Salamu – Julai, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe,
Tunamshukuru sana Mungu ametupa siku nyingine ya mwezi huu wa sita. Tumeumaliza mwezi wa tano tukiwa tumekuwa na semina mbili.
Katika mwezi wa saba tumekuwa na semina tatu: Itigi, Manyoni, na Mvumi. Tulikuwa na semina nzuri sana katika maeneo hayo.

Hebu tuanze kuzitazama salamu za mwezi wa saba.


JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA UNABII ILI UPATE KUFANIKIWA KIROHO WEWE NA WATU WENGINE (SEHEMU YA KWANZA)

NAMNA YA KUPIMA UNABII

Kuna njia nyingi za kupima unabii. Hebu tuziangalie njia hizi zifuatazo:

1: PIMA ROHO AU UNABII KWA NENO
Tunapoambiwa tupime roho, maana yake tupime neno la Mungu – yaani neno lililoandikwa ndani ya Biblia.

Angalia mistari hii:

“Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” (Yohana 6:63).

Maneno ambayo Mungu ametuambia ndiyo roho. Tunapoambiwa tupime roho, maana yake tupime neno.

Sasa sikia, unapokuwa ni mtu uliyelijaza neno la Mungu ndani yako, ni rahisi sana kwako kujua unabii ninaoupokea umetoka wapi, au ni roho gani iliyoleta unabii kwangu au kwa watu.

Ngoja nikupe mfano:
Siku moja alinifuata mtu mmoja, mtu aliyekuwa katika mji tunaoishi, alikua anaitwa muonaji. Kipindi hicho nilikuwa na mchumba wangu ninayetarajia kumuoa.
Huyo mtu akaniambia:

“Mungu ameniambia unaweza kufanya tendo la ndoa na huyo mchumba… Umeishi muda mrefu bila kufanya hivyo, sasa nakupa kibari ufanye.”

Kilichonisaidia kilikuwa ni neno la Mungu – yaani Biblia. Mungu alinifundisha kuhusu uzinzi na madhara yake, haraka nikajua unabii huo haukutoka kwa Mungu, na sikulifanya.

Pima unabii kama unapatana na neno la Mungu – yaani Biblia.
Sikia, kuna unabii ambao ndani yake unakufundisha chuki, kiburi, ugomvi au kutosamehe.
Ukiona unabii unakufundisha chuki na mtu au ndugu, nakuhakikishia unabii huo hautoki kwa Mungu.

Angalia mfano huu:

“Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mathayo 5:43-45).

Neno la Mungu linatufundisha tuwapende maadui na tuwaombee hao wanaotuudhi. Sasa, ukisikia unabii wa kumuombea vibaya adui, mimi nakwambia utazame vizuri unabii huo.

Ngoja nikupe mfano:
Leo hii mtu anakwambia “Fulani mchawi anakuloga,” utampenda mtu huyo? Kama huwezi kumpenda, ni ngumu sana Mungu kukupa unabii wa namna hiyo. Watu wengi leo wamejikuta wamebeba hasira na hata chuki kwa sababu ya unabii tu.
Utasikia mtu anasema:

“Mungu ameniambia fulani ndiye anataka kuniua…”

Sikia, pima unabii. Utagundua si Mungu kasema.
Ngoja nikupe kipimo: ni neno la Mungu lililoandikwa.
Bwana Yesu Kristo alijua wazi kuwa Yuda atamsaliti, lakini hakuwahi kumtaja mtu kuwa ni Yuda atakayefanya hivyo.
Hata Petro hawakujua. Ni watu wachache sana wanaoweza kuambiwa na Mungu kuhusu mambo kama haya – ni watu waliokua sana kiroho, hawana maneno na watu, si watu wa kukwazwa na maneno ya watu.

Ukiona mtu leo hasemi na wengine kwa sababu eti Mungu amemwonyesha “mbaya wake ni fulani,” sikia, aliyekuambia hayo wala si Mungu, roho nyingine imekuambia. Mungu hawezi kukuchomeka kwenye dhambi.


PIMA UNABII UMETOKA KWA NANI

Pima neno kwa neno. Ngoja nikupe mfano:
Leo hii watu wengi huwasikiliza mapepo na kufuata maelekezo ya mapepo.
Utamkuta mtu anakwambia: “Fulani amefanya hivi na hivi.”
Ukimuliza, “Nani kakuambia?” Atakwambia:

“Tulikua kwenye maombi, na mtu mmoja pepo akalipuka, tukapokea pepo, akasema hivyo.”

Sikia, unabii huo unajua kabisa umetoka kwa mapepo au mganga wa kienyeji au mtu anayeabudu miungu mingine. Usiyasikilize.

Biblia inasema hivi:

“Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44).

Mapepo ni waongo mno, hayasemi ukweli na hayatosema ukweli.
Ukipokea unabii wa kutoka kwa pepo, kuna mahali utapotea.
Mara nyingi Bwana Yesu Kristo aliyaamuru yaketi kimya.
Sikia, unapofungua mlango wa kuzungumza na pepo, unatakiwa uwe umejaa neno la Mungu.
Utaelewa roho hii inatafuta kukupiga wapi kitabia na kiimani.

Angalia mfano huu:

“Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu. Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena, Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake? Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi; Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo!” (Ayubu 4:12-19).

Kwa mujibu wa mistari hiyo utaona Ayubu aliona ono na alijua ono hilo limetoka kwa shetani, na sauti iliyosema hapo ilikuwa ya pepo. Pepo hilo lilileta unabii. Ukiutazama unabii huo, ndani yake ulibeba uongo mkubwa.


Naam, naamini umenielewa.
Tuonane tena katika kona hii ya salamu za mwezi.


UKIHITAJI MASOMO YETU UNAWEZA KUYAPATA KWA NJIA HIZI ZIFUATAZO:

  1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” – utaipata Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

  2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org.

  3. YouTubeMwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

  4. Facebook – Ingia katika tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), “like” na utapata maelezo ya kujiunga; au andika “SOMA NENO LA MUNGU” moja kwa moja kwenye Facebook.

  5. Instagram – Tafuta “Steven Mwakatwila”.

  6. DVDs au CDs.

  7. Vitabu – Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata vitabu, DVD na CD.

  8. Kwa njia ya Redio – Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:

    • Rungwe FM 102.5 – Kila Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.

    • Baraka FM 107.7 – Kila Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.

    • Bomba FM 104.1 – Kila Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
      Unaweza pia kutusikiliza kwenye Online Radio yetu: radio.mwakatwila.org.

Kwa mawasiliano zaidi, tupigie: +255 754 849 924 au +255 756 715 222.

Wako:
Mwl. Mr & Mrs Steven Mwakatwila.