Salamu – May, 2011

Bwana Yesu asifiwe sana. Tunakusalimu kwa jina la Bwana Yesu Kristo, Tunamshukuru sana Mungu aliyetupigania na kututunza, pia kutupa nafasi ya kukuletea tena salamu hizi za mwezi wa tano.  Kumbuka mwezi uliopita tulikuwa na salamu zenye kichwa “MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UMUOMBE MUNGU KILA SIKU. (ENEO LA KUYAJUA MPENZI YAKE AU MAKUSUDIO YA MUNGU).” 

Ili leo hii ndugu yangu uanze kupokea majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu, ni lazima ulijue jambo hili, Mungu kupitia neno lake anatufundisha akisema. “Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” (1 Yohana 5:14-15). Ukiyasoma maneno hayo utaona kuwa, Mungu ametupa utaratibu wa kumuomba. Anasema tukiomba sawasawa na mapenzi yake ndipo tutakapopewa kile tunachokihitaji toka kwake. Kwa maana nyingine ikiwa hatujaomba sawasawa na mapenzi yake hapo itakua ni vigumu sana kupewa chochote kile tumuombacho Bwana Mungu. 

Kumbuka neno Mapenzi ya Mungu maana yake sahihi ni Kusudi la Mungu, au Mipango ya Mungu. Katika somo hili tunajifunza namna ya kujua kusudi la Mungu kabla hatujakurupuka kumuomba. Sikiliza, weka bidii kwanza kujua ni nini kusudi la Mungu katika hilo unaloliona, au hilo unalolihitaji, ukilijua kusudi la Mungu hapo ndipo uombe sawasawa na hilo kusudi la Mungu ndipo utakapo fanikiwa sana katika eneo la kupokea majibu ya maombi yako. Ngoja nirudie tena kusema, jifunze kufanya kwanza maombi ya ufahamu, omba Mungu akupe ufahamu wa nini yeye amekusudia katika hicho unachokiwaza au hicho unachokihitaji. Ukipata ufahamu unajua unakuwa na ujasiri wa kumuomba, kwani tayari unakuwa unaomba sawasawa na mipango yake. 

Hebu tusonge Mbele… TATIZO HATUMUULIZI 

Tatizo kubwa ambalo limetukabili watoto wa Mungu wengi ni hili la kutokuwa na maombi maalumu ya kuyajua mapenzi ya Mungu ni nini. Ukisoma maandiko utaona Mfalme Sauli alimkorofisha Mungu kiasi ambacho Mungu aliamua kumkataa asiwe tena mfalme wa Israeli, moja ya sababu zilizomuudhi sana Mungu ni hii ya kutokumuuliza, ona maneno haya ya Bwana yasemavyo “Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi aulize kwake. Asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamuua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.” (1Nyakati 10:13-14). Ona mojawapo ya kosa la Sauli lilikuwa ni hili la kutotafuta kuuliza au kumuomba Mungu ushauri. Kwa maana nzuri kutafuta ufahamu kutoka kwa Mungu ili amfahamishe ni nini iliyo mipango ya Mungu. 

Ukisoma maandiko utaona kuna utofauti kati ya mfalme Daudi na mfalme Sauli katika jambo hili. Mfalme Daudi alijijengea tabia ya kutafuta kwanza kuyajua mapenzi ya Mungu ni nini katika kila jambo alilokuwa analifanya. Akilijua ndipo alikuwa anamuomba Mungu ampe hicho anachokihitaji kwani tayari alijua kuwa Mungu amekusudia kumpa. Ona mfano huu. “Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhari niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko. Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.” (1Samweli 30: 7-8). Ona mfumo wa maombi hayo aliyoyaomba Daudi yalikuwa ni maombi yaliyotafuta ufahamu, au kujua nini Mungu anaona katika jambo hilo ambalo mfalme Daudi analihitaji, Mfalme Daudi haanzi kuomba kulindwa katika vita hiyo. Anaanza kumuomba Mungu amfahamishe, je! Akienda huko atafanikiwa kuwakuta hao maadui zake? Ona jibu kutoka kwa Mungu jinsi lilivyojitosheleza kabisa anamwambia Daudi. “Naye akamjibu, fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote” Mungu alimjibu Daudi jibu lililobeba kila kitu. Daudi alipokea jibu la hitaji lake, akaenda vitani na akafanikiwa. Hata kama huko kungekuwa na matatizo, alikuwa na ujasiri mkubwa wa kumwambia Mungu amsaidie kwani Mungu ndiye aliyemwambia fuata. 

Ona mfano huu mwingine wa mfumo wa maombi ya Mfalme Daudi, soma maneno haya ninaamini utapata fundisho zuri hapo. “Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, lete hapa hiyo naivera. Ndipo daudi akasema, ee Bwana, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mikononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyo sikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye Bwana akamjibu, atashuka. Ndipo Daudi akasema, je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? Bwana akasema, watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda popote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje” (1Samweli 23: 9-13). 

 

Fikiri ungekuwa ni wewe umekutana na tatizo kama hili, ungeanzaje kuliombea jambo hili? Na amini ungeanza kuomba Mungu amzuie Sauli asije Keila, na ungebaki humo ndani ya huo mji kwani ungeamini kuwa umemuomba Mungu akulinde ukiwa humo ndani, na hao watu wa Keila hawatakutoa kwani tayari umemwambia Bwana akusaidie ili watu wa Keila wasikutoe kwa Sauli. Maombi ya namna hiyo ndiyo wayaombayo watoto wa Mungu wengi. Wengi hatumuulizi Mungu ni nini akionacho, au anacho kikusudia katika kila jambo. Daudi aliomba ufahamu kutoka kwa Mungu, Mungu alimjulisha kila kitu kitakavyo kuwa, Daudi akasalimika kwa sababu alifahamu adui yake anataka kufanya ni nini. Na hao watu wa Keila watamtendea nini hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kuondoka katika mji huo. Hebu badilika, anza kuomba maombi ya mfumo huo ninaokuambia ya kutaka kwa Bwana ufahamu wa kila kitu unacho kihitaji au kile ulicho kusudia kukifanya. Mungu anafurahi sana anapokuona wewe ukimpa nafasi ya kukushauri au kukujulisha mapenzi yake. 

Ngoja nikupe mfano mwingine, Mungu alikusudia kumuua mfalme Ahabu, alifikiria huyo Ahabu aende vitani na akafie huko vitani. Soma kitabu chote cha (1Falme 22:1-40) Ukikisoma kitabu hicho utaona kwa upana kile ninachokuambia, vita ikatokea, Ngoja nikuulize swali, Je! Ungekuwepo katika kipindi hicho ungemuombeaje huyo Mfalme? Kumbuka Mungu alitaka huyo mfalme akafie vitani, wewe hujui kusudi la Mungu, ungeombaje? Watu zaidi ya mia nne hawakuujua mpango huo wa Mungu wa kumuua mfalme Ahabu isipo kuwa mtu mmjo tu aitwaye Mikaya, yeye aliujua huo mpango, alifahamishwa na Mungu mpango huo. Sikia neno la Mungu lisemavyo. “Mikaya akasema, sikia basi neno la Bwana; nilimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. Bwana akasema, ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramothi-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi na huyu; akasema hivi akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, jinsi gani? Akasema, nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, utamdanganya na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. Basi angalia Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.” (1Wafalme 22:19-23). 

Ukiyasoma maneno hayo utaona jambo la kushangaza sana. Mungu alikusudia kumuua mfalme Ahabu, fikiri tena ungekuwa wewe upo hapo, ungemuombeaje? Naamini wengi tungeomba Mungu ampiganie Mfalme wetu. Fikiri Mungu ameamua kumuua sisi tunaomba ampiganiye unafikiri tungekipata kile tunachokiomba? Naamini tusingekipata na mfame angekufa tu, tungebaki kusema maneno mengi ya kuvunjika moyo. Lakini kama tungeanza kuomba kujua ni nini kusudi la Mungu angetujulisha kama alivyomjulisha Mikaya. Manabii mia nne, walimuombea mfalme Ahabu vibaya, yaani hawakumuuliza Mungu amekusudia ni nini katika vita hiyo. Nakwambia ukweli, hawakumuuliza Mungu awafahamishe mpango wake ni nini. Wao walikwenda kuomba ushindi na ulinzi juu ya mfalme. Matokeo yake walikosa kufahamu yaliyoamuliwa mbinguni ni nini. Mikaya alimwambia wazi Ahabu kuwa Mungu amemkusudia mabaya, fikiri hujui Mungu amekusudia mabaya wewe unaomba afanye mema unafikiri atakupa hayo mema kwa sababu umeomba tu? Mungu akitangulia kukuambia mabaya aliyokusudia kuyafanya itakua ni rahisi kujua mfumo mzima wa maombi unayotakiwa uyapeleke kwake nayo ni maombi ya toba. 

Ngoja nikupe mfano huu, siku moja nilikua sehemu fulani katika huduma ya maombi nikiwa pamoja na timu ya maombi. Baada ya yale maombi, alikuja baba mmoja, akaniambia kuna jirani yake ana mtoto wake anaumwa sana, na ametolewa hospitalini. Nikamwambia atangulie nitafuata, nikafanya maombi, nikamwomba Mungu aniambie. Je! Ananipa kibali cha mimi kwenda huko? Akaniambia nenda, nikataka kujua tena anataka kufanya nini na huyo mtu, au kwa lugha nzuri niseme nilimuuliza Je! Huko nikaombee nini? Bwana akasema nami, akaniambia hivi. Usishughulike na mwili wake, shughulika na roho yake! Nikafahamu nini kusudi la Mungu kwa mtu huyo. Nilipofika pale niliongea naye habari za Bwana Yesu anaeokoa na kusamehe. Sikia, akaamua kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wake, akaniambia kuwa amejisikia amani sana ndani yake, yaani rohoni, ambayo hajawahi kuwa nayo. Ila huku nje yaani mwilini, anajisikia maumivu sana, akaomba nimuombee ili Mungu amponye, nilikamwambia fumba macho nikuombee. Nikamuombea hivi! Bwana Yesu naomba iponye roho ya mtu huyu na uiokoe! Niliomba hivyo kwa sababu Bwana alisha nifahamisha kusudi lake ni kuiponya roho, hakuwa tayari kuuuponya mwili wa huyo mtu. Hebu fikiri, nisingelifahamu jambo hilo si ningekurupuka kuomba uzima kwenye mwili halafu mtu huyo Mungu asimponye ingekuwa ni taabu sana kwangu kiimani, yaani nimemwombea mtu hajapona, siku chache za mbeleni anakufa hiyo ingekuwa shida sana. Nasema hivyo kwa sababu yule ndugu alikufa baada ya siku chache. 

Hebu nimalize kwa kusema. Weka Bidii kumuuliza Mungu ni nini kusudi lake katika hilo unalotaka kuliomba kwa Mungu. Naamini umenielewa na Mungu akubariki sana  

Mr. Steven & Beth Mwakatwila