Salamu – Septemba, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana,

Ninakukaribisha sana katika kona hii ya salamu za mwezi. Katika mwezi uliopita tulikuwa na semina huko Kigoma, Katavi, Rukwa na Sumbawanga.

Tunawashukuru sana kwa maombi yenu. Tulikutana na tatizo kwenye lori letu. Wakati tunaenda Kigoma, lilichelewa sana kufika kule. Kule tukafanyia semina kiwanjani kwa kukodi hema, viti na vyombo.

Tulikutana na mambo mengi sana magumu. Afya yangu nayo ilileta tatizo. Lakini unajua, Mungu alinitia nguvu na kuniwezesha kufundisha nikiwa na hali hiyo.

Tukaanza Katavi. Lori letu liliwahi kufika hapo, kwa hiyo vifaa vyote kama hema, madhabahu, viti na vyombo vilifika. Tukawa na semina nzuri sana. Tukaenda Sumbawanga vizuri sana.

Tulipoelekea Songwe – Tunduma, gari letu, yaani lori, likaleta shida. Ilibidi tena tukodi hema, vyombo na viti. Hata hivyo, tulikuwa na semina nzuri sana.


HEBU TUANZE KUPOKEA SALAMU ZA MWEZI WA TISA

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA UNABII ILI UPATE KUFANIKIWA KIROHO WEWE NA WATU WENGINE (SEHEMU YA KWANZA)

TAFUTA HEKIMA YA NAMNA YA KUUTOA UNABII

“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye.” (Waefeso 1:17)

Kwa mujibu wa mstari huo tunaona moja ya jambo la kuomba, linalokusaidia katika mambo ya ufunuo (yaani unabii), ni hekima.

Mfano, hekima itakusaidia kupata muongozo mzuri: huu unabii upelekwe wapi, kwa nani, muda upi, wapi usiseme na wapi useme. Pia utumie sauti ipi kutoa unabii.

Watu wengi sana wanapokea unabii, lakini kwa sababu ya kukosa hekima unabii huo haupokelewi na watu.

Mfano: umepewa unabii wa kuonya au kuongoza, lakini mtu anajitengenezea ukali au kubadilisha sauti yake ili watu waogope. Kwa mtindo huo huwezi kupokelewa. Kwanza umedanganya watu, maana hiyo siyo sauti yako, umeiga. Hivyo unabii unaoutoa watu watajua tu kuwa umeiga.

Usimwambie kila mtu kile ulichokiona na kukisikia. Unaweza kumwambia mtu mbaya akakutesa au kukupinga mno, kama ndugu zake Yusufu walivyomfanyia. Yusufu aliota ndoto, akawaambia ndugu zake, wakataka kumuua.

Kwa hiyo omba Mungu akupe hekima ili ujue namna ya kutoa na kuupokea unabii.

Ngoja nikupe mfano:
Ukipata unabii wa kuwaonya viongozi, wawe wa kanisa au wa serikali, lazima uwe na hekima. Unabii huo ukiupeleka bila hekima utapata shida sana.

Angalia mfano wa nabii Nathani.
Nabii alipokea unabii unaomhusu mfalme Daudi, akapata hekima ya namna ya kuzungumza na mfalme.

“Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja mdogo, ambaye amemnunua na kumlea… (soma 2 Samweli 12:1–13).”

Ukiisoma mistari hii utaona namna Nathani alivyokuwa na hekima. Kama angekuwa hana hekima, angeenda kichwa kichwa, yangemkuta mambo kama yaliyomkuta Yohana Mbatizaji alivyokatwa kichwa.


Ebu tuishie hapo.
Tuonane katika salamu za mwezi ujao. Mungu akubariki sana.


UKIHITAJI MASOMO YETU, UNAWEZA KUYAPATA KWA NJIA HIZI ZIFUATAZO:

  1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” – utaipata Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

  2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org.

  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

  4. Facebook – Ingia katika tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), “like” na utapata maelezo ya kujiunga; au andika “SOMA NENO LA MUNGU” moja kwa moja kwenye Facebook.

  5. Instagram – Tafuta “Steven Mwakatwila”.

  6. DVDs au CDs.

  7. Vitabu – Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata vitabu, DVD na CD.

  8. Kwa njia ya Redio – Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:
    Rungwe FM 102.5 – Kila Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
    Baraka FM 107.7 – Kila Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    Bomba FM 104.1 – Kila Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

    Unaweza pia kutusikiliza kwenye Online Radio yetu: radio.mwakatwila.org.

Kwa mawasiliano zaidi, tupigie: +255 754 849 924 au +255 756 715 222.


Wako:
Mwl. Mr & Mrs Steven Mwakatwila