Salamu – Januari, 2022

WEKA BIDII YA KUUSHUGHULIKIA MOYO AU NAFSI YAKO

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninamshukuru Mungu mno ambaye ametupa kuuona mwaka huu mpya, ni neema.

Hizi ni salamu zetu za mwezi huu wa kwanza, na tutaenda nazo kwa kila mwezi kwa salamu mfululizo mpaka pale tutakapo zimaliza. Hebu zipokee na Roho Mtakatifu akufundishe vema; karibu.

Sikia, watu wengi ni wagonjwa, bahati mbaya hawajui kuwa ni wagonjwa, wanajiona wana afya nzuri kumbe ni wagonjwa… na wengine wanajijua kuwa ni wagonjwa lakini hawatafuti tiba. Na eneo hilo ambalo watu wengi ni wagonjwa ni nafsini au moyoni. Sikia, ninaposema moyo siuzungumzii moyo huu wa damu na nyama… nazungumzia nafsi. Unaposoma Biblia unaona nafsi ikizungumziwa kama moyo na moyo kama nafsi.

Pia unapoisoma Biblia unaona ukamilifu wako katika uumbwaji wako umefungwa katika vitu vitatu. Navyo ni roho,nafsi,na mwili au mavumbi. Angalia mistari hii. “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.” (Ayubu 32:8).

Ukiipitia mistari hiyo unaona kuna maeneo matatu yametajwa katika kuumbwa kwako. nayo mwili hapo umeitwa mwanadamu, na roho, na pumzi hai ya Mungu yaana nafsi au moyo. Biblia inasema Mungu aliumba mtu kwa mfano wake… neno mtu lina maanisha roho, kwa sababu Mungu ni Roho. “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Yohana 4:24).

Kwa maana nzuri ni kuwa roho ilipewa nyumba yake iitwayo mavumbi au mwili na ikapewa kitu cha tatu kiitwacho pumzi hai ya Mungu yaani nafsi angalia mistari hii. “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” (Mwanzo 2:7).

Ukiisoma Biblia unaona kuna utofauti wa roho na moyo. Watu wengi wakisikia neno moyo au roho wanafikiri ni kitu kimoja..sikia ni vitu viwili tofauti angalia mistari hii uone. “nawe utakapomrudia BWANA, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;“ (Kum 30:2)

Ukiisoma mistari hiyo unaona utofauti wa moyo na roho…. si kitu kimoja ni vitu viwili tulivyopewa na Mungu cha tatu ni mwili.

VITU HIVYO VITATU VINAWEZA KUUGUA AU KUDHOOFIKA AU KUVUNJIA NK.

Sasa sikia vitu hivyo vitatu vinaweza kuugua au kuharibika au kupata ugonjwa…angalia mfano

1. Roho kudhoofika au kupondeka na kuugua au kuwa dhaifu Angalia mistari hii. ”Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?” (Mithali 18:14) Angalia na hii mingine “Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini BWANA atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;” (Kum28:65)

Ukiipitia mistari hiyo utaona kuwa roho yako inaweza kuwa dhaifu na inaweza kudhoofika kabisa. Neno dhaifu maana yake ni kitu kisicho na mashiko, kisicho kuwa na sifa, kisichovutia, chenye afya mbovu, kilichokosa unono, ni kitu duni, ni kisicho na uwezo au nguvu, kisicho na ukakamavu au kigonjwa… kilicho choka au kukata tamaa na kuzimia

2. Nafsi au moyo kuugua au kuvunjika au kujeruhika Moyo unaweza kuugua au kupata jeraha au kuvunjika nk. Angalia mistari hii. ”Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao; kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na BWANA, ili atukuzwe.”(Isaya 61:1-3).

Kwa mujibu wa mistari hiyo moyo au nafsi unaweza kugua. Na ukatafutiwa mganga wa kutibu au kuuponya.. Kwenye eneo hili watu wengi ni wagonjwa mnoo.. ndani ya somo hili tutaangalia kwa sehemu namna nafsi inavyoweza kupata jeraha na namna ya kuiponya.

3. Mwili unaweza kuugua au kuumwa. Angalia mistari hii ”Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” (Mathayo 10:1).

Angalia na mistari hii. ”Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake.39 Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia.“ (Luka 4:37-39)

Kwa mujibu wa mistari hiyo yoote utaona mwili unaweza kuugua kabisaa. Eneo hili naamini wote tunajua kuwa mwili unaweza kubeba magonjwa ya aina mbalimbali Maeneo hayo yoote matatu yanaweza kuugua na yana hitaji tiba. Moyo au nafsi unaugua kabisaa.. na nafsi ikiugua lazima mwili utoe taarifa kuwa nafsi imeugua. Watu wengi wana afya si nzuri na wanajaribu kutibiwa hawapati nafuu kisa ni kutokujua kuwa nafsi ikiugua hata mwili utatoa ishara ya ugonjwa.. Katika salamu zijazo tutaangalia kwa undani namna tunavyoweza kupata uzima na afya nafsini. Hebu tuishie hapo tuona katika kona hii mwezi ujao

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
    • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
    • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
  9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.