Salamu – Disemba, 2022

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nina amini umekua na mwezi mzuri na ambao Mungu amekupigania mno ili uone mwezi huu wa mwisho wa mwaka huu wa 2021.

Mwaka huu umekua na mambo mengi mno, naamini mpaka tumekua hai na wazima ni Mungu tu katupigania.

Nimekuletea salamu za mwezi, na hizi ni salamu za mwisho kwa mwaka huu. Kwahiyo zitakua ndefu kidogo ili tumalizie vizuri.

Kumbuka tunasalamu zenye kichwa. VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

Hebu tuangalie jambo la tatu linaloweza kuwa ni kizuizi cha kusikia kwa mtu. Nalo hili…

3: SHETANI ANAWEZA KUKUTENGENEZEA MFUMO WA KUTOKUSIKIA.

Unaposoma Biblia unaona pia kuwa shetani anaweza kuwa chanzo cha watu kutokusikia na kulitii neno la Mungu. Biblia inatufundisha kuwa moja ya kazi ya wachawi ni kuzuia watu wasiwe na imani kwa Mungu. Kumbuka imani huja kwa kusiki neno la Mungu. Sasa adui ana tabia ya kuwatumia wachawi kuzuia watu wasisikie na kukosa imani.

Angalia mistari hii wachawi uone hiki ninachokuambia. “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?” (Mdo 13:6-10).

Ukiisoma mistari hiyo unaona wazi kuwa mchawi huyo alichokua anakifanya ni kumzuilia huyo ndugu asisikie au kulitii neno lile alilokua akilisikia kutoka kwa kina mtume Paulo. Mtume Paulo aliligundua jambo hilo akaamua kulishughulikia ndipo mtu huyo akalisikia neno la Mungu.

MFANO WA YUDA KUWAZUIA WATU WASIMSIKILIZE BWANA YESU KRISTO

Unaposoma Biblia unaona pia shetani aliwazuia watu wasimsikilize Bwana Yesu Kristo.

Angalia mistari hii “Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.” (Yohana 6:59-71)

Kwa mujibu wa mistari hiyo tunajifunza kitu kikubwa sana hapo, wanafunzi hao waliacha kuambatana na Bwana Yesu Kristo kisa ni shetani aliwazuia wasilisikilize na kulitii neno alilowaambia Bwana Yesu Kristo. Angalia hapo. Bwana Yesu Kristo aligundua kuwa shetani ndiye aliye waondoa na shetani alikua ndani ya Yuda.

JIFUNZE KUTUBU NA PIA KUMPINGA

Kwa hiyo unatakiwa ujifunze kutubia kosa hili kwanza na ujifunze kumpinga shetani ili asikuzuilie wewe kumsikiliza Bwana Yesu Kristo. Neno la Mungu linasema hivi “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. (Yakobo 4:7-8)

Kwenye maombi yako jifunze kumpinga mara kwa mara ili asikuzuilie kusikia kwako na kumtii Mungu. Shetani huwatengenezea watu kutokuwa watii wa neno la Mungu. Na huwatumia wachawi katika kulifanya kazi hii ya kuwazuilia watu kusikia na kulitii neno la Mungu.

ANAWEZA KUTUMIA PEPO LA HOFU, FAHAMU HOFU NI ROHO.

Adui anaweza kukutengenezea wewe roho ya hofu ili tu usiwe mtendaji na msikiaji wa neno la Mungu. Biblia inatufundisha kuwa hofu ni roho! “Tazama, nitatia roho ya hofu ndani yake, naye atasikia kivumi, na kuirudia nchi yake mwenyewe; nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.” (Falme 19:7)

Sasa sikia, kuna watu wana hofu mno katika habari ya kusikia kwao, wanaogopa kukosea, na wengine hofu hiyo imejengwa na pepo la hofu tu. Likikemewa likimtoka huyo mtu anaanza kuwa msikiaji na mtendaji wa neno hilo bila kuwa na mashaka.

4: JAMBO LA NNE LINALOWEZA KUWA KIZUIZI CHA KUSIKIA KWAMTU NI MTU MWENYEWE UNAWEZA KUJITENGENEZEA WEWE MFUMO WA KUTOKUSIKIA.

Unaposoma Biblia unaona kuna watu wao wenyewe ndiyo wanaojitengenezea mfumo wa kutokusikia. Angalia mistari hii uone hiki ninacho kuambia. “Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao.” (2Wafalme17:14)

Angalia na hii mingine “Kwa hiyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.” (2Nya 25:15-16)

Biblia inatufundisha kuwa mwanadamu yeye mwenyewe anaweza kuwa chanzo cha kutokusikiliza kile Mungu anamwambia, hapa unaiona haswaa dhambi ya kiburi.

5. JAMBO LA TANO NI MAFANIKIO AU CHEO.

Sikiliza jambo lingine linaloweza kumsababishia mtu asiwe mtendea kazi au msikilizaji wa neno la Mungu ni hili la kufanikiwa kiuchumi au kuwa na cheo. Biblia inasema hivi, “Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokuitii sauti yangu.Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote.” (Yeremia 22:21-22)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona hatari mojawapo ya mtu kufanikiwa ni hii ya kutokusikia na kutokulitii neno la Mungu. Wewe wafuatilie watu wengi walio na vyeo.au utajiri au kusoma sana sana nk..utagundua wengi hupoteza usikivu wao kwa Mungu.

Wanajaa dharau na kiburi, wanachagua watu wa kuwasikiliza, na matokeo yake ni kuumia tu. Biblia inasema hivi. “Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.” (Mithali 1:32).

TABIA ZA MTU HUFUNGWA KTK HABARI ZA KUSIKIA KWAKE

UKIONA MTU UNAMUONYA NA LAKINI ANATENDA MAKOSA WEWE SHUGHULIKA NA MASIKIO YAKE

Tabia zetu zote ziwe njema au mbaya pia zinavyanzo. Moja ya chanzo ni kusikia, sasa sikia, tabia njema ya mtu huja kwa kusikia kwake na tabia mbaya pia huja kwa namna ya kusikia kwa huyo mtu. Biblia inasema hivi “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” (1 Wakorintho 15:33)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona mtu anavyosikia ndivyo anavyokuwa na tabia fulani. Sasa ukiona mtu ana tabia mbaya na mmemwambia na hawasikii, anza kumwombea hayo masikio ili yaziburiwe na aanze kusikia neno jema mtu huyo atakua na tabia njema tu.

Angalia na mistari hii uone hiki ninachokuambia “Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;” (Isaya 48:8)

Masikio yakiziba mtu lazima atakua na tabia mbaya tu, mpaka masikio yake yazibuliwe ndipo hugeuka na kuanza kuwa mtenda mema..

Angalia na mistari hii mingine “Akisema, Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua;Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya. (Mdo 28:26-27)

Kitendo cha madikio yao kuziba na mioyo yao ikawamixito kusikia kilipelekea hao watu kuwa na tabia mbaya. Sasa sikia, anza kujiombea wewe mwenyewe na hao watu wengine Mungu ayazibue masikio yao. Masikio yakizibuka tu fahamu wataanza kusikia na kuaziacha tabia zao mbaya.

JIHADHARI NA KILA ULISIKIALO.

Biblia inatupa onyo kuwa tunatakiwa tuchukue taadhari mno katika kusikia kwetu. Maandiko yanasema hivi. “Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.” (Marko 4:23-24).

Jifunze kukichunguza kile ukisikiacho kabla haujaanza kukifanyia kazi, Angalia kila ushauri unaopewa, kila elimu unayokutana nayo je! Ina Mungu ndani yake? Usipokua makini katika habari za kusikia kwako fahamu utajikuta umebanwa kwenye kila ubaya na kuwa kinyume na Mungu, ni ngumu hata kuendelea kwako.

Angalia mfano huu uone? “Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao.Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu.” (1Nya21:1-4)

Mfalme Daudi alisikia wazo, la kuwa hesabu hao wana wa Israeli, hakuliangalia wazo hilo chanzo chake ni wapi, wazo lile chanzo chake alikua ni shetani. Kama angetulia na kulichunguza jambo hilo hata kwa maombi tu, naamini Mungu angemwambia asiwahesabu.

Adui anaweza kusema, na ukasikia kabisaa, kama masikio yako ni wazi, cha kufanya ni rahisi tu, ni kuliangalia lile unalolisikia je linafuata na maagizo ya Mungu? Lina amani ndani yake nk. Mara nyingi husema kinyume na Mungu, husema ili kukuondolea imani kwa Mungu, na husema ili wewe umsujudie, yaani utafute msaada na ushauri kwake.

Angalia mfano huu. “Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu.Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake? Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi;Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo! Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; Waangamia milele wala hapana atiaye moyoni.Je! Kamba ya hema yao haikung’olewa ndani yao? Wafa, kisha hali hawana akili.” (Ayubu 4:12-21)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona wazi kuwa alikua anasema maneno yaliyo nje ya ukweli. Mungu anasema wazi kuwa anawaheshimu watumishi wake. Mungu anawaheshimu malaika zake. Mungu anawaheshimu wanadamu yaani nyumba za udongo kiasi cha kuwafia msalabani.

Jiadhari sana usiyasikilize mapepo, watu wengi huyaamini mapepo na kuyasikiliza yanawapa ushauri na taarifa, pepo ni muongo, hasemi ukweli, usimsikilize, nirahisi kusema mbona yalimuomba Bwana Yesu Kristo na aliyapa ombi lao?

Sikiliza, wewe siyo Bwana Yesu Kristo, wewe ni mtumishi wa Bwana Yesu Kristo unatakiwa umsikilize yeye yaani Roho Mtakatifu.

Mfalme Sauli alitafuta habari kwa mapepo na yalimpa, Mungu akakasirika akaamua kumuua Sauli. Biblia inasema hivi “Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa BWANA, kwa sababu ya neno la BWANA, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake,asiulize kwa BWANA; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.”(1Nya 10:13-14)

Ukisoma mistari hiyo utaona wazi kuwa kifo cha Sauli chanzo chake ni hiki cha kutoliangalia lile alisikialo tu, alisikiliza mapepo yakimwambia atakufa na kweli alikufa.

NAMNA UNAVYOWEZA KUSIKIA.

 1. KATIKA WAZO LA NDANI.

Mungu anaweza kukuletea sauti yake kwa kutumia wazo lake kwako, mfano Biblia husema hivi neno la Mungu likamjia…… “Kisha neno la BWANA likanijia, kusema” (Ezekiel 13).

Mungu analo wazo juu yako na wazo hilo hukushirikisha kwa kukuletea wazo hilo mawazoni kwako angalia mfano; “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yeremia 29:11)

Fahamu hata wewe unayomawazo ya kwako na adui anayomawazo ya kwake pia kuna mawazo ya watu…sasa utajuaje wazo hili je ni la Bwana? Angalia amani, furaha na namna ulivyoliombea je limeendelea kukujia au?

WAZO LINAWEZA KUJA KWA NJIA ZIFUATAZO

 • Katika ndoto… au maono NDOTO NI SEHEMU YA WAZO, INATEGEMEA WAZO HILO LIMETOKEA KONA IPI

Si unajua kazi zetu nyingi za mchana na maneno yetu mengi yanaweza kuzaa ndoto?

“Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache.Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.” (Habakuki 5:2-3)

Si kila ndoto zimekuja kwa shughuli zako au kwa kazi zako za mchana, ndoto zingine hutoka kwa Mungu ni mlango wa taarifa kutoka ulimwengu wa roho.

Biblia inasema Mungu husema nasi kwa kutumia ndoto na maono “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;“ (Ayubu 33:14-17)

Mungu husema nasi sana kwa kutumia hata hizo ndoto na maono.

Mungu alimwambia Habakuki hivi; “Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.” (Habakuki 2:1-3)

Mungu alisema na Yusufu kupitia ndoto “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.14 Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;” (Mathayo 2:13)

(B) WAZO LINAWEZA KUJA KWA KUPITIA MFUMO WA AKILI.

Mungu huleta wazo moyoni kwenye eneo la akili, hapo ndani patatokea yafuatayo, linakuja wazo, kutatokea kurifikiri hilo wazo, kutatokea kulitafakari hilo wazo, ndipo kutatokea kujua au kulielewa na hata kulifahamu hilo wazo.

USIOGOPE KUPOKEA HILO WAZO LIPIME HILO WAZO NI LA NANI

Biblia inasema zijaribuni hizo roho. “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.“ (1Yohana 4:1-3).

Unaposikia neno roho..Bibliainatufundisha kuwa maneno ndiyo roho. “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”(Yoha 6:63)

Unapoambiwa pima roho maana yake pima neno..roho hupimwa kwa roho..yaani roho hupimwa kwa neno… neno lolote lile ambalo unalisikia lazima lisiende kinyume na Neno la Mungu lililo ndani ya Biblia.

Mungu hawezi kukuambia neno kwa kupitia wazo au ndoto au sauti au amani na furaha lililo kinyume na neno lake.. biblia ndiyo haswaa dira yetu..kwa hiyo ili uwe msikivu mzuri jifunze kusoma Biblia mara kwa mara

2. NAMNA YA PILI NI KUSIKIA SAUTI YAKE KUTOKA KWA WATUMISHI

Mungu anaweza kusema kwa kupitia Watumishi wake, wawe manabii, waalimu, mitume, wachunjaji na Wainjilisti.

Biblia inasema hivi. “Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu.Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao.” (2 Wafalme 17:13-14)

Biblia inasema wazi kuwa tuwasikilize watumishi wa Mungu angalia mistari hii “Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.” (2Nya 20:20)

Pia, jiwekee utaratibu wa kuyachunguza hayo maneno aliyoyasema huyo mtumishi, Je! Ni ya kutoka kwa Mungu? Mpime kwenye neno la Mungu lililoandikwa yaani Biblia.

3: UNAWEZA KUISIKIA SAUTI YAKE KWA KUSOMA BIBLIA

Sikia unaposoma Biblia Usisome tuuu kama hadithi, unaposoma Biblia usiisome tu, soma kwa malengo.

Angalia uhitaji wako moyoni unataka kujifunza nini? Tafuta daftari na kalamu, andika kila mstari unaozungumzia hicho unachokihitaji ujifunze, nenda kwenye Biblia angalia vile vifungu vya pembeni vinavyokuongoza kuangalia maneno yanayofanana.

Andika, tafakari, utaisikia sauti ya Mungu ikikupa maelekezo, au mafundisho katika hilo unalolitaka ulifahamu.

4: NJIA YA NNE NI KWA SAUTI

Mungu anaishi, anayo sauti mpaka hii leo, alisema (Biblia) anasema na atasema kwa sauti kabisa.

Angalia mfano huu “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. ”(MDO 9:1-7)

Ukiipitia mistari hiyo utaona Sauli na hao wenzie waliisikia sauti kabisaa ya Bwana Yesu Kristo.

Sikia, kama alisema kwa sauti siku ile fahamu hata leo anasema, tatizo ni masikio yetu na hatuna imani ya kumsikia akisema, amini anasema, na anaweza kusema kabisa!

JIFUNZE KUUOMBEA MOYO WAKO KWANI KUNA MAHUSIANO KATI YA MOYO WAKO NA KUSIKIA KWAKO.

Angalia mistari hii “BWANA akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyomwambia Musa.” (Kutoka 9:12)

Huko ndani ya moyo kuna akili, hisia na utashi. Sasa anza pia kuomba Mungu aushughulikie moyo wako ili uanze au uzidi kumsikia katika mifumo yoote anayoweza kuitumia kuzungumza na mwanadamu. Maombi ya mfumo huo ni ya mara kwa mara, usisite kufunga na kuomba ili Mungu azibue masikio yako.

Naamini umenielewa Mungu akutunze na kukufungua masikio yako katika jina la Bwana Yesu Kristo nimekuombea sema Amen!

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.