Salamu – Octoba, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe. Ninakukaribisha tena katika eneo hili la salamu za mwezi. ili tupate kujifunza somo hili muhimu. Mungu ametupa mwezi huu wa kumi tunamshukuru sana.

Hizi ni salamu za mwezi wa kumi Kumbuka tunamfululizo wa salamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

JAMBO LA TISA JIFUNZE KUOMBA REHEMA ZA MUNGU JUU YAKO NA JUU YA TAIFA NA JUU YA ULIMWENGU. ( HII NI AJENDA MUHIMU MNOO)

Unaweza kujiuliza rehema maana yake nini? Rehema ni tendo la kumuwezesha au kumchukulia mtu asiye na sifa za kusaidiwa au kuchukuliwa.

Kuna maneno mawili yamefanana. Neno Rehema na neno huruma. Ila yanasifa tofauti. Unaweza kumhurumia mtu lakini usimsaidie. Rehema ndani yake inahuruma inayowezesha au kuachilia.

Moja ya jambo muhimu mno unalotakiwa ulishughulikie ni hili la kumuomba Mungu sana aachilie rehama zake kwako,kwa taifa,kwa ulimwengu ili aondoe tauni aliyoileta.

Sikia Mungu anatabia ya ku rehemu watu. Ndani ya hiyo rehema ndiko kumefungwa nguvu ya kuzizuia hasira za Mungu ili zisiwaangamize wanadamu.

Rehema ya Mungu ikiachiliwa mahali fahamu hasira ya Mungu huondolewa. Kwasababu ndani ya rehema za Mungu kuna kusamehe,kuwezesha au kusaidia nk.

Ngoja nikupe mfano huu labda utanielewa nina maana gani. Haujawahi kuona mtu haombi kwa Mungu lakini Mungu anampa huyo mtu vitu?

Au haujawahi kuona mtu hana imani kabisa ya kupokea uponyaji kwa Mungu. Lakini ghafla Mungu anamponya wakati hata hajaomba? Ukiona hivyo unatakiwa ujue kuwa kilichopelekea apewe huyo mtu ingawa hakua na imani ni rehema za Mungu.

Mungu anapokasirika kinachoweza kumzuilia hasira yake ni rehema zake tu. Akiizuia hiyo rehema yake, fahamu hasira zake huwa zinakua kali sana.

Mwimba Zaburi huyu alilijua hili ninalokuambia ndiyo maana alisema hivi “Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa? Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote? Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema “(Zaburi 55:7-9)

Mungu anapoizuia rehema yake kwa watu,fahamu hasira yake huwa ni kali mnoo,atawaua watu wengi kwa dakika moja tu. Kinachomzuia hiyo tabia yake rehema. Akiikomesha tu rehema yake kwetu nakwambia kutokana na uovu tulionao hakuna atakaye pona.

Angalia mistari hii uone kinachomfanya Mungu atembee na sisi kila siku ni rehema zake tu. Hizo rehema ndizo zinazomfanya atusamehe huku akijua kabisa kuwa sisi ni waongo na watu wabaya tu hata tunapotubu tunakua waongo tu yaani tunamdanganya.

“Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi.”(Zaburi 78:34-39)

Ukiona Mungu anakutazama fahamu kinachomsababishia akutazame si kwasababu unahaki sana, ni kwasababu moja tu ya rehema zake. Angalia mistari hii.

“BWANA, akaniambia, Israeli mwenye kuasi amejionyesha kuwa mwenye haki kuliko Yuda mwenye hiana.Enenda, ukatangaze maneno haya kuelekea upande wa kaskazini, ukaseme, Rudi, Ee Israeli mwenye kuasi, asema BWANA; sitakutazama kwa hasira; maana mimi ni mwenye rehema, asema BWANA, sitashika hasira hata milele. Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi BWANA, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema BWANA.”(Yeremia 3:11-13)

UNAWEZA KUMUOMBA MUNGU REHEMA

Unaposoma maandiko matakatifu unaona wazi kuwa tunaweza kumuomba Mungu aturehemu. Maandiko yanasema hivi.

“Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.”(Zaburi 55:1)“

Angalia na mistari hii mingine” ..ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.”(Daniel 2:18)

Kwa mujibu wa hiyo mistari unaona rehema inaweza ikaombwa. Jifunze kuomba Mungu aachilie rehema zake juu yako au juu ya ukoo wako au juu ya taifa lako nk katika kipindi cha hasira zake.

Muombe akumbuke rehema zake anapoachilia adhabu, rehema hiyo ikija juu yako au taifa nk fahamu ndiyo wokovu wako utakapotokea.

Umewahi fikiri hivi, mfano tauni ya corona inaenezwa pia kwa kushikana, au kushika mahali penye vijidudu hivyo au kwa hewa nk. Fikiria kidogo, unaponaje? Hapo tunahitaji rehema za Mungu tu.

Ndiyo hapo unaona watu wawili wamepata woote tauni mmoja anapona mwingine anakufa kisa mmoja rehema za Mungu zipo juu yake na mwingine rehema za Mungu hazipo.

Ebu anza kumuomba Mungu sana katika kipindi hiki aachilie rehema zake katika ulimwengu. Ndipo hasira yake itazuiliwa. Maandiko yanasema huruma zake na rehema zake ndizo zinazo tufanya tusiangamie.

Angalia mistari hii. “Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.”(Maombolezo 3:22).

Naamini umenielewa. Mungu akusaidie kuomba maombi ya mfumo huu kila mara.

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.