Salamu – March, 2022

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninakukaribisha sana katika kona hii ya salamu za mwezi. Namshukuru Mungu aliyetupa mwezi huu wa tatu.

Hebu tuanze kuziangalia salamu za mwezi. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa “WEKA BIDII YA KUUSHUGHULIKIA MOYO AU NAFSI YAKO”

Katika salamu zilizopita tuliangalia eneo la SABABU ZINAZO WEZA KUSABABISHA JERAHA NAFSINI. Na tuliiangalia sababu ya kwanza nayo ilikua ni maudhi.

Hebu tuangalie sababu ya pili.

2: SABABU YA PILI INAYOWEZA KULETA JERAHA NAFSINI NI DHAMBI

Ukisoma Biblia unaona dhambi itendwayo na mwanadamu ina madhara mengi sana.

Watu wengi wanafahamu kuwa dhambi inawapeleka jehanamu tu..

Ni kweli watenda dhambi sehemu yao ni jehanamu. Lakini dhambi ina madhara mengine mengi mabaya kabla haijakupeleka huko jehanamu.

Moja ya madhara ambayo dhambi inaweza kuyasababisha ni kuiharibu nafsi ya mtu. Ngoja nikuonyeshe mifano michache

Angalia dhambi ya uzinzi namna inavyoiletea madhara nafsi ya mtu aziniye.

Angalia mistari hii “Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani. Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe?Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa; Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake.Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.” (Mithali 6:26-33).

Kwa mujibu wa mistari hiyo hapo juu unaona dhambi ya uzinzi inatabia ya kuijeruhi nafsi au moyo wa mtenda hiyo dhambi.

Unapozini tu fahamu kinachotafutwa ni moyo wako, maandiko hapo yanasema kazi ya kahaba ni kumwinda mtu ili ainase hiyo nafsi yake.

Nafsi yako au moyo unaweza kuwindwa kabisa na mwindaji wa hiyo nafsi yako fahamu ni mtu yoyote atakaye kuzini na wewe.

Akiiwinda na kuipata, yaani utakapo kubaliana naye tu na mkazini fahamu dhambi hiyo haiiachi nafsi ya huyo mtu salama.

Itakachofanya ni kuijeruhi hiyo nafsi. Biblia inasema mtu aziniye anaiangamiza nafsi yake, na atapata jeraha na mtu huyo atajikuta akifedheheka milele anasema fedheha yake haita futika.

Sikia, jeraha la nafsi ni baya mno kwa sababu huko kwenye nafsi kuna akili,hisia na utashi.. sasa ukijeruhika huko moyoni fahamu mfumo mzima wa akili, hisia na utashi wako utakua umeharibika.

Ninaposema akili nina maana hii yaani mawazo, fikra, kumbukumbu nzuri, kujua, kuelewa, kufahamu kwako na hata kubuni, kupanga kwako na hata utendaji wako utaharibika.

Nilipokua najifunza somo hili nilishangaa sana. Fikiria kidogo kuna watu leo tunawaona wana akili sana, wanajua sana, kama walifanya uzinzi fahamu kiwango chao cha ubora wa mfumo mzima wa akili zao kiliharibiwa.

Fikiria wasingepata hayo majeraha moyoni ingekuaje?

Watu wengi hawana ujasiri katika maisha yao, wanajikuta wakiwa na mifaiko mioyoni mwao..hawajui kiini ni nini! Biblia inasema dhambi hiyo ya uzinzi inasababisha jeraha la kufadhaika kwa watu wazinio.

Mungu hapendi tuwe watu wa fadhaa, yaani tusifadhaike. Uzinzi wenyewe hutengeneza tabia ya mtu kuwa na fedheha. Ndiyo maana unawaona watu wengi hawana amani mioyoni kabisa lakini huku nje wana kila kitu; unajua kisa? Ni hiki, nafsi zao zimejeruhika na kikicho wajeruhi ni uzinzi tu.

Fikiria umezini na watu wakajua na kweli ukatubu na ukarudi kanisani, sasa mtumishi anapozungumzia dhambi ya zinaa tu jeraha lile ulilolipata fahamu lilikutengenezea kovu (kumbukumbu za uzinzi ulioufanya)

Utashangaa ikitajwa hiyo dhambi tu wewe moyoni unaanza kukosa amani kabisa. Ukisikia tu kuna watu moyoni kunalia paaaa! Ndiyo utakuta mtu anatubu mara mbili mbili.

Fikiria watu walijua! Ukiwaangalia tu utafikiri wote wanakutazama wewe kama mzinzi.

Pia nikwambue ukweli jeraha hilo litakusumbua sana, kwasababu Mungu atakusamehe, shida ipo kwa watu, fahamu watu hawata kusamehe, wakikusamehe fahamu hawata kuamini na watakua wakikumbuka kila mara kuwa wewe ni mzinzi na wataambina kabisaa kuwa huyu ni mzinzi tu hilo jeraha litakupa shida sana.

Nakushauri na kukuonya achana na dhambi hii ni tamu kwa dakika tano tu, ila itakupa taabu maisha yako yote.

Mimi nakwambia ukweli, fikiria umeoa au umeolewa, na ukatoka nje ya ndoa, nakwambia ukweli hautakua na amani siku zote za maisha yako. Kumbukumbu zako zitakuhukumu usiku na mchana nakwambia.

Ilinde nafsi yako na kahaba, au malaya au na mwanamke au mwanaume atakaye kuzini na wewe.

Dhambi hii inaondoa ufahamu wa watu. Biblia inasema hivi. “Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.” (Hosea 4:11)

Ukiipitia mistari hiyo unaona madhara ya uzinzi mojawapo ni hii ya kuondoa ufahamu wa watu wazinio. Kumbuka ufahamu unakaa nafsini au moyoni.

Hebu ilinde nafsi leo kwa kutubia dhambi hii kwa Mungu, pili iache, tatu usiifanye dhambi katika maisha yako kabisa.

Nne muombe Mungu aitengeneze nafsi yako iliyojeruhika na uzinzi. Maombi haya ni ya mara kwa mara omba akupe moyo mpya, shughulikia mfumo wa hisia zako na mawazo yako yaliyoharibika ombea hivyo Mungu aviweke vizuri.

Jifunze kuomba nguvu na kujitia nguvu kwa Mungu ili usibanwe na fedheha ingia gharama ya kuyaombea hayo mpaka nafsi au moyo wako uone umekaa salama.

Maombi ya namna hii usiwategemee watu kukuombea, jiombee mwenyewe ukiweza kunena kwa lugha nena sana kwani Biblia inasema yeye anenaye kwa lugha anajijenga nafsi yake. “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa” (1 Wakorintho 14:4)

Jifunze kunena kwa lugha pia kwa mfumo huu wa kumruhusu Mungu aijenge hiyo nafsi yako iliyojeruhiwa au kubomolewa.

Naamini umenielewa.

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
    • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
    • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
  9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.