Salamu – Juni, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ni imani yangu kuwa Mungu amekupa uzima. Mi mi na familia yangu ni wazima tunamshukuru Mungu.

Nimekuletea salama za mwezi wa sita. Naomba zipokeee. Kumbuka tunasomo lenye kichwa

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

JAMBO LA SITA ACHA KUFANYA MAOVU ILI MUNGU ASIKUPIGE NA TAUNI

Sikiliza maneno haya: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Unapoisoma hiyo mistari utaliona hili jambo ninalokuambia, Maandiko yanasema: “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

Moja ya jambo ambalo Mungu ataliangalia ili aondoe tauni au nzige nk ni hili la hao waliomwudhi mpaka akaamua kuwaua kwa tauni wameamua kuacha matendo yao mabaya  ambayo kwa kweli yalikuwa yanamwudhi Mungu.?

Angalia mwenyewe hapo anasema wakiaziacha njia zao mbaya. Kwa mujibu wa hiyo mistari, hebu mwulize swali ikiwa hatutaziacha njia mbaya itakuwaje?

Jibu ni rahisi tu haondoi tauni au haponyi nchi.

Ili Mungu ainusuru nchi na janga hili kila mwenye mamlaka yoyote iwe kisiasa au kidini lazima awaambie watu wa nchi yake ukweli KUWA KILA MTU AACHE DHAMBI. NAWAAMBIA UKWELI HILI NDILO LITASAIDIA MNOO KULIKO JAMBO LOLOTE

UKITAKA MUNGU AKUOKOE KATIKA KIPINDI KAMA HIKI NI LAZIMA WEWE MWENYEWE UMHAKIKISHIE KUWA UTABADILIKA KATIKA MWENENDO WAKO.

Sikiliza ukitaka Mungu akuokoe wewe au watu wako, ni lazima pia uhakikishe kuwa unamhakikishia kuwa utabadilika kwa kuyaacha mambo yako yaliyo maovu au umhakikishie kuwa utafanya jitihada kubwa ya kuwashawishi hao unaowaombea waache tabia zao mbaya.

Ngoja nikupe mifano hii mizuri angalia mistari hii“Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate” (Luka 13:1-9)

Ukiisoma hii mistari utanielewa haraka mno nakufundisha nini. Hao ndugu walisikia namna watu hao walivyokutwa na magumu yaliyobebwa na mauti.

Na unapoisoma hiyo mistari utagundua hao watu walikufa kwa sababu ya matendo yao maovu. Bwana Yesu Kristo aliwaonya hao ndugu waliokuwa wamesikia kilichowapata wenzao kuwa hata wao wako kwenye hatari kama hiyo hiyo.

Ili hatari hiyo isiwapate aliwafundisha neno hili watubu.

TOBA ISIYO NA GEUKO HIYO SIYO TOBA

Fahamu ndani ya neno toba kuna kugeuka au kuacha kuyafanya yale maovu ya zamani. Kwa maana nzuri ni hii ili Mungu amwokoe mtu na tauni au gumu lolote linalotokana na hasira yake ni lazima huyo mtu au hao watu watubu au waache njia zao mbaya. Toba isiyo na geuko hiyo siyo toba.

Unapoisoma hiyo mistari utaona huyo mtu ambaye alisimama ili kuunusuru huo mti usikatwe alimshawishi huyo mwenye mti asiukate kwa sababu moja tu kubwa, kuwa mti huo kuanzia sasa utaanza kuzaa matunda.Kwalugha huo mti unaachana na tabia yake ya kwanza ya kutokuzaa matunda

Kwa maana nzuri zaidi mti huo utaacha mwenendo mbaya wa zamani na kuanza mwenendo mpya wa kuzaa matunda, fahamu mti huo ulipewa mwaka mmoja, mti huo ulitakiwa ndani ya mwaka huo mmoja ubadilike, usipobadilika katika kipindi hicho unakatwa.

Sikiliza katika kipindi kama hicho itategemea kasi ya tauni hiyo au nzige iliyopelekwa ulimwenguni ina kasi kwa kiwango gani. Kama kasi ni kubwa usifikiri hapo umepewa mwaka wa kubadilisha mfumo mzima wa maisha yako mpendwa.

Fikiria kidogo kipindi hicho mfano una mwomba Mungu usiugue ugonjwa huu, na inawezekana kabisa umekutana na hiyo tauni fahamu hapo kuna mambo mawili pia kuna kufa au kupona, swali langu unafikiri unatakiwa ufanye nini ili umshawishi

Mungu ili akuponye? KUMBUKA MPENDWA TAUNI IKILETWA KUNA KUWA HAKUNA DAWA.

Kama hakuna kinga na hakuna dawa maana yake TUNAMHITAJI MUNGU KWA UHITAJI MKUBWA.

Unafikiri ili kumwomba akupe siku nyingine yaani akukinge usipate, au akuponye unatakiwa umwambie neno gani zito hapo?

Rudi kwenye maneno yake aliyosema, anasema wakiziacha njia zao mbaya nitawaponya. Kwa hiyo kumbe tauni inapoletwa na Mungu, ina tabia ya kuwakwepa watu ambao wamefanya maamuzi thabiti moyoni ya kubadilika.

Na mtetezi wao ni mmoja tu ni Bwana Yesu Kristo ambaye atarudi kwa Mungu na kumwambia Baba huyu ndugu hebu tumwache tumpe siku kadhaa ameahidi kubadilika yaani kuzaa matunda.

Natamani unielewe mpendwa shoka limewekwa mtini, wewe ndiyo mti, ili usikatwe angalia hoja yako kwa mkataji unamwambia nini? Mwambie niache usinikate na ahidi nitakuzalia matunda yaani NABADILIKA KUANZI DAKIKA HII.

Angalia mfano huu uone ambao Yohana mbatizaji aliusema kwa watu ambao walikuwa wanajaribu kuikimbia adhabu ya Mungu, aliwaambia hivi: “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” (Mathayo 3:7-10)

Maandiko yanatupa akili hapo kuwa kipindi kama hicho kikimkuta mwanadamu anatakiwa ahakikishe anaikwepa hasira ya Mungu kwa kukimbilia kubadilika tabia yaani aache mwenendo wake mbaya.

Angalia mfano huu uone alichowaeleza Yohana hao watu wakifanye: “Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.” (Luka 3:9-14)

Yohana aliwajibu hao watu kwa kuwafundisha ni nini wanatakiwa wakifanye katika kipindi cha kukabiliana na hasira ya Mungu.

Aliwaambia waache uovu. Waache tabia zao mbaya. Sikiliza mpendwa unapokutana na janga la tauni ulimwenguni unatakiwa ufanye nini? Umemsikia Mungu hapo akupavyo akili ili akuponye na kukuokoa na tauni anataka uache huo uovu wako?

Basi mnyenyekee. Mwambie kwa kimywa kuwa umemkosea sana. Lia mbele zake. Mwambie kuwa UNAACHA MWENENDO MBAYA.

Anza sasa hivi kuuacha huo mwenendo. Mfano leo hii acha uzinzi, acha ulevi, acha sigara, sikia nikuambie Virusi vya tauni kama corona inawaua mno watu wenye tabia hizi. Mimi najua ninachokuambia. Mzinzi, mlevi, mtu wa sigara, madawa ya kulevya, n.k. ni ngumu kupona ukipata.

Unajua kwa nini? Yaani vitu hivyo vinaondoa mnoo nguvu ya kinga za mwili. Acha tabia ya uongo, acha kubambikizia watu kesi, umemsikia Yohana akiwaambia askari? Hiyo ni tabia ya dhambi mpendwa

Acha kuabudu miungu, leo hii ondoa hirizi, n.k. havitakulinda nakuambia.

Acha kuiba, acha kuiibia pia serikali kwa kulipa kodi au ushuru kuanzia sasa

Mwambie Mungu nitatosheka na mshahara wangu, acha kuiba mpendwa. Kumbuka sana hili badilisha mfumo wa tabia yako hili litakusaidia mnoo katika kuokolewa na shoka lililowekwa tayari ili kuukata mti yaani wewe.

Mungu akuwezeshe kunielewa na kuchukua hatua.

Tuonane katika katika salamu za mwezi ujao.

Ubarikiwe sana pia ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. Website yetu ya www.makatwila.org
  2. Youtube- Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU
  3. Facebook ingia katika hiyo tovuti au website yetu utaona alama ya facebook(f) like na utapata maelezo ya kujiunga
  4. Dvds au Cd
  5. Vitabu
  6. Kwa njia ya Redio mbalimbali Rungwe fm102.5 Kila siku Jumapili saa tatu mpaka saa nne usiku
  7. na Baraka Fm107.5 kila siku ya jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku na Bomba fm 104.1 kila siku ya ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku 7: Unaweza kutupata kwenye redio yetu online ya. radio.mwakatwila.org

Kwa mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi. 0754849924, 0756715222

Wako Mr &Mrs Steven Mwakatwila