Salamu - Januari, 2026

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana.

Ninakukaribisha sana katika eneo hili la salamu za mwezi. Heri ya mwaka mpya! Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mwaka huu mpya.

Mwezi uliopita tulikuwa na kambi ya 16 ya maombi. Ilikuwa kambi nzuri sana, na tunamshukuru Mungu kwa kila jambo alilotenda.

Pia ninakualika karibu katika kambi ya 17 ya maombi, itakayofanyika mwezi wa kumi na mbili. Tutakupa taarifa kamili kuhusu mahali itakapofanyika.

Sasa, ebu tuanze kuzitazama salamu za mwezi huu wa kwanza.


SOMO LA MWEZI

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)

Ebu tuendelee tukiangalia eneo lifuatalo:

KARAMA YA MIUJIZA HUTENDA KAZI KWA NJIA TOFAUTI TOFAUTI

Ni muhimu kufahamu kuwa utendaji wa karama ya miujiza haufanani kwa kila mtu au kila wakati.

Biblia inasema:

“4 Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.”
(1Kor 12:4–7)

Watu wengi hawajui jambo hili. Wengi hufikiri kuwa utendaji wa karama ya miujiza utafanana kwa kila mtu. Lakini Biblia inaonyesha wazi kuwa utendaji wake hutofautiana kulingana na mapenzi ya Mungu.


MFANO WA PAULO

Biblia inasema:

“11 Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;
12 hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”
(Matendo 19:11–12)

Hapa tunaona kuwa Mungu alitumia hata leso na nguo za Paulo kuponya wagonjwa na kutoa pepo wachafu.


MFANO WA HEZEKIA

“Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa…
Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.”
(Isaya 38:1–7)

Katika tukio hili, Mungu alitumia mkate wa tini kama sehemu ya muujiza wa uponyaji.


MFANO WA MUSA

“23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu…
25 Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu…”
(Kutoka 15:23–27)

Hapa tunaona Mungu akitumia mti kufanya muujiza wa kubadilisha maji kuwa matamu.

Pia Mungu alimtumia Musa kufanya miujiza kwa kutumia fimbo. Hii inaonyesha kuwa Mungu anaweza kutumia njia tofauti tofauti.


MFANO WA BWANA YESU KRISTO

Bwana Yesu Kristo hakutumia njia moja tu kufanya miujiza.

Mfano wa kwanza:

“41 Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka.
42 Mara akasimama yule kijana…”
(Marko 5:41–42)

Hapa Yesu alitamka neno tu, na muujiza ukatokea.

Mfano wa pili:

“5 Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya.”
(Marko 6:5)

Hapa Yesu aliweka mikono juu ya wagonjwa.

Mfano wa tatu:

“6 Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho…”
(Yohana 9:6–7)

Mfano wa nne:

“33 Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi…”
(Marko 7:33–35)

Hii inaonyesha wazi kuwa hakuna mfumo mmoja wa miujiza.


MFANO MWINGINE WA UPONYAJI

“23 Akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake…
25 Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akawa mzima…”
(Marko 8:22–25)

Na pia:

“14 Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana…”
(Yakobo 5:14–16)


MFANO WA ELISHA

“20 Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake…
21 Akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya…”
(2Wafalme 2:19–22)

Hapa Mungu alitumia chumvi kufanya muujiza wa uponyaji.


HITIMISHO

Kutokana na mifano hii yote, tunajifunza kuwa:

  • Karama ya miujiza hutoka kwa Mungu

  • Utendaji wa miujiza hutofautiana

  • Hakuna mfumo mmoja wa miujiza

  • Mungu anaweza kutumia njia mbalimbali kufanya miujiza

Naamini sasa umeanza kuikuza imani yako katika eneo hili la karama ya miujiza na uponyaji.


JINSI YA KUPATA MASOMO YETU

App: HUSONEMU (MWAKATWILA) – Play Store
Tovuti: www.mwakatwila.org
YouTube: HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
Facebook: SOMA NENO LA MUNGU
Instagram: Huduma ya Soma Neno la Mungu

Vitabu, DVD, CD: +255 763 109 733


REDIO

Rungwe FM 102.5 MHz – Jumapili saa 3:00–4:00 usiku
Baraka FM 107.7 MHz – Jumanne saa 12:00–1:00 usiku
Bomba FM 104.1 MHz – Ijumaa saa 3:00–4:00 usiku


ONLINE RADIO

radio.mwakatwila.org


MAWASILIANO

+255 754 849 924
+255 756 715 222


Wako katika Kristo,
Mwl Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila