Salamu – Juni, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe!Tunamshukuru sana Mungu ametupa siku nyingine ya mwezi huu wa sita. Tumeumaliza mwezi wa tano, tumekuwa na semina mbili.

Tulikuwa na semina ya Wanawake huko Sumbawanga mjini na tukawa na semina jijini Mbeya ndani ya Hema pale Otu. Tulikuwa na semina nzuri sana.

Hebu tuanze kuzitazama salamu za mwezi wa sita. Kumbuka tuna kichwa cha salamu zenye kichwa:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA UNABII ILI UPATE KUFANIKIWA KIROHO WEWE NA WATU WENGINE (SEHEMU YA KWANZA)

4: SAUTI KAMA MOTO MOYONI MWAKO

Sauti nyingine ambayo Mungu anaweza kuitumia ni moto moyoni mwa mtu. Angalia mistari hii:

“Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”
(Yeremia 23:29)

Neno la Mungu ni moto. Sikia, Mungu anaweza kuitumia ishara ya moto moyoni kama neno la Mungu.

Mungu anaweza kuachilia neno wewe haujalisikia au kulielewa, kitakachobaki huko moyoni mwako ni moto. Ukahisi kama kuna moto ndani yako, usipojua utaenda mpaka hospitali wakakupima weee, wasione ugonjwa—kumbe ni neno la Mungu limeachiliwa moyoni mwako.

Pia, moto moyoni mpaka kwenye mifupa unaweza kutumika kama muongozo kuwa kuna jambo la Mungu wewe hutaki kulifanya wakati unajua kabisa nini unatakiwa ukifanye.

Angalia mistari hii:

“Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.”
(Yeremia 20:9)

Moto huo ni sauti ya Mungu ambayo anaitumia ili huyo mtu afanye kile Mungu anataka mtu huyo akifanye. Hii ni njia mojawapo Mungu anaweza kuitumia kuzungumza na mtu.

Zipo njia nyingi ambazo Mungu anaweza kusema na mtu… mfano, mazingira, au hata wanyama nk… Punda aliwahi sema neno ambalo lilikuwa na maelekezo.

JIFUNZE KUPIMA KILA NENO LA UNABII KWA NENO LILILOANDIKWA

Angalia mistari hii:

“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.
Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu.
Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.”
(1 Yohana 4:1–3)

Kwa mujibu wa mistari hii, tunajifunza kuwa tunatakiwa tupime roho, yaani unabii na tabia ya mtu atoae unabii. Biblia inasema pimeni manabii, fahamu kuwa nabii hupokea unabii. Kama unatakiwa uwapime manabii, fahamu hata unabii wanaoutoa au kuupokea unatakiwa wapimwe.

Naamini umeelewa.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo

  1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www. mwakatwila. org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO: – Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102. 5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107. 7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104. 1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:- +255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako: Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.