Salamu – Disemba, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe. Ninakukaribisha tena katika eneo hili la salamu za mwezi. ili tupate kujifunza somo hili muhimu.

Hizi ni salamu za mwezi wa kumi na moja Kumbuka tunamfululizo wa salamu zenye kichwa.

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

JIFUNZE KUTUMIA CHAKULA CHA MAALUMU KATIKA MFUMO WA MAOMBI YA NAMNA HII.

Sikiliza ninapokufundisha suala hili nataka unielewe mpendwa kuwa si lizungumzii hili jambo kwa mfumo uliouzoea uliopo kanisani kwenu. Wala sina mpango wa kukutoa katika huo mfumo wa kushiriki chakula cha Bwana katika utaratibu mlionao kanisani kwenu.

Nimeanza kukueleza hivyo kwasababu masomo ya namna hii ni mageni kwa watu wengi sana lakini yapo kwenye Biblia. Ebu tuliangalie hili jambo kwa mfumo huu wa kula chakula maalumu katika eneo la maombi ya namna hii.

Angalia mistari hii. “ BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo.Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele”(Kutoka 12:1-14).

Unapoisoma hii mistari utajifunza hapo mambo mengi sana. Mimi nataka tuyaangalie mambo mawili tu hapo.

JAMBO LA KWANZA.

Unapo iangalia hiyo mistari unaona chakula maalumu kilicholiwa kililiwa kifamilia. Sijakosea nasema kifamilia. Angalia neno la Mungu linasema hivi ”Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu ….”

Kumbuka tuliko toka nimekuambia chakula hiki ninachokufundisha hapa usikihusishe na chakula cha ushirika mtakatifu au meza ya Bwana au chakula cha Bwana huko kanisani kwenu. Hiki ni cha kula maalumu kinacholiwa kifamilia, unaweza kuniuliza kivipi Mwakatwila? Angalia hiyo mistari. Chakula hicho maalumu kililiwa kifamilia katika kila nyumba, kila mtu alikaa ndani ya nyumba yake na waliomo humo ndani ya nyumba yake na walikula kifamilia. Kilikua chakula kamili kabisa cha kifamilia au niseme cha kila mtu na nyumba yake na waliomo ndani ya hiyo nyumba na walipewa agizo kutoka kwa Mungu la kula chakula hicho kifamilia. Unaweza kuniuliza chakula hiki si ndiyo kilekile kiliwacho leo makanisani mwetu? Ni kweli ndiyo hicho hicho. Lakini angalia kwa makini upo utofauti mkubwa wa mfumo wa hicho chakula katika eneo la kushiriki kwake.

Watu wanaokula chakula hiki huko kanisani si kifamilia. Ndiyo maana utaona wazi kabisa mama anaweza shiriki chakula hiki huko kanisani kwake ila mume wake akawa si mshirika hapo na asiruhusiwe kukila. Na hata mfumo wa ulaji haufanani kabisaa. Kanisani wataangalia sifa za huyo mwamini, huku katika familia wataangalia sifa za mtu anaishi ndani ya hiyo nyumba.

Hiki ninachokufundisha hapa ni cha kifamilia mpendwa kila mtu na nyumba yake. Najua wengi elimu hii ni mpya kwao. Ndiyo maana nimekueleza usifikirie kabisaa habari ya chakula kiliwacho huko kanisani hiki ni chakula maalumu kiliwacho katika nyumba za watu.

JAMBO LA PILI

Unapoitazama hiyo mistari utaona chakula hicho maalumu kililetwa au kilibeba kusudi maalumu. Yapo makusidio mengi tu, Moja ya kusudi lilikua ni kutengeneza alama maalumu ya ili kuizuilia tauni iliyoachiliwa isiingie kwenye nyumba ya hao waliomo ndani ya nyumba hiyo. Ili isiwaharibu waliomo ndani ya hiyo nyumba pia kumlinda mzaliwa wa kwanza wa hiyo nyumba. Ntakuelekeza vizuri huko mbele. Kumbuka mharibu aliyeachiliwa kufanya kazi kuwauwa wazaliwa wa kwanza alishindwa kuingia kwenye nyumba au familia ambazo walikula chakula hicho maalumu na kufanya mambo maalumu waliyoagizwa wayafanye kama familia.

Angalia waliagizwa, wale chakula na wa weke alama ya damu katika nyumba zao. Kuna kitu hapa nataka ukione nacho ni hiki wale chakula. EBU SEMA WALE CHAKULA,! Ili tauni isiwagonge kwenye hizo nyumba walifundishwa kula chakula maalumu pia. Inawezekana bado hauja nielewa, sikia. Ni rahisi kuona suala la damu tu kuweka miilangoni lakini usilone suala hili la kula chakula. Haya mambo mawili yalienda sambamba

Ni kweli tunaweza omba damu ya Yesu ilinde nyumba zetu. Lakini nikuambie kuna mwili wako kulishwa na kunyweshwa pia

Angalia kwa makini hiyo mistari. Hao ndugu walikula hicho chakula wote na waliweka damu katika miimo na vizingiti vya milango yao. Na hawakula nyama tu yaani huyo pasaka walikula mkate na hata mboga, angalia mistari hii hapo isemavyo. “Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu.” (Kutoka 12:8).

Swali la kujiuliza kwanini waliambiwa wale nyama na mboga na mkate? Naamini lazima walikunywa hata maji na ilikua chakula cha kila mtu kushiba. Hebu tujiulize haya maswali Kwanini waliambiwa wale na kuweka damu milangoni? Kwanini wasiweke damu tu milangoni?

Unajua nirahisi kuona damu tu mlangoni lakini usione umuhimu wa chakula. Ngoja nikuulize swali, kama ile damu ilikua ya kumlinda mzaliwa wa kwanza tu na tauni kwanini watu wengine ambao si wazaliwa wa kwanza waliambiwa wale chakula?

Pia lazima ufahamu hata huyo mzaliwa wa kwanza pia alikula hicho chakula. Kama na yeye alikula hicho chakula fahamu chakula hicho maalumu kilicholiwa kifamilia kilibeba siri kubwa mnoo.

Na unapoisoma hiyo mistari unajifunza vitu vingi sana. Angalia hapohapo mfano huu Mungu anasema . “Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazo kuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele”

Anaposema lisiwapate pigo lolote. Maana yake kulikua na mapigo si ya aina moja tu ya mzaliwa wa kwanza kama wengi tunavyojua. Angalia kama pigo lilimhusu mzaliwa wa kwanza tu, Mungu asingetumia neno lisiwapate pigo lolote, angetumia neno lisimpate( mzaliwa wa kwanza) pigo lolote.

Anaposema lisiwapate,maana yake kulikua na mapigo ambayo hayakumhusu mzaliwa wa kwanza tu. Ngoja nijaribu tena kukuonyesha, angalia tena Mungu anasema. “nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu”

Kwa mujibu wa hiyo mistari utaona kulikua na mapigo ambayo yaliweza kuwaharibu hata hao ambao si wazaliwa wa kwanza. Ndiyo maana Mungu akasema waweke damu na wale chakula hicho maalumu. Kwa mujibu wa hiyo mistari unaona damu na hicho chakula havikuwekwa kwa ajili ya kumkinga mzaliwa wa kwanza tu aliyomo ndani ya hiyo familia. Vitu hivyo viwili yaani damu na chakula vililenga kuwalinda pia watu wengine waliomo ndani ya hizo nyumba na mapigo ambayo yaliachiliwa huko misri.

Unaweza kuniuliza kwa nini unasema mapigo.? Angalia Mungu anasema hivi. “nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote” anaposema pigo lolote, maana yake halikuwepo pigo moja tu. Yalikuwepo mapigo mengi tu. Watu wengi wanaangalia pigo moja tu la mzaliwa wa kwanza. Kwa mujibu wa maneno hayo unaona tauni iliyoachiliwa Misri haikufanana. Ilikuwepo ya kumuua mzaliwa wa kwanza tu, pia kulikua na uharibifu mwingine unao haribu inawezekana mwili,uchumi nk.

Kwa hiyo lazima tujue kutumia damu ya pasaka na chakula. Kumbuka walikula mboga na nyama.

MUNGU HUTUMIA CHAKULA KUULINDA MWILI WA BINADAMU NA MARADHI MBALIMBALI

Sikiliza. Mungu ana njia nyingi tu za kutulinda dhidi ya malazi. Anaweza kutumia chakula pia. Mungu anapotufundisha kula chakula maalumu au chakula cha kiibada ndani yake fahamu anakua amekusudia kuulinda mwili wa huyo mtu. Katika agano hili jipya tumeruhusiwa kuula mwili wa Bwana Yesu Kristo na kuinywa Damu yake kabisaa kwa imani.

Mfano. Unapo kiandaa chakula hicho maalumu,Siku hiyo jenga imani kuwa unakua unakula mwili wa Kristo na unapoandaa maji,soda,au kimiminika chochote ambacho si pombe unakua unainywa damu ya Yesu Kristo.

Angalia jambo hili. “Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu;kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]”(Luka 22:15-20).

Angalia mpendwa, katika kipindi kile, wale ndugu walikula nyama na mboga na mkate. Kumbuka hao ndugu hawakua na mchele wala mahindi, kwa hiyo usifungwe kuandaa wali viazi nk. Usiseme mbona kanisani hatuli hivyo? Nimekuambia hiki chakula ni cha kifamilia ni chakula maalumu. Nichakula ambacho kinaliwa siku hiyo kwa IMANI.

Ngoja nikufundishe kitu, chakula cha mfumo huo fahamu ndani yake kinabeba ulinzi wa mwili wako wewe na hao ulionao humo ndani ya nyumba yako. Fikiria kitu hiki. Bwana Yesu aliwapa hao watu mkate kabisaa kitu halisia lakini akawaambia huo ni mwili wangu. Akawapa divai kabisaa halisia akawaambia hii ni damu yangu. Angalia kitu, mkate ulitakiwa kuliwa na divai ilitakiwa kunywewa. Lilikua ni tendo kamili. Utofauti wake ulikua katika picha ya machoni iliyoonekana. Walipokua wakila walikula mkate KWA IMANI ULIKUA MWILI WA BWANA YESU KRISTO WALI KUNYWA DIVAI KWA IMANI WALIKUA WAKIINYWA DAMU YA YESU KRISTO.

Unaweza kuniuliza kwa nini unasema walikula na kunywa kwa kwa Imani? Sikiliza imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyooneka “ ( Waebrania 11:1). Na imani huja kwa kusikia. (Warumi 10:17) Hao ndugu walisikia neno la Bwana Yesu Kristo kuwa wanakunywa damu na wanakula mwili. Wakaamini na bila shaka walikula na kunywa. Macho yao hayakuona damu wala mwili ila WALICHOKISIKIA KUTOKA KWA BWANA YESU KRISTO NDICHO WALICHOKUA NA UHAKIKA NACHO.

Hata wewe unapoandaa chakula hiki maalumu kwa ajili ya nyumba yako ili kutengeneza ulinzi wa nyumba yako na mwili wako katika kuokolewa na mapigo mbalimbali yaliyoachiliwa juu ya nchi amini unachokila ni mwili wa Bwana Yesu Kristo na hicho utakachokunywa na familia yako ni Damu ya Bwana Yesu Kristo.

Sikiliza kitu hiki. Wale ndugu kule katika agano la kale waliambiwa wale chakula na waweke damu kwenye miimo na vizingiti vya milango yao. Fahamu walifanya kwa imani. Hao ndugu hawakupewa nafasi ya kuinywa damu, walipewa nafasi ya kumla pasaka yaani ile nyama,mkate,na mboga. Wewe umepewa nafasi ya kuinywa damu ya Bwana Yesu Kristo na hata kuiweka kwenye miimo ya nyumba yako na kuula mwili wake yeye badara ya wewe kuchinja mnyama. Na unakula mwili huo kwa imani

Mkate au wali nk na mboga unavyo, na mwili wa Yesu ambao leo hii ndiyo pasaka unao. na naupata kwa imani, na damu ya Bwana Yesu Kristo unayo unaipata pia kwa imani. KUMBUKA ULAJI WAKE NI LAZIMA VIWEPO VITU ASILIA VINAVYOTUMIKA KATIKA ULAJI HUO. Mfano ili uinywe hiyo damu unatakiwa na kinywaji au kimiminika chochote ispokua pombe na sumu au chakula chochote. Fahamu unapokula na kunywa chakula hicho kuna kitu Mungu atakiachilia kwenye mwili wako ambao unawindwa na tauni.

Ngoja nikupe mfano halisi tu labda ndiyo utanielewa ninaposema ule chakula na unywe. Corona ni ugonjwa wa mapafu, unaweza kukohoa na mafua nk. Na kiukweli wenye kinga nzuri za mwili wakiupata ugonjwa huo wala hauwasumbui kabisaa. Atakohoa siku tatu hivi kwisa siku kumi na nne mzima kabisaa.

Binafsi mimi nilikua na shida mnoo ya mafua. Yaani niklikua nikikutana mavumbi kidogo tu mafua, nikikutana na baridi kidogo tu mafua. Yaani nisitumie mic ambayo imetumika na mtu mwingine nilikua napata mafua.

Siku moja nilienda duka furani la madawa, imepita miaka mitano hivi. Nilipokutana na hili ninalotaka kukuambia. Nilienda hapo dukani kutafuta dawa kwa ajili ya mafua niliona dalili za mafua. Sasa sikia,yule mwenye duka aliniuliza nikusaidie nini? Nikamwambia nataka dawa ya mafua,

Akaniambia kwa ukali ” Watu wengine sijui mkoje, yaani leo nikuambie ukweli wewe unapata mafua kipindi hiki ni kwasababu hunywi maji kwa wingi, na huli matunda kwa wingi hasa machungwaa ndiyo maana unapata shida hiyo. Hakuna dawa ya mafua!! Unajua alikua na dawa nyingi tu hakuniuzia aliniambia nenda nyumbani kachemshe maji na ununue machungwa mengi kula wee harafu uone!

Unajua ni kweli mimi nilikua simwi maji kabisa, yaani maji tokea nakua mama alikua ananichapa nenda kanywe maji!!! Ugomvi wangu na maji ni ulikua ni kwenda chooni. Mimi niknywa maji kidogo ntaenda chooni, niliwahi kutafuta daktari aniangalie lanpbda ninatatizo. Akaniambia huna tatizo ila figo zako ziko vizuri kweli.

Basi nikaanza kunywa ila siyo sana mpaka siku moja Roho Mtakatifu aliniambia, kunywa maji mengi. Tokea siku hiyo najitahidi kunywa maji.. Machungwa ndiyo kabisaa nilikua siyapendi, ehehee yaani mimi kwa kweli kwenye eneo la kula kwangu ilikua shida sana. Huwa nasahau kuwa hivi nimekula au bado!!!! Mke wangu Mungu amemsaidia kuniimiza kula na kunikumbusha Mungu amekuambia kunywa maji.

Nikanunua machungwa nikanywa na maji ya moto asubuhi sikua na mafua. Nilikua najua mafua ili yapone ni siku kama kumi na nne hivi. Hizo kinga za mwili zinatengenezwa na nini? Sikia inatengenezwa kwa mfumo wa chakula tunachokula na vile tunavyokunywa. Sasa basi kwa mfumo wa maisha ya watu wengi kinga hizi zinahitaji za miili yetu zinahitaji msaada mkubwa mnoo kwasababu watu wengi tena wengi mnoo eneo hili linashida. Kwa hiyo kinga hizi zina hitaji hapo ngoja nikuandikie kwa kiswahili ili unielewe vizuri (ZINAHITAJI BUSTA)

Kitakacho ziongezea nguvu hizo kinga zako za mwili ili corona hata ikikupata isikusumbue ni chakula mpendwa. Na ni chakula cha mfumo huu yaani maalumu. unakunywa damu ya Bwana Yesu Kristo na kuula mwili wa Bwana Yesu Kristo kwa KUPITIA HICHO CHAKULA MAALUMU UTAKACHOKILA HAPO NYUMBANI KWAKO. Kiukweli tunahitaji msaada mkubwa katika mfumo huu wa kula kwetu hasa watu wa mjini mjini. Hizi chips hizi weee acha tu!!!! Tuna hitaji msaada mkubwa katika chakula tunachokula ilikitumike katika kuulinda mwili. Fikiria ndiyo una malazi kama sukari,bp au ndiyo umri umeenda nk au ndiyo una afya mgogolo. Unafikiri kinga zako ziko vizuri. Kitakacho tusaidia ni hiki ninachokufundisha chakula maalumu. Kwa lugha nzuri chakula cha KIMUIJIZA KWA AJILI YA AFYA YA MWILI PIA. KUANZIA SASA LAZIMA TUISHI KWA IMANI NA TUANZE KULA KWA IMANI NA TUNYWE KWA IMANI ILI MIILI YETU ILINDWE NA NGUVU ZA MUNGU ZINAZOPITIA CHAKULA.

UNACHOTAKIWA UKIFANYE

Jambo la kwanza ni kuamini.

jambo la pili, kula chakula cha kuwatosha yaani mkimalize. Mfano ukikileta mezani hicho chakula maalu MLECHOOTE MSIBAKIZE. KIKIBAKI KICHOMWE. Soma hiyo Kutoka 12.

Jambo la taru TUBUNI DHAMBI ZENU YAANI MUWE SAFI.

Jambo la nne. Samehe woote waliokukosea usiwe na kinyongo nao.

Jmbo la tano Baada ya kula ombeni. Omba Mungu apitishe ulinzi mwilini kwako kwa kupitia hiyo damu na chakula ambao ni mwili wake.

Si unajua ukiula mwili au damu si inakwenda kukutengenezea afya mwilini? Lazima ujue pia upo utofauti wa matumizi ya damu ya Bwana Yesu Kristo na mwili wake. Unaweza kuitumia hiyo damu kwa kujitakasia nk pia ukaitumia kama kinywaji!!! Hata mwili wa Bwana Yesu unaweza kuliwa na unaweza kuutumia kukubebea dhambi na laana zako zoteee. NI WEWE TU UNATAKA NINI.

Kwa hiyo hapa nakufundisha matumizi ya damu ya Yesu Kristo kama kinywaji na mwili wake kama chakula. Sasa fikiri mwili wako umebeba damu Ya Bwana Yesu Kristo na mwili wako huo umebeba ndani yake umeubeba mwili wa Bwana Yesu Kristo nini kinatokea au nini kitauharibu mwili wako? Hakuna pigo litakalofua dafu nakwambia. Mwisho baada ya kula mshukuru Mungu. unaweza kwenda hata kutoa sadaka ya shukrani. Naamini umenielewa na umeona umuhimu wa kufanya maombi ya namna hii usiku. Kwasababu familia yoote inakua imeludi nyumbani na itakula chakula hicho kwa pamoja.

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.