Salamu – Januari, 2021

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Mimi na familia yangu tunawasalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo.

VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

UTANGULIZI

Ni imani yetu kuwa Mungu amekupatia mwaka huu mpya kwa lengo maalumu kabisa. Hebu tulia kwake na mwombe akuongoze katika mwaka huu.

Tumekuletea salamu za mwezi. Ni salamu maalumu kwa mwezi huu wa kwanza kwa mwaka 2021.

Naamini utapata kitu kipya cha kukusaidia mno katika maisha yako ya kiroho kwa kupitia somo hili lenye kichwa “VIPAUMBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.”

Hebu tuanze kujifunza. Naamini unaomba maombi mbalimbali. Sikia, MOJA YA JAMBO UNALOTAKIWA ULIWEKE KWENYE MAOMBI YAKO MARA KWA MARA NI HILI LA KUOMBA MUNGU AKUPE SIKIO LA KUMSIKILIZA.

Kabla hatujaenda mbali katika kujifunza hebu nikuonyeshe jambo hili muhimu mno.

LENGO LA KUJIFUNZA SOMO HILI.

Kila somo tupewalo na Mungu fahamu ndani yake linakua na makusudio au malengo maalumu. Hata katika somo hili kuna malengo maalumu yaliyokusudiwa.

Hebu tuyaangalie kwa ufupi malengo ya somo hili ni nini haswa.

1. LENGO LA KWANZA: KUIMALISHA MFUMO WA MAOMBI YAKO.

Unaposoma maandiko unaona wazi kuwa Mungu anataka tuombe. Angalia mistari hii isemavyo. “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;”(Wakolosai 4:2) Angalia na mistari hii “ombeni bila kukoma. (1The 5:17)

Kwa mujibu wa mistari hiyo unaona tumeagizwa mimi nawewe tuombe na tusikome kuomba. Suala la kuomba ni swala la kudumu, Biblia inaita kukesha, yaani ni jambo la kutokuacha.

Somo hili lengo lake ni kukuhimiza wewe mpendwa uweke bidii ya kuomba kila mara.

HILI SI SUALA LA KIKUNDI TU. Unapoisoma hiyo mistari unaona wazi kuwa Mungu anaongea na kila mtu anayemwamini kuwa ADUMU AU AKESHE KTK KUOMBA

Watu wengi hawana muda wa wao kuomba. Wengi hutegemea watu wengine wawaombee kwa Mungu. Sikia kama kuna kikundi cha maombi ni vizuri..lakini wewe mwenyewe unatakiwa uwe muombaji bila kuacha ..

Kitendo cha kutokuomba fahamu unakua unakwenda kinyume na maagizo ya Mungu, lazima utenge muda wa wewe binafsi kumuomba Mungu.

SI SUALA LA JINSIA. Unaposikia habari ya kuomba unaona kuwa wanaume wengi hawana muda wa kuomba. Kisa ni wazo lililo ndani yao kuwa wanawake ndiyo waliyopewa nafsi hiyo ya kuomba. Sikia, moja ya kosa kubwa ambalo wanaume wengi wanalifanya ni hili la kufikiri wao hawatakiwi kuomba ila wanawake.

ANGALIA HIYO MISTARI UTAONA HAKUNA ENEO KATAJWA MWANAMKE NDIYE INATAKIWA ADUMU KUOMBA..NI KILA MKRISTO.

MWANAUME KAMA KICHWA UNAHITAJI MAWASILIANO NA MUNGU KULIKO MWANAMKE. Unaweza kuniuliza swali kwanini mimi mwanaume niwe mwombaji kuliko mwanamke? Kuna sababu nyingi tu. Moja ya sababu ni hiii: Mwanaume kama kichwa unatakiwa uwe na mawsiliano na Mungu kwa ukubwa mnoo. Macho yako ndiyo yanatakiwa yaone njia ya kuipitisha familia yako

Mwanaume ndiyo anatakiwa aone njia ya kupita kama kiongozi. Angalia mistari hii “BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.”( Zaburi 103 6-7)

Wana wa Israeli wao hawakuona njia ya kupita, waliona matendo. Musa ndiye aliyepewa kuiona njia na njia hizo alijulishwa na Mungu.

Musa alikua na kawaida ya kumwendea Mungu kama kiongozi na kumuomba tena kwa kulia amjulishe cha kufanya. Angalia mistari hii uone alichokuwa anafanya kama kiongozi. “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.” (Kutoka 14:13-15)

Musa alikuwa na tabia ya kumwomba Mungu na Mungu alimpa maarifa ya kufanya. Wana wa Israeli hawakujua maarifa hayo aliyopewa Musa ni yapi, wao waliona tu fimbo ikiinuliwa na maji kupigwa na kutawanyika.

Wewe mwanaume kama kiongozi wa familia unatakiwa uwe na tabia ya kumwomba Mungu ili akujulishe namna ya kufanya ili uivushe vema familia yako kwenye kila jambo.

Hata viongozi wanaume, hebu tujifunze kuwa na muda mrefu na Mungu kwa kupitia maombi.

Kitendo cha kutokuomba kinapelekea kwa viongozi wengi kukwama na kujikuta wakitegemea akili zisizo na matunda. Kila mwanaume unatakiwa uwe mwombaji.

Sikia, mkeo akienda kuomba na wewe huendi fahamu kesho atakua ndiye mkuu wa familia. Kwa sababu Mungu atamjulisha njia za kuipitisha familia wakati wajibu huo uliwekwa mikononi mwako mwanaume. Kama watoto ndio waombaji fahamu Mungu hatawaficha njia za kupita, na hapo ndipo hutokea cheche kutokuelewana na watoto.

Watoto wataona njia na wewe baba hujui nini kikupasacho kukifanya. Hebu mwanaume anza kuomba utashangaa kuona njia zikupasazo kuzipita.

2: LENGO LA PILI NI KUJIFUNZA KUOMBA. HATUJUI KUOMBA TUNAHITAJIKA KUJIFUNZA KUOMBA. ROHO MTAKATIFU KAMA MWALIMU YUPO TAYARI KUTUFUNDISHA KILA JAMBO HATA KUOMBA

Biblia inasema wazi kuwa mimi na wewe hatujui kuomba ipasavyo. Angalia mistari hii. “Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.” (Warumi 8:25-27).

Kwa mujibu wa mistari hiyo hatujui kuomba, kwa kuwa hatujui kuomba tunahitaji kujifunza kuomba. Biblia inasema kuwa siku moja wanafunzi wa Bwana Yesu Kristo walimwendea na kumwomba awafundishe kuomba .

Angalia mistari hii isemavyo. “Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] Utupe siku kwa siku riziki yetu.Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].”(Luka11:1-4)

Wanafunzi walimwomba Bwana Yesu Kristo awafundishe kusali, unajua aliwafundisha, hata leo hii tunaye mwalimu wetu mkuu naye ni Roho Mtakatifu.. anaweza kutufundisha kila kitu, hata kuomba anaweza kutufundisha tukimwomba atufundishe.

Ndani ya somo tutajifunza kipao mbele kimoja wapo cha maombi ambacho wewe na mimi tunatakiwa tuombee mara kwa mara kwa Mungu. Hebu tufuatane katika kona hii mwezi ujao, naamini utapata kitu cha kujifunza.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.