Salamu – Julai, 2021

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Ninakukaribisha tena ndugu yangu katika kona hii ya salamu za mwezi. Mimi na familia yangu ni wazima tunamshukuru Mungu sana aliyetupigania na kututunza. Nimekuletea mfululizo wa salamu zenye kichwa.

VIPAO MBELE VYA MAOMBI YAKO WEKA BIDII YA KUOMBEA MASIKIO YAKO.

Hebu tusogee mbele kidogo tujifunze eneo hili la maana ya neno kusikia

MAANA MBILI ZA KUSIKIA.

Unapolitazama neno kusikia unaweza kukuta lina maana zaidi ya moja.. mimi ntakuonyesha maana mbili za neno kusikia.

A: MAANA YA KWANZA NI HII . MASIKIO KULISIKIA NENO LA MUNGU AU LA MTU NK

Kazi kubwa ya sikio ni kukisikia,kitu chochote kiwezacho kusikika.Biblia inasema kuwa mtu aliye na sikio inatakiwa asikie

Bwana Yesu Kristo alisema hivi. ”Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. (Marko 4:23-24)

Kusikia huku kunalilenga sikio la mtu aliyeumbwa na Mungu ili asikie.

B: KUSIKIA KWA KUSOMA.

Ndani ya neno la Mungu kuna sauti ya Mungu kabisaa…kwa hiyo kuna kusikia sauti ya Mungu au ya mwandishi kwa kupitia masikio ya ndani pale mtu anaposoma maandiko au vitabu mbalimbali.

Sikio hili ndiyo haswaa mimi nalitaka ujifunze kuomba kwa Mungu ili alizibue ili uisikie sauti ya Mungu anaposema na wewe kupitia Biblia au vitabu. Sikio lako la ndani kama ni zito huwezi kuisikia sauti ya Mungu unaposoma Biblia au vitabu.

Biblia imebeba sauti ya Mungu, unajua ukizibuliwa sikio lako utashangaa kuisikia sauti ya Mungu kupitia Biblia…utasikia akikuonya,akikufundisha,akikutia moyo,akikupa maarifa nk.

Si kila mtu asomaye Biblia huisikia hiyo sauti…wengi husoma ilimladi wamesoma.. hata ukimuuliza msomaji Mungu amekwambia nini hawezi kukujibu kwasababu hakuisikia sauti ya Mungu kwa kupitia neno alilokua ana lisoma.

C: AU KUISIKIA SAUTI YA MUNGU KUTOKA KINYWA CHA MTUMISHI.

Mungu anaweza kusema kwa kupitia mtu furani sasa sikia si kila neno asemalo mtu au mtumishi limebeba sauti ya Mungu.

Mungu anaweza kuachilia sauti yake kabisa kwa kupitia mtu..na watu hao huitwa watumishi..sasa sikio lako linatakiwa lizibuliwe ili uanze kuisikia sauti ya Mungu kwa kupitia mtumishi wake.

Angalia mfano huu.. labda utanielewa vizuri ”Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.” (Yohana 5:24-29)

Wafu hao waisikiao sauti ya mwana wa Mungu ni wanadamu wasio na huyo mwana wa Mungu ndani yao, sasa sikia Mwana wa Mungu yaani Bwana Yesu Kristo alipowaita hao watu hakuja yeye kimwili aliwatumia watumishi wake.

Anatumia vinywa vya hao watumishi..sasa sikio lako kama halijazibuliwa ni vigumu kuisikia sauti ya Bwana Yesu Kristo iliyopitia neno kutoka kwa mtumishi.

Watu wengi huisikia sauti ya mtumishi..hawaisikii sauti ya Mungu,ndiyo maana wengi hawabadiliki,hawana mafanikio na hawawezi kulitendea kazi hilo neno kwasababu tu masikio yao hayajaisikia sauti ya Mungu ila wameisikia sauti ya mtumishi.

Sikia..tunaweza kwenda wote ibadani, mtu mmoja akatoka hapo na furaha kabisa kwasababu amemsikia Mungu akisema naye kupitia huyo huyo mtumishi ambaye wewe unamdharau weee…

D: MFANO WA ISHARA NI SAUTI YA MUNGU UKIWA NA SIKIO LA KUSIKIA UTAISIKIA

Mungu anasauti yake nyingine ambayo masikio yako yanatakiwa yazibuliwe ili uisikie hiyo sauti pia… ni sauti iliyokuja kwa njia ya ishara..au muujiza nk

Angalia mfano wa mistari hii…. “Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea.BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea.BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji.Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili.”(KUTOKA4:1-8)

Ukiipitia mistari hiyo unajifunza kuwa kumbe ishara mbalimbali anazofanya Mungu kwa kupitia watumishi wake ni sauti ya Mungu kwa watu..

Mungu alimwambia Musa kuwa ishara hizo ni sauti ya Mungu kwa watu wake na ilitakiwa wasikie kwa kupitia ishara hizo…

Shida ipo hapa watu wengi wakiona na kusikia habari za ishara hawaisikii sauti hiyo kama ni Mungu badara yake humtazama mtumishi na kumheshimu badara ya kumheshimu Mungu aliosema nao kwa kutumia sauti ya ishara…

Na ishara hiyo ikifanywa na Mungu ndani yake itakupa maelekezo ya nini Mungu kakikusudia. Angalia mfano huu “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” (Mathayo 8:16-17)

Ishara hiyo ya uponyaji aliyoifanya Bwana Yesu Kristo ilibeba sauti ya Mungu akiwadhibitishia watu kuwa Huyu Bwana Yesu Kristo ndiye aliyetabiriwa na nabii Isaya..

Ndani ya uponyaji ule kulikua na sauti hiyo ya Mungu, sasa angalia watu wengi hawakuisikia sauti ile kwasababu masikio yao yalikua hayasikii..

Umewahi jiuliza kwanini Bwana Yesu Kristo alisema hivi. “Mwenye masikio na asikie.Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”(Mathayo 13:9-16)

Hao watu walisikia waliona ishara nk..lakini hawakuisikia sauti ya Mungu. Ndiyo ilivyo leo kwa watu wengi mnoo… hawana masikio yasikiayo sauti ya Mungu kwa kupitia ishara.

Ngoja nikupe mfano huu Biblia inasema wazi kuwa kutakua na ishara mbalimbali zikitupa taarifa kuwa tunaishi kwenye siku za mwisho….kama vile jua mwezi kupatwa,dhiki,vita,matetemeko, chuki, bahari kuvuma yaani sunami nk.

Hivi vitu vikitokea huwa unaisikia sauti ya Mungu au ya wanasayansi? Watu wengi hatuisikii sauti ya Mungu tunapoona ishara hizo zikitupa maelekezo kutoka kwa Mungu.

Ngoja nikupe mfano huu mwingine wa sauti ya Bwana Yesu Kristo kwa kupitia ishara “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu.Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]” (Marko 16:17-20)

Ukiona watu wakiwa wamebeba ishara za namna hiyo fahamu kuna sauti ya Mungu kwa kupitia ishara hizo.

Bwana Yesu Kristo leo hii huwa anatabia ya kudhibitisha neno lake lililobebwa na watumishi kwa kupitia ishara.

Sasa ona watu wengi leo hii hawaisikii hiyo sauti…wanaona muujiza tuu….na kumpa sifa mtumishi kumbe wangeisikia sauti ya Mungu wangemludishia Bwana Yesu Kristo sifa kwa kuachilia sauti yake kwa njia ya ishara aliyoifanya hapo.

Anza kuombea masikio yako hayo ya ndani na ya nje ili yasikie sauti ya Mungu katika maeneo hayo yoote

Mungu akubariki sana. Tuonane tena katika kona hii mwezi ujao.Naamini umenielewa sana.Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

  1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
  2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
  3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
  4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
  5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
  6. DVDs au CDs
  7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
  8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
    • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
    • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
    • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
  9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.