Salamu – Septemba, 2021

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninakukaribisha tena ndugu yangu katika kona hii ya salamu za mwezi.

Nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu ambaye ametutunza Mimi na familia yangu na kutupigania na kutupa mwezi huu wa tisa.

Mwezi huu Nimekuletea mfululizo wa salamu zetu kwako zenye kichwa.

VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

Mwezi uliopita tuliangalia salamu zilizokua ndani yake tukiangalia eneo lile la maana mbili za kusikia.

Hebu tusogee mbele kidogo jambo

F: KUSIKIA KWA KUPITIA SAUTI YA NDANI AMANI NA FURAHA

Unaposoma Biblia unajifunza kuwa Mungu anaweza kukuongoza au kukusemesha kwa kupitia sauti ya ndani ambayo ni furaha na amani.

Angalia mistari hii. “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.” (Wakolosai 3:15).

Ukiipitia hiyo mistari unaona hapo kuna neno zito kidogo liitwalo amani. Amani hiyo iliyopo hapo ukiitazama ndani yake inanguvu ya kufanya maamuzi ya mtu. Sikiliza, amani hiyo si amani ya mtu, ni amani ya Kristo. Lazima utofautishe amani ya mtu na amani ya Kristo. Ukisoma Biblia unaona kuna amani ya Kristo aliyotupa.

Angalia mistari hii uone. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” (Yohana 14:26-27).

Ukiisoma mistari hiyo unaona hapo Bwana Yesu Kristo amesema kuwa ameamua kutupatia kitu cha muhimu mnoo ambacho ulimwengu hauwezi kutoa. Nacho ni Amani yake. Biblia inatufundisha kuwa Bwana Yesu Kristo ndiye mfalme wa amani “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” (Isaya 9:6).

Huyu Bwana Yesu Kristo ndiye mfalme wa amani, kwa maana nzuri anayo amani yake, amani yake hiyo imebeba mambo mengi mnoo; moja ya kikichobebwa ndani ya hiyo amani yake ni sauti yake Mungu.

Sikia, Sauti hiyo ya Mungu iitwayo amani ndiyo itakayokupatia wewe muongozo kwenye maeneo ya maamuzi yako unayotaka kuyaamua. Watu wengi hawajui kazi ya amani ya Kristo ni nini. Wengi wanajua eneo moja tu la kuwafanya wasiwe na magomvi.

Sikia amani hii ukiitazama ni Roho Mtakatifu ambaye ana tabia ya kutusaidia na kutuongoza, sasa Roho Mtakaifu anayo sauti yake ya kukuongoza ambayo ni amani moyoni mwako.

Biblia inasema hivi. “Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima iashara vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.” (Isaya 55:12).

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona vitu viwili ambavyo vinaweza beba sauti ya Mungu ya kukuongoza. Navyo ni amani na furaha. Ukiona unataka kufanya jambo lolote na ukakosa amani nakushauri liache kwanza. Fahamu hiyo ni sauti ya Mungu kuwa jambo hilo haliko sawa.

Mfano wewe ni mfanya biashara unataka kufanya biashara fulani na ukapanga kuifanya yaani ukaanza hatua za kuifanya na ukakosa vitu hivyo viwili yaani amani na furaha nakushauri tulia!

Au ukakipata kimoja, mfano ukawa na amani na jambo hilo, lakini ukashangaa ulipoanza kulifanya tu ukakosa furaha nakushauri tulia. Jambo hilo ni kweli Mungu anataka ulifanye ila kuna sehemu unakosea. Rudi jipange upya kwa sababu Mungu amesema na wewe kwa kupitia sauti yake iliyobebwa kwenye amani na furaha.

Biblia inasema hivi “Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.”(Isaya 57: )

Ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu au mtu wa Mungu Ukitaka ujue kuwa hilo unalolifanya ni baya na Mungu halipendi wewe angalia amani moyoni mwako ilivyo.

G: ISHARA YA MOYO KUWAKA

Sauti nyingine ya kuwa Mungu anasema na wewe ni hii ya kuwaka moto moyoni mwako. Sikia ukiona kuna mtu anasema na wewe iwe ushauri, fundisho, au mahubiri n.k. na moyoni mwako ukaona moto ukiwaka fahamu Mungu anasema na wewe kwa kupitia huyo mtu. Au ukiona umepokea wazo lolote moyoni na ukashangaa ukaona moto au moyoni kuna waka kama moto fahamu Mungu anasema na wewe kwa kupitia hilo wazo.

Angalia mistari hii uone. “Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.” (Luka 24:30-34)

Bwana Yesu Kristo alipokua akisema nao hao watu mioyo yao ilikuwa ikiwawaka bahati mbaya hawakuijua hiyo sauti iliyowapa ishara ya moto moyoni mwao.

Yeremia anasema hivi “Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.” (Yeremia 20:9).

Yeremia alikutana na ishara hii ya moto ikimuongoza mwilini mwake kuwa inatakiwa amtaje au aendelee kumtumikia Mungu. Ishara hii ni sauti inayokupa wewe taarifa kuwa kuna kitu umekiacha ambacho Mungu alitaka ukifanye.

Hebu angalia mifumo hii niliyokuonyesha inaweza kubeba sauti ya Mungu kwa ajili yako, kanisa, taifa, n.k. Omba Mungu akufunulie masikio yako ya ndani ili uisikie sauti hii.

Naamini umenielewa.. tuonane mwezi ujao katika kona hii mwezi ujao.

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
    • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
    • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
  9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.