Salamu – Februali, 2021

Tunakusalimu ndugu yetu kwa jina la Bwana Yesu Kristo. Karibu tena katika kona hii ya salamu za mwezi. Namshukuru Mungu aliyetupatia mwezi huu wa pili. Naamini Mungu amekuvusha salama kuingia mwezi huu wa pili na pia ni imani yetu kuwa utabarikiwa mnoo na salamu za mwezi huu.

Kumbuka tuna salamu zenye kichwa “VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.”

Katika salamu zilizopita tulianza kwa kuangalia malengo hasa ya somo hili. Hebu tusogee mbele kidogo tuangalie lengo la tatu

3: KUSUDIO LA TATU: NI KUTUTENGENEZEA NIDHAMU KUBWA KATIKA HABARI ZA KUSIKIA KWAKO

Lengo la tatu la kupewa somo hili ni kututengenezea sisi watoto wa Mungu nidhamu au tahadhari kubwa katika habari za kusikia kwetu.

Unajua ni kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu mafanikio yako wewe na uzao wako au mateso yako na uzao wako yamefungwa katika kusikia kwako tu.

Angalia mistari hii isemavyo kuhusu habari za kusikia “BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari; Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.” (Isaya 48:17-19).

Ukiisoma mistari hiyo unaona kuwa kizazi hicho kilikatwa kwasababu ya mtu mmoja tu ambayealikosea katika eneo la kusikia kwake. KWA MUJIBU WA MISTARI HIYO UNAONA ILI MTU AWE NA AMANI KUBWA AU BARAKA KUBWA INATEGEMEA NAMNA ALIVYOSIKIA. NENO AMANI NDANI YAKE KUNA MAANA YA BARAKA.

Umewahi kujiuliza swali hili; kwa nini watu wengi leo hii hawana amani na hawana mafanikio? Jibu ni rahisi tu, na ni hili la namna wanavyosikia….. Unaweza kuniuliza umejuaje? Wewe isome hiyo mistari utaona hiki ninachokufundisha. Ukijifunza namna ya kumsikia Mungu nakwambia ukweli utajikuta unamafanikio na ukikosea tu kwenye eneo la kumsikia utajikuta upo kwenye magumu.

Ngoja nikupe mfano. BWANA YESU KRISTO ALIWAAMBIA WANAFUNZI WAKE WAOMBE ILI WASIINGIE MAJARIBUNI. WAO HAWAKUOMBA WALILALA. KITENDO CHAO CHA KUTOKUISIKIA ILE SAUTI KILIWAPELEKEA MAJARIBUNI.

Hata leo hii tumeagizwa tuombe ili tusiingie majaribuni, lakini angalia namna tunavyoomba, utaona hatuombi kisa ni hiki hatuna nidhamu katika habari ya kusikia kwetu.

Sikia mpendwa, ili ufanikiwe ni lazima uwe makini katika habari kusikia kwako. Biblia inasema hivi. “Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi BWANA, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng’ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa. Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.” (Kum 7:12-15)

Mafanikio yetu yamefungwa katika maeneo matatu, kusikia, kukishika kile ulichokisikia na kukifanyia kazi kile ulichokisikia.

Shida yetu kubwa hatujui kuwa tunahitaji kuwa wazuri mnoo katika habari ya kumsikia Mungu.

Pia tumeagizwa tuliangalie sana lile tulisikialo. Biblia inasema hivi “Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.” (Marko 4:23-24).

Ili tuongezewe au tukipoteze kile tulichonacho inategemea namna tunavyomsikia Mungu.

KATIKA MAOMBI YAKO JIFUNZE KUMUOMBA MUNGU AKUPATIE SIKIO LA KUMSIKIA NA AKUONDOLEE UGUMU WA MOYO WAKO WA KUTOKUMSIKIA.

Ukisoma Biblia kwa kutulia unajifunza kuwa unaweza kuwa na masikio kabisa lakini usisikie, na unaweza kuwa na masikio na ukapewa nguvu ya kutokusikia yaani ukawa na masikio yasiyosikia.

Angalia mistari hii uone hiki ninachokufundisha. “Haya ndiyo maneno ya agano BWANA alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu.Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote BWANA aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote;yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu;lakini BWANA hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi.” (Kumbukumbu la Torati 29:1-4)

UKIISOMA MISTARI HIYO UTAONA JAMBO LA AJABU SANA. Hawa watu walipewa macho na waliona. Lakini Biblia inasema hawakupewa macho ya kuona, walipewa masikio lakini hawakupewa kusikia. Cha ajabu ninachokiona hapo ni hiki Mungu aliwafanya wasisikie ingawa wana masikio na si viziwi.

KUNA VITU AMBAVYOHUVISIKII. HATA VIKISEMWA HUWEZI KUVISIKIA MPAKA UOMBE MUNGU ILI UVISIKIE.

Ngoja nijaribu kukuonyesha ni nini ninachotaka kukufundisha. NIMEKUA NA MASWALI MENGI KWA NINI KUNA WATU UNAJARIBU KUWAAMBIA NINI WAFANYE BAADA YA KUWAELEZA UTAWAULIZA MMENISIKIA WATAJIBU NDIYO. BAADAYE UTASHANGAA WATAKAVYOTENDA AU KUELEZA KILE WALICHODAI WAMEKISIKIA UTAGUNDUA KUMBE HAWAKUSIKIA ULIPOKUA UKIWAELEZA.

Watu wengi hawasikii nakwambia, kuna usikiaji maalumu ambao watu wengi wameukosa na bahati mbaya hawajui kuwa hawasikii. Mungu anasema sana na wewe lakini husikii kwa sababu haujapewa masikio ya kusikia. Lazima ujifunze KUOMBA MUNGU AYAFUNUE MASIKIO YAKO ili umsikie.
Biblia inasema hivi “Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu.“ (Ayubu 36:10)

Hao ndugu sikuwa walikuwa viziwi, walikuwa na masikio kabisaa lakini ili wasikie ilibidi Mungu ayafunue masikio yao.

Unajua dhambi ilipoingia pale bustanini Edeni iliharibu kila kitu, hata usikiaji wetu uliharibika kabisaa tunahitaji kurudi kwa Mungu kila mara kumuomba ayashughulikie masikio yetu ili tusikie vema.

Anza kuomba mpendwa kwa Mungu ili ayazibue masikio yako umsikie.

Kwaleo niishie hapo. Hebu tufuatane katika kona hii mwezi ujao naamini utapata kitu cha kujifunza. Mungu akubariki sana

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222