Salamu – Octoba, 2011

Bwana Yesu asifiwe sana. Mimi na familia yangu hatujambo kabisa na tunamshukuru Mungu. Pole na kazi zote na kila kitu kibaya kilichokutokea katika mwezi uliopita, inawezekana ni matatizo ya kifamilia au magonjwa ama kutofanikiwa katika kazi zako. Naamini mwezi huu Mungu atakufungua kutoka katika matatizo yako, pia Bwana Yesu atakufariji na kukujenga tena mahali pale ulipofiwa na nduguyo. Pia tuna mshukuru sana Mungu kwa ajili ya hii Website yetu. Kumbuka website hii tunalipia kila mwaka. Nina mshukuru Mungu ambaye ametulipia mwaka huu kwa kupitia familia moja ndio maana leo tupo tena hewani. Kwa kweli tunamwomba Yesu aibariki sana familia hiyo. Hata wewe naomba iombee familia hiyo. Hebu tusonge mbele tena katika salamu zetu za kila mwezi. Tumekuwa na salamu zenye kichwa hiki:-  

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU) 

Sikia maneno haya ya Bwana Yesu yasemavyo. 

“Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1Yohana 5:14-15) 

Ukiyasoma maneno hayo utaona kuwa, Mungu ametupa utaratibu wa kumuomba. Anasema tukiomba sawasawa na mapenzi yake ndipo tutakapopewa kile tunachokihitaji toka kwake. Kwa maana nyingine ikiwa hatujaomba sawasawa na mapenzi yake, itakua ni vigumu sana kupewa chochote kile tumuombacho Bwana. Katika salamu zilizopita tuliendelea kuona ile sehemu ya namna Mungu anavyoweza kusema na mtu na kumfahamisha kitu. Tuliendelea kuona ile sehemu ya njia ya pili ambayo Mungu anaweza kuitumia kusema na mtu ni kwa njia ya Maono na Ndoto. Hebu leo tuendelee mbele kidogo.  

ANZA KUOMBA MUNGU AYATIE MACHO YAKO YA NDANI NURU 

Inawezekana kabisa ndani yako umekuwa na kiu ya kusema na Mungu kwa njia hiyo ya maono au ndoto, na una swali kama hili moyoni mwako; Je! Nifanye nini ili Mungu awe na mawasiliano nami na kunipa ufahamu wa mambo mbalimbali kwa kupitia maono na ndoto? Ili leo hii ufanikiwe katika jambo hilo anza kufanya maombi maalumu ukiomba Mungu akupe wewe roho ya ufunuo na kuyafungua au kuyatia nuru macho yako ya ndani yaani ya moyoni. Sikia maneno haya ya Bwana yasemavyo. 

“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo….” (Waefeso 1:17). 

Neno la Mungu linanipa maarifa kuwa, ili macho yetu yaanze kuona mambo ya rohoni ni lazima yashughulikiwe kwa kupewa dawa ambayo neno la Mungu imeiita nuru. Sikia, ili uanze kufunuliwa mambo ya Mungu yeye anasema, ili tumjue Mungu, au niseme ili uyajue mapenzi yake ni lazima upewe roho ya ufunuo.

Mtume Paulo alijua kuwa hao watu wana tatizo la kutokumjua Mungu na kama hawakumjua Mungu maana yake hata mapenzi yake walikuwa hawayajui, ilibidi awaombee maombi ya namna hiyo. Hata wewe leo hii ukitaka kufanikiwa katika eneo hilo la kuona maono na ndoto zitokazo kwa Mungu ni lazima uanze kumuomba Mungu ayatengeneze macho yako yaliyo moyoni mwako yapate nuru ili uanze kuona kile ambacho yeye anakiona. Omba Roho Mtakatifu akutengenezee pia masikio yako ya ndani ili yaanze kusikia asemapo nawe na kukufahamisha ni nini mapenzi yake. Omba roho ya ufunuo utaona mabadiliko makubwa sana katika habari hii ya kuwa na mawasiliano na Mungu kwa njia ya ndoto na maono au mafunuo toka juu mbinguni kwa Yesu Kristo Baba yetu. 

MWILI WA ROHO UPO 

Macho yanayo zungumzwa hapo si haya ya nyama. Ni macho ya ndani ya moyo wako, fahamu huko ndani ya moyo au nafsini ndiko roho yako inakokaa, pia fahamu kuwa hiyo roho yako ndiyo inayowasiliana na Mungu kwa kuwa Mungu ni Roho 

“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” (Yohana 4:24) . 

Anapotaka kuzungumza fahamu atazungumza na wewe kwa kupitia roho yako. Ili uyaone yale ayatakayo kukufunulia ni lazima macho ya roho yako yashughulikiwe kwa kupewa dawa iitwayo nuru, na masikio yako ya rohoni, si haya ya nyama, yazibuliwe yaanze kumsikia Mungu Roho Mtakatifu kwa uwazi asemapo na roho yako. Ninaposema macho au masikio ya rohoni ni vigumu kuelewa kama hujui kuwa roho yako wewe ina mwili wake ambao una masikio na macho kabisa. Sikia; wewe unayo roho yenye mwili, pia unao mwili huu wa nje wa nyama, mwili huo wa ndani wa rohoni ndio unaoishi kwenye ulimwengu wa roho, na huu wa nje ndio unaishi kwenye ulimwengu huu unaoonekana. Mungu ametuumba tuishi sehemu zote mbili, yaani ukitaka kushiriki mambo ya rohoni utaweza kwa kuwa una mwili unaokuruhusu kuishi kwenye ulimwengu huo wa rohoni yaani kushirikiana na Mungu. Pia unaweza kuishi huku duniani kwa kuwa umepewa mwili huu wa nje ambao unakupa ruhusa ya kuishi kwenye ulimwengu huu unaoonekana. Neno la Mungu linasema 

“Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani;………. hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.” (1Kor 15:40-44). 

Kama unataka kufanikiwa sana katika eneo hili la kuwa na mawasiliano kati ya wewe na Mungu lazima ujue jinsi alivyokuumba. Amekupa roho ambayo ina mwili kabisa, ina macho, masikio, mdomo nk. Miili hiyo haiwezi kuoa au kuolewa! 

“Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni” (Mathayo 22:30). 

Hebu angalia maneno haya utaelewa ni nacho kuambia:- 

“Mimi Yohana, ndugu yenu mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, haya uyaonayo uyaandike katika chuo……. nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara saba vya dhahabu….….” (Ufunuo 1:9-20). 

Mtumishi wa Mungu Yohana anasema alikuwa katika roho, hakuwa katika mwili, aliona na alisikia, ninachotafuta ukione kama mimi ninavyokiona ni hiki cha roho kuona na kusikia! Hasemi alikuwa katika mwili, kumbuka macho yaliyoona mambo ya rohoni yalikuwa ni macho ya rohoni, si haya ya mwili, sasa kama unataka Mungu akuonyeshe maono mara kwa mara au ndoto ili uyajue yaliyo mapenzi yake ni lazima uanze kufanya maombi maalumu ya kuomba akupe Roho ya ufunuo katika kumjua yeye pia omba ashughulikie macho yako ya ndani yawe makali yaone mambo ya rohoni na masikio yako pia yawe makali yasikie kila neno asemalo Mungu. Ngoja nikuulize swali macho yako ya ndani yakoje? 

Ndani ya maandiko matakatifu nimeona jinsi wenzetu walivyokuwa na mafanikio makubwa ya mawasiliano kati yao na Mungu kwa kuwa macho yao na masikio yao ya rohoni yalikuwa makali, waliona mambo ya rohoni yaani yaliyo ndani ya watu na hata walijua nini Mungu anataka, au nini watu wanafanya, yaani hawakufichwa siri yoyote iwe ya mtu au ya yale ya mbinguni. Ona mifano hii michache ili na wewe ufanye bidii kumuomba Mungu akutengenezee macho hayo ya rohoni. Ona Bwana Yesu macho yake ya rohoni yalikuwa makali sana, aliona kila kitu kilichokuwa ndani ya mioyo ya watu, ndio maana hakushikwa au kukwama katika kila jambo. Yesu aliiona roho ya Yuda tokea zamani, alijua kuishi naye, aliona mioyo ya mafarisayo walipotaka kumtega nk. Mwone Mtume Paulo alivyokuwa 

“Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa ibilisi, adui wa haki yote, hauachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?” (Mdo 13:9-10). 

Mtume Paulo alimwona huyo mchawi aliyekuwa akiloga watu wasiliamini neno la Mungu kwa macho ya rohoni, alijaa Roho wa ufunuo, akafunuliwa mtu mchawi, neno linasema akamkazia macho, unafikiri alimkazia macho haya ya nje? Ni macho ya ndani, ona pia Elisha alimwona Gehazi akichukua sadaka kutoka kwa Naamani kwa kificho. Sikia kisa hiki; 

“Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake, Elisha akamwambia, watoka wapi, Gehazi? Akanena, mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukwenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi….” (2Fal 5:25-27). 

Gehazi hakujua kuwa Elisha macho ya moyo wake ni makali sana, yanaona mambo ya nje na ya ndani ya mioyo ya watu. Aliona kama amefanikiwa sana kumficha Elisha, kumbe alijidanganya, macho ya ndani ya Elisha yalimuona toka anaondoka mpaka aliporudi. Fikiri leo hii kila mtoto wa Mungu macho yake yawe makali kama ya Elisha unafikiri leo kutakuwa nakudanganyana na kudanganywa? Fikiri mkeo macho yake ya rohoni yametiwa nuru na anamwomba Mungu sana akulinde akutunze nk, na wewe ndio unamficha mambo yako unashinda kwa bi mdogo unafikiri Mungu hata muonyesha? Nakuambia moyo wake utaenda na wewe tu. hata wewe mwanamke ndio hivyohivyo itakuwa kwa mumeo  

Binafsi nimemuona Mungu akiwa mwaminifu sana kwenye eneo hili ninalo kuambia, nilipo anza kuomba Mungu anipe roho ya ufunuo, na kuyatia macho yangu nuru na kuyazibua masikio yangu ili nione nimjue na nijue nini mapenzi yake katika mambo mbalimbali, nakuambia ukweli, nimeona mabadiliko sana, sijafika bado, namuomba Mungu mara kwa mara maombi ya namna hiyo. Mungu ndipo alipoanza kusema na mimi na kunionyesha mambo mengi sana, mengine mpaka naogopa. Nikizembea kuomba maombi ya namna hiyo macho yangu ya rohoni hupoteza nuru, sioni kama kawaida, nikikimbilia kwenye maombi ya namna hiyo yanatiwa nuru, unajua mpaka watoto wangu hata ndugu zangu, na rafiki zangu wa karibu, hushangaa sana. Lakini siri ni hiyo. Nataka uwe na macho manne, yaani macho yako ya nyama yaone, na hayo ya ndani yaone, Mungu anataka uwe unaona pande zote mbili yaani rohoni na katika ulimwengu huu unaoonekana. Anza kufanya maombi ya namna hiyo ndipo utapata nguvu, ya kuona maono na ndoto kwa uzuri na mara kwa mara utapokea mafunuo mapya toka mbinguni. Mungu akubariki sana, tuonane tena kwenye kona hii mwezi ujao. 

Mr. Steven & Beth Mwakatwila