Salamu – Aprili, 2012

Tunakusalimu katika jina la Bwana wetu mwema Yesu Kristo. Mimi na mke wangu ni wazima tunamshukuru Mungu aliyetupa uzima. Ninaamini kuwa hata wewe Mungu amekupa uzima na afya njema, pia inawezekana una matatizo fulani, usiogope Bwana Yesu atakutoa kwenye hilo tatizo. Iwapo unahitaji maombi yetu, basi, unaweza kuingia kwenye eneo la mawasiliano katika tovuti yetu hii, na utapata sehemu imeandikwa maombi, andika hapo unahitaji nini tukuombee na tunakuahidi tutakuombea. Hebu tukuletee sasa salamu za Mwezi huu wa nne, kumbuka tuna salamu ndefu zilizo anzia mwezi wa Kwanza. Zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO. 

Katika salamu zilizo pita tuliona jambo la kwanza Muhimu ambalo kila mtu aliyepewa ndoa inatakiwa alifanye, nalo lilikuwa ni Kuuruhusu Ufalme Wa Mbinguni Uitawale hiyo ndoa. Kumbuka Ufalme wa Mbinguni maana yake ni serikali ya mbinguni kupewa nafasi ya kuitawala hiyo ndoa. Na tuliona serikali ya Mbinguni ina utaratibu wake, utaratibu huo ni HAKI. 

“Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” (RUM 14:17) 

Ukitafuta utawala wa Mungu uje na kuitawala ndoa yako utakachofanya ni kuleta utaratibu wake, ambao ni haki, amani, na furaha. Hebu tuanze kuliangalia jambo la pili ambalo unatakiwa ulifanye ili upate kuilinda na kuiponya ndoa yako. Nalo ni. 

MUWE WABUNIFU KATIKA SUALA LA MAPENZI (MSIONEANE HAYA) 

Moja ya jambo ambalo ndiyo kiini cha matatizo kwenye ndoa nyingi ni hiki cha wana ndoa wengi kutokuwa na ufahamu mkubwa wa suala zima la mapenzi au niseme mahaba. Watoto wa Mungu wengi sana hawana elimu toshelevu katika eneo hili. Neno la Mungu linasema wazi kuwa kila mwanandoa lazima ahakikishe anampatia mwenzie haki yake; 

“Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” (1KOR 7:7-5) 

Ukiyaangalia maneno hayo utagundua kuwa wanandoa wamepewa amri ya kuhakikisha kila mmoja anahakikisha anampa mwenzie haki yake ya kimapenzi au mahaba. Neno linasema wazi kuwa mwenye amri juu ya mwili wa mwanaume na mkewake, na mwenye amri juu juu ya mwili wa mke ni mumewake. Siku Mungu ananifundisha somo hili. ALISEMA NAMI WAZIWAZI NA KUNIONYESHA JAMBO HILI JINSI LILIVYO NA AKANIAMBIA WAZI KUWA TATIZO KUBWA LINALOPELEKEA NDOA KUWA NA SHIDA LIPO HAPO. Wanandoa wengi, hawako huru katika suala hili la mapenzi, wengi ni waoga, na wenye aibu sana kwa wake zao au kwa waume zao. Nilikuwa na maswali mengi sana moja wapo ni hili, kwanini wanandoa wengi wanatoka nje ya ndoa? Kwa nini wakitoka hawaludi kwa wake zao? Au kwa waume zao? Kwanini wanawake walioolewa wanapata taabu sana kwa sababu waume zao hawawajali na hawataki kuwatunza kabisa? 

Mungu alinijibu maswali yangu hayo yote, kwa kunifundisha kuwa, tatizo lipo kwa wanawake walio ndani ya ndoa, hasa Wakristo, hawana elimu ya suala hili la mapenzi, ngoja nikupe mifano hii utaelewa. Neno la Mungu lina sema malaya hawawaonei haya au aibu waume za watu, na hiyo ndiyo silaha yao kubwa sana wanayoitumia. Tazama maneno haya; 

“….Nikaona katikati ya wajinga, nikamtambua miongoni mwa vijana, kijana mmoja asiyekuwa na akili, akipita njiani karibu na pembe yake, akiishika njia iendayo nyumbani kwake. Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, usiku wa manane, gizani. Na tazama, mwanamke akamkuta, ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; anakelele, na ukaidi; miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, akamwambia kwa uso usio na HAYA. Kwangu ziko sadaka za amani; leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; ndiyo maana nikatoka nikulaki, nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, kwa matandiko ya Kimisri yenye misitari. Nimetia kitanda changu manukato, manemane na udi na mdalasini. Haya tushibe upendo hata asubuhi, tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba. Maana mume wangu hayumo nyumbani, amekwenda safari ya mbali; amechukua mfuko wa fedha mkononi; atarudi wakati wa mwezi mpevu. Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.” (MITHALI 7:6-21) 

Ukiyasoma maneno hayo utaona ni kwanini wanawake wengi leo hii ndoa zao zimewashinda. Ona mwanamke huyo alimpata huyo kijana kwa sababu alikuwa mjanja sana kwenye masuala ya mapenzi, kuanzia kuvaa kwake, kusema kwake, na neno linasema mwanamke hakuwa na haya au aibu kabisa. Alimfuata huyo mwanaume akambusu, akaanza kumweleza huyo mwanaume maneno yaliyojaa mahaba kweli, ona huyo kijana neno linasema kwa maneno mengi ya kimapenzi yaliyo laini yakamshawishi huyo kijana akaenda na huyo mwanaume. Ona neno linasema; “Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda”. Nataka nikuulize swali hili wewe mwanamke, Je! Wewe ukoje kwa mumeo? Mbona huna muda wa kumbembeleza kwa maneno laini, ya kimapenzi? Wewe unajua kumdai fedha ya kula na kukununulia nguo nk. Lakini haumpi mumeo haki yake ya kimapenzi, unajua siku akikutana na mwanamke mjuzi mbunifu wa mapenzi nakuambia ukweli, hawezi kukuludia, hata akiwa na wewe hata kutunza, yaani hatakupa mahitaji yako kama mwanzo, akili zake zote zinahamia huko kwa mwanamke huyo mtundu wa masuala ya mapenzi. 

Mungu analijua hilo ndio maana anasema hivi; 

“Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani.”(MITHALI6:25-26) 

Neno la Mungu linasema mtu yoyote yule ambaye amekutana na mwanamke mjuzi wa mapenzi ambao wengi wao ni malaya kwa sababu wao hutafuta sana wanaume za watu, hapo ndipo wanakuwa wabunifu kila siku wa masuala ya kuwafanyia hao waume za watu kuliko hao wake za watu ambao kwa ujinga wao wamejisahau kwa kujiamini kuwa wameolewa na hawaoni umuhimu wowote wa kubuni, kujituma na hata kutafuta mbinu za kunogesha mapenzi katika ndoa zao. Neno linasema mtu anayekutana na mwanamke wa namna hiyo uhitaji wake kwa huyo mwanamke unakuwa mkubwa sana, Mungu amefananisha na mtu aliye na njaa kali ambaye anahitaji angalau kipande kidogo cha mkate ili ale na ashibe. Sikiliza mwanamke wewe Mungu ameyaachilia maneno hayo makusudi ili akufundishe wewe ujue mbinu ya adui yako akuchukuliaye mumeo kama unataka kumlinda mumeo ujue silaha aitumiayo mwanamke huyo ni hii, hamuonei haya mumeo, na ni mbunifu wa mapenzi. Ndio maana mumeo kila wakati anamuwaza huyo mwanamke, kila wakati anamuhitaji, wewe hakuhitaji tena kisa ni hicho. 

Hebu tumalizie salamu zetu hizi kwa maneno haya. Jitahidini kuwa wabunifu wa masuala ya mapenzi na kutooneana aibu, katika salamu zijazo, tutaendelea kuliangalia jambo hili kwa upana sana.Ninataka nikutie moyo mama haujachelewa, anza kumuomba Mungu akupe akili ya kuyafahamu yale unayotakiwa uyafanye katika jambo hili la mapenzi kwa Mumeo. La muhimu usimuonee haya mumeo! 

Mungu akubariki sana 

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila