Salamu – Julai, 2011

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU)

Mimi na Mke wangu tunawasalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo aliye hai. Tunapenda kukuambia kuwa tunakupenda, na tunakushukuru sana kwa kutuombea na hata kutuwezesha katika kuujenga ufalme wa Mungu. Pia tunamshukuru sana Mungu ambaye ametupa nafasi ya kuuona mwezi huu wa saba. Mwezi huu tunakuletea salamu nzuri zenye kichwa “MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU” (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU)  

Huu ni mfululizo au mwendelezo wa salamu zetu hizo ambazo tumeanza kuzileta kwako tokea mwezi uliopita. Tumeanza kwa kuangalia wazi kuwa Mungu anataka mimi na wewe tumuombe. Kweli, watoto wa Mungu wengi wanaomba sana, lakini wengi, hawapati majibu ya maombi yao. Tumeanza kuona tatizo linaloweza kuwa ni miongoni mwa matatizo mengi yanayoweza kuwa kizuizi cha maombi yako. Nalo ni hili, kutokuomba sawasawa na mapenzi yake. 

“Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1YOHANA 5:14-15). 

Kumbuka neno mapenzi ya Mungu maana yake ni kusudi la Mungu au mpango wa Mungu, ili ufanikiwe katika sehemu ya maombi, lazima ujifunze kufanya maombi ya ufahamu. Ujue ni nini mapenzi ya Mungu katika hicho unachokiombea Kama utafahamu Mungu amekusudia nini itakuwa tayari umeyajua mapenzi yake. Katika salamu zilizopita tulianza kujifunza katika eneo la kujua au kufahamu kuwa Mungu aliye ndani yako anasema, anaweza kukufahamisha mambo yoyote yale. Hebu tusonge mbele. 

AINA MBILI ZA MANENO YA MUNGU 

Ili leo hii Mungu akufahamishe wewe kitu chochote kile fahamu atakupa neno lake, ambalo ndani yake ameweka maarifa au ufahamu. Kuna aina mbili za maneno ya Mungu, aina ya kwanza ni Neno lake alilolisema, Neno hilo ameliweka ndani ya maandiko matakatifu yaani Biblia. Ndani ya Neno la Mungu huko ndiko ameweka maarifa na ufahamu wa kutufahamisha sisi nini yaliyo mapenzi yake ili tuyajue na tuyafanye yale aliyotuagiza. Humo ndani ya Neno lake ndimo alimoachilia kila aina ya ufahamu. Ikiwa leo hii wewe ni msomaji wa Biblia utagundua ni nini unapaswa umuombe Mungu ambacho ni haki yako. Tazama maneno yake haya yasemavyo. 

“Unikumbushe; na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” (ISAYA 43:26). 

Mungu anataka wewe umkumbushe, uhojiane naye, umweleze mambo yako ili akupatie haki yako. 

Ili leo hii ujue nini iliyo haki yako ni lazima uingie ndani ya Biblia na uanze kutafuta kila sehemu ambayo Mungu ameeleza ni nini iliyo haki yako wewe. Humo Ndani ya Biblia ndimo Mungu ametufahamisha nini iliyo haki yetu, iwe haki ya watumishi, wanawake, wanaume, watu wote, watoto wa Mungu nk. Kuna haki za watumishi wa Mungu ambazo watumishi wa Mungu wanapaswa kumuomba Mungu awape, wamkumbushe na hata kuhojiana naye juu ya haki zao hizo ili apate kuwapa. Kuna haki za wanawake ambazo Mungu ameziweka ndani ya Biblia, wakiomba kinyume na haki zao nakuambia ukweli hata wafunge na kuomba siku mia moja Mungu hatawapa. Kwa sababu wameomba nje ya haki zao zilizoainishwa ndani ya Biblia. Mfano, Mwanaume amepewa haki ya kuwa kichwa neno la Mungu linasema hivyo. Sasa hata wanawake wafunge siku elfu moja hawawezi kupewa haki hiyo! Naona hapo sasa umeelewa kwa nini hatupokei majibu ya maombi yetu? Jibu lipo hapo, hatujui haki yetu ni nini. Hatujui haki zetu kwa sababu hatuna neno la Mungu ndani yetu, yaani hausomi Biblia. Sikia Yesu asemavyo, kama unataka kufanikiwa katika eneo la Majibu ya maombi yako. 

“Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (YOHANA 15: 7). 

Ili Mungu akupe kila utakalo ni lazima uhakikishe unalo neno lake ndani yako, maana yake nini? Sikia nilazima ujue nini iliyo haki yako na pia ujue nini lililo kusudi lake katika hilo ulitakalo akupe. Kama ni haki yako atakupa, kama si haki yako hakupi! Yesu anafahamu kabisa kuwa ndani ya neno lake tu ndiko kuna ufahamu wa kutosha wa kukufahamisha wewe nini iliyo haki yako, kama utajua hiyo ni haki yako itakuwa ni rahisi kuhojiana na Mungu kuhusu habari za haki zako. Sasa sisi hatujui haki yetu nini, ila ni mafundi wa kumwambia Mungu nipe kitu fulani, wakati hujui hata kitu hicho anacho, na hata kama anacho Je! Ni mapenzi yake wewe upewe kitu hicho? Nataka kuanzia leo hii weka bidii katika kusoma neno la Mungu utapata maarifa na ufahamu wa kujua nini iliyo haki yako. 

Aina ya pili ya neno la Mungu ni neno ambalo Mungu anasema sasa hivi. Watoto wa Mungu wengi sana wanapoomba wanatafuta maneno ya kusimamia, wanaomba kwa kuyasimamia maneno hayo yaliyomo ndani ya Biblia, wengi hawafahamu kuwa wanaweza kusimamia hayo maneno, na wakaomba kwa kuyasimamia hayo maneno ya Biblia na wasipate majibu kabisa. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu unaweza kusoma maandiko ukapata ufahamu, lakini ufahamu huo ukawa bado ni mdogo sana wa kukuwezesha kujua nini kusudi la Mungu. Ngoja nikupe mfano. Danieli alifanya maombi, na maombi hayo aliyafanya baada ya kusoma maneno ya Mungu aliyoyaandika nabii Yeremia, alipokuwa kwenye maombi Mungu akasema naye waziwazi, na baada ya kusema naye waziwazi ndipo alipopata ufahamu mpana, ambao ulipelekea kupewa haki yake. 

“Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjilia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.”(DANIEL 9:2-3). 

Ukiyasoma maneno hayo utaona Danieli alilisikia neno la Mungu lililoandikwa, anasema akapata ufahamu, akafahamu nini iliyo haki yake yeye na ya wana wa Israeli waliopelekwa utumwani ya kukaa utumwani mika sabini. Lakini ukisoma maneno haya yafuatayo utagundua aina ya pili ya neno la Mungu alilopelekewa Danieli. 

“Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akisema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate ufahamu.” (DANIELI 9:20-22). 

Ukiyasoma maneno hayo utagundua wazi kuwa, kuna aina ya pili ya neno la Mungu alilopokea Danieli, lilikuwa ni neno alilopokea wakati huohuo, aliongea na malaika waziwazi, Mungu alimpa akili na ufahamu kwa upana zaidi ya vile alivyo soma vitabu. Sikiliza, alipovisoma vile vitabu anasema alipata ufahamu akaanza kuomba, lakini baadaye Mungu aliletea neno lilojaa akili ili Danieli apate ufahamu zaidi wa nini kusudi la Mungu. Baada ya kupewa neno lile, aliambiwa mambo mengi sana yaliyo sababisha kuchelewa kwa majibu ya maombi yake. Wewe soma kitabu hicho chote utaelewa ninacho kuambia. Nilitaka uone aina mbili za maneno ya Mungu. Watoto wa Mungu wengi husoma neno, na kulisimamia, leo nataka ukue kiroho, fahamu Mungu anasema leo, anaweza kukueleza wazi kuwa unapaswa uombe nini na kwa mfumo gani wa maombi unayotakiwa uyaombe. Nataka tena nikusisitizie ujue kuwa kuna aina mbili za maneno ya Mungu, neno lililoandikwa ndani ya Biblia, na neno asemalo sasa, kumbuka yupo hai leo anasema kabisa. Anaweza kukufundisha sasa hivi namna ya kuomba, hata kukupa mfumo wa kuomba. Watu wengi wanaomba sana maombi ya kukariri, au ya kimazoea, wataamka usiku saa tisa kuomba kila siku, au kufunga kila siku ya jumapili nk. Unaweza ukawa na mfumo wa namna hiyo lakini ni wa kimazoea tu, wala si wa mapenzi ya Mungu.

Siku moja nilikuwa sehemu fulani, tuliombwa kufundisha huko, ilipofika sehemu ya kuwaombea watu wenye shida mbalimbali, walikuja mbele yangu watu wengi sanaa, kabla ya kuomba, nilimuuliza Roho Mtakatifu hivi. “Roho Mtakatifu watu hawa wamekuja wanashida niwaombeeje?” Akanipa neno akasema, waambie wainue mikono yao juu, halafu sema ‘Baba Mungu tazama watu wako hawa wanashida mbalimbali, naomba wasaidie, katika jina la Yesu’ halafu waambie ‘pokea!’ Nikawaombea sawasawa na nilivyo pokea neno toka kwa Bwana, nilipo sema katika jina la Yesu na kuwaambia pokeaaa! Unajua kilichotokea? Nikajikuta nipo katikati ya watu wengi walioanguka chini! Mimi nimesimama katikati yao nao wamelala chini wote. Mimi nilisukumwa na ile nguvu ya Mungu ilibaki kidogo nianguke na mimi, kila mtu siku ile aliyekuwa mgonjwa alipona. wengine walikuwa na matatizo yao mbalimbali Bwana aliwafungua kabisa, sitaisahau siku ile, kwani kila mtu aliogopa sana, hata mimi niliogopa sana. Siku zote nilizoea kusimamia mistari fulani fulani ya Biblia, sikuwahi kukutana na nguvu za Mungu za kiwango kile cha siku ile nilipopokea neno la Mungu alilosema nami waziwazi. Mungu analo neno lake sasa, la kukuongoza wewe katika maombi yako, jifunze kumsikiliza.

Kuna aina hizo mbili za maneno ya Mungu, anaweza kukupa ufahamu kwa kupitia neno lake lililoandikwa au kwa neno atakalo sema sasa hivi, bahati mbaya sisi tumelizoelea lile lililoandikwa tu. Naamini sasa umeelewa. Moja ya tatizo kubwa linalopelekea tusipokee majibu ya maombi yetu ni hili la kufahamu aina moja tu ya neno la Mungu. Ikiwa leo hii wewe umeokoka, fahamu umeketi pamoja na Bwana katika ulimwengu wa Roho, huyo Bwana ndiye Neno, alisema, anasema, atasema. Kwa kumalizia salamu zetu hizi za mwezi huu, nataka nikutie moyo, soma sana maandiko matakatifu, pia pata ufahamu kuwa kuna aina ya pili ya neno la Mungu nalo ni neno la wakati huu alisemalo Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Mungu akubariki sana.

Mr. Steven & Beth Mwakatwila