Salamu – Oktoba, 2011

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninakukaribisha tena katika sehemu hii ya salamu za mwezi. Hizi ni salamu zetu za mwezi wa kumi karibu uzipokee.

Kumbuka tuna salamu zenye kichwa.

VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

Baada ya kujifunza eneo la maana ya kwanza ya neno kusikia na namna unavyoweza kusikia.

Hebu tuanze kujifunza maana ya pili ya neno kusikia au kutokusikia ni nini.

2. MAANA YA PILI YA NENO KUSIKIA AU KUTOKUSIKIA NI KULITENDEA KAZI LILE ULISIKIALO AU KUTO KULITENDEA KAZI LILE ULILOLISIKIA

Sikiliza, unaposikia neno kusikia linaweza kuwa na maana hii ya kulitendea kazi lile lililosikika masikioni mwako. Pia unaposikia neno kutokusiki linaweza kuwa na maana hii kutokulitendea kazi lile lililosikika masikioni mwako.

Unaposikia watu wakisema huyu mtu hasikii kabisa. Inawezekana ni kwa maana hii ya mtu kutokuwa mtii wa lile aliloagizwa kulifanya. Masikio yake yalisikia kabisaa lakini akafanya maamuzi ya kutoku litendea kazi lile aliloambiwa na masikio yake yalilisikia kabisa. Mtu wa sifa hiyo anaitwa asiye sikia.

Ukisoma Biblia utaona Mungu anaposema nasi kwa kupitia mifumo ile niliyokuonyesha na usilifanyie kazi neno lile ulilolisikia, fahamu atakuweka kwenye kundi la watu waitwao wasiosikia.

Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia “Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu…” (1Samweli 15:22).

Ukiisoma mistari hiyo unaona Mungu aliambiwa Sauli jambo la kufanya, Sauli hakulifanya, Mungu akamwona ni mtu asiye sikia. Ndiyo maana akamwambia hivi, angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.

LEO HATULI MEMA YA NCHI KISA NI HIKI TU… KUTII KILE TULICHOSIKIA.

Mungu yupo tayari kutubariki mno sisi watoto wake. Lakini kwa sababu hatulitii na kulitendea kazi lile tulilolisikia Mungu anatuona sisi ni watoto tusiosikia. Yaani kama watu wasio na masikio.

Angalia mistari hii asemavyo. “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;” (Isaya 1:19). Hapo kuna maneno kukubali na kutii, Unaweza sikia kabisa na ukakubaliana nalo hilo neno ulilolisikia kuwa limetoka kwa Mungu. Lakini usiwe mtii wa hilo neno, kwa lugha nzuri usiliweke kwenye matendo. Matokeo yake unajikuta unazipoteza baraka au mema ya nchi uliyoahidiwa kupewa na Mungu.

BWANA YESU KRISTO ANASEMA KWA UKALI MNO JUU YA JAMBO HILI.

Unaposoma maandiko matakatifu unaona Bwana wetu Yesu Kristo alilizungumzia jambo hili. Alisema hivi.

“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” (Mathayo 7:24-27)

Kitendo cha kusikia neno la Mungu na kutokulifanyia kazi kinakufanya uonekane kwa Mungu kama mtu asiye na akili..

Hebu badilika leo fanyia kazi neno lile ulilolisikia kutoka kwa Mungu. Utaitwa asikiaye na mwenye akili. Kinyume cha hapo utaitwa asiyesikia na asiye na akili.

SABABU ZINAZOWEZA KUPELEKEA MTU ASILITENDEE KAZI LILE ASIKIALO

Unaweza kuwa na maswali moyoni kwanini watu wengi wanasikia lakini hawalitendeei kazi lile walilolisikia.?

Zipo sababu nyingi tu. Hebu tungalie sababu hizo.

A: SABABU YA KWANZA HOFU

KUWAOGOPA WATU

Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia. “Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.” (1Samweli 15:24)

Ukiisoma mistari hiyo unaona wazi kuwa kilichomfanya Sauli asimtii Mungu ni kitendo hiki cha yeye kuwaogopa watu.

Watu wengi sana Mungu anawaambia mambo ya kufanya na wanajua kile kiwapasacho kufanya lakini hawaitii sauti yake. Kisa wanaogopa watu.

Mtu anaweza kuwa mke, kiongozi, mzazi, bosi kazini n.k. Mungu anaweza kukutuma uonye, useme neno, ufanye jambo, au usiende au nenda lakini kwa sababu ya kuwaogopa hao watu utajikuta haukifanyii kazi kile Mungu kakuambia.

Biblia inasema hivi “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye BWANA atakuwa salama.” (Mithali 29:25). Kitendo cha kuwa na hofu kwa watu kuliko kuwa na hofu kwa Mungu kuna weza kukuletea mtengo wa kutokulitenda lile ambalo Mungu kakuagiza ufanye.

IBRAHIMU ALISIKILIZA SAUTI YA MUNGU LAKINI HAKUIWEKA KWENYE MATENDO

 • ALIMSIKILIZA SARA

Unaposoma maandiko unaona Ibrahimu alimwogopa Sara, akajikuta anafanya ya Sara badala ya kufanya lile Mungu kamuagiza angalia mistari hii. “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai.Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.” (Mwanzo 16:1-4)

Unaweza kujiuliza maswali kwa nini alifanya hivyo? Naamini alimuogopa Sara, angalia Sara alivyokua kitabia.

“Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe.Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe.Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.” (Mwanzo 18:3-6)

Angalia na mistari hii uone Sara alivyokua “Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.” (Mwanzo 21:8-12)

Sara alikua mkatili na inaonekana alikua jeuli, Ibrahimu hakutaka kugombana naye , alipomletea hoja ya kulala na binti wa kazi. Akaamua kumsikiliza badara ya kumsikiliza Mungu kisa alimwogopa

Angalia mfano mwingine ni huu wa Adamu,

ADAMU ALILISIKILIZA NENO LA MUNGU LAKINI HAKULIWEKA KWENYE MATENDO KISA ALIMUOGOPA MKEWE

Ukiipitia mistari hii utaona kuwa Adamu nayeye alijikuta akila tunda kisa alimwogopa mkewe badara ya kumwogopa Mungu. Hebu isome mistari hii “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;“ (Mwanzo 3:17)

ADAMU, Kwanini alikula tunda…? INAWEZEKANA ALIMUOGOPA MKEWE

Angalia maelezo ya Adamu. “Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” (Mwanzo 3:11-16)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona jambo lingine la kujifunza la maelezo ya Adamu akisema si huyu mwanamke uliyenipa? Inaonekana huyo mwanamke alikua mkorofi na Adamu hakutaka kugombana naye yaani alimwogopa, akaitii sauti yake badala ya kumtii Mungu.

Adamu akala lile tunda, matokea akajikuta akiingia kwenye matatizo makubwa sana. Adamu alipoteza nafasi ya kuishi bustanini Edeni, akajikuta akitumikia adhabu ya kuwa na maisha magumu mno, akajikuta akianza kutumikia kifo, akajikuta akiwa uchi n.k. kisa hakusikia, yaani hakutii kile Mungu kamwambia akifanye akakifanya kile Mungu kamkataza kufanya.

Hebu jichunguze kwako ikoje. Je! Unaogopa watu? Ondoa hofu ya kumwogopa mwanadamu atakaye kufa kesho, mwogope Mungu aishiye milele ili usiingie matatizoni.

Naamini umenielewa Mungu akubariki mnoo.

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.