Salamu – Disemba, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana.

Pole na kazi zote. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mwezi huu wa kumi na mbili. Pia tunamshukuru Mungu kwa mwezi uliopita ambapo tulikuwa na semina nzuri ya watumishi wa Mungu.

Tulikuwa na wachungaji, waalimu, mitume, wainjilisti, na viongozi wakuu wa kanisa kama maaskofu na wenyeviti. Tunamshukuru sana Mungu kwa mafanikio ya semina hiyo.

Pia tunamshukuru sana Mungu kwa kuipitia Tanzania katika jaribu kubwa la ugomvi nchini. Mpaka leo tupo salama, tunamshukuru sana Mungu kwa kutuvusha. Usiache kuiombea nchi yako.

Katika mwezi huu wa kumi na mbili, tunatarajia kuwa na kambi ya maombi tarehe 28–31/12/2025, ambayo itafanyika katika viwanja vya Mbeya Day Secondary School.

Karibuni sana. Ukija, utapewa malazi na chakula. Nauli ni ya kwako.


UTANGULIZI WA SOMO

Tuendelee kuzipokea salamu za mwezi huu zenye kichwa kisemacho:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)

Ebu tusogee mbele kidogo.


KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI INAWEZA KUFANYA MAMBO MENGI

Unaposikia karama ya miujiza, usifikiri ni mambo machache tu. Watu wengi hawaamini mambo mengi ambayo Mungu anaweza kuyatenda kwa kuwatumia wanadamu.

Unapotaka Mungu akupe karama ya miujiza, usifikiri ni mambo ya kawaida au machache. Watu wengi walioko kanisani leo hupata shida wanaposikia au wanapoona miujiza ikitendwa na Mungu.

Moja ya sababu inayomfanya Mungu asitende miujiza mingi ni kwa sababu ya kutokuamini kwa watu.

Biblia inasema:

“58 Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.”
(Mathayo 13:58)

Hii inaonyesha wazi kuwa kutokuamini kunazuia miujiza.

Watu wengi wanapoona miujiza, badala ya kumtukuza Mungu, hukimbilia kumhusisha shetani. Lakini Mungu anaitafuta imani yako ili atende miujiza kupitia maisha yako.

Watu wengi wana imani kubwa katika nguvu za shetani, lakini ukweli ni kwamba Baba wa mbinguni ndiye mwenye nguvu zote na ndiye bingwa wa miujiza.

Mimi binafsi katika maisha yangu nimemuona Mungu akitenda miujiza ambayo si rahisi kuamini hata ukiisimulia kwa mtu. Wengine wanaweza hata kusema si kweli au ni jambo lisilo la kawaida.

Kanisa likikosa miujiza, fahamu kuwa linakuwa dhaifu kiroho. Tutajifunza zaidi mbele ili kuelewa kwa nini Mungu anataka kufanya miujiza.

Mungu ni Mungu wa maajabu, na anataka kufanya miujiza katika maisha ya watu wake.

Anza kujenga imani kuwa Mungu anaweza kutenda miujiza mikubwa, hata inayoweza kuwashangaza watu wengi.


MUNGU ANAWEZA KUMPA MTU KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI KWA MAPENZI YAKE

Unaposikia kuhusu karama za Rohoni, fahamu kuwa Mungu humpa kila mtu kulingana na mapenzi yake.

Biblia inasema:

“10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”
(1 Kor 12:10–11)

Mistari hii inaonyesha kuwa Mungu ndiye anayegawa karama kama apendavyo.

Katika Biblia tunaona watumishi wakubwa kama Samweli, Yohana Mbatizaji, na Yeremia, ambao hawakuonekana sana wakifanya miujiza, lakini walikuwa watumishi wakubwa wa Mungu.

Hii inaonyesha kuwa unaweza kumtafuta Mungu akupe karama ya miujiza na uponyaji, lakini Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.


UPONYAJI KUPITIA IMANI YA KILA MWAMINI

Pia ni muhimu kuelewa kuwa kuna uponyaji unaopatikana kupitia imani ya kawaida ya Mkristo.

Biblia inasema:

“16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;”
(Marko 16:16–17)

Mistari hii inaonyesha kuwa kila anayeamini anaweza kuwa chombo cha uponyaji kupitia imani.

Ili imani ya uponyaji ikue:

  • Jifunze kusikiliza mafundisho ya uponyaji

  • Usiogope kuwaombea wagonjwa

  • Endelea kumwamini Mungu

Utaona watu wengi wakipata uponyaji.


HITIMISHO

Naamini umeelewa somo hili.

Ninakutakia umalize mwaka huu vizuri, na Mungu akutunze sana katika mwaka ujao.


JINSI YA KUPATA MASOMO YETU

Unaweza kupata masomo yetu kupitia njia zifuatazo:

1. App ya HUSONEMU (MWAKATWILA)
Inapatikana Play Store, ikiwa na masomo mengi.

2. Tovuti:
www.mwakatwila.org

3. YouTube:
HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

4. Facebook:
Tafuta: SOMA NENO LA MUNGU

5. Instagram:
Huduma ya Soma Neno la Mungu

6. DVDs au CDs

7. Vitabu
Wasiliana: +255 763 109 733


REDIO

Rungwe FM 102.5 MHz
Jumapili saa 3:00 – 4:00 usiku

Baraka FM 107.7 MHz
Jumanne saa 12:00 jioni – 1:00 usiku

Bomba FM 104.1 MHz
Ijumaa saa 3:00 – 4:00 usiku


ONLINE RADIO

radio.mwakatwila.org

Ratiba:

  • 12:00 Asubuhi

  • 07:00 Mchana

  • 12:00 Jioni

  • 03:00 Usiku


MAWASILIANO

+255 754 849 924
+255 756 715 222


Wako katika Kristo,
Mwl Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila