Salamu – Machi, 2012

Bwana Yesu apewe sifa sana, mimi na familia yangu tunamshukuru sana Mungu kwa mema mengi aliyotutendea. Naamini hata wewe Mungu amekutendea mambo mengi sana mema. Mwezi huu tumekuandalia salamu nzuri sana, kumbuka tuna mfululizo wa salamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUILINDA NA KUIPONYA NDOA YAKO 

Katika salamu za mwezi uliopita tulijifunza eneo lile la Ndoa na ni mpango wa Mungu na Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa. Hebu tuanze kuangalia mambo muhimu ambayo unatakiwa uyafanye ili upate kuilinda na kuiponya ndoa yako. Yapo mambo mengi sana, lakini yale ambayo Mungu amenijaalia kuyafahamu ndiyo nitakayo yaachilia ili upate kuyafahamu. Na ukiisha kuyafahamu anza kuyafanyia kazi, hapo ndipo utakapoona mabadiliko makubwa katika ndoa yako. 

JAMBO LA KWANZA: MRUHUSU MUNGU AITAWALE NDOA YAKO 

Siku moja usiku Mungu aliniwekea neno hili moyoni mwangu, aliniambia, Steven ndoa nyingi sana zina matatizo. Akaanza kunifundisha kuwa moja ya chanzo kikubwa cha hayo matatizo ni kwa sababu wanandoa wengi hawajamruhusu Mungu awatawale, au niseme hivi, ndoa nyingi hazijatawaliwa na Mungu. Kama kuna kitu kikubwa anachotamani Mungu akifanye na ni halali yake akifanye ni hiki cha kutawala kila kitu kilicho duniani, mbinguni na hata chini ya nchi. Ona siku moja wanafunzi wa Yesu walimuomba Bwana Yesu awafundishe kusali, na yeye aliamua kuwafundisha kusali, katika mafundisho yake aliyoyatoa alisema maneno haya. 

“Basi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko Mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe makosa yetu kama nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]” (Mathayo 6:9-13) 

Ukiyasoma maneno hayo utagundua hapo ndani kuna vitu vingi sana ambavyo ndio misingi mikubwa ya maisha ya mwanadamu na mambo yake yote. Bwana Yesu anafundisha anasema, tumuombe Mungu aulete Ufalme wake hapa duniani. Anaposema salini hivi “Ufalme wako uje” maana yake haupo! Ili uje inatakiwa wewe umuombe aulete, kama hautamwambia aulete fahamu hatauleta! Neno ufalme ni tofauti na neno mfalme. Neno ufalme maana yake ni eneo linalotawaliwa na mfalme, neno ufalme maana yake ni kuwa serekali ya mfalme ndiyo inayomiliki na kutawala kwa kuweka utaratibu wake, ambao unapaswa kufuatwa na wale wanaotawaliwa na huyo mfalme. Naamini umenielewa hapo. Sasa kama unataka leo hii ndoa yako iwe salama lazima uhakikishe unamruhusu Mungu aulete ufalme wake katika hiyo ndoa yako ili ipate kutawaliwa na Mungu Baba wa Mbinguni. 

Ukiziangalia ndoa nyingi utagundua kuwa hazitawaliwi na Mungu, yaani ufalme wa Mungu aujaruhusiwa kwenye hizo ndoa, haijalishi wanandoa hao walifunga ndoa kihalali kabisa na kupokea baraka kutoka kanisani, haijalishi hao wana ndoa wameokoka wote au mmoja wao nk. Unaweza kujiuliza swali, kwa nini unasema hivyo Mwakatwila? Sikiliza; watu wengi sana wanaomba sana Mungu azilinde ndoa zao lakini kila kukicha utaona jinsi ndoa hizo zinavyo bomolewa na adui shetani, wengine ndiyo wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji nk lakini hakuna lolote, kila siku ni matatizo tu. Unajua ni kwa nini ndoa yako haina amani, furaha, nk? Ni kwa sababu haujamruhusu Mungu aitawale ndoa yako. Ninaposema Ufalme wa mbinguni hautawali ndoa yako unaweza ukapata shida sana, ngoja nikuonyeshe maana halisi ya neno ufalme wa mbinguni ni nini. Angalia maneno haya ndio utaelewa kuwa ndoa yako inatawaliwa na ufalme upi. 

“Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” (RUM 14:17) 

Ukiyaangalia maneno hayo utaona maana halisi ya neno ufalme wa Mungu ni nini. Neno linasema ufalme wa Mungu ni haki. Katika Biblia Mungu anatufundisha haki ina kazi gani na ina matunda gani, ona maneno haya yanavyo izungumzia haki ilivyo. 

“Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima.”(ISAYA 32:17) 

Sikiliza, utakapomruhusu Mungu aitawale ndoa yako lazima ukubaliane na utaratibu wa serekali yake, serekali ya mbinguni yenyewe utaratibu wake wa kwanza ni kuhakikisha haki ndiyo inayotawala eneo hilo uliporuhusiwa ufalme wa Mungu uje. Ndoa nyingi zimepoteza amani, unajua ni kwanini? Ni kwa sababu haki, haijapewa nafasi ya kutawala hizo ndoa! Sikiliza mwanaume wewe na wewe mwanamke, ikiwa wewe mwanaume haumtendei mkeo haki, fahamu amani na utulivu na matumaini kwenye hiyo ndoa havitakuwepo kabisa. Hata wewe mwanamke ikiwa haumtendei mumeo haki, fahamu amani na utulivu na matumaini katika ndoa yako havitakuwepo, mtajikuta mkigombana na kupoteza matumaini na utulifu au furaha itatoweka tu. Kama mtakimbilia kumuomba Mungu awaletee amani, atakacho wafundisha ni hiki cha kila mmoja wenu ahakikishe anakubali haki iwatawale, yaani uhakikishe unatenda matendo ya haki kwa mwana ndoa mwezio. Kinyume cha hapo msitarajie amani, furaha na matumaini kwenye hiyo ndoa yenu, haijalishi mmeokoka au ni watumishi. Watu wengi hawajui Ufalme wa mbinguni ni nini, wengi wanaomba Ufame wa mbinguni uje kwenye ndoa yao, nchi yao, ofisini kwao nk. Hawajui kuwa ukija huo Ufalme utakacholeta ni haki. Yaani kila mmoja ahakikishe anamtendea kila mtu matendo ya haki, yaani kama ni ofisini wewe bosi lazima uwape hao watumishi wako haki zao, ukiwanyima tu, unakuwa unashindana na haki, hapo haki itakacho fanya ni kuondoa amani na utulivu, ndipo unaposikia wamegoma, wameiba nk. Hata kwenye ndoa ni hivyo hivyo. 

Haki ina matendo yake, yanaitwa matendo ya haki! Tazama maneno haya ya Bwana yasemavyo.  

“Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya mwana-kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI ya watakatifu. (UFU19:7-8) 

Haki ina matendo si maneno na kuamini tu, kama leo hii utamuomba Mungu aulete ufalme wake katika ndoa yako hiyo yaani unakubali akutawale, jambo la kwanza lazima ukubali kuanza kuyatenda matendo ya HAKI. Ngoja nikupe mifano hii ndiyo utaelewa ni nini ninacho kizungumzia. Wewe mwanamke umepewa mume huyo, huyo mume anazo haki zake kama mume ambazo wewe mwanamke unatakiwa uhakikishe unamtedea, mume ni kichwa, kama ni kichwa neno linasema ni mtawala, mpe haki yake ya kukutawala! Usipokubali tu fahamu amani utulivu na furaha vitatoweka tu, hata ufunge na kuomba sana, nina maana hii, ondoa kiburi ulicho nacho kwa mumeo mtii hiyo ndiyo haki yake. Iruhusu kwa kuitenda si kwa maneno ndipo utakapoona ulinzi kutoka kwa Mungu ukikulindia ndoa yako. 

Hata wewe mwanaume, umepewa huyo mwanamke, ana haki zake kama mkeo, haki ya mwanamke ni msaidizi wako, unajua neno msaidizi ki-biblia ni pana sana, si kukufulia nguo na kukupikia tu, ni zaidi ya hapo. Ni haki ya mkeo ajue na afahamu wewe unafanya kazi gani, una kipato cha kiasi gani, nk. Ona wanaume wengi hawaoni kuwa kwa kutowashirikisha wake zao kwenye eneo la kipato chao hawatendi haki kabisa, na hapo ndipo ugomvi unapotokea na furaha kuondoka kwa mkeo nk. Sikiliza mpendwa, kama unataka Mungu akutawale ruhusu haki itawale! Mpe heshima mkeo hiyo ndiyo haki yake, mtunze hiyo ndiyo haki yake, watu wengi hawajui kuwa mke ni haki yake kuheshimiwa ona maneno haya 

“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” (1PETRO 3:7) 

Haki inataka kukuona wewe mwanaume unamheshimu mke, unaweza kuniambia kuwa kwa kitendo chako cha kutokumpa mkeo habari za kipato chako, unamficha kitabu chako cha benki, je unatenda haki? Wewe angalia unapopata mshahara je! Unamuonyesha mkeo na mnakaa na kupanga mfanye nini? Kama haufanyi hivyo nakuambia ukweli hautendi matendo ya haki, kumbuka haki ikiondoka amani inaondoka na furaha inaondoka kunabaki magomvi na machungu. 

Sikia wewe mwanamke, ikiwa leo mumeo amekuletea fedha na akakupa fedha hizo kwa ajili ya matumizi fulani, halafu wewe bila kutaka ridhaa ya mumeo unakwenda sokoni kununua nguo zako, sahani, heleni, mafuta mazuri, nk, wakati alikupa fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya mboga, mahindi, au kulipa deni la maji umeme nk, kwa kufanya hivyo unakuwa unamtendea mumeo haki? Sikia; kwa kufanya hivyo utakuwa hautendi haki, kwa kuwa hujaitenda haki, fahamu kitakacho tokea ni ufalme wa giza kuitawala ndoa yako, yaani ugomvi na huzuni itawatawala tu. Kwa mifano hiyo michache umeelewa ninamaana gani ninapozungumzia habari za Ufalme wa Mungu kuitawala ndoa yako. Ukiziangalia ndoa nyingi utagundua hazitawaliwi na Mungu, kwa nini? Kwa sababu haki haijapewa nafasi katika hizo ndoa! 

Wanaume wengi leo hii, wanazini, kwa kufanya tendo hilo wanakuwa hawawatendei haki wake zao, na Mungu pia, kwa kufanya hivyo tu tayari ufalme wa giza unaanza kuitawala ndoa hiyo, hapo ndipo shetani anapoachilia magomvi, anaondoa furaha, na utulivu uliokuwepo kwenye ndoa unaondoka, matumaini kwa mkeo yanahama kabisa, na kuyarudisha ni gharama kweli nakuambia. Hata baadhi ya wanawake wanazini nje ya ndoa, kwa kufanya hivyo, hawawatendei waume zao haki na Mungu pia, kwa kutomtendea mumeo haki yake kwa kugawa penzi ambalo ni haki ya mumeo na kumpa mwanaume mwingine nakuambia ukweli amani itatoweka tu kwenye hiyo ndoa yako mama, na kuirudisha unahitaji kugharamia sana. Haki ina taka hivi 

“Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (EBR 13:4) 

Haki imeagiza ndoa na iheshimiwe na watu wote, wewe mwanaume ni mtu, na wewe mwanamke ni mtu, kila mmoja amegizwa ahakikishe hafanyi uzinzi, ona jinsi wewe ndugu yangu leo hii ulipoangukia, umesukumia haki mbali, kwa kutoiheshimu ndoa yako kwa kuzini na mwanamke mwingine na hata wewe mwanamke umefanya hivyo hivyo, sikiliza, Mungu atakuadhibu, kwa nini atakuadhibu? Kwa sababu umeikataa haki, haki ndio utaratibu wa serekali yake, wewe umeikataa isikutawale, umekubali kutawaliwa na ufalme wa giza, ndio maana wewe mwenyewe umepoteza furaha, amani, hata matumaini ndani ya moyo wako.  

Sikiliza mpendwa, leo unao uwezo wa kuanza maisha mapya yaliyojaa matumaini au mwangaza wa nuru mpya kutoka mbinguni katika ndoa yako hiyo kwa kufanya jambo moja tu. Nalo ni hili, omba ufalme wa mbinguni uje kwenye ndoa yako! Mwambie Mungu aje aitawale ndoa yako, usiogope, TUBU. Mruhusu aje sasa hivi, atakusamehe, na ataanza kuitawala hiyo ndoa yako, acha mambo yote uliyokuwa unayafanya ambayo hayakuwa ya haki. Anza kumtendea mkeo au mumeo matendo ya haki, mwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wako, mpokeeni Yesu katika mioyo yenu kwa imani, nawaambia ukweli ndoa yenu ndipo itakapopata amani na usalama mkubwa sana, fanyeni maombi, sameheaneni, haki ikitawala itataka kuona kila mmoja wenu akimsamehe mwezie pale alipomkosea na atakapomkosea. Haki ikiwatawala itawatengenezea ndani ya mioyo yenu moyo wa toba, kila mmoja wenu atakuwa tayari kumwambia mwenzie nimekosa, mwanaume utakuwa tayari kumwambia mkeo nisamehe, nimekukosea, na mwanamke pia utakuwa tayari kumwomba mumeo msamaha mahali pale ulipomkosea. Na muwe tayari kusamehana. Haki inavyotaka nyinyi wana ndoa mfanye kila siku kama mnataka Mungu awatawale. 

“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali barikini; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.” (1PETRO 3:7-9) 

Ndugu yangu nakusihi sana usikiapo maneno hayo, yaweke kwenye matendo. Mruhusu Mungu awatawale kwa kuuleta ufalme wake, pia kubalini kuishi sawasawa na utaratibu uliomo ndani ya Ufalme wa Mungu ambao ni HAKI. Tendeaneni matendo ya haki, hapo haki itatenda kazi ya kuleta amani, na itazaa furaha, matumaini mapya na utulivu katika ndoa yenu. Mungu awabariki sana. 

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila