Maisha Baada ya Kuokoka
Ndugu yangu baada ya kuokoka tu, kuna swali naamini liko ndani ya moyo wako, unajiuliza, sasa leo hii nimeokoka nifanyenini sasa? Ni kweli ikiwa umeokoka kuna mambo muhimu ambayo unatakiwa uanze kuyafanya, yapo mambo mengi sana, lakini hebu nikupe haya mambo ya msingi ambayo unapaswa kuyafanya.
Jambo la Kwanza
Jambo la kwanza ambalo Mungu anataka kuliona kwako likitendeka baada ya kuokoka, ni kukuona ukiukulia Wokovu. “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyo ghoshiwa,ila kwa hayo mpate kuukulia wokovu;” (1PETRO 2:2)
Baada ya wewe kuhamishwa kutoka katika ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa Nuru, yaani chini ya utawala mpya ambao unataratibu tofauti na ule utawala wa kwanza ambao inawezekana umeishi chini ya utawala huo kwa muda wa miaka mingi, Mungu anataka akuone sasa ukianza kuyajua mambo mapya yaliyoko katika utawala wake, anaposema kuukulia wokovu, maana yake kubwa ni kuzidi kuyajua mapenzi yake Mungu, Uzidi kujua kwa upana upendo wake kwako, uzidi kujua Uwezo wake ulivyo mkuu na nguvu zake zilivyo, uzidi kujua ni nini umekusudiwa ukipate baada ya kuingia katika Ufalme wa Nuru, ona maneno haya yasemavyo, “Kwa sababu hiyo mimi nami,tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu,na pendo lenu kwa watakatifu wote,siachi kutoa shukrani kwa ajiri yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,Baba wa utukufu,awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, MJUE tumaini la mwito wake jinsi ulivyo; na UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE KATIKA WATAKATIFU JINSI ULIVYO; kwa kadili ya utendaji wa nguvu za uweza wake;…” (WAEFESO 1: 15-
Neno la Mungu linatufundisha hapo kuwa Mungu anataka wewe na mimi baada ya kuokoka tu kwa njia ya imani, tuanze kuyajua hayo mambo aliyoyataja Mtume Paulo na mengine mengi, anataka ujue tumaini la wito wake jinsi ulivyo, Mungu amekuita baada ya kukita amekukusudia nini? Anataka ujue baada ya kuokoka nini unachotakiwa ukitalajie kutoka kwake, ujue baraka zako au haki zako ambazo Mungu amewa ahidia kuwapa wale wote walio upokea huo wokovu, kwa mfano Baada ya wewe kuokoka, Kuna kuna vitu ambavyo Mungu anakupa, anataka uvijue, angalia maneno haya “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wowote uketi mkono wangu wa kuume,hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale wataourithi wokovu!” (EBR 1: 13-
Neno la Mungu hapo linatufundisha kuwa moja ya baraka amabazo walioupokea wokovu wanazipokea ni hizi za kupewa wahudumu wa kuwahudumia, na wahudumu hao ni malaika. Mtume Paulo alijua wazi kuwa kunamambo mengi ambayo Mungu ameyakusudia kuwapa watu wote watakao urithi wokovu, akaamua kuwaombea hao watu ili Mungu awasaidie kuyajua hayo yote, akawaombea hao ndugu waliompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wao wapewe Roho ya ufunuo wa kumjua Mungu, pia akawaombea wapate ufahamu rohoni mwao wa kujua utajiri waliopewa na Mungu baada ya kuokoka, pia macho yao ya ndani yaone kila kitu ambacho Mungu anacho na amekiweka kwa ajiri ya watu wale walioamua kumpa Yesu maisha yao.
Na amini umeelewa maana ya kuukulia wokovu sasa, Sikia tena,unapozidi kujua ndipo unapozidi kukua, au kwa lugha nzuri ndipo ufahamu wako wa kumjua Mungu unapokuwa mkubwa, na hilo ndilo kusudi la Mungu kwako, anataka akukuze ufahamu wako katika kumjua yeye na pia uyajue mapenzi yake kwa upana zaidi, angalia maneno yake haya ya semavyo kuhusu jambo hili “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi.kufanya maombi na dua kwa ajiri yenu,ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni” (WAKOLOSAI 1:9.) Mungu anataka wewe ndugu upate kujazwa maarifa,hekima na ufahamu wa rohoni, mambo ya rohoni ni mambo ya Kimungu, anataka ujazwe ufahamu wa mambo ya kimungu, Hiyo ndiyo maana ya kuukulia wokovu.
Namna ya kufanya
Ili upate kukua au kuanza kuyajua mambo hayo yote, unatakiwa uanze kuyanywa maziwa yasiyoghoshiwa. Neno hilo lina maana maziwa yasiyochanganywa na maji, mtoto mchanga azaliwapo, huwa hapewi chakula kigumu, hunyonya maziwa ya mama yake, na kama akipewa maziwa ya ng’ombe au mbuzi, ni lazima maziwa hayo yachanganywe na maji kidogo, hata wewe ili leo hii uanze kuukulia wokovu inatakiwa uanze kunywa maziwa yasiyo changanywa na maji, “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ila kwa hayo mpate kuukulia wokovu;” (1PETRO 2:2) Maziwa hayo Neno la Mungu linayaita “maziwa ya akili”, au maziwa ya ufahamu, unaweza ukawa na swali maziwa hayo nini? Maziwa hayo ni Neno la Mungu, angalia maneno haya yasemavyo “ Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana,iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita) mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni motto mchanga. lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao kwa kutumiwa zimezoezwa kupambanua mema na mabaya. ” (EBR 5:11-
Ukisoma maneno hayo kwa kutulia utagundua wazi kuwa, Biblia inapozungumzia hapo kuhusu maziwa inataja wazi kuwa maziwa ni Neno la Mungu, Kwa maana hiyo kama unataka kuukulia wokovu unatakiwa uhakikishe unalitafuta neno la Mungu iliutoke katika hali ya utoto na ukue. Hao ndugu walikuwa watoto kwa sababu walikuwa wavivu wa kulisikia neno la Mungu, “ Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.” (EBR 5:11) Kitu kilichopelekea hao ndugu kukaa katika hali ya utoto kwa muda mrefu ni uvuvi waliokuwa nao wa kulisikia neno la Mungu, Kama unataka kuukulia wokovu unatakiwa uhakikishe unaondoa uvivu wa kulisikia neno la Mungu, neno la Mungu tunaweza kulisikia kwa namna nyingi sana, Kwa kulisoma, Fahamu unaposoma unasikia, weka bidii kusoma Biblia, kusoma vitabu mbalimbali ambavyo waalimu wa neno la Mungu wameviandika, pitia tovuti (website) mbalimbali za watumishi wa Mungu, soma waliyoyafundisha nenda kayahakikishe kwenye Biblia yako kama ni sahihi. Pia unaweza kusikia mafundisho kwa kupitia semina,mikutano, ibadani kwenu, hata kwa kununua kanda za mafundisho ya neno la Mungu, cd.au vcd ama dvd nk. Ukiweka bidii katika kusikia fahamu hata imani yako kwa Mungu itakuwa kubwa sana, pia ufahamu wako wa Mambo ya Mungu utaongezeka siku hata siku. Ndani ya neno la Mungu huko ndiko kuna maarifa na ufahamu wa kumjua Mungu na kumcha. Sikiliza haya maneno ya Mungu yasemavyo“ Mwanangu. Kama ukiyakubari maneno yangu na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, ukaelekeza moyo wako upate kufahamu; naam ukiita busara na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafuta kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, na kupata kumjua Mungu.” (MITHALI 2: 1-
Ili leo hii upate ufahamu, upate kujua kumcha Mungu, lazima uweke bidii ya kulitafuta neno la Mungu kama vile unavyotafuta fedha, kama unabidii kubwa ya kutafuta fedha bidii hiyo hiyo unafundishwa uiweke katika kulitafuta neno la Mungu, ndani ya neno la Mungu huko ndiko kuna maarifa yote, ili leo hii upate kuishinda dhambi yapo maarifa ndani ya neno la Mungu, ili leo hii upate kubarikiwa, maarifa ya kubarikiwa yapo ndani ya neno la Mungu, neno la Mungu ndio dila ya maisha yote atakayo Mungu uyaishi ukiwa hapa duniani, Mungu ameweka siri zake humo ndani ya neno lake. Ili uendelee kuokolewa kila siku maarifa yake yamo ndani ya hilo neno la Mungu, inawezekana ukawa na swali hili ikiwa nimekosea baada ya kuokoka ninatakiwa nifanyenini?, Sikia maarifa hayo yamo ndani ya neno la Mungu sikia neno lisemavyo “ Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki. Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu,bali na kwa dhambi za ulimwengu wote” (1YOHANA 2:1-
Jambo la Pili
Jambo la pili muhimu ambalo unatakiwa ulifanye ni kuomba. Nini maana ya kuomba? Kuomba ni kuzungumza au kushirikiana na Mungu, Mungu anataka kushirikiana na wewe, Kumbuka ulipo okoka alilejeza ushirikiano kati yake na wewe, kwa hiyo anataka kuudumisha ushirika huo, na ushirika huo utaudumisha kwa kupitia maombi, Neno la Mungu linasema hivi “Haya njooni tusemezane,asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera,zitakuwa kama sufu” (ISAYA 1: 18). Mungu anataka kusema nawe, na amekupa kibali cha wewe kwenda kuzungumza naye, ameamua kukusamehe, na baada ya kukusamehe,amekupa nafasi ya kusema naye, tunasema na Mungu kwa njia ya maombi.
Baada ya kumpokea Yesu fahamu yuko ndani yako, hayupo mbali na wewe yuko karibu, anachotaka ni wewe kumshirikisha kila jambo, ukiwa unauhitaji fulani anataka umwambie akusaidie, angalia maneno haya ya Mungu yanavyotufundisha, “ Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini, upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (WAFILIPI 4:4-
Mungu anataka umshirikishe kila unacho hitaji, hapendi kukuona wewe ukijisumbua peke yako, anataka ushirikane naye umweleze kila kitu, usimfiche ikiwa umekwama katika kona fulani mweleze nk. Hata ukikosea omba maombi ya kuomba msamaha, atakusamehe, ikiwa unaumwa omba uponyaji atakusaidia, ikiwa unashida yoyote ile mwambie, atakusikia kwa kuwa hayupo mbali nawe, kumbuka yupo karibu sana na wewe kuliko vile unavyo fikiri. Unaweza kuwaza moyoni mwako kuwa mimi sijui kuomba, sikiliza hakuna anaejua kuomba. Neno la Mungu lina sema hivi, “Kadharika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu,kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa, naye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.” (WARUMI 8: 26-
Mimi na wewe hatujui kuomba. Neno la Mungu linasema wazi hapo, wewe anza kuomba tu, usiogope kuwa utakosea, ondoa wazo kuwa Mungu anawasikia watu Fulani tu, Mungu anamsikia kila mtu aliye na imani kwake, na ambaye hamfichi dhambi zake, kumbuka anasema njooni tusemezane, amekuahidi kukusafisha dhambi zako zote, hata kama ni nyekundu sanaa, anachotaka ni hiki, usimfiche maovu yako, ziungame dhambi zako zote mbele zake, atakusamehe,ndipo umuombe, na ukimwomba atakupa hicho umwombacho, kama unataka kuukulia wokovu, weka bidii katika eneo hili la kuomba. Kinachotakiwa ukifanye kwenye maombi yako omba kwa Jina la Yesu Kristo. Usisahau kulitumia jina hili katika maombi yako, ili maombi yako yashughulikiwe mbinguni, lazima uyagonge muhuli wa jina la Yesu Kristo. Bwana Yesu anatufundisha kuhusu habari za maombi anasisitiza sana kuhusu jambo hili la kuomba, na anapo tufundisha kuomba anatutaka tunalitumia jina la Yesu katika maombi yetu. “ Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin, nawaambia,mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni nayi mtapata; furaha yenu iwe timilifu” (YOHANA 16:23-
Jifunze kulitumia jina la Yesu katika maombi yako, pia jifunze kuwasamehe watu wote waliokukosea kabla hujaingia kwenye maombi. Neno la Mungu lina sema hivi “ Nanyi kila msimamapo na kusali,sameheni mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. (Lakini kama ninyi hamsamehe,wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu)”
(MARKO 11: 25-
Jambo la Tatu
Jambo la tatu ni hili, waambie watu wegine kuwa umeokoka. Sikiliza ikiwa leo hii unataka Mungu azidi kukukuza katika wokovu unatakiwa ujifunze kumkiri Yesu kwa kupitia kinywa chako kama Bwana na mwokozi wako, sikiliza maneno haya yanavyotufundisha. “Kwa sababu ukimiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa bni Bwana, na kuamini moyoni kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu uamini hata kupata haki,na kwakinywa hukiri hata kupata wokovu” (WARUMI 10:9-
Mungu ana tabia ya kuyaumba yale uyasemayo, sasa ikiwa leo hii utaanza kukiri au kusema Yesu ameniokoa, ndipo Mungu atapo umba wokovu kwako! Umeona hilo jambo la tatu lilivyo muhimu? Kama leo hii hutaki kwenda mautini, lazima ujifunze kuumba pamoja na Mungu wokovu wa kukutoa mautini. Unaweza kujiuliza nitaumbaje pamoja na Mungu? Sikiliza Mungu anayaumba yale uyasemayo, ukisema umeokoka kutoka mautini na Yesu ndiye mwokozi wako, fahamu ndipo utakuwa unaumba wokovu huo pamoja na Mungu, kwa kuwa Mungu anaumba yale tuya semayo, ebu angali maneno haya yasemavyo. “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; na wao wa upendao watakula matunda yake.” (MITHALI 18 : 21). Kuna nguvu kubwa sana ya uumbaji kupitia maneno uyasemayo, neno la Mungu hapo linasema mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi. Yaani kile unachokisema ndicho kitakacho kupa Uzima au mauti, iwapo utaanza kusema kuwa umeokoka, basi fahamu ndipo utakapokuwa unaumba uzima katika maisha yako . Basi ndugu yangu mpendwa ikiwa umeokoka usisite kusema kwa watu kuwa umeokoka! Hapo utakuwa unaukulia wokovu.
Na amini kwa sehemu umefahamu ni mambo gani muhimu unayotakiwa uyafanye baada ya kuokoka, ya fanyie kazi na ndipo utakapo ukulia wokovu, Mungu Yesu Kristo akubariki sana