Salamu – Novemba, 2021

SALAMU ZA MWEZI WA KUMI NA MOJA 2021

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nichukua nafasi hii kukukaribisha ndugu yangu katika eneo hili la salamu za mwezi.

Tunamshukuru Mungu muumbaji aliyetupa nafasi hii ya kuuona tena mwezi huu wa kumi na moja. Naamini Mungu amekupigania katika mambo mengi mnoo. Hebu jiachie kwake atakutunza na kukupigania.

Hebu tuanze kuziangalia salamu za mwezi huu wa kumi na moja. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa. VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

Katika salamu za mwezi uliopita tuliangalia lile eneo la SABABU ZINAZOWEZA KUPELEKEA MTU ASILITENDEE KAZI LILE ASIKIALO

Tuliangalia lile eneo la hofu. Na tuliangalia hofu ya kwanza ni kuwaogopa watu.

Hofu nyingine inayoweza kukupelekea wewe ndugu ushindwe kuwa mtii wa neno la Mungu ni hofu hii

B. KUOGOPA KUKOSEA

Watoto wa Mungu wengi hawapendi kukosea na hujitahidi mnoo kuona hawakosei, hili ni jambo zuri mnoo. Lakini jambo hili linaweza kumtengenezea mtu huyo kosa la kutokuwa mtii wa maagizo ya Mungu na akaingia katika kundi lile watu waitwao wasio sikia.

Watu wengi huogopa kufanya mambo ambayo Mungu anawaelekeza kisa ni kuogopa, huwa wanajiuliza swali hili Je! LISIPOTOKEA? Nikikosea je! Itakuaje?

Fikiria wewe ni mtumishi wa Mungu na upo mahali unaendesha semina au unahubiri injili nk. Na Mungu anakuambia waite watu wa kuokoka wapo hapa leo.

Na kiukweli kwa macho yako wewe unaona kama watu hao ni wagumu mnoo na ulipokua ukiwahubiria hukuona dalili yoyote ile ya kuwa wanapokea ujumbe wako huo, unajua ni rahisi sana kuogopa kuitii sauti ya Mungu kwasababu ya hofu ya kutokutokea hicho ulichoambiwa ukifanye.

Mara nyingi huwa tunaangalia mazingira na kujijengea mioyoni mwetu fikra mbovu kuwa huenda sijasikia vizuri kweli hili jambo linawezekana? Ni Mungu huyu anayeniambia jambo hili?

Hebu angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;” (Mwanzo 12:1-2).

Hebu fikiria kidogo, Ibrahimu alipoambiwa atoke katika nchi yake na aende katika nchi atakayo onyeshwa na Mungu usifikiri lilikua ni jambo jepesi. Fikiria Mungu hakumwonyesha Ibrahimu ile nchi, ila alimwambia toka na ntakuonyesha.

Unajua ni rahisi kutokutii kwa kisingizio cha kumuuliza Mungu swali unataka niende wapi? Siendi mpaka uniambia unapotaka niende, kwa kuwa sijui huko inchi iliko nikikosea je?

Ibrahimu alipojitokea na Kuingia nchi ya Kanani na kufika Shekemu ndipo alipotokewa na Mungu na kuambiwa nchi atakayopewa ni hiyo. “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea.” (Mwanzo 12:5-6).

Ibrahimu aliposikia sauti ya Mungu alitiii bila kuogopa kukosea, akatoka akaanza safari mpaka alipofika hapo ndipo Mungu akamwambia ni nchi hiyo aliyokusudiwa kumpa.

Mara nyingi Mungu hutuambia mambo na kwa kweli swali la kwanza tunalokutana nalo ni hili la je! Ni Mungu kweli? Je Nikikosea itakuaje?

Sikiliza ukiamini kuwa Mungu kakuambia ufanye jambo furani wewe anza kulifanya. Mungu kama si yeye aliyekuambia ulifanye fahamu atakuambia tu kuwa si yeye aliyekuambia ufanye hivyo, kumbuka zile ishara za sauti ya Mungu kwa kutumia amani yake au furaha yake vitu hivyo vitakuongoza na kukupa dira kuwa ni Mungu au si Mungu.

C. KUOGOPA KUPOTEZA.

Hofu nyingine ambayo inaweza kuwa kizuizi cha kulitendea kazi lile ambalo Mungu anakuambia ulifanye ni hii ya kupoteza. Sikia, kuna vitu Mungu anaweza kusema nawe uvifanye na ambavyo vitakupelekea upoteze vitu vingine ulivyokua navyo. Angalia Mfano huu tena wa Ibrahimu alipoambiwa atoke, kuna vitu ambavyo Ibrahimu katika utii wake alivipoteza na alikubali kupoteza, navyo ni jamaa zake na marafiki zake na mali kama ardhi nk.

Angalia mistari hii “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;” (Mwanzo 12:1)

Watu wengi wamejikuta leo wameingia kwenye kundi la watu waitwao wasiosikia kwa sababu ya hofu ya kulitenda lile Mungu anawaagiza walifanye ndani yake limebeba kupoteza vitu vyao. Mungu anaweza kukuambia neno la kuacha kufanya jambo ambalo wewe unaliona ndiyo linalokuingizia kipato ni rahisi mno kujikuta huitii sauti yake kwa sababu ya kuogopa kwako kupoteza hicho kipato unachokiingiza kwenye hiyo kazi uifanyayo.

Ngoja nikwambie ukweli kuna wanawake hawawezi kwenda mbinguni leo kisa hawawezi kuwaacha waume ambao kiukweli si halali kabisaa kwao. Kwa sababu hao wanaume wanawatunza na kuwalelea watoto basi hawawezi kumfuata Bwana Yesu Kristo kisa wanaogopa wakimtii tu, kitakachotokea ni kuachwa na hao wanaume. Haujawahi kumsikia mtu anasema mimi natamani niwe Mkristo, lakini naogopa nitatengwa na familia yangu yote? Unajua kinachosababisha asifanye hivyo ni kuogopa kuipoteza familia yake hiyo.

Bwana Yesu Kristo anasema hivi; “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.” (Mathayo 16:24-25).

Ukiipitia hiyo mistari utanielewa ninapokuambia kuwa jambo lingine linaloweza kuwa chanzo cha watu kutokuwa watii wa sauti ya Mungu ni hili la kupoteza kile walichonacho. Mungu anaweza kukuambia toa kitu furani , lakini ukagoma kisa unaogopa tu kupoteza hicho kitu…

Sababu ya Pili inayoweza kupelekea mtu asisikie au kutii sauti ya Mungu ni hii

2: MAGUMU AU TESO JIADHARI NA UCHUNGU

Magumu husababisha uchungu na mtu akiwa na uchungu mara nyingi hujikuta hawezi kusikiliza kile watu wanamwambia au kile Mungu anamwagiza akifanye.

Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia. “Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu.” (Kutoka 6:9).

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona kilichopelekea watu hao kutokuitii sauti ya Mungu kupitia mtumishi wake Musa ni hiki cha uchungu ulikua moyoni mwao. Uchungu huletwa na umivu furani, inawezekana ni mfumo wa maisha,kuteswa,au kufiwa au kuugua au kupoteza vitu kunenewa mabaya nk.

Sasa sikia, ukiwa ni mtu mwenye kuhifadhi uchungu moyoni ni ngumu mnoo kumsikiliza Mungu asemapo na wewe na ni ngumu kutii kile Mungu anakuagiza ukifanye.

Angalia mifano hii uone. Angalia mistari hii “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” (Mathayo 26:36-39)

Gumu lililomletea Bwana Yesu Kristo huzuni moyoni lilitaka kumfanya asilifanye lile Mungu anataka alifanye ila alishinda. Huzuni huleta uchungu moyoni na kufadhaika na kukata tamaa pia. Bwana Yesu Kristo alijua nini mapenzi ya Mungu, lakini kulikua na jambo lililomuuzunisha mnoo kiasi akaomba kikomba hicho kimuepuke.

Unajua Bwana Yesu Kristo alijua kabisa kuwa akiichukua dhambi yetu sisi na ulimwengu atatengana na Mungu, na hilo jambo la kupoteza Baba yake lilimletea huzuni kubwa.

Hata kwako inawezekana umekua na uchungu na huzuni kubwa kisa umempoteza baba yako au mama yako au rafiki, kiasi ambacho unahuzuni kubwa moyoni inayokupelekea masikio yako yazibe au hutaki kuyatenda yale ya Mungu kisa uchungu.

Mfano unaweza kuumizwa na mume,rafiki,mke nk na Mungu amesema samehe na umpende huyo mtu, unajua usipoondoa uchungu na huzuni uliyonayo kwa kuumizwa na huyo mtu utajikuta huwezi kumsamehe huyo mtu na hata kumpenda tena.

Petro alipokutana na gumu alimkana Bwana Yesu Kristo mara tatu. Wakati anamjua kabisa Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye mwokozi wake na ni masihi wa Mungu.

MFANO WA UTUMISHI KUPITIA MAGUMU NA MAGUMU HAYO YATAKUTENGENEZEA UCHUNGU NA KUTOKUMTII MUNGU.

Unaweza kuitwa kabisa umtumikie Mungu mahali nk, lakini kutokana na magumu unayoweza kukutana nayo ni rahisi ukaliacha lile neno ulilolisikia la kumtumikia Mungu kwa nafasi aliyokupa.

Biblia inasema hivi angalia mistari hii. “Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu.Je! Mtu aweza kuvunja chuma, naam, chuma kitokacho kaskazini, au shaba? Mali yako na hazina zako nitazitoa kuwa nyara, bila kulipwa thamani yake; naam, kwa sababu ya dhambi zako zote, hata katika mipaka yako yote.Nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana moto umewashwa katika hasira yangu, utakaowateketeza ninyi. Ee BWANA, unajua wewe; unikumbuke, unijilie, ukanilipie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na mashutumu.Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi.Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.” (Yeremia 15:10-21)

Nabii Yeremia aliumizwa mnoo, na umivu lile lilipelekea uchungu moyoni mwake, na akajikuta ameacha kulifanya lile Mungu alitaka alifanye. Mungu alimwambia ukiludi, maana yake Yeremia aliondoka kwenye kusudi la Mungu. Na lililomuondoa ni magumu yaliyomletea huzuni na uchungu moyoni.

Biblia inatuagiza hivi “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.” (Ufunuo 2:10-11).

Mtumishi unapohifadhi moyoni uchungu fahamu uchungu huo utakufanya usiwe mtii wa maagizo ya Mungu, ondoa uchungu moyoni utaanza kumsikia Mungu

MUNGU ANATUKATAZA TUSIWE NA UCHUNGU WA KUKAA.

Moja ya agizo tuliloagizwa na Mungu ni hili la kutokuwa na uchungu wa kukaa moyoni mwetu. “Muwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe ibilisi nafasi.” (Waefeso 4:26)

Sikia usiukalishe uchungu moyoni mwako, kuna hasara nyingi utakutana nazo ukiwa ni mtu wa kuhifadhi hasira na uchungu moyoni, mojawapo ya hasara nii MTU ALIYEJERUHIWA MOYONI HASIKII.

Watu wengi waliokutana na magumu na mioyo yao ikaingia uchungu hawawezi kusikia, masikio ya ndani huziba. Wafuatilie watu waliofiwa, au waliokataliwa, wenye madeni makubwa nk. Watu hao ni wabishi mno na huwa hawasikii ushauri, na mara nyingi hujifanyia yale tu wayatakayo kwa kisingizo utasikia unajua wewe haujafiwa bado!

JIPE MOYO OMBA MUNGU AKUTIE NGUVU KTK TESO LAKO.

Angalia hii ya Bwana Yesu Kristo. Kikichomfanya Bwana wetu ashinde huzuni ile ni maombi aliyoyaomba siku ile. Biblia inasema hivi. “Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba,akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]” (Luka22:40-44)

Bwana Yesu Kristo aliomba sana siku ile. Unajua aliomba mambo yawezekana mengi tu, lakini mojawapo lilikua ni kuomba Mungu amtie nguvu moyoni, malaika alikuja kumtia nguvu ile huzuni ikaisha. Ukijikuta una hali kama hii tubu, na anza kuomba Mungu akutie nguvu ili ulitende lile alilokuagiza.

Unaweza kusikia maagizo kuwa mwanaume mpende mkeo na mwanamke mtii mumeo na pia wanaume tumeagizwa tusiwe na uchungu na wake zetu nk. Sasa ili ulitende hilo agizo jifunze kuomba Nguvu za kukuwezesha kuwa mtendaji wa agizo la Mungu. Nje ya nguvu hizo ni rahisi kutokuyafanya maagizo ya Mungu.

UWE MPOLE UTAKUA NA AMANI.

Jifunze kuwa mpole na mnyenyekefu utajikuta kila wakati ukimtii Mungu. Biblia inasema hivi. “Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani.” (Zaburi 37:11)

Bwana Yesu Kristo aliubeba mzigo wake kisa ni hiki hiki, angalia anasema tujifunze kwake yeye ni mpole na mnyenyekevu Angalia mistsri hii “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” (Mathayo 11:28-30)

Ukiwa mpole na mnyenyekevu utajikuta lazima utakua mtii. Biblia inasema hivi. ”Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” (Wafilip 2:5-8).

Bwana Yesu Kristo alikua mtii ingawa alikua anajua ugumu wa msalaba ule. Mariamu alikubari kutii kuchukua Mimba ingawa alijua gharama yake ni kifo na kutengwa na mchumba wake. Kipindi kile ilikua mtu akizini lazima auawe kwa mawe, sasa fikiria Mariamu alilijua teso lake lakini hakuliangalia akamtii Mungu kwenye mazingira ya magumu.

Sasa sikia ondoa uchungu, na huzuni jitie moyo katika Bwana Yesu Kristo mtii utaona baraka mwisho wake.

Naamini umenielewa Mungu akubariki mnoo.