Salamu – Agosti, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe,

Tunamshukuru sana Mungu kwa kutupa siku nyingine ya mwezi huu wa nane.
Mwezi wa saba tumekuwa na semina za Chimala na Ubaruku. Zilikuwa semina nzuri sana.

Hebu tuanze kuzitazama salamu za mwezi wa nane:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA UNABII ILI UPATE KUFANIKIWA KIROHO WEWE NA WATU WENGINE (SEHEMU YA KWANZA)

3: JIFUNZE KUOMBA KWA MUNGU ILI UPIME UNABII KWA UNABII

Sikia, unabii ni neno linalotoka kwa Mungu. Sasa, unaweza kupokea unabii, na ili uupime huo unabii unaweza kuomba ili Mungu akupe kuhakikisha juu ya unabii huo.

Mungu anaweza kukuhakikishia neno lako hilo limetoka wapi kwa kukuletea unabii mwingine. Kumbuka, unabii ni neno. Sasa, ukilipokea hilo neno kwenye ulimwengu wa roho, Mungu anaweza kukujulisha kuwa ujumbe huo umetoka kwa nani kwa kukupatia unabii.

Ngoja nikupe mfano:
Kuna mtu aliwahi kuja kwangu akasema Mungu amemtuma kuniambia niache nafasi ya uongozi kazini kwangu. Mimi nilipomsikia akisema hivyo nilimuuliza Roho Mtakatifu: “Ni kweli umemwambia neno hilo?”

Akaniambia hivi: “Mwambie usiku afuatilie ndoto ambayo Mungu atamuonyesha.”
Basi nikamwambia hivyo hivyo.

Kesho yake nikaonana naye. Akaniambia: “Nimeona ono hivi: Nimemuona fulani, akaniambia, kisha huyo fulani akabadilika akawa nyoka. Huyo nyoka akaanza kuniambia mambo, akasema niachane na nafasi ya uongozi niliyopewa kazini. Baadaye yule nyoka akakimbia na akageuka tena kuwa mtu.”

Nilipomsikia akiniambia hivyo, nikamwambia: “Aliyekuambia wewe kuhusu hilo neno la kuacha uongozi kazini ni shetani. Unabii huo chanzo chake ni shetani.”

Unajua akaniambia: “Hata mimi nimejua kuwa ujumbe ule si wa Mungu.”

Fahamu, hata kwako unaweza kupokea unabii. Kabla hujaanza kuusema au kuufanyia kazi, muombe Mungu akudhibitishie ujumbe huo umetoka wapi. Ni roho gani imeachilia unabii huo kwako? Mungu akiamua atakujulisha kwa kukuletea unabii.

Anaweza akakupa wewe, au akampa unabii huo mtu mwingine ambaye atakudhibitishia.
“Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.” (1 Kor 14:29–30)

Kwa mujibu wa mistari hiyo, utajifunza kuwa unabii unaweza kupimwa kwa kutumia unabii. Nabii mmoja akitoa unabii, nabii mwingine anaweza kupokea neno la kudhibitisha unabii huo. Sasa Mungu anaweza kukuletea ono au ndoto kukudhibitishia unabii huo umetoka kwa nani.

Naamini umeelewa.
Mungu akubariki, na tuonane katika kona hii mwezi ujao.


UKIHITAJI MASOMO YETU, UNAWEZA KUYAPATA KWA NJIA HIZI ZIFUATAZO:

  1. App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” – utaipata Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana hapo.

  2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org.

  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).

  4. Facebook – Ingia katika tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), “like” na utapata maelezo ya kujiunga; au andika “SOMA NENO LA MUNGU” moja kwa moja kwenye Facebook.

  5. Instagram – Tafuta “Steven Mwakatwila”.

  6. DVDs au CDs.

  7. Vitabu – Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata vitabu, DVD na CD.

  8. Kwa njia ya Redio – Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:
    Rungwe FM 102.5 – Kila Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
    Baraka FM 107.7 – Kila Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    Bomba FM 104.1 – Kila Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.

    Unaweza pia kutusikiliza kwenye Online Radio yetu: radio.mwakatwila.org.

Kwa mawasiliano zaidi, tupigie: +255 754 849 924 au +255 756 715 222.


Wako:
Mwl. Mr & Mrs Steven Mwakatwila