Salamu – Feb, 2011

Bwana Yesu asifiwe sana, Tunakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo.  Mimi na familia yangu ni wazima tunamshukuru Mungu. Tumekuletea tena salamu  zetu za mwezi. Na katika mwezi huu wa pili, tumekuletea salamu nzuri sana ambazo tuna amini kuwa kuna kitu Mungu Roho Mtakatifu atakiweka ndani ya moyo wako kitakacho kwenda kukutoa sehemu moja na kukupeleka sehemu ya pili.  Kumbuka tumekua na mfululizo wa somo zuri la kugeuzwa nia zetu. Angalia maneno haya. .  ” …..bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu,mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema,ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Rum 12:2b)   Mungu anataka mimi na wewe tugeuzwe nia zetu, kumbuka neno nia ni fikra au  kusudi, kwa maana nzuri ni mfumo nzima wa akili zako.

Tumeanza kuangalia mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza lilikua ni kujua kuhusu habari nzima za wewe kugeuzwa fikra zako. Jambo la pili tulianza kuangalia vitu vinavyoweza kuharibu mfumo mzima wa akili zako. Tuliangalia mambo matatu. Jambo la kwanza ni dhambi. Jambo la pili mazingira, jambo la tatu ni  nguvu za giza. Baada ya kuyaangalia mambo hayo matatu, ebu tuanze kuangalia mambo muhimu ambayo unatakiwa uyafanye ili kuigeuza hiyo nia yako.

Hebu tuliangalie jambo la kwanza nalo ni.

NJIA YA KUIGEUZA FIKRA YAKO.  NJIA YA KWANZA NI : KUOMBA MAOMBI MAALUMU YA KUGEUZWA NIA

Sikiliza, Neno linaposema mgeuzwe nia zenu, linatupa ufahamu kuwa sisi hatuwezi kujigeuza. Kwanini nasema hivyo? Sikiliza, neno linasema MGEUZWE halisemi MJIGEUZE. Ukiliangalia haraka haraka neno hilo, unaweza kufikiri anazungumzia uwingi. Lakini ukitulia ndipo utagundua hiki ninacho kuambia anasema mgeuzwe. Maana yake yupo atakaye wageuza sio nyinyi.

Mwenye uwezo wa kigeuza au kuitengeneza fikra ya mtu iliyo haribiwa ni Mungu.  Kwa kuwa Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kuigeuza hiyo fikra yako unatakiwa uanze kumuomba azigeuze fikra zako. Ukisoma maandiko matakatifu utaona moja ya  mambi ambayo watumishi wa Mungu walikua wakiyaomba kwa Mungu lilikua ni jambo hili la kupewa fikra mpya au akili nzuri. Ngoja nikupe mifano hii michache uone. Mtume Paulo alipokua analiombea kanisa mojawapo  ya  maombi yake lilikua ni hili la kupata akili au ufahamu. Sikiliza maombi yake haya akiliombea kanisa la Kolosai “ Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajiri yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katia hekima yote na ufahamu wa rohoni;” (WAKOLOSAI 1:9)

Mtume Paulo aliwaombea hao ndugu Wakolosai Mungu awape Ufahamu. Kwanini aliomba hivyo? Mtume Paulo alijua wazi kuwa hao wakolosai wanatakiwa kuwa na ufahamu mzuri.  Na alijua kuwa Mungu peke ndiye mwenye uwezo wa kuwapa, tena kwa kuwajaza  ufahamu na maarifa. Ukitulia hapo utaona alichokuwa anakitafuta Mtume Paulo kwa Mungu ni kuwaombea hao ndugu wageuzwe fikra zao za kizamani ambazo tayari zilikua hazifai tena. Anaposema mjazwe maana yake walikua na maarifa kidogo, kiwango chao cha maarifa kilikua kidogo ndio maana aliwaombe wajanzwe hayo maarifa. Kumbuka tunapozungumzia neno nia tunazungumzia mfumo mzima wa kusudi la mtu. Katika kila kusudi, akili itatumika,fikra zitatumika,mawazo yatatumika, ufahamu utatumika, na maarifa yatatumika hekima itatumika busara itatumika. ukiangalia hapo utaona kuwa mfumo mzima wa akili zako ndio unaotakiwa ujanzwe mahali pale ulipopungua. Na atakaye kujaza ni Mungu, na njia unayotakiwa uitumie ili akujaze ni maombi.

Hata kwa kanisa la Efeso, Mtume Paulo aliwaombea maombi ya namna hiyohiyo. Angalia maneno haya “ Kwa sababu  hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajiri yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, baba wa utukufu,awape ninyi roho ya hekima naya ufunuo katika kumjua yeye: macho ya mioyo yenu  yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;…….” (WAEFESO 1:15-19). Mtume Paulo aliwaombea Waefeso Kwa Mungu maombi ya ajabu sana, aliwaombea hao watu Mungu awape roho ya hekima,  ukitulia hapo utaona kuwa alichokuwa anakiomba Mtume Paulo ni kilekile cha mfumo mzima wa akili za Waefeso kikae sawa.   Mtume Paulo aliwaona hao Waefeso kuwa wamepungukiwa na hekima, akaamua kuwaombea kwa Mungu awape roho ya hekima. Mungu amesema wazi kuwa mtu yeyote yule aliyepungukiwa na hekima amuombe hekima na ameahii kutupa hekima. “ Lakini  mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima,na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa ila aombe kwa imani, pasipo shaka yeyote;…” YAKOBO 1:5-6).Mungu anajua umuhimu wa sisi kuwa na hekima, ndio maana anatupa nafasi ya kumuomba atupe hekima au kwa maana nzuri kuwa na fikra nzuri zilizojaa ufahamu na maalifa, anasema tumuombe,ngoja nikuulize swali hili… Je? ni mara ngapi umefanya maombi ya namna hiyo? Umeridhika na hekima hiyo uliyonayo? Kama haujaridhika anza kuomba sasa maombi ya namna hiyo utaona mabadiliko makubwa sana katika maisha yako yote utakayoishi hapa duniani.

Mfalme Daudi alilijua sana jambo hili, ndio maana akaamua kumfundisha Sulemani habari za  kuomba akili na fikra njema. Kumbuka neno nia ni fikra, ni dhamili ni kusudi. Mfalme Daudi alimfundisha Sulemani jinsi Mungu alivyo. Alimwambia maneno haya.“ Nawe Sulemani mwanangu mjue Mungu wa baba yako, ukamtuikie kwa moyo mkamilifu, na kwa NIA ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikra;…” (1NYA 28:9).  Mfalme Daudi alijua kuwa mafanikio ya mtoto wake yatategemea na aina ya fikra, mawazo atakayokuwanayo.  Alijua kuwa Mungu pekee ndiye mwenye uwezo kuchunguza mawazo au niseme mfumo wa akili za mtu. Kumbuka akili,mawazo,fikra,hekima, vyote hivyo vipo ndani ya moyo wa mtu, sasa mwenye kuvichunguza hivyo ni Mungu, Mungu ndiye anajua kwa wakati huu wewe unatakiwa uwe na akili au fikra za kiwango gani, bahati mbaya watoto wa Mungu wngi hawalijui hili. Tunaishi kwa mawazo yaleyale ya nyuma, ndio maana tunakwama kwenye mambo mengi sana. Kanisa halijafundishwa masomo ya namna hii kwa upana, ndio maana watu wengi hawana muda wa maombi ya kuomba wapewe akili,au wageuzwe hizo nia zao za kizamani.

Ona siku ile Mfalme Sulemani alipokutana na Mungu, na Mungu akampa nafasi ya kumuomba jambo lolote lile, Mfalme Sulemani alimuomba Mungu ampe akili nyingi, Umewahi kujiuliza swali Mfalme Sulemani alijua wapi maombi ya namna hiyo? Mungu alinifundisha kuwa baba yake ndiye aliye mfundisha namna ya kuomba maombi maalumu ya namna hiyo. Sikia maneno haya.”  Sasa mwanangu, Bwana awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako. Bwana na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya  Israeli; ili uishike torati ya Bwana, Mungu wako. Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu Bwana alizomwagiza Musa juu ya Israeli; uwe hodari na moyo mkuu, usiogope wala usifadhaike.” ( 1NYA 22:11-13). Mfalme Daudi alimfundisha mwanae kuwa Mungu atampa akili, siku alipopata nafasi ya kuomba tu, hakusita kukiomba kile ambacho baba yake alimfundisha.

Wewe sikia maombi ya Mfalme Sulemani. “Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, omba  utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sas Ee Bwana Mungu, limyamkinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya  watu hawa….” (2NYA 1:7-10)  “ Mfalme Sulemani alimwomba Mungu ampe hekima na maarifa, Mungu alifurahia Maombi ya Sulemani, akampa sehemu nyingine neno la Mungu lina sema Mungu alimpa Sulemani akili nyingi ona. “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu kama mchanga uliopo pwani.” (11FAL 4:29).

Hata leo hii ndugu yangu Mungu anataka akuone ukimuomba akupe akili, au azigeuze hizo fikra zako ziwe kama atakavyo, ukianza kumuomba maombi ya namna hiyo nakuambia ukweli atakupa akili, unaweza kusema mbona ninazo akili. Sikiliza, Unazo chache, fanya maombi Mungu akupe akili nyingi, Mungu ametuagiza sisi watoto wake tuwe na akili na tuzitumie vema,  “ “Tumia akili kama ipasavyo..” ( 1KOR 15:34A) Kama anataka tutumie akili zetu vema fikiria tunaakili za namna gani? Za kiwango gani? Mimi nilipopokea somo hili nilijiona sina akili kabisaaa. Na nimeamua kufanya maombi kila siku ili Mungu anipe akili na nizitumie vema, Ili utoke kwenye umasikini unahitaji fikra njema, zakukutoa hapo,unahitaji maarifa, unahitaji mawazo safi kwa maana nzuri unahitaji mfumo mzima wa fikra zako uwe sawasaw. Sasa ona jinsi watoto wa Mungu wengi tulivyokwama kwenye umasikini, tunaomba kila siku Mungu atubariki, unajua kama unataka utoke hapo lazima ubadilishwe nia yako hiyo. Ukianza kumuomba Mungu akubadilishe hiyo nia yako kwa kupitia maombi maalumu, nakuambia ukweli atakupa akili za kutoka hapo! Kinachokukwamisha ni namana unavyojiwazia, unavyofikiria,unavyo kusudia au kupanga kwako mambo. Huoni njia ya kutokea kwa sababu macho yako ya ndani yaani mfumo wa kufikira kwako haujakaa vizuri, unahitaji kubadilishwa, Mtume Paulo analiita jambo hilo kuwa macho ya mioyo yetu  ya tiwe nuru. “Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajiri yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, baba wa utukufu,awape ninyi roho ya hekima naya ufunuo katika kumjua yeye: macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;…….” (WAEFESO 1:15-19).

Ukisoma maandiko matakatifu, utaona kuwa Mungu ndiye awapaye watu akili, ona hawa ndugu Mungu aliwapa ndani ya mioyo yao akili. “Basi Bezaleli na Oholiabu watenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana ametia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana alivyowaagiza. Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, amabye Bwana alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimza ili aende kuifanya kazi hiyo;” (KUTOKA 36: 1-2).

Umesikia maneno hayo, kama Mungu ndiye  aliyewapa hao ndugu akili kwanini usianze kumnyenyekea leo na kumuomba akupe wewe akili? Naamini ukimuomba atakupa akili na kuigeuza kabisa hiyo nia(fikra) yako iwe kama Mungu atakavyo, kumbuka Mungu anataka uwe na akili nzuri kila siku.

Hizi ndizo salamu zetu za mwezi huu. Zipokee, na zifanyie kazi. Mungu akubariki sana tunakutakia mafanikio katika kila jambo jema ulifanyalo.

Ni sisi

Mr Steven & Mrs Beth Mwakatwila.