Salamu – Januari, 2020

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Nina kukaribisha mpendwa karibu katika kona hii ya salamu za mwezi. Kwanza tunamshukuru Mungu ambaye ametupa mwaka huu mpya. Ni neema kuuona.

Naamini hata wewe mpendwa umepokea neema hii ya kuanza mwaka huu mpya kwa namna ya kipekee. Tumekua na semina nyingi sana mwaka jana tunaamini hata mwaka huu tunatarajia kuwa na semina nyingi.

Tumekua na semina Songea, Tumekua na semina Ubaruku mwishoni mwa mwezi wa kumi na moja,tumekua na kambi la maombi ambalo tunalifanya kila mwishoni mwa mwaka. Lilikua kambi zuri sana..

Nimekuletea salamu mpya kabisa ambazo. Tutatembea nazo mpaka pale Roho Mtakatifu atakapotufikisha. Salamu hizo zimebeba somo lenyekichwa

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE WOKOVU (ENEO LA KUOKOLEWA KATIKA KIPINDI CHA MAJANGA ULIMWENGUNI)

Nichukue nafasi hii kukukaribisha ndugu yangu mpendwa ili kwa pamoja tupate kujifunza somo hili muhimu sana ambalo Roho Mtakatifu aliliweka ndani ya moyo wangu.

Na ndani yangu nimepata kibali cha kukushirikisha hata wewe kitu hiki ambacho nimejifunza.

Naamini hata wewe kuna kitu utajifunza na ninaamini kitakusaidia sana. Na ukiona umepokea kitu chema usisite kumpatia somo hili na mtu mwingine. Hebu tuanze kujifunza.

Ninaamini kabisa kuwa unajua kuwa Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi. Na sijui kama unajua huyu Bwana Yesu Kristo ndiye mwenye uwezo wa kutuokoa katika mambo mengi sana.

Angalia mfano huu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yohana 3:16-17).

Ukiipitia hiyo mistari kwa kutulia utaona uwezo alionao Bwana Yesu Kristo katika eneo la kuokoa ni mkubwa kuliko watu wengi tunavyowaza na kufikiri. Watu wengi wanapolitazama suala la wokovu wanalitazama kwa kiwango kidogo sana.

Bwana Yesu Kristo yeye ndiye pekee mwenye uwezo wa kuuokoa ulimwengu. Kuna utofauti mkubwa wa maneno haya mawili. Ulimwengu na neno Dunia.

Neno ulimwengu kwa maana nzuri ni mkusanyiko wa vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu ikiwemo hiyo Dunia.

Mwanadamu anaishi Duniani, na Dunia imo ndani ya ulimwengu. Mungu ameumba vitu vingi mno, vinavyoonekana na visivyoonekana, vitu hivyo vyoote vimo ulimwenguni.

Mwenye uwezo wa kuviokoa vitu hivyo ni Bwana Yesu Kristo peke yake. Sikia kama anaweza kuviokoa maana yake yeye pekee ndiye mwenye kuvifahamu vema, na yeye pekee ndiye mwenye mamlaka na huo ulimwengu.

Huwezi kuviokoa vitu ambavyo huna uwezo navyo, na pia unaposikia neno kuokoa maana yake ulimwengu ulikuwa hatarini. Bwana Yesu Kristo yeye pekee ndiye mwenye uwezo au nguvu au mamlaka ya kummudu huyo aliyeuweka huo ulimwengu katika hatari au aliyeuteka huo ulimwengu.

Kwa nini nasema hivyo ni kwa sababu yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu. Kama yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu maana yake huyo aliyeutia ulimwengu hatarini hawezi kumzuia Bwana Yesu Kristo kuuondoa ulimwengu katika hatari yoyote ile ambayo ulimwengu ulitiwa ndani yake.

Watu wengi sana hufikiri Bwana Yesu Kristo hufanya kazi ya kuwaokoa wao tu. Sikiliza huyu Bwana Yesu Kristo tuliye naye yeye ana uwezo wa kukuokoa wewe mwanadamu na vitu vyoooote vinavyoonekana na visivyoonekana!!!

BWANA YESU KRISTO ANAWEZA KUIKOA ROHO YAKO MWILI WAKO NA NAFSI YAKO

Sikiliza, kuna maeneo mengi tu huyu Bwana anaweza kabisa kuyatoa kwenye maangamizo. Nataka nikuonyeshe machache ndipo utanielewa zaidi ninapokuambia nini unatakiwa ufanye ili uokolewe kwenye majanga yaliyotokea ulimwenguni kama vile tauni. Au njaa au vita nk

BWANA YESU KRISTO ANAWEZA KUUOKOA MWILI WAKO

Bwana Yesu anaweza kuuokoa mwili. Angalia mistari hii: “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” ( Mathayo 10: 28).

Ukiipitia hiyo mistari utagundua kuwa mwili wako unaweza kabisa ukajikuta kwenye hatari ya kuuawa. Angalia mistari hiyo uone, anayeuua huo mwili hapo si MUNGU, Neno la Mungu linasema hapo hivi wauuao mwili.

Kwa maana nzuri wapo wauuwao mwili ambao si Mungu. Fahamu, mwili wako huo usiku na mchana nakuambia hao wauuao mwili wanautafutia kifo huo mwili wako.

Biblia haiwezi kusema kuwa hao wauuao mwili kama hawapo. Wapo, na wanautafuta huo mwili wako ili wauue. Mwenye uwezo wa kuuokoa na kuambia ni mmoja tu NI BWANA YESU KRISTO.

Sikiliza huyu Bwana ndiye mwokozi wa mwili wako ili USIUAWE. Sikiliza sizungumzii hapo wokovu wa mwili katika eneo la kupata uzima wa milele.

Kwenye eneo hilo mwili hauokoki wenyewe umechagua mauti. Nazungumzia kwenye eneo la mwili kutafutiwa kifo na watu.

BWANA YESU KRISTO ANAWEZA KUIOKOA ROHO YAKO

Eneo la pili ni lililo katika hatari ya kuuawa ni roho yako. Neno la Mungu linasema wapo watu wanaotafuta kuziua roho za watu.

Ngoja nikupe mfano huu uone: “Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.” (Ezekieli 13:18:-21)

Unapoisoma hiyo mistari naamini utaona roho za watu namna zilivyo kwenye hatari ya kuuawa. Biblia ipo wazi inasema kuna watu wanawinda roho za watu ili waziue kabisa. Maana yake hizi roho zipo hatarini mno.

Natamani leo hii uanze kumtazama Bwana Yesu Kristo kama mwokozi wako kwa kiwango kingine kabisaa. Watu wengi humtazama kama mwokozi wao katika eneo la kuwatoa kwenye jehanum tu na kutupa uzima wa milele.

Hiyo roho yako inaweza kujikuta kwenye hatari kubwa mnoo ya kutafutiwa kuuwawa mwokozi wako ni mmoja tu ni Bwana Yesu Kristo

BWANA YESU KRISTO NDIYE MWOKOZI WA NAFSI YAKO

Huyu Bwana Yesu ndiye mwokozi wa nafsi zetu pia. Sikiliza, shetani anaweza kuifungia nafsi kifungo.

Ngoja nikuonyeshe kitu uone namna nafsi ya mtu inavyoweza kukaa kifungoni kabisa, Angalia kwanza mistari hii. “Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.”(Mithali 4:20-23).

Biblia inasema linda moyo wako.maana yake moyo unaweza kuwa hatarini ndiyo maana unatakiwa uwekewe ulinzi mkali.

Huko ndani ya nafsi au moyo kuna vitu vingi vimewekwa na vinatakiwa viwe na uzima yaani visifishwe au kuuwawa.

Angalia baadhi ya hivyo vitu vilivyoko kwenye nafsi ni. “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.”(Ayubu 32:8).

Huko ndani ya nafsi kuna akili. Fahamu nafsi ndiyo pumzi hai ya Mungu. Maandiko yanasema hivi.”BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”(Mwanzo 4: 7)

Huko kwenye nafsi au moyo Mungu ameweka vitu vingi sana. kuna akili, hisia na utashi, huko kuna mawazo, fikra, n.k.

Nafsi inaweza kutekwa na adui ndiyo maana Biblia inasema Tunatakiwa tuziteke nyara fikra za watu: Angalia mistari hii. “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;” (2 Wakorintho 10:3-5)

Biblia inasema wazi kuwa fikra zinahitajika kutekwa. Angalia zinatekwaje kama hazikutekwa? Fikra zinakaa moyoni au nafsini, fikra ni sehemu ya akili. Kwa mujibu wa hiyo mistari unaona wazi moyo au nafsi inaweza kutekwa.

Kama unafikiri nakutania wewe angalia mfumo wa wapendwa wengi kwenye eneo la akili, iwe kuwaza kwao, kufikiri kwao, kutafakari mambo, kuelewa kwao au kujua, kukumbuka au kupanga au kubuni, nk. Utagundua kuna shinda na wengi wanahitaji msaada.

Mwenye uwezo wa kuwaokoa kwenye eneo hili ni mmoja tu ni Bwana Yesu Kristo. Naona sasa umenielewa ninavyokuambia Bwana Yesu Kristo ndiye mwokozi wa ulimwengu.

Bwana Yesu pekee ndiye mwokozi wa hayo yoote. Pia sikiliza Bwana Yesu Kristo ni mwokozi wa majanga yoote

BWANA YESU KRISTO NDIYE MWOKOZI KATIKA MAJANGA YOYOTE

Sikiliza, mwanadamu anayeishi duniani na dunia iliyo ndani ya ulimwengu anaweza kujikuta akikutana na hatari za namna tofauti tofauti ulimwenguni.

Na hatari hizo zoote zina nia ya kutafuta uhai wa mwanadamu. Na moja ya hatari anayoweza kukutana nayo ni hii ya kukutana na tauni.

Tauni ni magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza ambayo kwa kweli hayana tiba. Magonjwa ya mtindo huo ndani yake yamebeba mauti ya mwili. Yaani kuua mwili.

Kuna aina nyingi sana za tauni. Moja ya tauni ni corona, ndui, kuhara damu, mafua ya aina mbalimbali nk. Biblia inasema wazi juu ya tauni, dunia iliishashuhudia tauni nyingi mnoo.

Tokea agano la kale unaona kuna tauni za aina mbalimbali zilizoachiliwa na kuwauwa watu. Tauni ni ugonjwa wa mlipuko unaoambukiza na kuua mwili. Na ni ugonjwa hatari sana.

Ngoja nikupe mfano wa ugonjwa wa corona. Utaona wazi ugonjwa huo ni miongoni mwa tauni. Sikiliza kwa kizazi cha sasa jinsi kilivyojaliwa akili na maarifa utaona kimepata shida mnoo kupata dawa na kinga ya ugonjwa huo.

Fikiria kidogo, Ugonjwa huo unawaua watu wa kila aina, wawe matajiri au maskini, viongozi na wanaoongozwa, watumishi wa Mungu na wasio watumishi, Wazungu kwa Wachina, Waarabu kwa Waafrika n.k.

Sikiliza, ili ndugu yangu upate kupona katika majanga ya namna hii yanapotokea duniani ni lazima ujue ni mambo gani unatakiwa uyajue na uyafanye ambayo mwokozi wa ulimwengu anayosema kuhusu tauni inapotokea ulimwenguni.

Na ili uyajue nilazima uyatafute kwenye Biblia. Humo ndani ya Biblia ndiko kuna maarifa mbalimbali ambayo Mungu kayaweka.

MAMBO MUHIMU YA KUFANYA PINDI DUNIA INAPOANGUKIA KATIKA JANGA LOLOTE BAYA

Angalia mistari hii uone mambo muhimu ya kufanya: “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” ( 2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Unapoisoma hiyo mistari utagundua vitu vingi mnoo vimewekwa hapo ambavyo ndivyo kila mtu au taifa watatakiwa wavifanye.

Kitu cha muhimu cha kujifunza hapo ni chanzo cha hayo majanga huwa ni nini? Ukiisoma hiyo mistari utagundua kuwa Mungu anaweza kuwa ndiye chanzo.

Angalia anasema kuwa anaweza kuleta njaa, Neno la Mungu linasema Mungu anaweza kuzifunga mbingu isiwepo mvua dunia.

Kama dunia itakosa mvua maana yake itakosa chakula. Na kitakachotokea ni njaa, na njaa hiyo huwa ni kali mno mpendwa. Na njaa hiyo ndani yake hubeba mauti kwa ajili ya mwili wa mwanadamu.

Anasema anaweza kuleta nzige, nzige wakiingia mahali watasababisha njaa, na hiyo njaa ndani yake inakuwa imekusudiwa iuue mwili.

Jambo lingine hapo utaona ni tauni. Tauni nayo ndani yake inakuwa imebeba mauti ili kuua mwili au kuwaua walioko ulimwenguni.

Sikiliza, kwa mujibu wa hiyo mistari utaona tauni hiyo pia hutoka kwa Mungu, Nzige hao pia hutoka kwa Mungu, Njaa hiyo iletwayo na ukame pia hutoka kwa Mungu.

Unaweza kusema kivipi? Msikilize Mungu nasema,hivi ‘Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;”

Mungu ndiye amesema hapo kuwa anaweza kuwapelekea watu wake mambo hayo. Watu wengi sana wanamtazama Mungu kama ni Baba mmoja hivi asiyechukia.

Sikiliza Mungu anapoona watu wake wamemwacha na kuanza kufanya dhambi na kuabudu miungu mingine fahamu anaweza kuviachia hivyo vitu kabisa, iwe kwenye taifa, au miji au duniani pote

Sasa sikia anapoviachia hivyo vitu na hao watu ili wapate wokovu kutoka kwa Mungu kuna mambo hapo Mungu amesema watu hao wanatakiwa wayfanye.

JAMBO LA KWANZA LAZIMA UWE MTU ULIYEITWA KWA JINA LAKE

Angalia tena mistari hii. Inasema hivi. “ BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2 Mambo ya Nyakati 7: 12-15)

Angalia vizuri hiyo mistari. Kama unataka leo wokovu kutoka kwenye majanga ya tauni ni lazima uhakikishe wewe ni mtu wa Mungu tena uliyeitwa kwa jina lake.

Unaweza kujiuliza nifanyeje ili niwe mtu niliye itwa kwa jina la Bwana? Sikiliza Ni lazima uhakikishe unamwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana wako na mwokozi wako:

Biblia inasema hivi. “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka” (Warumi 10:9-13)

Ukiipitia hiyo mistari utaona wazi kabisa ili uokoke: iwe rohoni, mwilini, nafsini, n.k unatakiwa umwamini Bwana Yesu Kristo aliyekuja kwa jina la Mungu.

Msikilize Bwana Yesu Kristo asemavyo naamini ndiyo utaelewa iliuitwe kwa jina lake unatakiwa ufanye nini.

Anasema hivi “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie” (Yohana 17:11-12)

Kwa mujibu wa mistari hiyo utaona Jina hilo alilonalo Bwana Yesu anatuambia wazi kuwa si jina lake, ni jina la Mungu. Sasa ili wewe uitwe kwa jina lake Mungu ni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ili uwe mtu uliyeitwa kwa jina la Mungu ambalo ni YESU.

Hapo ndipo utaanza kupata ulinzi mpendwa. Ukiwa humu ulimwenguni. Msikilize Vizuri Bwana Yesu anasema hivi: “Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” (Yohana 17:14-16)

Umeyasikia maneno hayo? Huyo mwokozi wa ulimwengu anasema wazi kabisa kuwa anao uwezo wa kuwalinda waliomo ulimwenguni ambamo yumo hata mwovu yaani shetani.

Ili uupate ulinzi humu ulimwenguni lazima umwamini Bwana Yesu Kristo ndipo UNAPOPATA TIKETI YA KULINDWA HUMU ULIMWENGUNI. Nje ya hapo ni ngumu kupokea ulinzi kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

Sikiliza Mungu anasema hivi. “ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu…IKIWA UNATAKA KUOKOLEWA NA TAUNI lazima uhakikishe wewe umeitwa au umo ndani ya jina lake Mungu liitwalo YESU.

Kama haumo humo ndani tafuta haraka kuingia humo ndani kwa imani. Tafuta kila uwezalo kumruhusu Bwana Yesu Kristo awe ndani yako.

JAMBO LA PILI: JIFUNZE KUWA MNYENYEKEVU

Sikiliza unaweza ukawa ndani ya Bwana Yesu Kristo lakini ukakosa sifa hii ya kuwa mnyenyekevu. Fahamu ndani ya unyenyekevu kuna utii.

Ngoja n ikuulize swali wewe ni mtii katika maagizo aliyokupa Bwana Yesu Kristo?

Watu wengi wameokoka na wanajifariji mnoo kuwa aiseee! Mungu atatulinda katika majanga mbalimbali yaukumbayo ulimwengu.

Hawajui kuwa Mungu ameweka utaratibu huu wa watu wake walioitwa kwa jina lake wanatakiwa wawe wanyenyekevu kwa Mungu.Ili awaokoe au awaponye na majanga au na tauni yoyote

Angalia wewe ni mnyenyekevu? Kweli unampenda Mungu? Angalia mistari hii utaona sifa za mtu atakaye okolewa katika majanga ya namna hiyo yakitokea.

Maandiko yanasema hivi “Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;” (Zaburi 91:3-15)

Angalia hapo anasema yupo tayari kutuokoa na tauni, lakini kuna neno hili anasema KWA KUWA AMEKAZA KUNIPENDA NITAMWOKOA!!” Si unajua ndani ya upendo kuna kutii yoote?

Angalia hapo kwa kutulia hasemi nitamwokoa kwa sababu ameitwa kwa jina langu tu, anasema kwa kuwa amekaza kunipenda. Angalia leo hii ukoje? Mungu akiangalia moyoni mwako anauona upendo ule wa kwanza?

Mbona umeacha kumtumikia, leo hii hata kusoma Biblia tu husomi, angalia mwenendo wako ulivyo wewe mwenyewe unaona wazi haujawa mnyenyekevu kwa Mungu. Haumtii, kuna dhambi amekutaza usifanye lakini unafanya kabisaa hata huna hofu ya Mungu.

Sikiliza yaani ili Mungu akuokoe ni lazima uhakikishe leo hii unaanza kumnyenyekea Mungu yaani mtii. Mpende, fanyia kazi yale anayokuagiza Acha njia zako mbaya mpendwa.

Sikiliza unaweza kuwa mtu aliyeitwa kwa jina la Mungu lakini ukawa ni mtu mwenye njia mbaya kabisa. Anasema acha njia mbaya.

Asante kwa kunisikiliza Mungu akupe nafasi nyingine ya kuuona mwaka ujao wa 2020. BARIKIWA SANA

Ukihitaji masomo yetu unaweza kuyapata kwa njia hizi zifuatazo:-

 1. App yetu ya huduma yenye jina  “MWAKATWILA (HUSONEMU)” utaipata Play Store ambapo kuna masomo mengi sana hapo.
 2. Tovuti yetu ya www.mwakatwila.org
 3. YouTube – Mwakatwila au HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU (HUSONEMU).
 4. Facebook ingia katika hiyo tovuti (website) yetu utaona alama ya Facebook (f) “like” na utapata maelezo ya kujiunga au ingia Facebook halafu andika “SOMA NENO LA MUNGU”
 5. Instagram ingia Instagram app halafu andika “Steven Mwakatwila”
 6. DVDs au CDs
 7. VITABU. Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733, ili kupata VITABU, DVD & CD.
 8. Kwa njia ya REDIO:- Utapata mafundisho yetu kwa redio zifuatazo:-
  • Rungwe FM 102.5 Kila siku ya Jumapili  saa tatu mpaka saa nne usiku.
  • Baraka FM 107.7 Kila siku ya Jumanne saa kumi na mbili jioni mpaka saa moja usiku.
  • Bomba FM 104.1 Kila siku ya Ijumaa saa tatu usiku mpaka saa nne usiku.
 9. Unaweza kutupata kwenye ONLINE RADIO yetu:-  radio.mwakatwila.org

Kwa Mawasiliano zaidi Utatupata kwa namba hizi:-

+255 754 849 924 au +255 756 715 222

Wako

Mwl Mr & Mrs Steven Mwakatwila.