Salamu – Apr, 2011

Bwana Yesu asifiwe sana, mimi na familia yangu hatujambo na tunamshukuru sana Mungu aliyetupatia uzima na afya njema. Pia tunamshukuru sana Mungu kwa kutupatia Salamu nzuri sana katika mwezi huu wa nne. Mwezi huu tumepewa salamu zenye kichwa. “Mambo Muhimu Unayopaswa Kumuomba Mungu Kila Siku (Eneo La Kuyajua Mapenzi au Mipango Ya Mungu)”

Nilipokua namuomba Mungu kwa ajili ya tatizo linalonisumbua la kutokupokea majibu ya maombi yangu, Mungu alinijibu kwa kunifundisha mambo mengi sana ambayo yanaweza kupelekea kushindwa kupokea majibu ya maombi yangu. Ni imani yangu kuwa tatizo hilo lililonisumbua mimi kwa miaka mingi sana hata wewe unalo. Unamuomba sana Mungu lakini kwenye eneo la kupokea majibu yako unajikuta unakwama, mpaka unafikiri kuwa huenda Mungu siku hizi ameacha kujibu. Mungu hajaacha kujibu wala hataacha kujibu. Yeye amesema tukiomba atatupa, sikia asemavyo “Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amini, amini, nawaambia mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” (Yohana 16: 23-24).  

Swali langu lilikua, Bwana unasema upo tayari kutupatia neno lolote lile tukikuomba, kwa nini mimi hunipi kile nikuombacho? Hata wewe inawezekana una swali kama hilo hilo nililokua nalo mimi. Mungu alianza polepole kunifundisha ni kwa nini sipokei majibu ya maombi yangu, moja ya sababu ni hii ya kutokujua mpango au kusudi la Mungu katika hilo niliombalo. Sikiliza maneno yake haya jinsi yasemavyo. “Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1 Yohana 5:14-15). Neno la Mungu linasema wazi kuwa,Mungu ameahidi kutupatia kitu chochote tunachokihitaji kwa kupitia maombi, hilo nililijua tokea siku nyingi ndio maana nilikua na uhakika kabisa kuwa nikimuomba anipe kitu chochote kile atanipa. na mstari huo niliukariri na kuusema kila ninapomuomba, lakini bado tatizo la kupokea majibu kwangu lilikuwepo. Siku moja nilipokua naipitia tena mistari hiyo, nikashangaa Roho Mtakatifu akinionyesha kwa msisitizo neno linalosema. “Tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia.” Unajua, maneno hayo yaliendelea kupiga kelele moyoni mwangu sana. Nikatulia na kumuomba Mungu anioneshe nini anachotaka kunifundisha, Kile alichonifundisha ndicho leo hii nimepata kibali cha kukileta kwako mpendwa ili hata wewe upate kukifahamu na ukikifahamu itakuwa ndiyo ufunguo wako wa kupokelea majibu yako kutoka kwa Mungu.

Neno mapenzi lina maana nyingi sana, neno mapenzi ya Mungu kwa maana nzuri sana ni mipango au kusudi la Mungu. Anaposema tukiomba sawasawa na mapenzi yake atatupa tunaweza kusema hivi, tukiomba sawasawa na mipango yake au makusudi yake hapo ndipo Mungu atatupatia hicho tunachohitaji. Moja ya tatizo kubwa linalopelekea watoto wa Mungu wengi sana wajikute wanakwama kwenye eneo hilo la kupokea majibu yao lipo hapo. Watoto wa Mungu wengi sana wanakimbilia kuomba tena kwa machozi lakini wengi kabla ya kuomba kwao huwa hawalijui kusudi la Mungu katika hilo wanaloliombea. Sikia kama utaomba kinyume cha mpango wa Mungu usitegemee Mungu kukupa hicho unacho kihitaji!

Mungu anayo mipango yake, na anataka sisi watoto wake tuijue hiyo mipango yake, tukiijua itakuwa ni rahisi sisi kumuomba sawasawa na alivyopanga hapo ndipo inakuwa rahisi sisi kupokea hayo tuliyomuomba kwa sababu tumeomba sawasawa na mipango yake. Ebu sikia maneno haya “For I know the plans I have for you, declares the Lord, plans to prosper you and not to harm you, plans to give you hope and a future” (Jeremiah 29:11). Tukisoma maneno hayo kwa kiswahili yanasomeka hivi. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yeremia 29:11).

Nimeona tuyaangalie maneno hayo kwa lugha mbili, moja ya kiingereza na ya pili ni lugha ya kiswahili ili tupate maana nzuri zaidi. Katika lugha ya kiingereza anasema ninayo “mipango niliyokupangia”. Katika kiswahili anasema “mawazo”. Sasa ona Mungu anayo mipango tayari ambayo amekupangia wewe, iwe ya kula kwako, kuvaa kwako, kuoa kwako, kuolewa kwako, watoto wako, huduma yako, kuishi kwako hapa duniani Mungu yeye amekwisha kukupangia hiyo mipango na anayo tayari. Elewa si kwamba anaipanga sasa hivi, anasema anayo! Kosa letu kubwa lipo hapo, kwanza hatujui kuwa anayo mipango (mapenzi) aliyotupangia tayari. Pili hatuna haja ya kuijua hiyo mipango yake au niseme hatumtafuti Mungu kwa ajili ya kumuuliza au kumuomba atujulishe nini mipango yake aliyoipanga kwa ajili ya mahitaji yetu.

Mungu anayo mawazo au mipango yake kwa ajili yako na anataka sisi watoto wake tuyajue kwanza hayo mawazo aliyoyawaza katika hilo ambalo tunalihitaji. Tukiyajua mawazo yake yaani mapenzi yake hapo ndipo tunapaswa kuwa na ujasiri wa kumuomba atupe, na hapo ndipo itakua rahisi kupewa kwa sababu tumeomba sawasawa na kusudi au mpango wa Mungu. Kama utaomba bila kujua kusudi la Mungu ni nini katika hilo unaloliomba akupe fahamu ni rahisi zaidi kuomba kinyume cha kusudi lake, na ukiomba hivyo usitegemee jibu toka kwa Mungu. Ona mfano huu mzuri wa Bwana wetu Yesu Kristo, Soma maneno haya, “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke: walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe……. Akaenda mara ya pili, akaomba, akisema Baba yangu ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.” (Mathayo 26:39,42) Umeona kwa mara ya kwanza hapo Bwana alikwama katika kupokea kile alichokihitaji kwa kupitia maombi yake, nini kilicho mkwamisha? Ona Mara ya kwanza aliomba kikombe kimuepuke, wakati Mungu mpango wake ulikua ni lazima Yesu Kristo akinywe hicho kikombe. Aliposema mapenzi yako yafanyike, ndipo jibu toka mbinguni linakuja kwa malaika kuja kumtia nguvu. Fikiria kama angeendelea kuomba asikinywe hicho kikombe hata kwa siku arobaini je! Mungu angemsikiliza na kumkubalia? Nakwambia ukweli asinge msikiliza. kwa sababu mpango wa Mungu aliokuwa anao tayari na si kwamba alikuwa anakwenda kuutafuta alikuanao na ni huu Yesu lazima afe kwa ajili ya wenye dhambi.  

JIFUNZE KUMUULIZA MUNGU

Ikiwa leo hii unataka kuyajua mapenzi ya Mungu katika kila jambo, lazima ujifunze kumuuliza nini yaliyo mapenzi yake katika kila jambo unaloliombea, Mungu ametupa kibali cha kumuuliza habari za mambo mbalimbali na ameahidi kutupasha, sikiliza maneno haya ya Bwana yasemavyo. “Bwana, mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.”(Isaya 45:11) Mungu anataka umuulize habari mbalimbali, anasema habari za watoto wake yaani kanisa au watu waliookoka, anasema muulize habari za kazi ya mikono yake, yaani habari ya kila kitu alicho kiumba, yupo tayari kukupasha habari zitakazo kuja, anasema muulize na umwagize. Nilipoyasoma maneno hayo niligundua jambo la ajabu sana, Mungu yupo tayari kukuambia wewe habari ya mipango yake ni nini katika hicho unachokihitaji, pia yupo tayari kukufundisha hata namna ya kuliombea hilo unaloliombea. Ngoja nikupe mifano hii michache: Siku moja wana wa Israeli walijikuta wapo kwenye shida kubwa iliyotokana na makosa yao waliyomkosea Mungu. Wakajikuta wanaingiliwa na roho ya mauti, Mungu akamfundisha mtumishi wake Yeremia namna ya kuliombea jambo hilo, alimwambia afanye hivi. “Bwana wa majeshi asema hivi, fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; wanawake wenye ustadi, ili waje; na wafanye haraka na kuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.” (Yeremia 9: 17-18) Ukiyasoma maneno hayo utaona wazi kuwa Yeremia alijilishwa mpango mzima wa Mungu katika habari za maombi amabayo wana wa Israeli wanatakiwa wayaombe, yaani mfumo wa wamaombi ayatakayo Mungu. Mungu alimwambia awaite wanawake waombolezao tena walio wastadi ndio wanaotakiwa waomboleze hapo ndipo watakapopata kile wanachokihitaji.anasema waite hao ili waje, waje wapi? Waende kwa Mungu ili wakamlilie kwa ajili ya hilo tatizo. Hebu fikiri kama Yeremia asingelijua mpango huo wa Mungu, hao ndugu wangeomba maombi yasiyo ya kuomboleza wasingelisikiwa Mbinguni. Tatizo tulilo nalo watoto wa Mungu wengi ni hili, hatumuulizi Mungu habari mbalimbali, ziwe za nchi yetu, watoto wetu, kanisa la Mungu nk. Mungu anayo mipango aliyoipangia nchi yako, pia anao mfumo wa namna unatakiwa uombe ili akupe hicho unacho kihitaji. Watu wengi wanafikiri wakifunga ndipo atawapa, ngoja nikuulize swali, ni nani amekwambia hilo unaloliombea unatakiwa ufunge? Unatakiwa uyajue mapenzi ya Mungu kwanza hapo ndipo uombe. Ikiwa utaomba sawasawa na hiyo mipango aliyoipanga Mungu na kwa mfumo alioupanga hapo ndipo utakapoyapokea hayo unayoyahitaji. Pia lazima ujue ninini yaliyo mapenzi ya Mungu kwa ajili ya nchi yako, ukiyajua hayo mapenzi ya Mungu na ukaomba sawsawa na hayo aliyoyapanga hapo ndipo utakapoona mabadiliko katika nchi yako. 

Mungu anayo mipango aliyoipangia familia yako wewe, usipomuuliza kuhusu kusudi lake alilolipanga kwenye hiyo familia yako, hutaomba sawasawa na mipango yake, utashangaa mnapishana, wewe unaomba hivi yeye anataka hivi! Mwisho wake utaona kama Mungu hajibu maombi, kumbe anajibu sana tatizo unapishana na mipango yake. Mungu anayo mipango aliyoipanga kwa ajili ya utumishi aliokupa, ona mfano huu. “Neno la Bwana lilinijia, kusema, kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” (Yeremia1:4). Angalia maneno hayo kwa kutulia, utagundua kuwa, Mungu alimpangia Yeremia mpango wa kutumika, anasema mpango huo aliupanga kabla hata Yeremia hajazaliwa na mama yake, hebu fikiria, kama Yeremia asingeujua mpango huo unafikiri angefanikiwa katika utumishi wake? Naamini angetumbukia kwenye ukuhani, wakati yeye ni Nabii nk.

Ukiangalia watoto wa Mungu wengi sana wamekata tamaa katika habari za kuomba. Kwa sababu ya kutopokea majibu yao kwa Mungu, mara nyingi majibu ya maombi yao yanakuja tofauti na walivyotarajia, ona mfano wa namna tunavyoiombea nchi yetu, iwe kwenye vipindi vya uchaguzi nk, utaona baada ya hizo chaguzi, watoto wa Mungu wengi wanajikuta wana majeraha mioyoni mwao, kisa, wamepokea jibu kinyume na matarajio yao. Wengi hukata tamaa, na kufikiri kama Mungu hawasikii. Moja ya jambo alilonifundisha Mungu ni hili nikuambialo, kama tutajua mipango ya Mungu aliyoipangia nchi yetu hapo ndipo itakuwa ni rahisi kumuomba Mungu atupe viongozi wenye sifa zinazofanana na mipango ya Mungu aliyoipangia nchi yetu. Ngoja nikuulize swali, unajua Mungu ameipangia nini au anaiwazia nini nchi yako kwa miaka hii na ijayo? Kama hatujui unafikiri tutaomba sawasawa na Mungu anavyoiwazia nchi yetu? Ngoja nikupe mfano huu mzuri. Mungu alimwambia Ibrahimu habari za taifa la Israeli kabla halijaenda utumwani Misri, alimwambia litakaa huko utumwani miaka mia nne, alimwambia jinsi litakavyotoka huko Misri litatoka na mali nyingi nk. “Bwana akamwambia Abrahamu, ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali nyingi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee, mwema” (Mwanzo 15:14-15) 

Ibrahimu aliufahamu mpango kamili wa Mungu kuhusu taifa lake na mwisho wa maisha yake yeye utakuwaje. kwa kuufahamu huo mpango wa Mungu kuhusu taifa lake, na amini mfumo wa maombi wa Ibrahimu kuhusu taifa lake ulikuwa ni rahisi sana kwa sababu tayari alikuwa anajua nini kinacho kuja au kilichopangwa na Mungu kwa ajili ya taifa la Israeli. Ona, Sisi tunapoliombea taifa au nchi yetu tunaomba maombi ya kubahatisha. Hatujui Mungu anatuwazia nini kwa sasa hivi na pia huko mbele yetu. Ni Wakristo wachache wanajua hilo. Mungu anasema tumuulize habari mbalimbali ikiwemo hii ya nchi yetu, tukifahamu anacho kiwaza juu ya nchi yetu, hapo ndipo tuombe sawasawa na mapenzi yake, ndipo tutakapoona mabadiliko katika nchi yetu, yawe ya kiuchumi, nk. Kwa kuwa hatuujui mpango wa Mungu kwa ajili ya taifa letu, ni rahisi kuomba kwa mapenzi yetu wala si ya Mungu, na matokeo yake ni kutopewa kile tukitakacho. Anza leo hii kujifunza kuomba maombi ya kuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yako yote, itakua rahisi kuomba sawasawa na mpango wa Mungu. Na hapo utajikuta ukipokea majibu yako. 

Mungu akubariki sana tuonane tena mwezi ujao. 

Ni sisi 

Mrs Steven & Mrs Beth Mwakatwila.