Salamu – Februali, 2020

Ndugu yangu ninakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo. Nimekuletea salamu za mwezi huu wa pili. Mwezi wa kwanza umeanza kwetu tukiwa na semina Katika kanisa la Bethel Kkkt,tukawa na semina Chuo cha wachungaji cha Moravian Utengule na pia tulikua na semina maalumu ya shukrani jijini Mbeya.

Semina hizi zilikua za baraka sana. Ebu tuanze kupokea salamu za mwezi huu. Kumbuka tunasalamu zenye kichwa
MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Katika salamu zilizopita nilikuonyesha  mambo mawili ambayo unatakiwa uyafanye ili upate kuokolewa na tauni iliyoachiliwa ulimwenguni kutoka kwa Mungu. Ambayo yalikua.

Ni lazima uitwe kwa jina la Bwana tukaona lazima umwamini na umpokee Bwana Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako

Jambo la pili lilikua ni lazima uwe mnyenyekevu. Naamini ulijifunza kitu. Ebu tusogee mbele kidogo tuliangalie jambo la tatu.

JAMBO LA TATU. LAZIMA UOMBE KWA MFUMO WA MAOMBI YA KUUTAFUTA USO WA MUNGU

Angalia hii mistari tena: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2Mambo ya Nyakati 7: 12-15)
Ninachotaka tukione katika hili jambo la tatu ni hiki Mungu asemacho hapo kuwa. “Tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso…”

Mungu anaporuhusu tauni kama Corona nk au nzige au vita nk, ili iwapige watu na kuua miili yao. ili awaokoe hao watu na hiyo tauni au awalinde hao watu na hiyo tauni anasema ni lazima hao watu waingie katika maombi ya kuutafuta uso wake.

kumbuka hao watu wanaoambiwa wafanye hivyo  ni wale walioitwa kwa jina lake na walio wanyenyekevu. Ili leo hii mpendwa Mungu akulinde na kukuokoa na tauni inatakiwa ujifunze kuomba ili Mungu akuokoe wewe, nduguzo, taifa lako, n.k.

Unajua unaweza ukasema si nimeokoka mimi na nina matendo mema mimi tauni haitanipata kwa sababu nimeahidiwa na Mungu kulindwa. Sikia ndugu, Mungu huyo aliyetuahidi kutulinda ndiye anatupa maarifa hapo ya nini tufanye ili tauni isitupige.

Anasema watu walioitwa kwa jina lake walio wanyenyekevu lazima waombe tena maombi ya kuutafuta uso wake.

Unapokutana na kipindi cha namna hiyo fahamu ni kipindi ambacho kwa kweli wewe uliyeokoka unatakiwa uombe kuliko kipindi chochote. Usijidanganye kuwa utapona kisa umeokoka. Msikilize Mungu anasema wakijinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu….!!!!
Watoto wa Mungu wengi sana hawajui pona yao itategemea kiwango cha wao kuomba.

Ngoja nikupe mfano huu. Msikilize Bwana Yesu Kristo asemavyo: “Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.” (Luka 22:40-46)

Ukiipitia hiyo mistari utaona hiki ninachokuambia. Bwana Yesu Kristo aliwapa hao ndugu maarifa ya nini wafanye ili wasiingie kwenye magumu. Kumbuka magumu hayo Mungu ndiye aliyeyaruhusu.

Unaweza kuniuliza ulijuaje? Sikiliza, Bwana Yesu Kristo aliwaambia hao ndugu shetani anawataka ili awapepete kama ngano. Umewahi jiuliza aliwataka kwa nani?

Angalia alitafuta kibali kwa Mungu. Bwana Yesu alilijua hili, akawahi haraka kuwapa taarifa hao walioitwa kwa jina lake kuwa na wao waende kwa Mungu wakaombe Mungu awapitishe mbali na ombi hilo.

Wao walizembea walilala. Unaweza kujiuliza kwa nini Mungu asiwaokoe tu na hilo jaribu au teso au gumu? Sikiliza, Mungu ameweka utaratibu huo tokea zamani sana. Usipoomba yeye haangalii tu kuwa wewe ni nani kwake.

Ngoja nikupe mfano huu labda utaelewa. Siku moja wana wa Israeli waliambiwa na Mungu kuwa, Mungu amepania kuleta tauni Misri. Tauni iliyowalenga watu wa sifa ya wazaliwa wa kwanza, wawe wanyama n.k.
Ili tauni hiyo isiwapige wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli ambao ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake, Mungu aliwaambia kila mmoja akaweke alama katika milango ya nyumba zao.

Ili tauni ikianza isiwapige hao wazaliwa wa kwanza waliomo ndani ya nyumba zao. Fikiria kwa nini asiwaokoe tu? Kwani alikuwa hawajui hao wazaliwa wa kwanza wa wana Waisraeli
Mungu aliwafahamu wazaliwa wa kwanza wooote wawe wa Wamisri au wa Wana wa Israeli. Lakini alitafuta kuona unyenyekevu na uhitaji wa kuokolewa wa hao wana wa Israeli.

Fahamuni wapendwa kuwa Mungu anatafuta kuona mtu akiomba kuokolewa, asipoomba usifikiri atamuokoa.

Ngoja nikupe mfano huu mwingine. Angalia mistari hii: “Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.” (Kutoka 2:23-25)
Ukiipitia hiyo mistari utaona kitu hiki ninachokufundisha. Hao ndugu, Mungu aliwaona na kuwaangalia na kulikumbuka agano hilo kipindi hao watu walipotafuta msaada kutoka kwake, tena walipolia na kuugua kwa sababu ya ule utumwa.

Fahamu, walipokuwa hawalii, hawaugui, kwa sababu ya utumwa wao Mungu hakuwaangalia wala hakuwaona.

Kumbuka sana hao ndugu ni watu wa Mungu walioitwa kwa jina lake kabisaa. Ili Mungu awaokoe alisubiri waombe kwa maombi ya mfumo huo ndipo akawaokoa.
JIFUNZE KUJIWEKEA ALAMA ILI TAUNI ISIKUPATE Unapoingia kuomba kwa ajili ya tauni ili isikupate ndipo unapojiwekea alama maalumu ili tauni inapoijilia nchi yako au mji wako ikiona alama hiyo inakupita.

Usipojiwekea hiyo alama fahamu itakupiga tu haitajalisha wewe ni askofu, daktari, mchungaji, n.k.

Ngoja nikupe mfano huu ili uone tauni inaletwaje katika ulimwengu wa roho na watu watakaopona wanakuwa na sifa zipi hasa.

Pata picha hii ndiyo utanielewa sana ninapokuambia omba, Angalia mistari hii.
“Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji. Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu? Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni. Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao. Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.” (Ezekieli  9:1-11)

Hebu irudie hata mara tatu kuisoma hiyo mistari. Utaona kinachofanyika katika ulimwengu wa roho kinakuwaje.
Ni rahisi ninyi huku duniani kuona virusi. Lakini kwenye ulimwengu wa roho huwa ni viumbe kamili wanaoifanya hiyo kazi. Sikiliza jambo hilo Ezekieli aliliona likifanywa katika ulimwengu wa roho. Na likatokea kabisaa katika ulimwengu huu wa mwili.

Fahamu katika kila mji au taifa kuna malaika wamewekwa ili kuwa wasimamizi wa miji au taifa. Kazi yao ni kutoa taarifa kwa Mungu kwa ajili ya hiyo miji au hilo taifa.
Sikiliza Mungu anapotaka kuachilia tauni ikaipige miji au mataifa hao unaowasikia hapo wapo hata hii leo ndiyo wanaohusika kuyafanya hayo. Wapo ambao kazi yao ni kutia alama watu ambao tauni inatakiwa isiwapate.. Hata ikiwapata hawata kufa
Kwa taarifa yako hakuna kinga zaidi ya hiyo alama. Kama unafikiri nakutania Angalia mfano, tauni ya corona ilipokuja ulimwenguni wanadamu waliambiwa wanawe mikono nk.
Umewahi kufikiri Ulaya na Marekani walivyo wasafi? Huku sisi ndiyo tunafundishwa kunawa, wenzetu hunawa na hizo sabuni za kuua wadudu kila siku.

Lakini virusi hivyo havikuja wewe ni nani vimewavaa hata mawaziri wakuu, wafalme, n.k. Kuna waziri mkuu wa nchi kubwa ya Uingereza alikutwa na tauni hiyo, Kama waziri mkuu anatauni hiyo fahamu baraza looote la mawaziri hawakua salama.
Cha ajabu watu wengine usishangae hawapati hiyo tauni. Ni sawa na UKIMWI nakuambia ungejua kinachotendeka kwenye ulimwengu wa roho mpaka mtu akapata UKIMWI nakuambia ukweli watu wengi wangeacha kuzini kwasababu HAKUNA KINGA.

Ngoja nikuonyeshe labda utaniekewa. Angalia mistari hii: “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.” (Ufunuo 2:18-24)

Ukiipitia hiyo mistari utanielewa haraka ninapokupa picha hii ili uone ni nini huwa kinafanyika kwenye ulimwengu wa roho.  Haya mambo yanavyofanyika kwenye ulimwengu wa roho ni ngumu huku kwenye ulimwengu wa mwili kukinga.
Lazima utafute msaada kutoka kwenye ulimwengu wa roho ili Mungu aamue yeye kukuwekea alama. Tauni inapoachiliwa usifikiri kuna kinga, ni malaika hutumwa kufanya hivyo. Angalia Ezekieli aliona picha nzima llivyokwenda. Aliyewekewa alama alipona; hakufa.

Ukiitazama ile mistari waliowekewa alama ni wale tu waliokuwa wanaomba au kulia kwa ajili ya maovu yaliyokuwa yakifanywa katika mji ule. Nitakuonyesha vizuri katika huko mbele
Fikiria kidogo, adhabu ile au tauni ile ilianzia madhabauni pa Mungu. Wale viumbe walimwacha Ezekieli kwa sababu tu alikuwa na alama, kumbuka huyo alikuwa mtu wa madhabahuni. Wenzie walikufa, kisa hawakua na alama.

Kwa lugha nzuri walikuwa hawaombi hao. Nikuulize swali umenielewa? Unaposikia tauni usifikiri itakaa mahali furani tu, fahamu inaweza kuja kwenye taifa lako au mji wako,
Mfano tauni ya corona ilipoanza huko china, Wamerekani na ulaya na Afrika nk hawakufikiri kuwa tauni hiyo itawapiga, angalia mfano,Waitalia wengi walifikiri itawapiga Wachina tu, sikiliza ukisikia tauni au nzige nk wapo katika taifa furani au mji furani. Lazima uombe ili isije au ikija isilete madhara.
Lazima Watanzania tuombe tena tuombe sana tunaposikia mambo kama haya yakitokea katika mataifa furani.
Sikilizeni viongozi wa serikali hii MUNGU ANALIPENDA SANA TAIFA HILI. Si kuwa sisi ni wema kuliko hayo mataifa mengine. Ni NEEMA.
Inapotokea tauni au majanga ya nzige, viongozi wa nchi kuwahimiza watu kuomba sana. Itakuwa vema sana kila kiongozi eneo aliopo ahimize watu wa eneo hilo waombe juu ya tauni au nzinge nk.
Ni vema wpaangeni hata siku maalumu ya maombi ya mfumo mzuri wa watu wakae mkao wa kuomba kama Taifa, Mkoa, Wilaya, Kitongoji, n.k.

NAWAAMBIENI UKWELI KWA KUFANYA HIVI NDIYO TUTAVUKA.
Naamini kwa sehemu umenielewa FANYIA KAZI HAYO.

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
    • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
    • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
  9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.