Salamu – Novemba, 2025

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana.

Pole na kazi zako zote. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mwezi huu wa kumi na moja. Naamini Mungu amekupigania sana katika mwezi uliopita. Ninakuletea salamu za mwezi huu ili kwa pamoja tujifunze Neno la Mungu.


UTANGULIZI

Tunaanza kujifunza somo jipya lenye kichwa kisemacho:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)

Somo hili ni mwendelezo wa somo lenye kichwa hicho, ambapo katika sehemu hii tutajifunza kuhusu kutaka karama ya miujiza na uponyaji.

Unaweza kuwa na swali: kwa nini tujifunze somo hili?

Biblia inatuambia hivi:

“Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu… Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.”
(1Kor 12:1 na 31)

Kwa mujibu wa mistari hii, tunajifunza kuwa kuna mambo ambayo Mungu anataka kila mtoto wake asikose kuyajua. Moja ya mambo hayo ni habari za karama za Roho.

Mungu anataka uzijue karama hizi, na si kuzijua tu, bali pia uzitake.

Kwa kweli, ni nadra sana kusikia mafundisho kuhusu karama za Roho katika makanisa au semina nyingi. Mara nyingi, masomo yanayosikika sana ni kuhusu baraka za fedha, mali, vyeo, au ushindi dhidi ya maadui.

Lakini Neno la Mungu linatutaka sisi sote tusikose kujua kuhusu karama za Roho. Hii ina maana kwamba hata wewe unatakiwa uzisikie na uzitake karama hizi.

Kama Mungu anasema tusikose kuzijua, fahamu kuwa ni jambo muhimu sana.


JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI

Maana ya Neno Karama

Neno karama maana yake ni zawadi.

Unaposikia kuhusu karama za Roho, maana yake ni zawadi ambazo Mungu huwapa watu kupitia Roho Mtakatifu kwa kusudi la kusaidia wengine.

Mungu alipotuumba, alituumba katika sehemu kuu tatu:

  • Roho

  • Nafsi

  • Mwili

Karama za Roho hutolewa katika roho ya mtu. Roho yako inapopewa karama, maana yake Mungu anakupa uwezo wa kiungu ndani yako.

Kuna zawadi nyingi Mungu hutoa, na mojawapo ni karama zinazotolewa moja kwa moja rohoni.


Maana ya Karama ya Miujiza

Karama ya miujiza ni uwezo ambao Mungu hutumia kufanya mambo yasiyowezekana kwa nguvu za kawaida za mwanadamu.

Miujiza ni ishara au maajabu ambayo hayawezi kufanywa kwa uwezo wa kibinadamu, bali kwa uwezo wa Mungu.

Ni muhimu kuelewa kuwa miujiza si kazi ya mwanadamu, bali ni kazi ya Mungu akimtumia mwanadamu.

Ukiona miujiza inafanyika kupitia mtu, fahamu kuwa ni Mungu anayetenda kupitia mtu huyo.

Biblia inasema:

“3 Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao.”
(Mdo 14:3)


Karama ya Miujiza Hufanya Kazi Pamoja na Karama Nyingine

Karama ya miujiza mara nyingi hufanya kazi pamoja na karama nyingine.

Mfano: Karama ya Imani

“36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
37 Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
38 Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu.
40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.”
(1Fal 18:36–40)

Katika tukio hili, Mungu alifanya muujiza kwa kumtumia Eliya. Eliya hakufanya kwa uwezo wake mwenyewe, bali kwa uwezo wa Mungu.


Mfano wa Imani Maalumu

“1 Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
2 Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.
3 Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake…”
(1Fal 19:1–4)

Hii inaonyesha kuwa Mungu humpa mtu imani maalumu kwa wakati wa kufanya muujiza.


Mfano: Karama ya Maarifa

“15 BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.
16 Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.”
(Kutoka 14:15–16)

Hapa tunaona karama ya miujiza ikifanya kazi pamoja na karama ya maarifa.


Mfano: Karama ya Uponyaji

“24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?
25 Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu…
26 …kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”
(Kutoka 15:24–26)

Na pia:

“21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya…
22 Hivyo yale maji yakapona hata leo…”
(2Falme 2:21–22)

Hapa tunaona karama ya miujiza ikifanya kazi pamoja na karama ya uponyaji.


HITIMISHO

Kwa sehemu hii, umejifunza kuwa:

  • Karama ya miujiza hutoka kwa Mungu

  • Mungu humtumia mwanadamu kufanya miujiza

  • Karama ya miujiza hufanya kazi pamoja na karama nyingine

  • Mungu humpa mtu imani maalumu ili kufanya miujiza

Naamini umeelewa. Tuonane tena katika salamu zijazo.


JINSI YA KUPATA MASOMO YETU

Unaweza kupata masomo yetu kupitia njia zifuatazo:

1. App ya HUSONEMU (MWAKATWILA)
Inapatikana Play Store.

2. Tovuti:
www.mwakatwila.org

3. YouTube:
HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

4. Facebook:
Tafuta: SOMA NENO LA MUNGU

5. Instagram:
Huduma ya Soma Neno la Mungu

6. DVDs au CDs

7. Vitabu
Wasiliana: +255 763 109 733


REDIO

Rungwe FM 102.5 MHz
Jumapili saa 3:00 – 4:00 usiku

Baraka FM 107.7 MHz
Jumanne saa 12:00 jioni – 1:00 usiku

Bomba FM 104.1 MHz
Ijumaa saa 3:00 – 4:00 usiku


ONLINE RADIO

radio.mwakatwila.org

Ratiba:

  • 12:00 Asubuhi

  • 07:00 Mchana

  • 12:00 Jioni

  • 03:00 Usiku


MAWASILIANO

+255 754 849 924
+255 756 715 222


Wako katika Kristo,
Mwl Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila