Salamu – Mei, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe,

Tunamshukuru sana Mungu ametupa siku nyingine ya mwezi huu wa tano.

Tunamshukuru sana Mungu kwa mwezi uliopita tulipokuwa na semina nzuri sana pale Bethania Mbalizi. Tunamshukuru sana Mungu kwa kutupa neema hii ya kutupatia salamu za mwezi huu.

Kumbuka tunalo kichwa cha salamu hizi:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA UNABII ILI UPATE KUFANIKIWA KIROHO WEWE NA WATU WENGINE (SEHEMU YA KWANZA).

Hebu tuendelee mbele kidogo:


3: NJIA YA TATU AMBAYO MUNGU ANAWEZA KUSEMA NA MTU – AMANI NA FURAHA MOYONI

Sikia sauti nyingine ambayo Mungu anaweza kuitumia kusema na mtu ili kumpa mwongozo au namna ya kufanya maamuzi, nayo ni amani na furaha moyoni.

Angalia mistari hii:

“Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.” (Wakolosai 3:15).

Kwa mujibu wa mstari huu, utaona amani inayotajwa hapo ni amani inayoweza kukuwezesha wewe kufanya maamuzi. Amani hiyo si ya mtu, bali ni amani ya Bwana Yesu Kristo.

Sikia, unaweza kutaka kufanya jambo fulani, ukashangaa ghafla huna amani moyoni mwako au rohoni mwako.

Ukiona umekosa amani, usifanye maamuzi haraka. Rudi kwa Mungu, muombe akusaidie ujue ni kwa nini umekosa amani. Usishangae, Mungu hakutaka ufanye jambo hilo kwa wakati huo. Muda ukifika, utashangaa jambo hilo hilo ulilotaka kufanya linakupa amani. Hapo lifanye.

Ukiona kila ukilifikiria jambo hilo unakosa amani, nakushauri usilifanye.
Angalia mistari hii:

“Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani; mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; na miti yote ya kondeni itapiga makofi.” (Isaya 55:12).

Sikia, Mungu anaweza kukuongoza kwa kutumia amani na furaha. Mungu anaweza kutumia amani na furaha kukupa mwongozo wa jambo unalopaswa kufanya.

Ukiona kuna jambo ambalo wengine wanalifanya, lakini wewe umekosa amani na furaha moyoni, fahamu Mungu amekukataza. Nenda kamuombe.

Pia kama kuna jambo baya, yaani hatari kwa ajili yako au ndugu zako, inaweza kuwa ni ishara kwamba Mungu anakupa tahadhari kuwa jambo haliko sawa. Kaliombee. Omba mpaka uone amani moyoni imeludi.

Jambo hilo linaweza kukaa moyoni kwa muda mrefu au siku nyingi. Liombee, tenga muda uliombee. Usiishie kushangaa; unaweza kuomba na kulia sana bila kujua ni kwa nini una huzuni hiyo.

Angalia mfano huu:

“Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.” (2 Wakorintho 7:8-11).

Mungu anaweza kutumia sauti ya namna hii – akiondoa amani moyoni na ukajikuta una huzuni bila kujua sababu. Mungu akikupenda na akitaka uingie kutubu, fahamu ataondoa amani na furaha moyoni. Ukikutana na hali hiyo, inawezekana kuna dhambi umefanya na hujui, au unaijua ila umeificha. Mungu atakuletea sauti ya namna hii ili utubu. Ukitubu tu, amani inarudi moyoni.

Watu wengi waovu, kiukweli, hawana amani. Hiyo ni sauti ambayo Mungu anawaambia kila siku watubu.
Angalia mistari hii:

“Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.” (Isaya 57:21).

Ukiwa mtu mbaya, fahamu huwezi kuwa na amani. Utaijaribu kuitafuta, lakini huwezi kuipata mpaka utubu.

Naamini umeelewa.


Tuonane tena katika kona hii ya salamu za mwezi.


UKIHITAJI MASOMO YETU UNAWEZA KUYAPATA KWA NJIA HIZI ZIFUATAZO:

  1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” – utaipata Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

  2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org.

  3. YouTubeMwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

  4. Facebook – Ingia katika tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), “like” na utapata maelezo ya kujiunga; au andika “SOMA NENO LA MUNGU” moja kwa moja kwenye Facebook.

  5. Instagram – Tafuta “Steven Mwakatwila”.

  6. DVDs au CDs.

  7. Vitabu – Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata vitabu, DVD na CD.

  8. Kwa njia ya Redio – Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:

    • Rungwe FM 102.5 – Kila Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.

    • Baraka FM 107.7 – Kila Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.

    • Bomba FM 104.1 – Kila Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
      Unaweza pia kutusikiliza kwenye Online Radio yetu: radio.mwakatwila.org.

Kwa mawasiliano zaidi, tupigie: +255 754 849 924 au +255 756 715 222.

Wako:
Mwl. Mr & Mrs Steven Mwakatwila.