Salamu – Agosti, 2011

Bwana wetu Yesu Kristo ni mwema sana, ametujalia tena kupata nafasi hii ya kukutana kwenye kona hii ya salamu za mwezi. Ngoja tuseme Bwana Yesu asifiwe Mpendwa! Sisi ni wazima, tumemaliza semina Mbeya mjini, semina ilikuwa nzuri sana, Mungu alileta watu wengi sana. Amewaokoa na kuwaponya wengi sana, tumejifunza somo zuri sana lenye kichwa cha “Vizuizi vya Mafanikio Sehemu ya Eneo Unaloishi”. Umeisikia hiyo? Unajua kuwa eneo unaloishi linaweza kuwa ndio chanzo cha mafanikio yako yote, yawe ya kiroho au kiutumishi ama ya kiuchumi au kiafya nk? Ukitaka somo hili tuna vitabu, CD, kanda za kaseti, VCD, na DVD, unaweza kuwasiliana nasi ili tukupe nakala uitakayo, na kukujulisha ni kiasi gani unacho takiwa kuchangia. Usiogope, gharama ni ndogo sana, ni ya kuchangia huduma hiyo ili wengine wapate kanda, au CD, ama vitabu nk. Hivi ninavyokuletea salamu hizi nipo Tukuyu Mjini, tunaendesha semina ya siku saba ndani ya kanisa la Moravian Tukuyu mjini. semina hiyo imeandaliwa na Umoja wa Wakristo Tukuyu mjini. Tuna somo la Vizuizi vya mafanikio, ni somo pana sana na zuri, tunahitaji maombi yako. Hebu sasa nikuletee salamu za mwezi huu wa nane.  

Sikiliza, tumekuwa na mfululizo wa Salamu zenye kichwa, MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU).  

Mungu yupo tayari kutupa majibu ya maombi yetu, lakini ili tupewe ni lazima tujifunze kuomba sawasawa na mapenzi yake. Sikia asemavyo. 

Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1Yohana 5:14-15) 

Mapenzi ya Mungu maana yake ni kusudi la Mungu, au mipango ya Mungu. Ili usikike mbinguni na upewe kitu unachokihitaji kutoka mbinguni, unatakiwa kwanza uanze kufanya maombi ya ufahamu kujua ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu katika hicho unacho kihitaji. Katika salamu zilizopita tuliona sehemu ya aina mbili ya maneno ya Mungu. Yaani neno lililoandikwa, nalo lipo ndani ya Biblia, na neno asemalo sasa hivi Mungu kwa kupitia Roho wake Mtakatifu au malaika aliyetumwa kutoka kwa Mungu. Leo tusonge mbele tuone njia atumiazo Mungu kusema nasi. 

Watu wengi wamekuwa na swali hili ndani ya mioyo yao, Mungu atanijulishaje neno lake? Fahamu, Mungu anasema na ana njia nyingi sana ambazo anaweza kuzitumia kuzungumza na mtu, hapo haijalishi sifa za huyo mtu ni mtu wa namna gani na wa umri gani. Neno la Mungu linasema kuwa anaweza kusema nasi kwa njia ya sauti, ukaisikia kabisa akizungumza na wewe, kwa njia ya maono na kwa njia ya ndoto.  

MAONO NA NDOTO 

Neno la Mungu linatufundisha wazi kuwa Baba yetu wa mbinguni anaweza kusema na sisi kwa njia ya maono na ndoto, sikia maneno haya

“Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ijapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, usingizi mzito uwajiapo watu, katika usingizi kitandani; ndipo huyafunua masikio yao, ili amwondoe mtu katika makusudio yake, kumfichia mtu kiburi” (Ayubu 33:14-17) 

Neno la Mungu linatupa akili hapo, linasema hivi, Mungu anaweza kusema na mtu zaidi ya mara moja, kwa kutumia njia tofauti tofauti, anasema anaweza kusema mara ya kwanza, akiona huelewi au hujamsikia asemavyo na wewe atafanya hivi; atakutegea usiku unapolala, ndipo anapo sema na wewe kwa kupitia ndoto au maono. Maono ni jambo la wazi, linaeleweka kabisa, ndoto huja kama fumbo. Ona mfano wa ndoto zilivyo. 

“Ndipo Farao akapeleka watu , akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani, akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye          kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri; Yusufu akamjibu Farao, akisema. Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto na tazama, ng’ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini. Kisha, tazama ng’ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng’ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng’ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha  nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga,wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake. Yusufu akamwambia Farao, ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni. Wale Ng’ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng’ombe saba, dhaifu, wabaya waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa.” (Mwanzo 41:14-27). 

Ukiyasoma maneno hayo utagundua ninacho kuambia kuwa ndoto, ina fumbo, haiko wazi kama ono, ono lipo wazi, ni kitu kinachoeleweka kabisa. Mungu alisema na Farao akampa neno la ufahamu akimwambia mbeleni kuna nini. Alitumia ndoto au njozi. Sikiliza ndugu, Mungu anaweza kuzungumza na wewe kwa kupitia ndoto au maono ukiwa umelala kabisa.Bahati mbaya Wakristo wengi wanapokwenda kulala wanasema wana kwenda kupumzisha mwili, hawajui kuwa kitendo cha kwenda kulala kinaweza kuwa ni sehemu ya kwenda kuzungumza na Mungu. Hawajipangi kwa tendo hilo, ndio maana hata kama akizungumza nao hawawezi kuwekea maanani na kukichunguza na kukitafakari kile walicho kiona usiku walipolala usingizi. Neno  linasema usiku Mungu anatufungua masikio na kusema nasi, na kutuonyesha mambo ambayo ndani yake yanatujulisha yaliyo mapenzi yake Mungu na kututoa kwenye makusudio yetu yaani mapenzi yetu. Sikia mistari hii isemavyo.  

“Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ijapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, usingizi mzito uwajiapo watu, katika usingizi kitandani; ndipo huyafunua masikio yao, ili amwondoe mtu katika MAKUSUDIO yake, kumfichia mtu kiburi” (Ayubu 33:14-17) 

Nilitaka uone neno makusudio yake, neno makusudio ni mipango au mapenzi. Sasa ili leo hii ufanikiwe katika maombi yako lazima ujifunze kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu wala si kwa mapenzi yako. Sasa, ili leo Mungu akujulishe wewe nini yaliyo mapenzi yake fahamu atasema na wewe katika maono au ndoto hizo  unazoziota mara kwa mara. Ngoja nikupe mfano huu; Kuna jamaa mmoja ni rafiki yangu sana, amenipa ruhusa ya kuutoa mfano huu kwako ili somo likukolee. Yeye alikuwa na mchumba wake, walipatana kuoana, siku moja anasema aliona hivi, aliona yupo yeye na dada yake, wanatengeneza barabara, anasema mwisho      wakashindwa kuitengeneza barabara    hiyo, ilikuwa ngumu sana kuitengeneza. Anasema, waliposhindwa kuitengeneza hiyo barabara wakakaa chini, walipokaa na kukata tamaa ya kuitengeneza hiyo barabara, akasikia sauti ikitokea mbinguni, ikamwita jina lake, akaitika, sauti hiyo ikamwambia, ‘njoo kwangu  uniombe nikupe mke, kwani huyo unayemfikiria kumuoa anakwenda kuolewa na mtu mwingine.’ Anasema, akajibu, akisema, ‘Mungu wewe ndiwe ulieniambia kuwa mwanamke huyo ndiye mke wangu, sasa iweje wewe tena uniambie kuwa anakwenda kuolewa na mwanamume mwingine?’ Anasema akasema ‘mimi sikuombi mwanamke mwingine, ila huyo najua ndiye ntakaye muoa.’ Anasema akasikia sauti ile ikamwambia ‘shauri yako!’ Ono likaisha akaamka. Wakati huo ndio mapenzi kati yake na huyo msichana yalikuwa yamekolea    kweli!  

Unajua baada ya miezi michache tu, yule dada akaja akamwambia huyo ndugu  wavunje uchumba, kwani amepata mwanamume mwingine anaona huyo atamfaa kuliko huyo rafiki yangu. Huyo rafiki    yangu alikuwa ni mtu wa maombi sana,    aliliombea mara kwa mara jambo hilo la kuoa kwake, siku moja alipotoka kwenye maombi usiku ndio akaona ono hilo.    Alilipuuzia, lakini baada ya lile tukio la huyo dada kumkataa, akapata ufahamu kuwa Mungu alikuwa amempa taarifa ya jambo analoliombea kuwa halitakuwa  sawasawa na maombi yake, jibu lilipokuja la huyo mwanamke kumkataa, alifadhaika sana, alijiona kama ni mtu aliyekosa  imani, nk. Unajua, inawezekana hata wewe kuna vitu unavyoviomba sana  Mungu akupe, na Mungu anakujibu wewe kwa kupitia maono au ndoto lakini huelewi, na inawezekana umekwama hapo ukisubiri majibu. Mungu anasema na wewe sana kwa kupitia maono au ndoto ila wewe unaona ni kitu cha kawaida        tu. Sikia, ukiomba lazima Mungu atakujibu kama atakupa au hakupi, ama amekupa ila adui kazuia, ona mfano huu… 

“Mimi nitasimama katika zamu yangu,  nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. Bwana akanijibu, akasema iandike njozi ukaifanye iwe wazi katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.    Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikia mwisho wake; wala haitasema uongo; ijapokawia, ingonjee. Kwa kuwa haina budi kuja haitakawia.” (Habakuki 2:1-3) 

Habakuki alikuwa kwenye maombi,unaweza kusema umejuaje, wewe soma kuanzia sura ya kwanza, utaona Habakuki alikuwa amezama kwenye maombi fulani. Habakuki anasema, ntasimama ili niangalie nione lile atakalo nijibu. Ona, hasemi nitasikia kile atakacho nijibu, anasema ataona kile atakachomjibu, tena ataangalia. Nataka uone kuwa Habakuki alifahamu kuwa Mungu huwa anatabia ya kukuonesha kile ajibucho! Mungu anaweza kukuletea jibu la nini mapenzi yake kwa kukuonesha ono wewe ili uliangaliye na ukiliona tayari utakuwa umepewa jibu la nini akionacho Mungu katika hicho  unachokiomba kwake. Baada ya maombi ya Habakuki, utaona kuwa Mungu alimwambia, ajifunze kuandika njozi au ndoto. Mungu alimwambia, atamjibu kwa kupitia ndoto. Swali langu kwako je! Wewe ukoje, una daftari la kuandika yale uyaonayo ulalapo? Unajaribu kuzipitia ndoto au maono uliyo yaona usiku? Au ndio ukiamka unakurupuka tu? Sikia,    nakwambia ukweli Mungu anasema na wewe sana ila haujali. Nataka nikutie moyo leo, pata ufahamu huo, Bwana anataka akuambie mambo mengi sana ila hauzijui njia zake azitumiazo kusema na watu, anaweza kutumia njia hiyo. Nataka kumalizia salamu hizi, kwa kusema tafuta kalamu, na daftari, andika kila unachokiota au kukiona ulalapo, halafu fuatilia    unaweza kuona humo ndani ya maono au hizo ndoto Mungu kasema kitu na wewe ambacho kinakupa ufahamu wa kujua nini yaliyo mapenzi ya Mungu katika hilo  unaloliomba. Habakuki alipewa ndoto. Soma Habakuki sura ya tatu yote utaona jibu alilolipokea lilikuwa ni nini. Nakushukuru sana kwa kusoma ujumbe huu. Bwana Yesu akubariki sana. 

Mungu akubariki sana.

Mr. Steven & Beth Mwakatwila