Salamu – Septemba, 2011

Bwana Yesu apewe sifa sana. Tunaamini kuwa Mungu amekulinda na kukupigania sana katika mwezi uliopita. Mwamini tena Mungu kwa ajili ya mwezi huu wa tisa kukulinda na kukupigania na kukubariki. Mimi na Mke wangu tunapenda kukushirikisha habari hii kuwa tokea tarehe moja mwezi wa nane tumekuwa na huduma katika sehemu mbalimbali, tulianza huduma Tukuyu, tukaenda Mbeya Mjini, tukaenda Pwani. Tunamshukuru Mungu kwa kututumia na kwa yote aliyoyatenda kwenye semina hizo. Kwa kweli tumemuona Bwana Yesu akitenda na kuwafungua waliofungwa na hata kuokoa watu wengi sana na kutufundisha mambo ambayo tulikuwa hatuyafahamu kabisa. Ndugu, hebu tuombee, ili Bwana azidi kufanya kila alichokikusudia kwenye semina zilizo mbele yetu. Unaweza kuingia kwenye sehemu ya ratiba za semina zetu katika tovuti yetu (www.mwakatwila.org) utaona ratiba kwa upana zaidi. Baada ya taarifa hizo sasa nikuletee salamu za mwezi huu wa tisa. Hebu tusonge mbele katika zile salamu zetu zenye kichwa.  

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU).  

Mungu yupo tayari kutupa majibu ya maombi yetu, lakini ili tupewe ni lazima tujifunze kuomba sawasawa na mapenzi yake. Sikia asemavyo. 

“Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1YOHANA 5:14-15) 

Mapenzi ya Mungu maana yake ni kusudi la Mungu, au mipango ya Mungu. Ili usikike mbinguni na upewe kitu unacho unakihitaji kutoka mbinguni, unatakiwa kwanza uanze kufanya maombi ya ufahamu kujua ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu katika hicho unachokihitaji. Katika salamu zilizopita tuliendelea kujifunza kuhusu njia ambazo Mungu huzitumia kuzungumza na mtu. Tuliona njia ya kwanza ni kwa neno lake lililoandikwa yaani Biblia. Na tukaanza kuangalia njia ya pili ni njia ya maono na ndoto. Mungu anaweza kusema na wewe kwa kupitia njia hii ya maono na ndoto, akakufahamisha mipango yake au mapenzi yake ni nini. Ili maombi yako yapate majibu kwa haraka, ni lazima kuanza kuomba kwanza ufahamu kutoka kwa Mungu, akufahamishe ni nini alichokikusudia katika hilo unalolihitaji, na majibu yake anaweza kukufahamisha kwa kupitia ndoto au maono. Hebu tundelee kuona mifano hii katika neno la Mungu inavyozungumzia namna Mungu alivyowafahamisha mipango yake watu mbalimbali. 

Mungu alipokuwa anataka kumfahamisha Ibrahimu kuhusu habari za kupewa baraka za kuirithi nchi ya Kanani, Mungu alizungumza na Ibrahimu kwa kupitia Ndoto.  

“Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likisema, usiogope, Abramu, mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana Abramu akasema, Ee Bwana Mungu, utanipa nini nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua na mwana njiwa, akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kulekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa, uzingizi mzito ulimshika Abrahamu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Bwana akamwambia Abramu, ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi ya isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu baadaye watatoka na mali nyingi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.” (MWANZO 15:1-14).

Ukiyasoma maneno hayo kwa kutulia utaona vitu vingi sana hapo, lakini ninachotaka mimi ukione ni namna Mungu alivyomfahamisha Ibrahimu kuhusu mpango wake wa kumpa Ibrahimu Mtoto na urithi wa nchi ya Kanani, ona mazungumzo kati ya Mungu na Ibrahimu yalifanyika kwa kupitia njozi, fahamu njozi ni ndoto. Mungu alimjibu pia Ibrahimu jibu linalohusu habari ya kupata mtoto, Ibrahimu yeye alifikiri atakaye irithi mali yake ni huoyo mfanyakazi wake, Mungu akampa ufahamu kuwa atakaye irithi nyumba ya Ibrahimu ni mtoto kabisa wa Ibrahimu, tazama, tena Mungu alimpa pia Ibrahimu ufahamu wa uzao wake utakavyo kwenda utumwani miaka mianne, na hata habari za kufa kwake Ibrahimu Mungu alimwambia, alimwambia kwa kupitia ndoto, hilo ndilo nataka ulione. 

Neno linasema hata habari za kupewa nchi na hata maarifa ya kufanya alipewa kwa kupitia neno la Mungu. Aliwambia atoe Ibrahimu akatoa, tazama, inawezekana wewe Mungu kakuahidi kukupa kitu fulani, umesikia na umekimbilia kwenda kumtolea sadaka fulani, swali langu ninalo taka kukuuliza ni nani kakuambia sadaka ya namna hiyo ndiyo Mungu alitaka umtolee? Ibrahimu aliambiwa atoe nini, sisi hatuna muda hata wa kumuuliza swali tutoe nini, si kila sadaka Mungu anataka, mfano, ungekuwa wewe ndio unataka umtolee Mungu unafikiri ungemolea Mungu mbuzi mke? Si ungetoa beberu kama kumunyesha kuwa unampenda sanaaa! Kumbe yeye alitaka mbuzi mke; ungetoa ndama kweli? Si ungetoa dume la ng’ombe kubwa kweli, kumbe yeye alitaka ndama wa ng’ombe. Kwa nini nakuonesha hayo, nataka ujenge tabia ya kuomba maombi ya ufahamu kwa Mungu kwa kila unachotaka kufanya, ili akuonyeshe nini mapenzi yake. Na anaweza kusema na wewe kwa kupitia ndoto au maono. Huu mfano mwingine; 

“Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Bee-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Isareli katika ndoto ya usiku, akaema, Yakobo, Yakobo, akasema, mimi hapa. Akasema, mimi ni Mungu, ni Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.” (MWANZO 46: 1-4). 

Sikia maneno hayo mpendwa, Mungu alimpa Yakobo ufahamu wa nini anachokiona Mungu katika habari za safari ya Yakobo kwenda Misri, naamini Mungu aliona hofu ya moyo wa Yakobo katika safari hiyo, inawezekana Yakobo alikuwa anahofu kuwa je! Mungu yupo naye katika safari hiyo? Pia je! Atafika salama huko Misri na kumuona mtoto wake waliyepotezana miaka mingi sana Yusufu? Alikuwa na mashaka. Mungu aliamua kuzungumza na Yakobo kwa ajili ya hayo anayoyaogopa Yakobo, akamwambia wazi kuwa aende Misri, na atakakuwa naye na atamfanya kuwa Taifa kubwa huko, ona hapo, inawezekana Yakobo asingeenda Misri asingekuwa taifa kubwa! Inawezekana Yakobo alikuwa anaomba sana Mungu amfanye kuwa taifa kubwa kama alivyomuahidi, akamwambia nenda Misri huko ndiko ntakufanya kuwa taifa kubwa. Fikiri alisema naye hayo yote kwa kupitia ndoto! Na amini hata wewe Mungu amekuambia mambo mengi sana kwa kupitia ndoto ila:- Moja; hujui kuwa anasema na wewe, Pili; ukijua unapuuzia, Tatu; unaziogopa sana ndoto na maono! Fikiri leo hii inawezekana unaishi au umepanga kuishi sehemu Fulani, upo katika mipango ya kuhamia huko au unaishi huko, lakini huna uhakika kama Yakobo, fanya maombi ya ufahamu ujue nini yaliyo mapenzi ya Mungu, naamini kama kweli upo tayari kupokea kile atakacho kuambia bila ubishi. Atasema nawewe, na anaweza kusema na wewe kwa kutumia maono au ndoto. Mungu alisema sana na watakatifu wake kwa kupitia ndoto hata leo yupo tayari kusema na wewe kwa kupitia ndoto na maono. Katika kitabu cha Zabauri anasema kuwa, alisema na watakatifu wake kwa kutumia ndoto. 

“Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, ukasema, nimempa aliye hodari msaada; nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu nimemwona Daudi, mtumishi wangu, nimempaka mafuta yangu matakatifu”. (ZABURI 89:19-20). 

Mungu yupo tayari kusema na watakatifu wake leo kama alivyosema nao watakatifu wa zamani kwa kupitia njozi, ona hapo neno linasema alisema nao habari ya nani kamchagua ili awe kiongozi, leo Wakristo wengi hawajui hata ni kweli Mungu kawachagua hao watawala wanaotuongoza, ni kweli aliwatia mafuta ili wawe viongozi, au wamejitia wenyewe mafuta au wametiwa mafuta na vyama vyao au na watu fulani? Kanisa tunatakiwa kabla ya chaguzi tufanye maombi ya ufahamu kujua ni nani kawekwa leo kuwa kiongozi wetu, iwe kanisani, serikalini nk. Sisi tuaangalia sifa kwa nje, tunaangalia elimu, umri, uzuri wa miili nk, lakini Mungu alipomchagua Mfalme Daudi hakuangalia nje, aliangalia moyo, akamtuma Samweli amtie mafuta. Neno la Mungu linasema Mungu alisema na watu watakatifu juu ya kutiwa mafuta Daudi, hebu fikiri wewe hujui kuwa ni nani katiwa mafuta si utajichagulia yule unaye mwona kwa macho yako kuwa ana elimu, mzoefu, nk? Nataka utazame kwa macho ya rohoni, si ya mwilini, unajua ukianza kuomba leo hii kwa Mungu akufahamishe ni nani kiongozi aliyemtia mafuta, atakakufahamisha, kama hayupo katika hao walioteuliwa, bora ujikalie nyumbani kuliko kupoteza muda wako kuwapigia kura watu ambao Mungu hajawachagua.  

Sikia, kwa kupitia njozi Mungu anaweza kutupasha habari za nani kiongozi au nani si kiongozi aliyemchagua. Kama amemtia mafuta mtu fulani na akakuambia mapema, unatakiwa ndio uanze kuomba sawasawa na kusudi lake, ili amuweke hapo madarakani. Tatizo la waombaji wengi, tunaomba kwa kufuata maneno ya magazeti au vyombo vya habari, watu wakisikia anatajwa fulani basi hapo hapo tunauliza kabila gani, dini gani, dhehebu gani nk. Kama yupo sawa na utakavyo unaanza kufunga na kuomba Mungu amchague. Majibu yakija kinyume na ulivyoomba unaanza kufikiri mambo mengi sana. Mungu alimchagua Nebukadreza kuwa mtawala juu ya taifa la Israeli, fikiri, alisema ni mtumishi wake, huyo Nebukadreza hakuwa anamwabudu Mungu wa Ibrahimu wa Isaka na Yakobo, hata Yeremia alipowaambia watu kuwa huyo ndiye Mungu kamwinua kuwatawala wa Isareli lazima wakubali kuwa chini yake, ilikuwa ngumu sana kumuelewa Yeremia. Soma kitabu chote cha Yeremia utagundua ninacho kuambia. Mungu alipanga kuwashikisha adabu wana wa Israeli kutokana na ukorofi wao waliokuwa wanamkorofisha kila mara kwa kuabudu miungu mingine, akapanga kuwapeleka utumwani chini ya Nebukadreza. Ilikuwa ngumu kumpokea, kwanza si mwana wa Israeli, pili hamuabudu Mungu wao, nk. Sikia; Yeremia alioneshwa na Mungu kuwa huyo Nebukadreza ndiye atakaye watawala Waisraeli, na Mungu ndiye aliye mchagua. Walikufa Waisraeli wengi hata Wafalme wa Israeli waliomkataa huyo mfalme mpagani. Sikia asemavyo kuhusu huyo Nebukadreza; 

“Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, nimetia nira ya chuma juu ya shingo ya mataifa haya yote, ili wamtumikie Nebukadreza, mfalme wa Babeli; nao watamtumikia; nami nimempa wanyama na nchi pia” (YEREMIA 28:14). 

Mungu ana mipango yake, sasa ukifanya kinyume cha hiyo mipango yake utapata taabu sana. Leo sisi tunajiombea viongozi tuwatakao bila kupata muongozo kutoka kwa Mungu. Anza kufanya hivi, muulize ana mipango gani na nchi yetu? Na kanisa lake? Muulize ni kiongozi gani atakaye mchagua ili ayatekeleze hayo makusudi ya Mungu? Kama Kanisa tunamkorofisha kwa kubaguana, kufanya uzinzi, kupenda fedha kuliko Mungu nk. Unafikiri hawezi kutuchapa? Atatuchapa, kama alivyowafanya wana wa Israeli, anaweza kutufanyia hata sisi, kama Watanzania tumemkorofisha na anataka kutunyoosha anaweza kutuchapa, atatuinulia mtawala ambaye kila mmoja atajuta na kumkumbuka Mungu, ili tujue yupo Mungu anayetawala na tutubu makosa yetu, kama tulibaguana tuunde umoja. Fikiri leo kanisa lipo vipande vipande kila mmjoa anajiona yeye bora kuliko mwenzie, na Mungu anataka kutukusanya unafikiri atafanya nini? Kama si kumuinua Nebukadreza atutawale na kutunyoosha kweli ili turudi pamoja kwa umoja na kufanyika kama mwili wa Krsito mmoja wenye viungo vingi. Mungu anaweza kabisa kutujulisha mipango yake hiyo kwa njia ya maono au ndoto. 

Ni imani yetu kuwa salamu hizi umezipokea kwa mikono miwili na utaanza kuzifanyia kazi. Mungu akipenda, tuonane tena mwezi ujao katika kona hii. 

Mungu akubariki sana.

Mr. Steven & Beth Mwakatwila