Salamu – Mei, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ndugu zangu niwape pole kwa na,na taifa na ulimwengu tunavyopitia kutokana na janga la corona.

Niwape pole wote mliougua,au kufiwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya jambo hili. Tuendelee kumsihi Mungu sana ili atuvushe salama katika janga hili.

Kwa kuwa mwezi wa nne serekali ilikataza makusanyiko hata sisi tumesimamisha ratiba yetu yoote ya semina mbalimbali ambazo ilikua tuzifanye. Nikuletea salamu za mwezi wa tano.

Tunasalamu zenye kichwa hiki

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Mwezi huu nataka tuendelee mbele kidogo. Tuangalie jambo la tano muhimu.

JAMBO LA TANO: JIFUNZE KUOMBA MUNGU AONDOE ADHABU

Angalia mistari hii: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” ( Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu anaahidi hapo kuwa, watu wake walioitwa kwa jina lake wakijinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wake na kuziacha njia zao mbaya anasema atasikia, na kusamehe dhambi yao na kuiponya nchi yao.

Anaposema kuiponya nchi yao maana yake ni kuwa ataondoa tauni au nzige na kuwarudishia hao watu afya na kuwapa chakula tena.

Sasa sikia, unapomwendea Mungu kama kuhani katika eneo la kuomba toba, lazima tujifunze pia kumwomba na kumbembeleza kwa kilio ili aondoe adhabu aliyoipeleka.

UTOFAUTI WA TOBA YA UPATANISHO NA TOBA YA KUONDOA ADHABU

Kuna utofauti sana tu wa toba ambayo ndani yake imelenga kumwomba Mungu aondoe adhabu na toba ambayo ndani yake imelenga kufanya upatanisho kati ya Mungu na wanadamu.

Angalia mistari hii naona utanielewa nasema nini: “Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.” (Kutoka 32:9-14)

Ukiipitia hiyo mistari utaona alichokuwa anakishughulikia Musa ni toba iliyolenga kuondoa adhabu.

Musa alijua kuwa Mungu kakasirika na kaamua kuwaua hao watu. Mungu alimwambia kabisa Musa kuwa na waua wote nakubakiza wewe tu. Musa akaamua kufanya toba maalumu akimsihi Mungu aondoe adhabu hiyo aliyoiweka dhidi ya wana wa Israeli.

Fikiria Musa aliutafuta uso wa Mungu katika toba ya namna hiyo kwa muda wa siku arobaini. Mungu alikubali kuondoa adhabu. Lakini hakuwa tena patano au ushirika na wana wa Israeli.

Unaweza kujiuliza ulijuaje kuwa hakuwa na ushirika au patano nao?

Angalia katika kitabu hicho hicho hapo chini kidogo maandiko yanasema hivi: “Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa BWANA, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa BWANA akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.  BWANA akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.” (Kutoka 32:30-35)

Hebu itazame kwa makini mistari hiyo. Utagundua kuwa Musa alirudi tena kwa Mungu kwa kazi maalumu ya kuwapatanisha au kuurejeza ushirika uliopotea kati ya Mungu na hao wana wa Israeli.

Sikiliza toba ile ya kwanza na hii ya pili hazifanani kabisaa. Toba ya kwanza Musa alishughulikia adhabu iondolewe. Toba ya pili alishughulikia upatanisho kati ya Mungu na wana wa Israeli.

Mfano Angalia Tena mistari hiyo shuka chini kidogo utaona Mungu anasema hivi:

“BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri.” (Kutoka 33:1-4)

Mungu aliwasamehe hao watu kwa kuwaondolea adhabu. Lakini alikataa kwenda nao au aliondoa ushirika kati yake na hao wana wa Israeli. Wana wa Israeli walijua kabisaa kuwa wamesamehewa adhabu ya kifo hawatakufa lakini Mungu hatakuwa nao tena katikati yao.

Wakalia na kuomboleza sana, walijua kitendo cha kuto kuongozana na Mungu ni janga kubwa mno.

Musa ikabidi aingie tena kwenye maombi mazito ya toba na kumwomba Mungu aende nao au awe katikati yao. Mungu alikubali.

Hata leo tunapoomba toba kwa ajili ya Corona au nzinge au tauni ya aina yoyote ile ulimwenguni, makuhani wa Bwana lazima pia tumsihi aondoe adhabu. Tunaweza kuomba msamaha, akatusamehe kabisaa lakini adhabu ikabaki pale pale, mpaka tutakapoanza kumlilia kuwa ondoa adhabu

Angalia mfano huu uone: “Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?” (2 Samweli 12:7-18)

Unapoisoma hiyo mistari utajifunza kwa upana kidogo hiki ninachokufundisha.

Mfalme Daudi alifanya dhambi, dhambi hiyo ilipofanywa Mungu aliamua kumwadhibu.

Adhabu haikuwa moja, ilikuwa nyingi sana, mojawapo ni ya yeye kufa. Mfalme Daudi alipotubu dhambi yake hiyo unaona Mungu alimwambia hivi: “Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.”

Najifunza kitu hapo, mfalme Daudi alishughulikia dhambi na pia alishughulikia adhabu yake ya kifo. Mungu alimsamehe akaondoa dhambi akamwondolea na adhabu ya kifo.

Kuna kitu kingine cha kujifunza hapo, Daudi hakufanya toba ya kuondoa adhabu ya upanga na tendo la wakeze kulala na mtu mwingine. Hakufanya hivyo.

Cha ajabu mfalme Daudi alishughulikia adhabu ya kifo cha mtoto wake mtarajiwa ambaye alimpata ki-uzinzi na kuua watu. Mungu hakumsikiliza kabisa adhabu ilibaki palepale. Mtoto alikufa.

Ninachotaka nikutazamishe ni hiki. Fikiria kidogo kama Daudi angefunga na kumlilia Mungu ili aondoe adhabu ya upanga na wakeze kulala na mwanaume mwingine unafikiri Mungu angefanyaje? Mimi naamini angesikia.

Mfalme Daudi hakuwa na mzingo wa watoto wake wengine kukumbana na kifo cha upanga na wakeze kubakwa, akawa na mzingo wa mtoto wake mmoja tu tena aliyesababisha magumu hayo yoote.

Mungu hakumsikia, Daudi aliwabagua hao wengine hakuona umuhimu wa kuwalilia, Mungu na yeye akamnyamazia.

Nataka utanue wigo wa fikra zako, kuhani wewe usiwe mbaguzi unapoombea maombi ya Mungu kuondoa adhabu.

Walilie watu woote ili Mungu awaondolee adhabu. Usifikiri Mungu anataka watu fulani wafe. Mungu hapendi mtu yeyote apotee bali kila mtu afikilie toba.

Angalia tauni inavyoua watu. Wengi wanaokufa hawamjui Bwana Yesu Kristo. Kuhani mwenye akili hawezi kuwabagua hao.

Anza leo kushughulikia pia maombi maalumu Mungu aondoe adhabu.

Naamini umenielewa.

Ubarikiwe sana na ufanyie kazi somo hili

Tuonane katika katika salamu za mwezi ujao.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.