha gani katika mfumo mzima wa maisha yake

Sikiliza huko ndani ya moyo wako kijana umepewa fursa ya kuona mambo yako ya mbeleni. Muonaji ni wewe. Kama huna ono lolote huko ndani maana yake utaishi maisha ya kukopy au  maisha yasiyo ya kwako. Pili utamnyima Mungu fulsa ya kuliumba hilo ono lako.

Maandiko yanasema hivi.”Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA.Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huzipima roho za watu.Mkabidhi BWANA kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.”(Mithali 16:1-3).

Mungu anatabia ya kudhibitisha au kuumba mawazo yako au kile unachokiona huko moyoni mwako. Sasa ukiwa  mvivu  wa kufikiri tu yaani kutokuwa na mipango ya maisha yako usitegemee kuishi kimafanikio.

Kama leo hii utakuwa ni mtu ambaye unapicha hiyo au ramani hiyo nakuhakikishia kila utakalolipata au kulihitaji ni kuja kuiumba au kuitimiza picha hiyo uliyo nayo moyoni mwako. Hata ukihitaji mke. Huwezi kumhitaji kila mwanamke ambaye hana sifa ya kulitimiza ono lako.

Unapoomba Mungu akupe mke usitafute mke wa kuzaa naye tu watoto au unayempenda tuuu!!! Sikia unampenda ili iweje? Sikia tafuta mke  au muombe Mungu akupe mke atakaye kusaidia katika kuyatimiza maono yako. Si kuzaa tu. Unaweza zaa watoto ambao hata huna ramani au maono kwa ajili yao.

Ukiwa kijana lazima uwe na maono au malengo hata ya hao watoto wako. Siyo kuzaa tu. Wewe soma Biblia utagundua Kwanini Mungu alimcheleweshea Ibrahimu kumpa mtoto. Mungu alitaka kuona kitu ndani ya Ibrahimu ambacho Mungu alikikusudia.

Mungu alikua na picha au ono dhidi ya uzao wa Ibrahimu unatakiwa uweje ukae wapi na nini uzao upitishe. Ibrahimu hakuwa na picha kamili ndani yake. Ndiyo maana alikubaliana hata na ujinga wa mkewe wakaanza kuzaa mtoto ambaye hana hata lengo naye. Tunaita mtoto ilimladi mtoto.

Watu wengi sana hapa ndipo tumebanwa. Wewe muulize mtu wewe kama mzazi wa mtoto huyu unampango gani naye? Au mtoto huyo unapicha gani moyoni mwako  au unaono gani dhidi ya mtoto huyu?

Liwe ono kutoka kwa Mungu au kutoka kwako mwenyewe, utaona wengi hawana kabisaa. Utasikia aisee Mungu ndiye anayejua. Muulize ulipokua unamleta duniani Mungu ulimuuliza kuwa unajua leo namleta huyu duniani? Kama Mungu hajui hata kuhusu mpango wako wa kumpata huyo mtoto unasemaje Mungu anajua? Nimeongea na wewe kwa elimu kubwa kidogo.

Nakwambia kuna masomo kama tukiyapata tutatamani tuwaludishe watoto wetu viunoni mwetu au tumboni mwa mama zao. Kisa tuliwazaa bila kuwa na picha  au maono yoyote mioyoni mwetu.

Sisi tunafurahia tu kuwa aisee tumepata watoto. Wewe soma Biblia utaona Mungu kawapa watu furani watoto na watoto hao wazazi wao wanapewa ramani yooote ya nini watoto hao wafanye.

Wazazi wana hiyo huwaandaa hao watoto wao ili wapite kwenye ono au ramani hiyo.  Mfano Mungu alimpa mfalme Daudi picha ya mtoto wake aitwaye Sulemani. Alimuelekeza wazi wazi kusudio Alilolikusudia juu ya huyo mtoto nini na ndiyo maana Daudi alimweleza mtoto wake kuwa Mungu amekuchagua wewe umjengee nyumba.

Fikiria Daudi asingelijua jambo hilo si angempa mtoto wake mkubwa aliyekua anaitwa Daniel. Mtoto mkubwa wa mfalme Daudi alikua akiitwa Amnoni alifariki. Angalia mistari hii uone”Basi kulikuwa na vita siku nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi, lakini nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika.Naye Daudi akazaliwa wana huko Hebroni; mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, wa Ahinoamu wa Yezreeli; na wa pili wake Danieli, wa Abigaili mkewe Nabali wa Karmeli; na wa tatu Absalomu, mwana wa Maaka binti Talmai, mfalme wa Geshuri na wa nne Adoniya, mwana wa Hagithi; na wa tano Shefatia, mwana wa Abitali;na wa sita Ithreamu, wa Egla, mkewe Daudi. Hawa walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni.”(2Samweli 3:1-5)

Sulemani alikua hajazaliwa hapo, Adoniya alitaka kuchukua nafasi ya baba yake lakini baba yake alisema wazi kuwa ono alilonalo moyoni mwake kwa ajili ya watoto wake ni hili Sulemani ndiye mrithi. Na ndiye atakaye ijenga nyumba ya Mungu.

Mfalme Daudi alikua na picha hiyo moyoni imuhusuyo mtoto wake. Natamani hata wewe kijana ili ufanikiwe ondoa uvivu wa kufikiri. Pata picha ya mfumo wa maisha yako. Ukiwa binti mwenye maono ya maisha yako nakuhakikishia utajizuia na vitu vingi mno.

Maandiko yanasema”Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”(Mithali 29:18).

Anza leo kuwa na maono ya maisha yako. Maandalizi ya moyo niyakwako. Usiishi kama kunguru panga moyoni mwako unataka kuwa nani. Kaa kwenye maono hayo. Utaona mafanikio tu huko mbeleni.

Picha hiyo ndiyo inakua kama dira ya maisha yako. Utajua namna ya kuitumia kila fulsa njema ili kuiumba hiyo picha iliyomo moyoni mwako.

Ondoa uvivu wa kufikiri. Naamini umenielewa tuonane tena katika kona hii

Mungu akubariki sana

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila

Tunapoachana nataka nikupe taarifa hii  uunaweza kupata masomo yetu mengine kwenye maeneo yafuatayo.

1. Website yetu ya www.makatwila.org

  1. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

3.Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga

  1. Dvds au Cd
  2. Vitabu
  3. Kwa njia ya Redio mbalimbali Rungwe fm102.5 Kila siku Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku
    na  Baraka Fm107.5 kila siku ya jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku na  Bomba fm 104.1 kila siku ya ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924-0756715222