Salamu – Disemba, 2011

Ndugu yangu katika Bwana Yesu Kristo; Bwana Yesu asifiwe sana. Sisi na familia nzima ni wazima na tunamshukuru sana Mungu kwa kutuweka wazima na pia kwa kututia nguvu za kuingia mwezi huu wa mwisho katika mwaka huu wa 2011. Ni neema kubwa sana hata kwako kwa kuona mwezi huu wa kumi na mbili. Ni imani yetu kuwa Bwana atakuvusha na kukuingiza mwaka mpya wa 2012. Mwaka huu wa 2011 kwetu sisi tumekuwa na changamoto nyingi sana katika eneo la utumishi. Tulijiwekea malengo mengi sana katika eneo la kumtumikia Bwana, tumemuona Mungu ambaye ametusaidia sana katika kuyathibitisha yale tuliyoyakusudia.

Katika salamu zijazo, tutakupa kwa upana kidogo ni nini tulipanga na tumefanikiwa wapi, na wapi hatujafanikiwa kabisa au tumefanikiwa kwa hatua fulani. Hebu tusonge mbele tumalizie mwaka kwa mwendelezo wa salamu zetu ambazo zimekuwa ndefu sana. Lakini naamini kila mwezi umepata kitu kipya. Kama una maoni au maswali, tuandikie, anuani zetu zipo kwenye ukurasa wa [Wasiliana Nasi]. Basi tundelee mbele kuangalia salamu zetu zenye kichwa:-

MAMBO MUHIMU UNAYOPASWA KUMUOMBA MUNGU KILA SIKU (ENEO LA KUYAJUA MAPENZI AU MIPANGO YA MUNGU)

Angalia maneno haya ya Bwana ya semavyo.

“Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” (1YOHANA 5:14-15)

Baba Mungu amesema wazi kuwa yupo tayari kutupatia kitu chochote tukitakacho, lakini ametupa mwongozo, mwongozo huo ni huu atuambiao kuwa lazima tuombe sawasawa na mapenzi yake. Neno Mapenzi ya Mungu maana yake nini? Neno Mapenzi ya Mungu maana yake ni kusudi au mipango ya Mungu

Ili ufanikiwe kwenye eneo la maombi yako lazima uhakikishe kwanza unalijua ni nini kusudi au mapenzi ya Mungu katika hilo unalomuomba au hilo unalo lihitaji kutoka kwake. Katika salamu zetu za mwezi uliopita, tuliendelea kujifunza katika sehemu ile ya njia ambazo Mungu huzitumia kutujulisha mapenzi yake. Tuliangalia sehemu ile ya njia ya pili, ya ndoto na maono, na tulijifunza kipengere kile cha; namna tunavyotakiwa tufanye ili tupate kufasiriwa ndoto au maono ambayo hatujayaelewa. Leo tusonge mbele tena tuone eneo linalofuata ambaloni:- KUJUA AINA ZA NDOTO NA MAONO

Watu wengi sana huziogopa ndoto na hawataki hata kusikia neno lolote liitwalo maono au mafunuo. Kwa sababu wamesikia kuwa kuna madanganyo sana kwenye ndoto au maono. Ni kweli neno la Mungu linatufundisha kuwa kuna aina mbili za ndoto na pia kuna aina mbili za maono. Aina ya kwanza, ni ndoto zitokanazo na Bwana Mungu, na Ndoto za pili ni zile za udanganyifu.

Ndoto hizi za udanganyifu zimegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ni udanganyifu uliotokana na shetani (roho za pepo wabaya) nk. na sehemu ya pili ni tabia ya udanganyifu alionao mtu mwenyewe. Hata maono yako hivyo hivyo. Kuna maono ya udanganyifu ambayo yamegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ni udanganyifu uliotokana na shetani (roho za pepo wabaya) nk. na sehemu ya pili ni tabia ya udanganyifu alionao mtu mwenyewe.

NDOTO NA MAONO YATOKANAYO NA TABIA YA UONGO YA MTU

Na tuanze kujifunza kwenye eneo la ndoto na maono yatokanayo na tabia ya mtu ya uongo au ya udanganyifu. Ninavyosema hivyo maana yangu ni hii, mtu anaweza kabisa akasema ameona ono, au ameota ndoto fulani au akasema Bwana ameniambia, wakati hakuona kitu, wala hakuota ndoto kabisa! Tena wala hakuisikia sauti ya Mungu wala ya shetani. Ila akakimbia akasema nimeona, nimesikia au nimeota. Na watu wakamsadiki kabisa kumbe muongo tu. Mungu anasema wazi kwenye neno lake kuwa wapo watu wa namna hiyo na mimi nakuambia ni wengi sana.

Ona maneno haya ya Bwana yasemavyo;

“Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake. Kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana! Na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?” (Yeremia 23:25-29)

Ukiyasoma maneno hayo utaona wazi kuwa kuna watu ambao wanaweza sema Mungu kawaonyesha maono wakati hajawaonyesha na hata wakasema wamesikia wakati hawakusikia kabisa. Ona hata hapa kasema vivyo hivyo.

“Kisha Neno la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, lisikieni neno la Bwana; Bwana Mungu asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lolote! Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa. Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya Bwana. Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, Bwana asema; lakini Bwana hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa. Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, Bwana asema; ila mimi sikusema neno.”(Ezekieli 13:1-7).

Ukiyaangalia maneno hayo utaona kuwa zipo ndoto au maono ya uongo kabisa. Sikia, mtu anaweza kutunga uongo akasema ameona wakati hajaona jambo lolote lile au hajaota ndoto yoyote ile. Hiyo ni aina ya kwanza ya ndoto au maono ya udanganyifu yatokanayo na tabia ya uongo ya mtu.

NDOTO AU MAONO YATOKANAYO NA ROHO YA UDANGANYIFU

Aina ya pili ya ndoto au maono ya udanganyifu ni hii ya kupokea ndoto au maono kutoka katika roho ya shetani au mapepo ya udanganyifu. Neno la Mungu linasema wazi kuwa shetani anaweza kutumia ndoto au maono kumletea mtu udanganyifu wa kupoteza. Ona mfano huu;

“Basi nililetewa neno kwa siri sikio langu likasikia manong’ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku hapo usingizi uwajiapo wanadamu. Hofu iliniangukia na kutetema, iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake; mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa na haki kuliko Muumba wake? Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; na malaika zake huwahesabia upuuzi; Je! Zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, ambazo misingi yao i-katika mchanga, hao waliosetwa mbele ya nondo! Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; waangamia milele wala hapana atiaye moyoni. Je! Kamba ya hema yao haikungo’olewa ndani yao? Wafa, kisha hali hawana akili.” (Ayubu 412-21)

Ukiyasoma maneno hayo utagundua kuwa pepo au shetani anaweza kutumia njia hii ya maono kumletea mtu habari za udanganyifu ambazo si za kweli kabisa. Ona tena maneno haya yasemavyo

“……Akatoka pepo akasimama mbele za Bwana akasema, mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, jinsi gani? Akasema nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, utamdanganya na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.” (1 Fal 22:1-40).

Ukiyasoma maneno hayo kwa kutulia utagundua kuwa, pepo alipeleka neno la uongo kwa hao manabii, inawezekana alisema nao habari hizo za uongo kwa sauti iliyokuja kwa kupitia maono au ndoto, nao wakasikia na kupokea uongo huo. Hiyo ndiyo aina ya pili ya ndoto au maono yaliyo ya udanganyifu yanayokuja kwa kupitia roho ya udanganyifu kutoka kwa shetani au mapepo wabaya. Kumbuka shetani aliwahi kukutana na Yesu na kujaribu kumdanganya ageuze jiwe liwe mkate na kumtaka Yesu amsujudie ili ampe mali.

NTAJUAJE SASA KUWA NDOTO HII AU ONO HILI NI LA SHETANI?

Unaweza kujiuliza nitajuaje sasa kama roho hiyo iliyozungumza nami ni roho ya udanganyifu au la? Sikia neno la Mungu linatufundisha kuwa; tunapaswa kujaa sana neno la Mungu ndani yetu.

“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote……..(Wakorosai 3:316)

Kumbuka tulikotoka katika somo hili, Neno la Kristo ndilo liwezalo kukujulisha wewe kuwa, hilo lilosemwa ni kweli au uongo, neno la Mungu linaitwa kweli

“Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndio kweli” (Yohana 17:17).

Unaweza kujiuliza unamaana gani kusema hivyo? Hebu yatazame maneno haya

“Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake; mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu? Je! Mtu atakuwa na haki kuliko Muumba wake? Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; na malaika zake huwahesabia upuuzi; Je! Zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, ambazo misingi yao i-katika mchanga, hao waliosetwa mbele ya nondo! Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa; waangamia milele wala hapana atiaye moyoni. Je! Kamba ya hema yao haikungo’olewa ndani yao? Wafa, kisha hali hawana akili.” (Ayubu 412-21).

Hebu jiulize swali hili; Je! Ni kweli Mungu hawajali watumishi wake? Neno linasema kila atakayeamua kumtumikia Mungu, Mungu anamuheshimu mtu huyo.

“Mtu akinitumikia na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakuwepo tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu” (Yohana 12:26)

Mungu anawajali sana watumishi wake, anawapigania na kuwatunza. Sehemu nyingine anasema huwafanya watumishi wake kuwa viunga vya moto. Kwa hiyo unaposoma maneno ya Mungu na ukayalinganisha na hayo pepo aliyoyasema unagundua ni tofauti. Ukiona ono halipatani na neno la Mungu hapo unatakiwa usiyakubali hayo maono au hiyo ndoto.

Angalia mfano huu mwingine, shetani alimletea Adamu maneno yaliyo kinyume na maangizo ya Mungu alimwambia ale tunda hatakufa, kumbuka Mungu alimwambia kuwa akila hayo matunda atakufa. Jambo linguine, ukiona unaota ndoto na kuongea na waliokufa nk fahamu hayo si maono kutoka kwa Mungu usiyafanyie kazi yaache, tena ikemee hiyo roho. Pia Mungu hawezi kukuletea neno la kusema acha mkeo na uoe mwanamke mwingine, au ono la kukufanya uache kumwabudu yeye na kuanza kuabudu miungu mingine. Naamini umenielewa; sikiliza maneno haya ya Bwana yasemavyo

“Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribu mambo yote lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila aina” (1 The 5: 16-21)

Ukisoma maneno hayo utagundua kuwa, Swala si kuogopa kuona, kuota au kusikia, kinachotakiwa ukifanye ni kukiangalia kile ulichokiona, ulichokiota au ulichokisikia. Anasema jaribuni, usiache kuomba, pokea kila unachokiona au kukisikia na ukijaribu. Kama kizuri pokea na kama kibaya kiache, Wengi wamemzimisha Roho kwa kuogopa kukosea hawatafuti kuyajua mapenzi ya Mungu kwa sababu wanaogopa kuota ndoto au kuona maono ambayo yanawachanganya. Nakushauri pima ono au ndoto. Kwa leo Tumefikia mwisho wa salamu zetu hizi. Tuonane tena mwezi ujao na Mungu akubariki sana

Wako

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila