Salamu – Februali, 2012

MAMBO MUHIMU UNAYO TAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO  

Ndugu yangu Bwana Yesu asifiwe sana, pole na shughuli zote za mwezi uliopita ambao ndio mwezi wa kwanza katika mwaka huu, mara nyingi mwezi huo unakuwa na pilika pilika nyingi sana. Ninaamini Mungu amekuwezesha katika kila ulilolikusudia ulifanye, sisi tulikuwa na semina tatu, semina ya kwanza tumeifanyia mbeya tarehe 01-03-2012. Katika ibaada maalumu ya kufungua mwaka, tulikuwa eneo la St. Mary Secondary School, jijini Mbeya. Semina hiyo ilikuwa ni ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya mambo yote aliyotufanyia mwaka jana na kumuomba kwa ajili ya mwaka huu wa 2012. Watu wengi sana waliitikia, na tulikuwa na maombi maalum ya kuomba mkono wa Bwana utupiganie na kutubariki katika mwaka huu wa 2012 na tunamwamini Mungu kwa ajili ya mwaka huu atakuwa nasi na kujibu maombi yetu. Tulikuwa na somo lenye kichwa; JITUNZE KUFANYA MAOMBI MAALUM YA KUTENGENEZA NJIA ZILIZONYOOKA MBELE YAKO. Pia tulikuwa na semina katika Kongamano la Wachungaji na Maskofu waliookoka toka sehemu Mbalimbali nchini Tanzania. Tulimuona Mungu sana katika semina hiyo. Tulikuwa na somo lenye kichwa; WEKA BIDII YA KUMZALIA MUNGU MATUNDA MPAKA SIKU YA KUFA KWAKO. Pia tulikuwa na semina katika kanisa la Moravian Ruanda, tulikuwa na somo lenye kichwa; MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE KABLA NA BAADA YA KUMTOLEA MUNGU SADAKA YAKO KAMA MBEGU. Kwa ujumla masomo hayo ni mazuri sana, ukitaka kanda au CD au DVD, wasiliana nasi tutakupa maelekezo ya namna ya kuzipata. Hebu tukuletee sasa salamu zetu za mwezi huu, tukiwa na mfululizo wa salamu zenye kichwa;  

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO. 

Tulimalizia katika kile kipengere cha Mungu anachukia ayaonapo matatizo katika ndoa. Tuliona jinsi Mungu alivyo mkasirikia sana Haruni na Miriamu kwa sababu hawakuiheshimu ndoa ya Musa, ona maneno haya yasemavyo; 

“Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi……… Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma kisha haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu, nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika, hapo atokapo tumbo la mama yake. Musa akamlingana Bwana, akasema, mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana. Bwana akamwambia Musa, je! Kama baba yake angalimtemea mate usoni tu, hangaliona aibu muda wa siku saba? Na afungwe nje ya kambi muda wa siku saba, kisha baada ya hayo ataletwa ndani tena.” (Hesabu 12: 1-14) 

Ona anasema habari za baba kumtemea mate mwanawe, unajua maana yake nini? ni kumlaani au kumwona kama kinyaa vile, au kumdharau kabisa. Mungu alimtemea mate Miriamu usoni kisa hakuiheshimu ndoa ya Musa. Kilichomsaidia Haruni kilikuwa ni ule ukuhani aliokuwa nao, siku alipostaafu tu, neno linasema alipovua vazi la kikuhani tu, alidodoka akafa. Mnisikilize watumishi wote wa Mungu. Heshimuni ndoa za watu, kwani Miriamu alikua ni Nabii; 

“Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni……..” (Kutoka 15:20) 

Mungu alimpiga kwa ukoma kisa, hakuiheshimu ndoa ya mtu. Hebu fikiri uone jinsi Mungu anavyo heshimu ndoa, alikuwa tayari kumpiga nabii Miriamu kwa ukoma kwa sababu hakuiheshimu ndoa ya kaka yake, kumbuka Haruni, Musa, na Miriamu hawa ni ndugu kabisa. Leo hii kina dada wengi hawaziheshimu ndoa za kaka zao, kisa eti hawamtaki wifi yao, unajua kinachowatokea katika ulimwengu wa roho? Wanapigwa na ukoma! Ndio maana wengi hawasongi mbele, iwe kwenye uchumi nk, wanabeba laana bila wao kujua. 

Ukisoma maandiko kwa kutulia utagundua kuwa Mungu anaheshimu ndoa sana, na hapendi kuona matatizo kwenye ndoa yoyote ile. Mungu yupo tayari kumtenga mtu na hata kutoipokea sadaka yake kwa sababu tu, huyo mtu haiheshimu ndoa yake. Sikiliza maneno haya. 

“Bwana atamtenga mtu atendaye hayo; yeye aliye macho, na yeye ajibuye, atamtenga na hema za Yakobo, pia atamtenga yeye amtoleaye Bwana wa majeshi dhabihu. Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana kwa machozi, kwa kulia na kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi. Ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” (Malaki 2:12-16) 

Umeyasikia maneno hayo? Anasema, Mungu anamtenga na hatapokea sadaka (dhabihu) ya mtu mwenye tabia ya kutoiheshimu ndoa yake. Ona hapo kasema na wanaume waziwazi. Anasema, jihadharini roho zenu, kwa maana nzuri hiyo ni habari ya maonyo kwa kila mwanaume. Anasema, mtu mwenye ufahamu angalau kidogo asingemfanyia mkewe mambo ya hiana au kwa maana nzuri mambo mabaya. Ikiwa wewe mwanaume hauiheshimu ndoa yako Mungu alisha kutenga siku nyingi. Inawezekana kabisa kanisani kwako hawajakutenga, lakini Mungu amekutenga kwa sababu tu, umekuwa jeuri kwenye ndoa yako. Swali langu kwako; wewe ukoje?  

Mbona Mungu anaona katika madhabahu yake machozi na kilio cha mkeo au cha mumeo? Unafikiri ikiwa leo hii Mungu amekuchukia siku utakapo kutana naye itakuwaje? Leo hii Machozi ya mkeo au mumeo yanakuzuilia baraka zako. Yaani hata ukitoa sadaka ili akubariki hazipokei sadaka hizo. Je! Akikutemea mate kama alivyomtemea Miriamu unafikiri atakua anakuonea? Sikia, Mungu anasema mtu amfanyiaye mkewe mambo ya hiana Mungu anamchukia, je! Wewe Mungu anakupenda au anakuchukia? Jijibu mwenyewe. Fikiri jinsi unavyofanya, huiheshimu ndoa yako, unatembea na wanawake wengine nje ya ndoa yako, pia hata wewe mwanamke haujaiheshimu ndoa yako unatembea na wanaume wengine nje ya ndoa yako. Hata wewe dada ona namna ulivyo, haujaiheshimu ndoa ya mtu, unatembea na Mume wake unafikiri sifa, Mungu atakutemea mate kama alivyomtemea Miriamu. Na utabeba laana itakayo kusumbua wewe na uzao wako. Na pia inawezekana umekuwa jeuri na mkatili kwa mkeo na wewe mama ni jeuri sana kwa mumeo fahamu Mungu anakuchukia, tubu, acha tabia hiyo. 

Usipoacha hiyo tabia yako mbaya, naamini atakutenga na kukutengenezea jela fulani kama alivyomfunga Miriamu. Siwezi kujua kwako wewe ni jela gani atakayokutupa labda ni ya ukimwi, kansa au mapepo nk. Nakushauri achana na huyo mume wa mtu, kwani kilio cha mke wake kimesikika mbinguni, kama ni mwanaume achana na huyo mwanamke, iheshimu ndoa yako kwani kilio cha mkeo kimesikika mbinguni. Nataka kukuambia bila kukuficha Mungu hakupendi anakuchukia kwa sababu hujaiheshimu ndoa ya mtu. Hata wewe mama na wewe baba na wewe dada na wewe kaka, angalia jinsi mnavyoivuruga ndoa ya huyo ndugu yenu, kwa sababu zenu binafsi, Mungu anaichukia hiyo tabia yenu mbaya, nawashauri tubuni, msiingilie maisha ya ndoa ya huyo ndugu yenu. Sikiliza mwanamke wewe, je! Unaiheshimu ndoa yako? Mbona unasababisha maumivu makali moyoni mwa mumeo? Mungu anaichukia sana hiyo tabia yako mbaya uliyo nayo ya uzinzi kiburi na nk. Fikiri, Mungu kakupa mume na wewe unamvunjia mumeo heshima kwa kulala na mwanaume mwingine, unajua, Mungu anakuchukia sana, badilika, kabla hajakutemea mate usoni, kama alivyomtemea Miriamu. Utapata aibu siku si nyingi, aibu ambayo itapelekea utengwe hata na jamii nakuambia. Jifunze kuiheshimu ndoa yako. 

Mungu anasema anachukia kuachana, kuna neno kuachana na neno kutengana, watu wengi wameyachanganya hayo maneno mawili. Maneno hayo yana maana mbili tofauti. Kutengana ni pale wanandoa wanapo kuwa mbali kila mtu na mwenzake, na jambo hilo linakuwa wazi, yaani kila mtu anajua kuwa kumetokea nini katika ndoa ya fulani. Kuachana kunaweza kuwa ni siri. hakuna anaye fahamu, hata mumeo au mkeo na jamaa zako wasijue kabisa kuwa umemuacha mumeo au mkeo, ona mfano huu. 

“Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.” (Mathayo 1:19) 

Yusufu aliamua kumwacha Mariamu kwa siri. Kumbe upo uwezekano kabisa ukaamua kumwacha mkeo au mumeo kwa siri, yaani hata yeye asijue kuwa kaachwa. Mungu anasema anachukia kuachana. Kumbuka kutengana kunatokea baada ya kuachana. Hebu jiangalie ulivyo leo hii, je! Haujamuacha mumeo au mkeo? Ngoja nikupe kipimo hiki ujipime ndio utagundua umemuacha au la. Mbona unamawazo kuwa ulikosea kuoa au kuolewa? Kama unamawazo kuwa ulikosea, basi tayari umemuacha huyo uliye naye, ni kweli umezaa naye watoto mnalala kitanda kimoja lakini una mawazo na umepokea kuwa ulikosea kuoa au kuolewa na huyo ndugu. Kwa maana nyingine yupo ambaye unafikiri ndiye aliyefaa kukuoa au kuolewa naye. Unajua ukiwa ni mtu mwenye sifa hizo, unakuwa umemwacha huyo mumeo au mkeo. Mungu anachukia kuachana. 

Ona zamani ulikuwa na ujasiri wa kuongozana na mkeo au mumeo, mbona sasa hivi hunaujasiri huo tena? Unajua ni kwanini? Umemuacha kwa siri! Zamani mama ulikuwa unapata taabu sana mumeo akisafiri, lakini sasa hivi, akisafiri unapiga magoti na kumshukuru sana Mungu kuwa asante kwa huyo ndugu kupata safari, akikutaarifu kuwa atachelewa kurudi wewe una mwambia Mungu akutie nguvu, kumbe hupendi arudi kabisa! Ukiwa ni mtu wa tabia hiyo fahamu tayari ulishamwacha mwenzi wako. Mbona zamani ulipenda kukaa naye karibu hata kanisani mlikuwa na kawaida ya kwenda wote nk. sasa hivi hutaki kabisa, unajua hizo ni dalili kuwa umemuacha, nakushauri, mrudie mkeo au mumeo. Kwani Mungu anachukia kuachana. Badilika, usikubali shetani akutenganishe na Mungu kwa kukuletea tabia hiyo ya kumuacha mkeo au mumeo. 

NDOA NI MPANGO WA MUNGU NA MUNGU NIYE MWANZILISHI WA NDOA 

Kwanini leo hii ndoa nyingi zina matatizo kiasi cha kupelekea wanandoa wengi sana kuachana? Sababu kubwa ni hii, shetani ndiye chanzo cha matatizo ya ndoa nyingi sana. Watu wengi kunapotokea matatizo kwenye ndoa zao haraka sana huwaangalia wake zao au waume zao na kuwalaumu kuwa wao ndio chanzo cha matatizo hayo. Kwanini shetani anaziharibu ndoa? Ni kwasababu anafahamu kuwa ndoa ni mpango wa Mungu na Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa. 

Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa, na pia anaziheshimu sana ndoa za watu, kwa kuwa Mungu anaheshimu ndoa na ndiye aliyeianzisha ndoa, adui anatafuta kumuudhi kwa kupeleka tabia mbaya kwa baadhi ya wanandoa ili wagombane na kuachana. Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa, na ndoa ya kwanza kabisa ilifungwa mbinguni. Ukisoma maandiko utagundua kuwa, Mungu aliianzisha ndoa huko mbinguni. Tazama maneno haya ya Bwana yasemavyo. 

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwuumba mwanaume na mwanamke aliwaumba Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia zaeni mkaongezeke, mkaijaze, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini , na ndege wa wa angani na…..”( Mmwanzo 1:27-28) 

Ukiyaangalia maneno hayo ya Bwana utagundua kuwa ndoa ilianza kufungwa huko Mbinguni, Kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu, hii; Mungu ni Roho, anaposema na tufanye mtu kwa mfano wetu maana yake aliwaumba kama yeye alivyo yaani ziliumbwa roho mbili kwa mfano wa Mungu. Na roho hizo ziliumbwa siku moja, yaani mtu mume na mtu mke. Alipowaumba hao wawili siku ile akawaambia wazaane waijaze nchi na watawale vitu vyote. 

Ninachotaka uone ni hiki, Mungu yupo mbinguni, na hao waliumbwa kwanza kwenye ulimwengu wa roho yaani huko mbinguni, kumbuka waliumbwa kwanza kwa mfano wa Mungu ambaye ni Roho 

“Mungu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Yuhana 4:24) 

Mungu na malaika zake waliishangilia siku ile ndoa ya Adamu na mkewe Hawa huko mbinguni kabla hata hajawaleta hapa duniani au katika ulimwengu huu unaoonekana. Hata alipomtanguliza Adamu hapa duniani, alimpatia mke. Nilichotaka ukione ni hiki ndoa ni mpango wa Mungu na Mungu ndiye mwanzilishi wake. Adui analijua hili ndio maana anapigana usiku na mchana ili aziharibu ndoa na anapofanya hivyo anamuudhi sana Mungu, na wewe unapokubali kufanya mambo mabaya katika ndoa yako unashirikiana na shetani kumuudhi Mungu. Hebu kwa leo tuishie hapo tuonane tena katika salamu za mwezi ujao, Mungu akubariki na akupe mwanga wa kuona namna anavyoiheshimu ndoa yako. Na utubu pale unapojiona umemkosea kwa kutokuiheshimu ndoa yako. 

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila