Salamu – Machi, 2026

Bwana Yesu Kristo asifiwe. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mwezi wa tatu; ni neema kubwa sana. Mwezi uliopita tumekuwa na mambo mengi, na mojawapo ni semina ya siku moja ya ndoa.

Ilikuwa semina nzuri sana. Ikimpendeza Mungu, tunatarajia kuwa na semina kama hii tarehe kama hiyo mwakani. Unapoomba, hebu tenga muda uombee ndoa za watu wengine na ya kwako pia.

Hebu tuanze kuzipokea salamu za mwezi huu. Kumbuka tuna salamu yenye kichwa:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)

SABABU ZINAZOMFANYA MUNGU AFANYE ISHARA, MIUJIZA AU MAAJABU

Mungu anapofanya muujiza, iwe kwa kumtumia mtu au moja kwa moja kutoka mbinguni bila kumshirikisha mtu, hufanya hivyo kwa malengo, sababu au kusudi.

Unaposoma Biblia, unaona zipo sababu nyingi zinazomfanya Mungu atende miujiza na kuponya.

Hebu tuanze kuziona sababu hizo:

1. SABABU YA KWANZA: MUNGU HUTUMIA MIUJIZA KAMA SAUTI YAKE KWA WATU

Mungu anasema, na ana sauti yake. Sasa sikia: Mungu ana njia nyingi za kuiachia sauti yake kwa wanadamu. Mojawapo ya njia hizo ni muujiza.

Angalia mistari hii uone:
“1 Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea.
2 BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.
3 Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake.
4 BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)
5 ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea.
6 BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa na ukoma, umekuwa mweupe kama theluji.
7 Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake.
8 Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili.
9 Kisha itakuwa, wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu.”
(Kutoka 4:1–9)

Kwa mujibu wa mistari hiyo, unaona wazi kuwa Mungu huitumia miujiza kama sauti yake. Watu wengi wanapoona au kusikia habari za muujiza, hawajui kuwa muujiza wowote unaotoka kwa Mungu hubeba sauti ya Mungu.

Watu wengi wanaomba Mungu aseme nao au waisikie sauti yake, lakini hawajui kuwa muujiza wowote ambao Mungu ameufanya—iwe kwa kumtumia mtu au mazingira—ni mojawapo ya njia ya sauti ya Mungu.

Angalia mfano huu:
“36 Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma.
37 Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona.”
(Yohana 5:36–37)

Ukisoma mistari hiyo, utajifunza kuwa muujiza unaotoka kwa Mungu ni sauti yake. Kazi alizokuwa anazifanya zilikuwa ushuhuda au sauti ya Mungu.

Watu wengi wakisikia habari za muujiza hawajui kuwa tukio hilo ni sauti ya Mungu au ni neno ambalo Mungu analisema au analishuhudia kwa watu wanaoona au kusikia muujiza huo.

Naamini umenielewa. Tuonane tena katika eneo hili la salamu ya mwezi ujao.

Mungu akubariki sana.


Ukihitaji masomo yetu, unaweza kuyapata kwa njia zifuatazo:

  1. App yetu ya huduma yenye jina “HUSONEMU (MWAKATWILA)” — inapatikana Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana.

  2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org

  3. YouTube: HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

  4. Facebook: ingia kwenye tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), kisha “like” ili upate maelezo ya kujiunga, au tafuta “SOMA NENO LA MUNGU”

  5. Instagram: tafuta “Huduma ya Soma Neno la Mungu”

  6. DVDs 📀 au CDs 💿

  7. Vitabu

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733 ili kupata vitabu, DVD na CD.

8. Kwa njia ya redio:
➖ Rungwe FM 102.5 MHz — Jumapili saa 3:00 hadi 4:00 usiku
➖ Baraka FM 107.7 MHz — Jumanne saa 12:00 jioni hadi 1:00 usiku
➖ Bomba FM 104.1 MHz — Ijumaa saa 3:00 hadi 4:00 usiku

9. Online Radio: radio.mwakatwila.org
Ratiba ya vipindi:
Saa 12:00 asubuhi
Saa 07:00 mchana
Saa 12:00 jioni
Saa 03:00 usiku

10. Ingia MWAKATWILA YouTube Online

Kwa mawasiliano zaidi:
+255 754 849 924
+255 756 715 222

Wako,
Mwl. Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila