Salamu – Mar, 2011

Ndugu yetu tuna kusalimu katika jina la Bwana Yesu Kriasto.  Mimi na familia yangu tuna kila sababu za kumludishia Bwana heshima na shukrani nyingi sana kwa mambo mengi mema aliyotutendea ndani ya mwezi uliopita. Mungu ametulinda na kutupigania kwenye mambo mengi sana. Tumemuona akitupatia kibari cha kumtumikia kwa kutupa nafasi ya kufundisha katika semina karibu zote tulizozipanga kwa miezi hii mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu wa 2011.  Kwa kweli tunamshukuru sana Mungu. Mwanzoni mwa mwaka huu tulikuwa na mipango miwili ambayo tumemwomba sana Mungu atufanikishie nayo ni utanuzi wa hema letu ambalo tunalitumia kama darasa la linalo tembea. Pia tumekua na mpango wa pili nao ni wa kununua viti, kwa ajiri ya huduma hii. Tunamshukuru Mungu ambaye amewagusa watu wengi sana kwa kutusaidia katika kuikamilisha mipango yetu hii.  

Katika suala la kutanua hema na jukwaa, tunaenda vizuri, tayari tumekusanya vyuma vingi kiasi cha fundi kuanza kuunganisha. Tunamshukuru kila mtu ambaye amejitoa mali zake fedha zake kwa ajiri ya kazi hii ya utanuzi wa hema. MUNGU YESU KRISTO AKUBARIKI SANA. Pia tunamshukuru Mungu sana kwa kila mtu aliyetoa fedha zake kwa ajiri ya kununulia viti, na kwa wale wote waliotoa viti kwa ajiri ya kazi hii ya Bwana. MUNGU YESU KRISTO AKUBARIKI SANA. Pia tunatoa shukrani zetu kwa kila mtu aliyechangia fedha zake kwa ajiri ya huduma za ledioni. MUNGU YESU KRISTO AKUBARIKI SANA. Tunamwamini Mungu kuwa atakwenda kukubariki sana na ataikumbuka kazi yako hiyo uliyoifanya. Tunaludia tena kusema Asanteni sana. 

Pia tunakushukuru sana ndugu yetu unayetukumbuka kwenye maombi yako, Tuna amini maombi yako ndiyo yanayopelekea mambo hayo makubwa yaonekane. MUNGU YESU KRISTO AKUBARIKI SANA.Tunaomba endelea kutuombea, kwa kweli tuna yahitaji maombi yako sanaaa. Pia ikiwa unataka kuchangia kwa ajiri ya huduma hii. Unaweza kuangalia kwenye tovuti hii eneo la kuchangia huduma utapata maelekezo hapo na namba za simu kama unataka kuuliza au kuchagia kitu. 

Hebu sasa tuanze kuangalia salamu zetu za mwezi huu wa tatu ambazo tumekuletea. Tumekuletea salamu nzuri mno. Kumbuka tumekua na mfululizo wa salamu zilizobeba ujumbe wa KUBADILISHWA NIA YAKOAU KUGEUZWA NIA YAKO.  “Bali  mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zetu,…  ” {RUM 12:2}. Katika salamu zetu za mwezi uliopita, tulianza kuona jambo la kwanza muhimu ambalo unatakiwa ulifanye kama unataka ugeuzwe hiyo nia yako. Kumbuka neno nia ni fikra, ni dhamiri,ni kusudi. Kwa maana nzuri sana ni mfumo mzima wa akili zako, huko ndani kumebeba mawazo, hisia zako zote hiyo ndiyo maana ya neno nia. Mungu anataka sisi tujue kuwa nia inaweza kugeuzwa na kuwa nia nzuri sana ya kumpendeza Mungu. Kwa maana nzuri tunatakiwa tuwe na akili nzuri tena zilizo toshelevu kabisa.  

Neno la Mungu linapozungumzia juu ya suala hili, linazungumzia mpango wa Mungu ni kukuona wewe na mimi hatupungukiwi na akili na hekima ona maneno haya “ Kwa maana watu wangu ni wapumbavu; hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu, ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema  hawana maarifa.” {YEREMIA 4:22} Mpango wa Mungu anataka wewe na mimi tuwe na akili na pia maarifa katika kutenda mema. Au kwa lugha nzuri niseme kutenda yaliyokusudiwa na Mungu uyatende katika siku zote ulizopewa kuishi hapa duniani. Anza kufikiri mambo mema ni yapi? Wengi wanafikiri kutokuzini,kutokunywa pombe nk, sikiliza yapo zaidi ya hayo. Mfano Mungu anataka uishi duniani kama mtawala! Hilo ni jambo jema kabisaaa, kwani huo ndio mpango wake tokea siku ile ana kuumba, wewe soma maneno haya uone mambo mema ni yapi ambayo Mungu ameyakusudia wewe uyafanye. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha, mkatawale samaki  wa baharini, na ndege wa angani….” {MWANZO 1:27-28}. Miongoni mwa mambo mema ambayo Mungu anataka akili yako isipungue katika kulijua na  uwe na maarifa ni hili la wewe kutawala au kumiliki hapa duniani kwa niaba ya Mungu. Sikiliza pia maneno haya uone.  “Nao waimba wimbo mpya wakisema, wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wakila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” {UFU 5:9-10}.  

Hilo ni jambo jema sana ambalo lilimghalimu Yesu kufa msalabani ili wewe na mimi tuludishiwe ile haki ya kumiliki juu ya nchi, yaani kutawala kusimamia mali zote. Ebu fikilia sisi watoto wa Mungu tuna akili toshelevu katika jambo hili jema?  Fikiri uone moja ya kazi ambayo Yesu aliifanya ni kukupatia wewe nafasi hii ya kumiliki juu ya nchi. Swali langu unayo maarifa ya kumiliki? au ninani anayemiliki juu ya nchi yako aliyokuweka Mungu?, kama wanaomiliki ni wamataifa basi fahamu kuna tatizo katika nia yako au katika akili yako.  Ebu fikiri, damu ya Yesu ilikununua wewe, kwanini watu wasio na Yesu ndio wamiliki mali? wewe uliyenunuliwa kwa damu upo katika hali mbaya sana . Hapo lazima kunatatizo kwenye akili zetu.  Mungu anataka tupate akili katika kuyajua makusudi yake yaliyo mema. kama hatumiliki maana yake  tuna akili zilizo kinyume na mapenzi yake. Mungu anataka ujazwe akili na maarifa katika kuyajua, kuyafanya yaliyo mapenzi yake. 

Ona pia maneno haya. “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu,wala hakemei;…”{YAKOBO1:5}. Mungu anataka tusipungukiwe hekima, na pia tusipungukiwe akili. Katika salamu hizi Mungu ameendelea kutufundisha namna ya kuigeuza hiyo fikra yako ili iwe kama Mungu alivyoikusudia iwe. Katika salamu zilizopita tulianza kuona eneo la maombi katika kuigeuza hiyo fikra yako. Leo tuone jambo la pili nalo ni hili. 

 

JIFUNZE KUPENDA KULISOMA NA KULISIKIA NENO LA MUNGU 

 

Ebu yasikilize maneno haya ya semavyo “Mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana zitakuongezea wingi wa siku, na miaka ya uzima, na amani rehema na kweli zisifarakane nawe; zifunge shingoni mwako; ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu” { MITHALI 3:1-4}  

Neno la Mungu linasema wazi kuwa iwapo tunataka kuwa na akili nzuri basi hatuna budi kuhakikisha tunasikiliza na kuzishika sheria za Mungu. Neno sheria ni utaratibu. Na utaratibu  ambao Mungu anataka tuufuate ameuweka ndani ya neno lake. Ebu  yaangalia maneno haya ya semavyo                      “ Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, ukauelekeza moyo wako upate kufahamu; naam, ukiita busara, na kupaza sauti yako  upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafuta kama hazina iliyositirika; ndipo utakapo fahamu kumcha Bwana, na kupata kumjua Mungu.” {MITHALI 2:1-5}  

Maneno hayo yanatupa mwanga kuwa ili mimi na wewe tupate ufahamu au akili kinachotakiwa tukifanye ni kuweka bidii ya kuyasikiliza maneno yatokayo katika kinywa cha Mungu. Ndani ya maneno hayo huko ndani ndiko kuna akili,ufahamu, maarifa, nk. Sikiliza ndani ya neno la Mungu huko ndiko kuna siri kuu ya wewe na mimi kupata akili, ngoja nikupe mifano hii michache uone wazi kuwa ndani ya neno la Mungu huko ndiko kuna maarifa, akilia au fikra sahihi ambazo mwanadamu atakaye akili lazima alitafute neno hilo la Mungu. 

 

Silikiza, kama leo hii unatafuta ufahamu wa namna ya kuishi na watu vizuri wewe nenda ndani ya neno la Mungu utaona namna linavyoelekeza. “Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; asije akakukinai na kukuchukia” {MITHALI 25:17}. Neno linakupa akili kuwa kama hutaki huyo ndugu yako au jirani yako akukinai na kukuchukia, basi hakikisha hauendi nyumbani kwake kila wakati. Akili hiyo na maarifa hayo yapo ndani ya neno la Mungu, watu wengi hawajui ni kwanini majirani zao wanawachukia na wamewakinai, wengi hufikia mambo mengi sana, sikiliza neno linasema chanzo cha tatizo hilo ni kwa sababu unaenda nyumbani kwa huyo jirani yako mara kwa mara.   

Kama unataka leo hii kila mtu akuone wewe ni mtu wa maana hata kama si wa maana neno la Mungu linakuelekeza hakikisha unafanya hivi “Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa ufahamu.” {MITHALI 17:27-28}. Acha kutanua kinywa chako hovyo-hovyo,  kama ni mpumbavu kwa kupitia kinywa chako kila mtu atajua wewe ni mpumbavu,  Kama utakuwa msemaji sanaa, utawapa watu faida ya kukutambua kuwa wewe ni mtu usiyejua kitu. kwa lugha nzuri kusema kwako ndiko kunakokutambulisha kwa watu kuwa wewe ni mtu wanamna gani, ni mtu usiyefaa au ni mtu unayefaa.  

 

Kama leo hii umepata nafasi ya kukaa meza moja na kula chakula na watu wakubwa, yaani wenye mamlaka,  neno la Mungu linakupa akili ya namna ya kula nao hapo mezani, wala haina haja ya kukalishwa shule ya namna ya kula na wakuu mezani. Sikiliza akili hii itokayo ndani ya neno la Mungu “Utakapo keti kula chakula  pamoja na mtawala, mwangalie sana yeye aliye mbele yako. Jitie kisu kooni, kama ukiwa mlafi” {MITHALI 23:1-2}. Umesikia maarifa hayo? Kama wewe ni mlafi, ukipata nafasi ya kula meza moja na mtawala hakikisha unajizuia, ukimuona yeye ka agiza chakula au kachukua chakula kidogo kwenye sahani yake, basi wewe nawe ufanye hivyo hivyo, akiimaliza na kuinuka basi na wewe hakiksha unaiuka na unamaliza hata kama njaa bado inauma, au hata kama haujakimaliza chakula hicho katika sahani yako. Hakikisha haumalizi chakula wewe mapema kabla ya mkuu. Sikiliza usiagize chakula cha bei ya juu wakati mkuu ameagiza chakula cha bei ya chini. Akili hiyo imo kwenye neno la Mungu 

Kama mwanao leo hii ni mwizi na unataka kuikomesha tabia hiyo ya uizi basi neno la Mungu linakupa akili hii kabla hauja anza kumchapa viboko. “Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema si kosa mwana huyo ni rafiki wa mtu mbaya” {MITHALI 28:24}.  Neno la Mungu linakupa akili kuwa ukiona mwanao ana tabia ya uizi,  basi fahamu ana rafiki mbaya, chakufanya si kumchapa aache uizi tu, bali mchape aachane na huyo rafiki  yake au hao rafiki zake. Ngoja nikupe mifano mingine. Kama leo hii unataka kutengeneza meli, nenda kwenye neno la Mungu litakupa akili ya namna Nuhu alivyopewa akili ya kuitengeneza hiyo meli. “Mungu akamwambia Nuhu, mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia. Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami. Hivi ndivyo utakavyofanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini  kwenda juu kwake. Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, chini, pili, na ya tatu”. {MWANZO13:13-16}” Mungu ndiye aliyempa Nuhu akili ya kutengeneza meli.  

Kama unataka leo hii akili au ufahamu kwa ajiri ya masuala ya sayansi eneo la Sayari nenda kwenye neno la Mungu. Mungu amesema wazi juu ya sayansi ya anga za juu sikiliza “Je! Waweza kuufungua myororo wa kilimia? Au kuvilegeza vifungo vya Orioni? Je! Waweza kuziongoza sayari kwa wakati wake?” {AYUBU 38:31-32} Sikiliza Mungu anatupa akili  kuwa zipo sayari, na anaziongoza kwa wakati wake, kwa maana nyingine hizo sayari zinahitaji kuongozwa, maana yake kuna sehemu zinapita au zinazunguka, ukitaka kujua anaziongozaje na zipo ngapi soma neno lake au muulize atakufundisha.  

Sikiliza unataka kujua umbo la dunia lilivyo? Sikiliza asemavyo katika neno lake “Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia? Yeye ndiye anayeketi juu ya DUARA ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa.” {ISAYA  40:21-22}. Neno la Mungu linatupa akili kuwa dunia ni duara, na inamisingi yake, kwanini nakuambia maneno hayo? Nataka upate hamu ya kusoma neno la Mungu iliupate ufahamu zaidi na zaidi wa vitu mbalimbali ambavyo umeumbiwa wewe uvimiliki kwa niaba yake Mungu. 

Kama unataka leo kufahamu ya habari ya tiba nzuri ya mtu yeyote au mwae  neno linasema  hivi “ Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.” {MITHALI 17:22}. Sikiliza ndani ya mifupa kuna mafuta, kazi ya hayo mafuta ndio chanzo cha kutengeneza damu. Sasa iwapo mtu atakosa furaha moyoni mwake kinachotokea hayo mafuta yanakauka, yakikauka, mtu huyo anakosa hewa ya kutosha ya 0xygen. Mtu akikosa hewa hiyo kwa kiwango kile kinachotakiwa, fahamu ndipo matatizo ya maradhi mbalimbali humtokea, kama moyo kutanuka, kuwa na vidonda ndani ya mwili, kukosa hamu ya kula nk. Sasa Mungu ametupa akili kupitia neno lake kuwa ili tupate dawa nzuri ni lazima tuhakikishe tunachangamka mioyoni mwetu ueelewa hapo?

Wewe unaumwa nini? Sikiliza leo hii mtu akikutwa ana virusi vya ukimwi, yule asiyejali ndiye atakaye ishi maisha marefu sanaaa, mwenye kulialia na kujiwazia sana kwa huzuni hufa mapema. Dawa yake ni kuhifadhi furaha moyoni ili asife mapema. Ngoja nikupe mifano hii mingine labda utaelewa zaidi. Kama leo hii unataka mtoto wako awe na akili yaani ni mjigamjinga, neno linasema hivi. “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali” {MITHALI 22:15}. Umeelewa hapo?  

Kama leo hii umeumia unataka kutibu hivyo vidonda neno la Mungu linasema hivi “Lakini, msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; …” {LUKA 10:33-34}. Msamalia alitumia divai kama sehemu ya tiba,  ili aponye huyo mtu majeraha yake, ndio maana hata Mtume Paulo alimwagiza Timotheo atumie mvinyo kidogo kama sehemu ya tiba ya ugonjwa wa tumbo lake “ Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.” {1TIMOTHEO 5: 23}. Hakumwambia unywe kama kinywaji bali kama tiba.  

Ukitaka  kujua habari za mtu kufanyiwa upasuaji nenda ka angaliye jinsi alivyo mpasua Adamu siku ile na kumtoa ubavu wake alifanya nini “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akaufunika nyama mahali pake” {MWANZO 2:21}. Hata leo hii wataalamu mabingwa wa upasuaji akili ya upasuaji wameipata pale bustanini Edeni, bila kuwalaza hao watu au kuwapa ganzi hawawezi kupasua nk.  

Unataka kujua jinsi mvua inavyotengenezwa? Sikiliza neno lake “ Hivyo  ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua. Wala hapana mtu wa kuilima aridhi,; ukungu ukapanda katika nchi, ukaitia maji juu ya uso wote wa aridhi.” {MWANZO 2:4-6}. Sikiliza Mungu anaupandisha ukungu au mvuke kwenda juu, akiupandisha unafika sehemu ambapo kuna baridi kali sana, unaganda na kuwa mapande ya barafu, yeye ameita ghala za theluji “Je! Umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe.” {AYUBU 38: 22 } ona tena asemavyo juu ya hili ninavyokuambia, Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?  Maji hugandamana kama  jiwe na uso wa vilindi huganda kwa baridi” {AYUBU 38: 28-30}. Unatakakujua namna anavyoyabomoabomoa mapande  hayo ya barafu yaliyoganda huko juu? Anatumia radi “Ni nani aliyepasua mfeleji kwa maji ya gharika, au njia kwa umeme wa radi kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu juu ya jangwa asiyo kaa mtu.”{AYUBU 38:25}. Soma na kitabu hiki cha AYUBU 37:1-16}. Radi hiyo inauwezo mkubwa wa kutikisa vitu kuliko nyuklia. Unataka kujua kwanini mito inapeleka maji baharini lakini bahari haijai? Sikiliza maneno haya “ Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko itokako ” {MHUBIRI 1:7}.  kumbuka anayapandisha hayo maji juu kwa kutumia mvuke, na anayaludisha tena baharini kwa kupitia mito, na anayapeleka tena juu kwa kutumia mvuke, hiyo ndiyo akili aliyoitumia. Ndio maana nasema huko itokako ndiko iludiko, yaani maji ni yaleyale, kipimo ni kilekile umeelewa hapo? Umegundua kuwa kumbe kama tunataka akili lazima tusome neno la Mungu? 

Kama leo hii  unataka ufahamu wa wewe kushika mali siku zote za maisha yako nenda kwenye neno la Mung utaona namna neno linavyotupa akili likisema hivi “….Na watu wakali  hushika mali siku zote.” {MITHALI 11:16b}. Angalia tena maneno haya “ Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; na miaka ya maisha yako itakuwa  mingi. {MITHALI 4:10}.Ukitaka leo hii upate akili ya kuishi maisha marefu hapa duniani neno la linasema hivi “Mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana zitakuongezea wingi wa siku, na miaka ya uzima, na amani. ndivyo utakavyopata kibari na akili nzuri, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu.” {MITHALI 3:1-3}.  

Kama leo hii unataka upate uzima yaani afya njema, unatakiwa upate akili hiyo. Sikiliza, neno la Mungu limejaa akili na maarifa. Tatizo la wanadamu wengi ni hili hawajui siri iliyomo ndani ya neno la Mungu, wengi wanafikiri kusoma sanaaa mpaka chuo kikuu ndio watapata akili. Wengi wanasema imaandikwa mshike sana elimu usimwache aende zake, sikiliza msome huyo elimu anayetakiwa wewe umshike, utagundua kuwa elimu huyo  unayetakiwa umshike sana ni Mungu. Wewe soma huo mlango mzima wa {MITHALI 4:1-22} Kama utasoma maneno hayo yote utagundua ninacho kuambia, sina maana usiende shule,au usipeleke mtoto wako shule, ila maana yangu ni hii, akili au ufahamu unapatikana katika neno la Mungu tu, kama unataka Mungu ageuze nia yako au akuongezee akili, jifunze kulitafuta neno  lake kwa bidii, hapo ndipo utakuwa na akili na nia mpya tena njema kila siku iitwapo leo. Tumalizie kwa maneno haya. “Mwanangu yasikilize mausia ya baba yenu, tegani masikio mpate kujua ufahamu” {MITHALI 4:1} 

Hebu weka bidii katika kusikiliza mausia ya Baba yako. Kumbuka Baba yetu ni Mungu, ukipenda kumsikiliza kwa  kupitia neno lake ndipo utakapo pata kujua, na ufahamu, yaani utakuwa mjuzi na mjuzi mwenye ufahamu. Na amini umetuelewa katika salamu zetu hizi tulizo kuletea  mwezi huu. 

Mungu akubariki sana tuonane tena mwezi ujao. 

Ni sisi 

Mrs Steven & Mrs Beth Mwakatwila.