Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ndugu yangu naamini unaendelea vema. Mwezi uliopita yaani wa pili nchi yetu imetangaza rasmi kuhusu ugonjwa wa corona.
Kumbuka salamu hizi ndani yake zimebeba maarifa ya nini ufanye ikiwa mtu utakutana na tauni kama hizi. Fanyia kazi yale Mungu atakufundisha katika somo hili.
Mwezi uliopita tumekua na semina nyingi sana. Tumekua na semina iliyochukua wiki karibu mbili katika kanisa la Kkkt Bethel. Tulikua na semina ilikua inaanza saa kumi na moja mpaka saa moja yaani Morning glory
Pia tulikua na kongamano la maombi pale Kkkt Mjini ilikua ni kongamano la wiki mzima. Lilikua kongamano zuri. Pia tulipata nafasi ya kufundisha ibada mbili pale katika kanisa la Moravian Luanda.
Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya maombi yenu. Pia nikuhimize ombea sana taifa letu madhara ya corona yasitupate. Usikae kimya omba. Kumbuka tunasalamu zenye kichwa
MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)
Ebu tusogee mbele kidogo.
Katika salamu zilizopita tulijifunza jambo la tatu nalo lilikua LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU.
Katika salamu za mwezi huu wa tatu Nataka tuendelee mbele kidogo kwenye eneo hilo hilo.
MUNGU HUWA ANATABIA YA KUUFICHA USO WAKE
Angalia tena mistari hii: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)
Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu anasema “….Watajinyenyekesha, na kuomba na kunitafuta uso …..” Ukisikia neno tafuta maana yake hakipo, kimepotea, au hakionekani au ni kazi kubwa kukiona, n.k.
Kwa nini Mungu katika kipindi hicho ambacho anasema akipeleka tauni inatakiwa watu walioitwa kwa jina lake waombe na wamtafute uso wake?
Uso wake unakuwa umekwenda wapi? Na kwa nini kipindi hicho watu wake walioitwa kwa jina lake waingie gharama ya kuutafuta uso wake? Kwa nini ajifiche? Mungu hawezi kusema mnitafute kama hajajitenga na hao watu.
Sikiliza, sababu inayomfanya Mungu aufiche uso wake katika kipindi hicho inakuwa ni kwasababu ya hasira yake
Sikiliza, Mungu huwa anakasirika sana tu, na pia huwa anafurahi sana tu n.k.
Hasira zake hutokea anapoona dhambi za wanadamu zimezidi kiwango, hapo ndipo hukasirika sana. Na akikasirika ana tabia ya kuachilia adhabu na anapoachilia adhabu huwa ana tabia kuuficha uso wake kwa sababu nyingi tu.
Moja ya sababu ya kuuficha uso wake ni hii, ILI ASISIKIE KILIO CHA HAO WATU!!!! Kwa maana nzuri ndani yake huwa ana kua na hasira kali.
Mungu anapofurahia watu wake huzungumza nao uso kwa uso na haufichi uso wake. Na apouleta uso wake maana yake watu hao hukaa nuruni ambako ulinzi wao huwa ni mkubwa mno.
Mungu anapo wafurahia watu wake uso wake anauleta au haufichi, Angalia mistari hii uone hiki ninacho kuambia. “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.” (Kutoka 33:11)
Mungu alizungumza hapo na Musa uso kwa uso kabisaa kama rafiki yake. Angalia mistari hii mingine utaona kitu cha kujifunza katika eneo ambalo anasema wakiutafuta uso wake.
“BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. …….Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.” (Kutoka 33:1-5 na 13-17)
Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli aliuficha uso wake. Alisema akiingia kati yao au akiuleta uso wake kwa sababu ya dhambi zao atawaangamiza dakika moja.
Sikiliza, Mungu anapokasirika na kuachia adhabu fahamu anakuwa ameuficha uso wake. Kipindi hicho usifikiri utakutana naye kama ulivyokuwa unakutana naye zamani.
Ngoja nikupe mfano. Mungu alipowakasirikia wana wa Israeli baada ya kuabudu sanamu, Musa alikaa mlimani akiutafuta uso wa Mungu kwa muda wa siku arobaini.
Fikiria siku ya arobaini ndipo akauonyesha uso wake na kumwambia Musa amekubali.
Kwa lugha nzuri siku zooote hizo thelathini na tisa Mungu aliuficha uso wake.
Ngoja nikupe mfano mwingine. Unakumbuka Bwana wetu Yesu Kristo alipoichukua tu dhambi ya ulimwengu Mungu aliyekuwa pamoja naye siku zoote aliuficha uso wake?
Bwana Yesu Kristo alijua ndiyo maana alilia “Baba mbona umeniacha?” Uso wake Mungu ulifichwa, dunia yoote ikawa giza, muda wa masaa matatu hivi. Alipourudisha uso wake nchi ikapata nuru tena.
Mungu anapouficha uso wake fahamu giza hutawala, hapo ndipo wanadamu hukutana na magumu kutoka ulimwengu wa giza kwa kiwango cha juu mno.
Sikiliza nikuambie. Uso wa Mungu unapotutazama humu ulimwenguni ulinzi wa ulimwengu na kila kitu huwa mkubwa. Mimi nakuambia Mungu akificha uso wake ambao ni nuru kwa ulimwengu watu waishio humo ulimwenguni hujikuta kwenye misiba ya kila aina.
Uso wake unapokwenda nasi fahamu anatuona na anatuhurumia mnooo na kutuokoa na maradhi nk. Sasa Anapokasirika na kuachilia tauni ulimwenguni au nzige nk. Ana tabia ya kuuficha uso wake ili asiwaone wanadamu wanavyoteseka. Ili akawaokoe. KWASABABU ANA HURUMA SANA!!!
Mungu ana akili nyingi mnoo anajua akituangalia tu atatuonea huruma kwa hiyo hukimbilia kuuficha uso wake ili asiangalie.
Umewahi kufikiri siku ile ya Sodoma na Gomora kwa nini hakwenda kule? Unaweza kuniuliza kivipi. Sikiliza maneno haya: “BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za BWANA. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? …..Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake….” (Mwanzo 18:20-23 na 32)
Angalia na hii mistari uone ninachokuambia: “Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi.” (Kutoka 19:1)
Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu alipomfuata Ibrahimu hakuwa peke yake, alikuwa na malaika wawili. Mungu alibaki na Ibrahimu akiongea naye kwa ajili ya Sodoma na Gomora, wale malaika wawili wakawaacha wakiongea.
Mungu alipomaliza mazungumzo na Ibrahimu aliondoka. Biblia haisemi alienda Sodoma na Gomora. Walioingia Sodoma na Gomora ni malaika wawili. Jiulize Mungu alienda wapi?
Mimi naamini alirudi mbinguni na alienda kuuficha uso wake. Kwani alichokitarajia kukipata kutoka kwa Ibrahimu alikikosa, nacho kilikuwa ni utetezi. Ibrahimu hakufanya toba iliyoshiba kwa ajili ya watu wa Sodoma na Gomora kama Musa alivyofanya kwa ajili ya wana wa Israeli.
Malaika walichoma Sodoma na Gomora kilio chao hakikusikika kwa sababu Mungu aliuficha uso wake asione.
Mungu hapendi kututesa au kutuua: “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.” (Maombolezo ya Yeremia 3:31-33)
Mungu ukiona ameamua kuachia tauni fahamu hata uso wake huuficha kwa sababu hapendi kuona wanadamu wakiteseka.
Mungu ni Baba yetu, ndiye aliyetuumba, kama mzazi yoyote yule mwenye uungwana anatabia ya kuwachapa au kuwapiga watoto wake ili wawe na adabu.
Unajua watu wengi hawajui kuwa Mungu anapiga. Angalia mistari hii: “Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” (Ezekieli 7:8-9)
Umesikia maneno hayo mpendwa? Anasema “nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.” Mungu akikasirika anapiga tena anapiga kweli. Unaweza kusema haiwezekani bwana!!
Umewahi kufikiria hivi. Kama Mungu huyu alimwua mtoto wake wa kwanza ampendaye sana yaani Bwana Yesu Kristo ili amuokoe mwanadamu?
Kama aliweza kuua mtoto wake mpendwa asiye na dhambi kwa ajili ya wenye dhambi unafikiri itakuwa shida kuwaua hao wanadamu halafu wenye dhambi na jeuri na ukorofi?
Mimi nawaambia ukweli Mungu anaweza kabisa kuruhusu tauni na akauficha uso wake kabisaa ili dawa au adhabu iwaingie vizuri wanadamu!!!!
Angalia mistari hii, tena ipo katika agano jipya: “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.” (Waebrania 12:5-11)
Mungu anaweza kabisa kuturudi sisi watoto wake. Fikiria wasio watoto wake itakuwaje? Kumbuka watoto wake tu huturudi ili tuwe na adabu fikiria watu wake waliomo ulimwenguni je!
Kama anaweza kupiga kuanzia madhabahuni huko nje itakuwaje? Ebu tuliangalie pia jambo la Nne
JAMBO LA NNE: JIFUNZE KUUTAFUTA USO WAKE KWA TOBA NENDA KWA KUTUMIA NAFASI YA UKUHANI TU.
Sikiliza Mungu anapokuwa katika hali ya namna hii lazima wamwombao wabadili mfumo wa maombi yao, inatakiwa waanze kuomba maombi ya toba tu.
Pia fahamu ili Mungu asikie huko aliko katika kipindi kama hicho atawasikia makuhani tu.
Kwasababu kuhani ni mpatanishi, au kwa lugha nzuri ni mwombezi. Kuhani si mchungaji, au nabii, au mwalimu, au mtume. Mungu akikasirika na kuuficha uso wake ni kuhani peke yake anaweza kumsikiliza.
Kipindi hicho hasikilizagi nabii, mwalimu, mchungaji au mtume. Ngoja nikupe mfano uone: “Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.” (Hesabu 16:46-50)
Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Musa ni nabii hakugusa chetezo wala hakuingia katika huduma ya kufanya upatanisho.
“`Huduma hiyo ya upatanisho aliifanya kuhani tu. Mungu anapoleta tauni na tauni ikaanza kuua watu fahamu uso wake anakuwa ameuficha. Wanaoweza kumbembeleza na uso wake ukaonekana ni makuhani peke yao.
Hapo hakuna wafalme, wakuu, manabii au walimu, au waimbaji, au wainjilisti au mitumie. Atawasikiliza makuhani peke yao.
Sikiliza makuhani leo hii ni kanisa, unaweza kuwa mchungaji au askofu au mwalimu au padri au mwinjilisti au mtume au nabii lakini usiwe kuhani.
Katika agano jipya kuhani ni mtu yeyote aliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo
“Tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.” (Ufunuo 1:5-6)
Angalia na mistari “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” (Ufunuo 5:9-10)
Kila aliyenunuliwa kwa hiyo damu ni kuhani. Sikiliza makuhani, wewe ndiwe pekee umewekewa kazi hii ya kufanya maombezi yaliyobeba toba iletayo upatanisho ili Mungu aturehemu na tauni izuiliwe.
Kanisa tusipojitambua katika kipindi na sisi tukakaa kama watu wengine nawaambia ukweli uso wa Mungu utakuwa mbali; ataendelea kuuficha tu na tauni haitazuiliwa ulimwenguni.
Angalia mistari hii uone hiki ninachokuambia: “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao? Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa; lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.” (Yoeli 2:17-20)
Ukiipitia hiyo mistari utaona Mungu aliuficha uso wake ili awaadhibu wanadamu. Alichokifanya ili aone yaani uso wake urudi kuwatazama hao watu, aliagiza makuhani walie au wakamtafute.
Hakusema manabii, n.k. Alisema makuhani. Sikilizeni kanisa, MUNGU ANAWASUBIRI NINYI MLIE. Bahati mbaya kipindi kama hiki akili ya kanisa inakua kwa viongozi wa nchi, au kwa maaskofu au kwa manabii, n.k.
Sikiliza wewe kuhani yaani wewe uliyenunuliwa kwa damu ya Bwana Yesu Kristo unaweza ukawa askofu, kiongozi fulani au mchungaji, mwinjilisti na inawezekana kabisa usiwe kiongozi au nabii au mwinjilisti, n.k. ANZA KUUTAFUTA USO WA MUNGU KWA TOBA UONAPO TAUNI AU NZIGE NK VIMEPELEKWA ULIMWENGUNI NA MUNGU.
Utafute uso wa Mungu, ingia gharama, kwa ajili ya watu wako, nchi yako, taifa lako, na ulimwengu woote.
Tubia maovu au dhambi au makosa ya aina yoyote ambayo ndiyo chanzo cha hasira kutoka kwa Mungu.
Jifunze KULIA , SI KUKEMEA TUUUU MPENDWA; KUHANI LIA MBELE ZAKE MUNGU NDIPO USO WAKE UTAONEKANA NA TAUNI AU NZINGE AU MAJANGA YOYOTE KAMA CORONA NK ZITAZUIWA KWA MAARIFA ATAKAYOYAACHILIA.
Au kama tauni Imepelekwa Mungu akiuleta uso wake fahamu atawaokoa wale waliao kwa ajili ya uovu utendwao katika mji wao au taifa lao au nyumba yao.
Nataka kukutia moyo usijidharau wewe kuhani ndiwe pekee mwenye kuurejesha uso wa Mungu ili uende na watu walioko duniani.
Unaweza kumshirikisha mpendwa mwingine ujumbe huu.
Tuonane mwezi ujao katika kona hii ya salamu za mwezi. BARIKIWA
Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-
- App yetu ya huduma yenye jina “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
- Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
- YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
- Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
- Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
- DVDs au CDs
- VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
- Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
- Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku.
- Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
- Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
- Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:- radio.mwakatwila.org
Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-
+255 754 849 924 au +255 756 715 222
Wako
Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.