Salamu – Jun, 2011

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU.  

Bwana Yesu asifiwe sana. Tunakusalimu kwa jina la Bwana Yesu Kristo aliye hai. Ni imani yetu kuwa Mungu kwa neema yake ameendelea kukutunza na kukulinda. Sisi tunamshukuru sana Mungu ambaye ametupigania sana mwezi uliopita. Pia alituwezesha kufanya huduma Mbili kubwa kama ratiba yetu ilivyokuwa. Kwa kweli tumemuona Mungu akiokoa, akifungua waliofungwa, na kutupa maarifa katika semina hizo mbili. Semina moja tumeifanya Mbeya mjini eneo la Forest, waandaaji wa semina hiyo walikuwa ni kanisa la KKKT Ushirika wa Forest.  

Waliwaalika watu kutoka madhehebu mbalimbali, na watu waliitikia sana. Semina ya pili tumeifanya eneo la Mbalizi, waandaji walikuwa ni kamati ya maandalizi ya semina zetu ya Mbalizi, ambayo inamchanganyiko wa watu kutoka madhehebu mbalimbali. Kwa kweli tulikuwa na semina nzuri sana na Roho Mtakatifu alitufundisha somo lenye kichwa “KUTOKA KATIKA UTUMWA AU MKANDAMIZO WA AINA YOYOTE” Tulimuona Bwana katika semina hiyo tuliyoifanyia kwenye viwanja vya Mahubiri tukiwa tumefunga hema letu. Hebu tusonge mbele katika salamu zetu za mwezi.   

Kumbuka tumekuwa na Salamu zenye kichwa Mambo muhimu unayotakiwa umuombe Mungu kila siku (Eneo la kuyajua mapenzi yake au makusudio ya Mungu).  

Mungu kupitia neno lake anatufundisha anasema. “Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1 Yohana 5:14-15). Ukiyasoma maneno hayo utaona kuwa, Mungu ametupa utaratibu wa kumuomba. Anasema tukiomba sawasawa na mapenzi yake ndipo tutakapopewa kile tunachokihitaji toka kwake. Kwa maana nyingine ikiwa hatujaomba sawasawa na mapenzi yake hapo itakua ni vigumu sana kupewa chochote kile tumuombacho Bwana Mungu. Kumbuka neno mapenzi ya Mungu maana yake sahihi ni kusudi la Mungu, au mipango ya Mungu.  

Katika sehemu iliyopita tulipita na kuona eneo la tatizo kubwa tulilonalo watoto wa Mungu nalo ni la kutokumuuliza Mungu. Inawezekana umekuwa na swali kama hili, je! Nikimuuliza Mungu atanijibuje?  

FAHAMU MUNGU YUPO HAI NA ANASEMA NA KUSIKIA 

Kabla ya kuanza kufahamu namna Mungu anavyoweza kukujibu, kwanza lazima tumjue huyo Mungu wetu alivyo. Ili leo hii ndugu yangu ustawi sana kwenye eneo hili la kupokea majibu yako kutoka kwa Mungu, kwa kuyajua mapenzi yake nini, ni lazima ujue na uamini kuwa Mungu tunayemuabudu yupo, na yu hai, anasikia, na anasema! Sikiliza maneno haya ya Bwana yasemavyo “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko…..” (Ebr 11:6). Kama kuna jambo ambalo leo hii linawasumbua sana watoto wa Mungu wengi ni hili la kutokuwa na ufahamu wa kutosha katika kujua kwa upana habari za Mungu. Mungu tunayemuabudu yu hai anaweza, kwa kuwa yuhai anasema. Ona maneno haya ya Bwana yasemavyo “Basi, nduu zangu, kwa habari ya karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa mataifa mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa. Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Bwana, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu”. (1 Kor 12:1-3). Ona, moja ya jambo ambalo unatakiwa ulijue ni hili la kuhusu sifa za Mungu uliyenaye. Ni Mungu anenaye, sanamu haziwezi kunena, ila Mungu uliyenaye sasa hivi moja ya sifa zake ni hii, anasema.  

Wakristo wengi wanaamini kuwa Mungu yupo, ila hawazijui sifa zake, Mungu tunaye mwabudu si bubu. Ni Mungu aliye hai na anazungumza, jenga imani yako katika neno hilo!  Fahamu Mungu ni Roho. “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Yohana 4:24) Huwezi kumtenganisha Mungu na Roho Mtakatifu, pia huwezi kumtenganisha Yesu, Roho Mtakatifu na Mungu. Hawa ni wamoja. Huyo Mungu Roho Mtakatifu leo hii anaishi ndani yako, Ona maneno haya ya semavyo. “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa mwanawe mioyoni mwetu, aliaye Aba yaani, Baba.” (Gal 4:6). Angalia pia maneno haya, “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kufungua mlango, nitaingia kwake; nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”. (Ufu 3:20). 

Ukiyasoma maneno hayo, utagundua kuwa Roho Mtakatifu aliye ndani yako ni Roho wa Kristo. Maana yake ni Kristo mwenyewe. Ni Mungu, anaishi ndani yako, ikiwa tu umefanyika Mwana, na tunafanyika wana siku ile tulipomuamini Yesu na kumpokea kama Bwana na Mwokozi wetu “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12). Kama umempokea Yesu amini Roho Mtakatifu yuko ndani yako, huyo Roho Mtakatifu aliye ndani yako ana sifa hizi, ona sifa zake, analia Aba, kwa maana Nzuri anasema Baba. Anao uwezo wa kusema kabisa. Angalia tena hayo maneno ya Bwana Yesu anasema mtu akiisikia sauti yangu, leo! Kwa maana nzuri huyo Roho Mtakatifu anayo sauti kama anayo sauti basi anasema!

Moja ya kazi azifanyazo Roho Mtakatifu ni kutupasha habari za mambo mbalimbali “Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.” (Yohana 16:13-16)          

Ukiyasoma maneno hayo utagundua kuwa Roho Mtakatifu analo neno, tena ni neno la Bwana Yesu Kristo. Anaweza kusikia na kukupasha wewe habari, tena hata habari ya mambo yajayo anaweza kukupasha kwa maana hiyo Roho Mtakatifu anayajua hata mambo yote ya mbeleni. Kama anaweza kutupasha habari, maana yake anasifa ya kuzungumza, huyo Roho Mtakatifu aliye ndani yako si bubu anasema, ila haujampa nafasi ya kuzungumza na wewe, kwa sababu hujui kuwa anasema, na hata kama unajua ila huamini. Yaani huna uhakika kama anaweza kusema na mtu kama wewe, hujiamini, unafikiri anaweza kusema na watu fulani fulani tu.  

Ngoja nikupe mifano hii michache uone namna ndugu zetu mbalimbali walivyo sema na Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu naye akasema nao. “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia, wakajaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa.” (Mdo 16: 6-7). Hebu yaangalie hayo maneno, utagundua kuwa Roho Mtakatifu, anaweza kusema, alisema na hao ndugu zetu, akawaambia mambo ya kufanya. Fahamu Roho huyo ndiye huyo uliyenaye wewe na mimi, hajabadilika. Ona mfano mwingine. “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga. Roho Mtakatifu AKASEMA, nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” (Mdo 13:1-3) 

Nimekupa hiyo mifano michache ili uone ninachokuambia kuwa Mungu anasema. Kumbuka Mungu ni Roho, na yupo hai leo hata milele, anza kujenga imani yako kwenye maneno hayo. Neno la Bwana linasema. “Imani huja kwa kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” (Rum 10:17). Jenga imani yako kwenye neno hilo la Kristo, ambalo linakuambia wewe kuwa Roho Mtakatifu atayanena maneno yote yaliyosikiwa. Ebu nimalizie salamu hizi kwa kusema, unaye ndani yako Mungu aliye hai, analo neno analotaka kukuambia na ndani ya neno hilo huko ndiko alikoweka ufahamu wa kila aina. Kama unataka kupata ufahamu wa jambo lolote, atakachofanya Mungu ni kukuletea neno au atakupa neno. Katika salamu zijazo tutaanza kuangalia aina mbili za maneno ya Mungu na njia azitumiazo Mungu kuzungumza na mtu. 

Mungu akubariki sana.

Mr. Steven & Beth Mwakatwila