Salamu – Disemba, 2010

Bwana Yesu asifiwe Sana…. Tunakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo aliye hai. Mimi na familia yangu tu wazima tunamshukuru Mungu kwa kutupa uzima, pia tunapenda kukushirikisha jambo hili, Kutokana na huduma aliyotupa Mungu kukua kila siku, tumeanza kulitanua hema letu au darasa letu linalotembea pia kununua viti kwa ajili ya hilo darasa, mpango wetu ni kuwa na hema linayoweza kukalisha watu zaidi ya elfu tano, pia tumeanza kulitanua jukwaa tunalolitumia katika huduma yetu. Tunapenda kukushirikisha Baraka hizi, ikiwa utakuwa na mchango wa aina yoyote ile unaweza kuuwakilisha kwetu, Angalia katika ukurasa wako wa tovuti yetu sehemu ya kuchangia huduma utapata maelezo ya namna ya kuchangia au sehemu ya wasiliana nasi, Mungu akubariki sana kwa mchango wako.   

Hebu sasa pokea salamu zetu za mwezi huu wa kumi na mbili. Katika mwezi uliopita tuliendelea na mfululizo wa salamu zetu katika eneo la kugeuzwa nia zetu, Sikiliza maneno haya ya Bwana ya semavyo “…Bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yakupendeza, na ukamilifu.” (WARUMI 12: 2B). Tulianza kuona kuwa Mungu anataka kutuona sisi watoto wake tukiwa na nia njema kabisa, neno nia ni fikira, au makusudio, au ufahamu wako, kwa maana nzuri ni mfumo mzima wa akili zako. Kuna mambo mengi sana yanayo msikitisha Mungu, moja ya jambo linalomsikitisha Mungu ni pale anapowaona watoto wake wakiwa na nia mbaya, au fikra mbaya. Sikia, Mungu anataka akuone ndugu yangu ukiwa na fikra zilizo sahihi, au niseme ukiwa na AKILI NZURI. 

Hebu msikilize asemavyo katika maneno yake haya, “Kwa maana watu wangu ni wapumbavu; hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu, ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa” (YEREMIA 4: 22) Ukiyasoma maneno hayo utaona wazi kuwa, unaweza kabisa kuwa mtoto wa Mungu lakini ukawa huna akili! Au huna ufahamu! Ama huna maarifa! Kitendo hicho Mungu hakipendi kabisa, Mungu anataka watoto wake tuwe na akili, Ndio maana anasema anataka tugeuzwe nia zetu. Mungu anataka akuone ukiitumia akili yako ipasavyo ona asemavyo “Tumieni akili kama ipasavyo….,” (1KOR 15:34) Sehemu nyingine anasema tusiwe wajinga ona maneno haya “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga…” (WAEFESO 5:17). Mungu anataka watoto wake tuwe na akili na tujue namna ya kuitumia hiyo akili aliyotupa katika kufanya au kuyafahamu yaliyo mema, nina posema yaliyo mema, wengi wanafikiri ni kutokutenda dhambi tu, sikia Mungu anataka uwe na ufahamu katika kufanya mambo ya kimaendeleo yawe ya kiroho au kiuchumi.  

Ona tulivyo leo utaona hiki ni nacho kuambia. Watoto wa Mungu wengi sana kwa maneno yao, kwa matendo yao, utawaona tu wengi ni wajinga sana. Mjinga ni mtu asiye fahamu, au asiye na maarifa, Mungu anasema watoto wangu hawana maarifa tena wamepungukiwa na akili, kumbe akili zinaweza kuongezeka, kwanini nasema hivyo? Sikiliza kama anasema wamepungukiwa akili maana yake zinaweza kuongezeka. Ngoja nikuulize swali hili je! Wewe zinaongezeka au zinapungua?  

Katika somo hili tumeanza kujifunza namna ya kuzigeuza au kuzitengeneza fikra zetu, tulianza kuona katika eneo la kama unataka kugeuzwa nia yako au fikra zako lazima ujue vitu vinavyo weza kuharibu fikra au akili ama ufahamu wako, ukivifahamu ni rahisi kwako kuvikwepa na kwa kufanya hivyo utaanza kuwa na akili au ufahamu mzuri. Tuliona jambo la kwanza linalo haribu au kupunguza au kuondoa akili za mtu ni dhambi. Leo twende mbele kidogo tuone jambo la pili linaloweza kuharibu nia yako AU MFUMO MZIMA WA KUWAZA KWAKO ni hili. 

MAZOEA AU MAZINGIRA UNAYO ISHI 

Siku moja Roho Mtakatifu alinifundisha jambo hili, Mazingira au mazoea yanaweza kuharibu kabisa akili za mwanadamu. Mungu Roho Mtakatifu alinifundisha kuwa ni kwanini wana wa Israeli walimsumbua Musa kule jangwani wakimdai awape nyama nk, Mungu alinifundisha kuwa tatizo lilikuwa katika mfumo wa mawazo au fikra za wana wa Israeli, kumbuka hawa ndugu waliishi utumwani Misri miaka mia nne na thelathini, walizoea kutumikishwa, walizoea kuletewa chakula na hao mabwana zao, walizoea kutunzwa, Miaka hiyo yote katika vizazi vyao walizoea hali hiyo ya kitumwa. Una jua mazoea hayo yaliwajengea tabia ya kijinga sana, tabia gani hiyo? Ni hii hawakujua kujitafutia kitu chao, au kusimamia mali zao, walizoea kula nyama ya kupewa si ya wao kutafuta, mfumo mzima wa kuwaza kwao ulizoezwa hivyo. 

Mungu alipowatokea kwa kupita mtumishi wake Musa, nakuambia ukweli ilikuwa ngumu sana kwa watu hao. Kwanza kuondoka kwao Misri ilikuwa shida sana kwa sababu walizoea kuishi huko Misri. wewe soma kitabu chote cha KUTOKA utaona ninacho kuambia, ilikuwa ngumu sana kwa Musa kutembea na watu ambao akili zao kwa miaka mianne na thelathini zilizoezwa kuwa watumwa.Ujuzi wao wote ulikuwa ni kuwatumikia wa Misri, unajua unaweza kuwalaumu hao ndugu lakini nataka nikuambie ilikuwa ngumu sana kwao, Akili zao zilizoea mazingira ya Misri ya kutumikishwa na kuwaona hao wa Misri kama ni mabwana zao, unajua hata Musa alipotokea bado akili za hao Waisraeli ziligoma kumpokea. 

Ona mfano huu, Siku moja Musa aliamua kwenda kuwa tembelea hao ndugu zake Waebrania, kipindi hicho anaishi kwenye nyumba ya Farao, akaamua kuwasaidia hao ndugu zake, lakini kwa kuwa akili za hao ndugu zake zilijengwa kwa kuwaona Wamisri kama ndio mabwana ilikuwa ngumu sana kumpokea Musa. Sikiliza maneno haya yasemavyo, “Akamwona  mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, enyi ndugu zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? Musa akakimbia kwa neno hilo akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani ……” (MDO 7:24-29)  

 

Ukiyasoma maneno hayo kwa kutulia utagundua kuwa hao ndugu zetu wana wa Israeli walikuwa hawana ufahamu, walikuwa hawafahamu kuwa Mungu anaweza kuwaletea mwamuzi mwingine zaidi ya Wamisri, hawakuwa na ufahamu kuwa Mungu anaweza kuwainulia mkuu mwingine tena kutoka kwa miongoni mwao, walijiona wao hawawezi ila Wamisri ndio wanaoweza. Ukikaa na kutulia utaona kilicho wasababishia hao ndugu zetu wasijue kuwa Mungu anaweza kuwaletea mkuu mwingine zaidi ya Wamisri kilikuwa ni mazoea au mazingira waliyokulia.  

Hata walipotoka huko Misri walijikuta wanakwama njiani, kisa kilikuwa mazoea, walizoea kula nyama na matango huko Misri, walipokutana na kitu kipya akili zao ziligoma kabisa kukipokea, wakataka kuludi Misri, unajua nakuambia mifano hiyo iliujue kuwa mazoea ni mabaya sana, yanaweza kukufunga akili zako kabisa na ukawa mjinga tena mbumbumbuu kabisaa ingawa umeokoka. Ngoja nikupe mfano huu labda utaelewa, niliwahi kwenda nchi moja ya Kiafrika sitaitaja jina lake, nilikwenda kule kikazi, shirika ninalofanyia kazi wasimamizi wake wakuu ni Wamalekani, mimi nilipata nafasi ya kusimamia shirika letu kwa kipindi kile nchini humo. Sasa hao ndugu waliposikia kuna msimamizi atakuja kuwasimamia walifikiri ni mzungu, naamini kitendo chakuniona mimi Mtanzania tena mweusi ndiye msimamizi wao kiliwapa taabu. Nilipo kaa katika ile nchi niligundua jambo ambalo linafanana kabisa tabia ya hao watu na Wana wa Israeli kipindi kile wanatoka Misri wakielekea Kanani, niliwaona hao watu jinsi akili zao zivyojengwa kumuona mzungu kama ni bwana, au kama ni mtu mkubwa sana, Watu wan chi ile wanamdhamini mzungu kweli, wakipishana na mzungu barabarani wako tayari hata kupiga magoti, yaani ni taabu kweli. Nilifanya utafiti ni kwanini watu hao wako hivyo, niligundua kuwa ufahamu wao ulihalibiwa tokea kipindi kile cha ukoloni, na hata baada ya kupata uhuru kutokana na mfumo wa utawala uliokuwepo baada ya kupata uhuru wao, bado walijengewa akilini mwao kama bila mzungu hakuna linalofanyika. 

Akili za hao watu zilihabiwa na mazingira ya utawala waliokuwa nao, walitawaliwa na mzungu kwa miaka mingi, wakapokea ndani ya akili zao kuwa mzungu ni bwana, basi mpaka leo hii wengi kwao nzungu ni bwana, hata akiwa mtoto mdogo lakini ni mzungu watamsalimia shikamoo! Mazingira yanaweza kukuharibu kabisa akili zako ukawa ni mtu ambaye huoni pa kutokea au pa kuingilia, utaishi kwa mfumo ulioukuta katika hayo mazingira unayo ishi. Nakumbuka kipindi kile marehemu Raisi Nyerere anaamua kupumzika kazi, watu wengi sana walipata shida kukubariana na wazo lake la kupumzika. Nakumbuka kuna watu walilia sana, wakisema tumekwisha! unajua ni kwanini walisema hivyo? Sikia, walizoea hali ya maisha wakiwa chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, wengi hawakufikiri kabisa kuwa kuna mkuu mwingine anaweza kutokea, fikira za Watanzania wengi zilifungwa kwenye mazoea waliyoyazoea ya kumuona Nyerere tu. Ndio maana hata leo utawasikia watu wa aina hiyo wakikuambia ANGEKUWEPO NYERERE LEO! Akili zao hazioni wala hazitambui wakuu wengine wanaotokea katika nchi yetu, hata mema wanayoyafanya, hawayaoni hayo mema, wala hawafahamu nini kipya kinachoendelea wako kama Wana wa Israeli wakikumbuka Misri walikokula nyama ya kupewa ila ya kutafuta wao hawaoni kama jambo hilo linawezekana!  

Ngoja nikupe mfano mwingine wa mazingira au mazoea jinsi yanavyoweza kuharibu kabisa mfumo wa fikra za watu, wakati ule wazungu wanaleta msimamo wao wa kuzilazimisha nchi nyingine ziingie katika mfumo wa vyama vingi, Watanzania wengi waligoma kabisa kulipokea jambo hilo geni, wengi walisema, nchi itaingia katika vita nk, unajua mazoea ni mabaya sana. Akili zetu zilifungwa kabisa katika eneo hilo la kupokea vyama vingi, Nakumbuka hata vilipo anzishwa Watanzania wengi ilikuwa ngumu hata kuvitamka hivyo vyama kwa majina yao, ilionekana kama ni kukosa uzalendo kabisaa wa nchi yetu. Unajua hata watu waliokuwa wanaingia kwenye hivyo vyama tuliwaona kama waleta vita, Nakumbuka kuna mkutano ulifanyika eneo lile mimi naishi kipindi hicho ni mdogo mdogo bado, mkutano huo uliandaliwa na watu wa chama kipya, unajua watu wengi tuliogopa sana, tukiambiana vita itatokea, kina mama walihimiza watoto kutotembea hovyo kwani vita imeingia mjini kwetu, vita yenyewe wala haikutokea ila wengi wakaamini vita ipo au itakuja.  

Leo hii nimekuwa mtu mzima bado nasikia watu wengi wakisema vyama vya upinzani ni vita! Unajua nakupeleka wapi? Nataka uone madhara ya mazoea ya kimazingira yanavyoweza kukuloga kabisa na ukawa na upungufu wa akili au fikra, Unajua leo hii mazoea uliyojizoelea ndiyo yanayo itawala hiyo akili yako. Hilo ndilo jambo la pili linaloweza kuiharibu akili yako kabisaa. Umewahi jiuliza swali hili, kwanini leo hii watanzania tunaishi maisha ya kimasikini wakati Mungu ametupa utajiri mkubwa sana? Mungu alinifundisha kuwa tatizo kubwa lipo kwenye akili au fikra zetu zilivyologwa na mazingira au mazoea tuliyonayo, Watanzania wengi wamezoea kupokea misaada, akili zao zimelala hapo! Wanataka serekali iwatandikie mpaka vitanda vyao vya kulala! Kwanini? Walizoe vya bure tokea tulipopata uhuru, wanapoambiwa kufanya kazi wengi jambo hilo ni taabu kwao, Mimi nina fanya kazi na Wamalekani, mara ya kwanza ilikuwa shida sana kwangu kuamka asubuhi, kuingia kazini mapema kufanya kazi mpaka usiku wa manane tukiwa wote na hao wazungu, kesho hivyo hivyo hakuna muda wa kupiga hadithi ofisini, kazi ni kazi. Unajua akili yangu mara ya kwanza iliona kama huo ni utumwa, swali langu lilikuwa mbona hawa jamaa nao wanachapa kazi pamoja nasi mpaka usiku? Wakisema kesho tuonane saa moja saa moja wako ofisini na chai waliisha kunywa, ila mimi hapo chai sijanywa na ofisini nimechelewa. 

Mpaka Bwana Mungu aliponifundisha habari za kugeuzwa nia yangu, yaani fikra zangu zigeuzwe na kuona kuwa jambo la kufanya kazi kwa bidii si la utumwa, bali huo ndio wajibu wa kila mtu afanye kazi tena kwa bidii, ona sasa leo atokee kiongozi nchini anaye himiza watu wafanye kazi kwa bidii, utaona atakavyo onekana kama ni mshetani Fulani aliyetokea katika nchi ya Tanzania. Kwanini katika nchi yetu watu wanatafuta utajiri wa haraka haraka? Wanataka wachukue rushwa, wanafanya ujambazi, wanakwenda kwa waganga kupata eti mali kwa kuwaua watu na kuchukua viungo vya miili yao ili kupata utajiri wa haraka haraka, unajua ni kwanini inatokea hivyo? Tatizo lipo kwenye mazoea ya kutofanya kazi, akili imezoezwa kupokea vya bure, kwa kuwa imezoe kupata vya bure hivyo ndiyo inakuwa rahisi sana kuyafanya hayo mambo yasiyofaa. 

Sikia mazoea yanajenga tabia, na tabia chanzo chake huanzia kwenye nia au fikra za mtu, Sasa lazima ujue kuwa leo hii shetani anaweza kuyatumia mazoea ya mazingira unayoishi ili tu aharibu akili zako. Mungu hapendi uishi kimazoea, anataka leo uwe makini kwenye eneo hilo, usikubali mazingira ya haribu fikra zako, anataka ugeuzwe fikira zako zisikae katika mfumo wa kimazingira bali zikae sawasawa na Mungu atakavyo ziwe. Inawezekana ndugu yangu miaka mingi umekaa kwenye hayo mazingira uliyonayo, yamekujengea tabia Fulani ambazo zimeiloga nia yako, Mungu anataka leo ugeuke, ona mfano huu, Wana wa Israeli walikaa jangwani miaka alobaini. Miaka alobaini ni mingi sana, hao jamaa walizoelea maisha ya jangwani, na hata akili ziliharbiwa na mazingira waliyokuwa nayo, unajua hawakuona njia ya kutoka hapo walipo kwama mpaka siku Mungu alipowaambia WAGEUKE! Njia ya kutokea hapo walipokwama ilikuwepo kabisa, ila hawakuiona kwa muda wa miaka alobaini, sikia maneno haya ya Bwana yasemavyo “Bwana, Mungu wetu, alituambia huko HorHebu, akasema, mlivyokaa katika mlima huu vyatosha; geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na Lebanoni, mpaka mto mkubwa, mto Frati. Angalieni, nimewakea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.”(KUM 1:6-8). 

Ndugu hao walikwama hapo siku nyingi sana, mpaka Mungu alipowaonea huruma na kuwaambia, sasa yatosha, mmekaa hapo mlimani sasa yatosha! Unajua alichokifanya Bwana ni kuwaambia GEUKENI! Kwa maana nzuri wageuze mtazamo wao wa kukaa hapo mlimani, Mungu aliona wazi kuwa mazingira ya mlimani ndiyo yalikuwa yamewachochea hao ndugu kukaa hapo, naamini walikuwa hawana wazo lingine la kutoka mlimani hapo walizoelea mazingira ya hapo mlimani, mpaka siku Bwana alipoinglia kati na kuwaambia geukeni, au badilisheni mtazamo wenu mimi sijawaambia mkae hapo mlimani. au si mpango wangu mkae mlimani, mlimani hapo si mahali pa nyinyi kuishi au si pa kudumu, baada ya kuwaambia hilo hao ndugu ndio walipoiona njia ya kutokea hapo na kufahamu kuwa wao si wa hapo mlimani.  

Ngoja nimalizie salamu zangu kwa maneno haya, Je! Upo kwenye mlima gani? Inawezekana umeishi mlimani hapo kimazoea miaka mingi sana, hata akili zako zimelidhika na mfumo wa mlimani hapo ulivyo. Sikia Mungu anakuambia geuka leo, unaweza kupata swali kama hili, ugeuke wapi? Jibu ni Kwenye nia yako au fikira zako, Sikia usipogeuka katika mtazamo wako utakaa kwenye hiyo nyumba ya kupanga mpaka Yesu atakapo ludi, usijizoeze kukaa kwenye nyumba ya kupanga, au usikubari utawaliwe na mazingira hayo na ukayazoea. Hata kwenye hari ya elimu uliyonayo, ama uchumi ulionao, au kwnye utumishi ulionao, watoto wa Mungu wengi wamekwama hapo, hawaoni njia ya kutokea, kisa mazoea ya mazingira waliyonayo yamewaharibu, Sikia Geuza leo nia yako, Omba Mungu akugeuze Sikiliza tena maneno haya. “…Bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yakupendeza, na ukamilifu.” (WARUMI 12: 2B). 

Na amini umenielewa baada ya kuliangalia jambo hili la pili linalo weza kuwa ndio chanzo cha wewe kuharibikiwa ufahamu wako, Hebu, basi jitadhimini wewe mwenyewe ukoje? Anza kuyafanyi kazi haya uliyojifunza. Mungu akubariki sana. Hizo ndizo salamu zetu kwako. 

Ni sisi ndugu zako katika Bwana Yesu Kristo  

Mr Steven na Mrs Bett Mwakatwila